WANANCHI: Washtakiwe - MAWAZIRI WABURUZWE KORTINI

nngu007

JF-Expert Member
Aug 2, 2010
15,862
5,797

Washtakiwe
• WANANCHI: MAWAZIRI WABURUZWE KORTINI

na Mwandishi wetu - Tanzania Daima

SIKU moja baada ya Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuridhia mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yanayotarajiwa kufanywa wakati wowote kuanzia hivi sasa na Rais Jakaya Kikwete, wananchi wametaka viongozi hao wafikishwe mahakamani.


Tanzania Daima Jumapili lilizungumza na viongozi wa siasa na wananchi ambao wameweka bayana kuwa hatua ya kufanya mabadiliko kwenye baraza la mawaziri ni nzuri lakini haitakuwa na maana iwapo wanaotuhumiwa kwa ubadhirifu hawatafikishwa mahakamani.


Baadhi ya mawaziri walitajwa kwenye ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na zile za kamati za kudumu za Bunge kuwa wizara zao zilibainika kuwa na vitendo vya ubadhirifu wa mali ya umma, hivyo kushinikizwa kuachia madaraka.

Miongoni mwa waliotakiwa kujivua ‘gamba’ ni Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo, Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, George Mkuchika, Waziri wa Viwanda na Biashara, Cyril Chami na Waziri wa Uchukuzi, Omari Nundu.


Hata hivyo baadhi ya mawaziri kwa wakati tofauti walikaririwa kuwa hawaoni sababu ya kujiuzulu, kwakuwa tuhuma zinazoelekezwa kwao ni uzushi na zenye lengo la kupakana matope.

Jitihada za mawaziri hao kulinda nyadhifa zao juzi ziliingia shubiri baada ya Kamati Kuu ya CCM kubariki mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yanayotarajiwa kufanywa wakati wowote kuanzia sasa.

Zitto anena

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashirika ya Umma, Zitto Kabwe, amesema uamuzi wa CC ya CCM unaonyesha kuwa ripoti za CAG na kamati za Bunge zinatambulika na kuheshimika.
Zitto alisema hatua ya kulifanyia mabadiliko Baraza la Mawaziri uwe mwanzo wa kuelekea kwenye hatua nyingine ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria waliohusika na ubadhirifu wa rasilimali za taifa.

“Hatuwezi kila siku kuwa walalamikaji, ni lazima tuanze kuwajibishana, mimi nilishaanza kukusanya sahihi 73 za wabunge ili tupige kura ya kutokuwa na imani na waziri mkuu.


“Mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yakifanywa nitakaa pamoja na wabunge wenzangu kujadili nini cha kufanya, kwakuwa suala hilo tayari nililipeleka kwa Spika,” amesema.


Lipumba amshangaa JK

Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, amesema Rais Kikwete alipaswa kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri mapema, kwakuwa yeye aliiona mapema ripoti ya CAG.

Alisema kusuasua kwa maamuzi ya kiongozi huyo ndiko kulikowafanya wananchi na wabunge washindwe kuwavumilia mawaziri wanaohusishwa na ubadhirifu.


Lipumba alisema anatarajia mawaziri na maofisa wote walioshiriki kwenye vitendo vya ubadhirifu watafikishwa mahakamani ili kujenga nidhamu kwa watendaji wengine.


Alisema serikali ya CCM imekuwa na tabia ya kuwalinda waovu ndiyo maana walioshiriki kwenye ubadhirifu wa ununuaji wa rada licha ya ushahidi kupatikana hawajafanywa lolote.


“CCM wanalindana lakini wanasahau kuwa upepo wa sasa si ule wa nyuma, wakishindana nao wataumia. Waache sheria zichukue mkondo wake kwa wabadhirifu,” amesema Lipumba.


Mrema alia

Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, Augustine Mrema, alisema kelele za wabunge wanazozipiga juu ya ubadhirifu angalau zinaanza kufanya kazi.

“Kamati yangu imekuwa ikizikagua halmashauri mbalimbali, madudu tunayokutana nayo kweli yanatisha, naona sasa tusiishie kwa kujiuzulu kwa mawaziri, bali tuwafikishe mahakamani wabadhirifu wote,” amesema.


Wananchi wakerwa

Baadhi ya wananchi wamesema kuwa ubadhirifu hauwezi kukoma kama kila anayeufanya atakuwa akijiuzulu bila kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.

Abdul Juma, mkazi wa Kigogo jijini Dar es Salaam, alisema Tanzania ina fursa ya kupiga hatua za kimaendeleo iwapo viongozi watajenga utamaduni wa kuwajibika kwa masilahi ya umma na watakaotumia kwa ubadhirifu rasilimali za taifa wafikishwe mahakamani.


Jenister Peter amesema Rais Jakaya Kikwete ni vema akafanya uteuzi wa mawaziri pasipo kuangalia urafiki, bali azingatie uadilifu na uwezo wa kiutendaji wa mhusika.


JK kwenye mtihani

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii wamelidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa Rais Kikwete hivi sasa yupo katika wakati mgumu wa kufanya uteuzi wa mawaziri wapya na wengine kuwahamisha wizara.

Wanabainisha kuwa ugumu huo unatokana na mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi yaliyolikumba taifa, ambapo serikali na chama anachokiongoza vinaonekana kutojali matatizo ya wananchi.


Wachambuzi hao wanaona hii ndiyo karata muhimu kwa Rais Kikwete kurejesha imani yake na ya chama anachokiongoza mbele ya wananchi, kwa kuwachagua viongozi watakaowajibika ipasavyo.


Kutoaminiwa kwa chama na serikali ya CCM kwa kiasi kikubwa kunasababishwa na makundi yanayohasimiana ndani ya chama hicho, yakiwa na lengo la kuandaa safu za uongozi katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.


Hatua hiyo ilikifanya chama hicho kupoteza viti vingi vya ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2010 pamoja na kura za mgombea urais kushuka kutoka asilimia 81 hadi 60.


CCM na serikali vimekuwa vikiyumba tangu kushamiri kwa vita ya mapambano ya ufisadi ambayo yanawahusisha makada wake.



 
Kuna Sheria zinawakinga Mawaziri Mafisadi, Sababu Waandishi wetu wa habari hawawi wachunguzi na Wadadisi ni Waoga

Na Sheria za Nchi zinamlinda huyo waziri kuliko Mwananchi fukara, Jembe na Nyundo mmm waziri ni Nyundo
 
Back
Top Bottom