Wakili msomi Msando ame over react?

Wakili msomi Msando ame over react?

Elius W Ndabila

JF-Expert Member
Joined
Jul 17, 2019
Posts
340
Reaction score
678
FALSAFA YA SHERIA INATUFUNDISHA NAMNA FURAHA INAVYOTOFAUTIANA

Na Elius Ndabila

Mwalimu wangu wa Sheria katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, Dkt. John, maarufu kama John Kisomo, alinifundisha kozi ya Jurisprudence (Falsafa ya Sheria). Katika kozi hii nilipata fursa ya kujifunza mitazamo mbalimbali ya wanafalsafa kuhusu Sheria, haki, wajibu, maadili na namna jamii inavyopaswa kuongozwa.

Leo nataka nikupitishe katika nadharia tatu muhimu za kifalsafa ambazo naamini zinaweza kutusaidia kutafakari jambo lililotokea jana Kimara. Nadharia hizo ni Utilitarianism, Deontology na Justice as Fairness.

Ninadhani Msomi na Mwanasheria, Adv. Msando, atakuwa na jambo la kuongezea katika mjadala huu kutokana na kile kilichotokea jana Kimara.

1. UTILITARIANISM: FURAHA YA WENGI ZAIDI

Nadharia hii ilihusishwa na mwanafalsafa Jeremy Bentham. Katika falsafa yake, Bentham alitoa hoja maarufu kwamba:

"The greatest happiness of the greatest number is the foundation of morals and legislation."

Kwa tafsiri rahisi, furaha ya kiwango kikubwa kwa idadi kubwa zaidi ya watu ndiyo msingi wa maadili na utungaji wa sheria.

Bentham aliamini kwamba ubora wa tendo au uamuzi unaweza kupimwa kwa kuangalia matokeo yake. Kwa hiyo, katika kutunga Sheria, kufanya maamuzi au kuchukua hatua za kiutawala, tunapaswa kujiuliza: Je, uamuzi huu utaleta manufaa, ustawi na furaha kwa jamii kwa kiwango gani?

Kwa mfano, Serikali inapochukua uamuzi wa kujenga barabara, inaweza kuangalia idadi ya wananchi watakaonufaika, muda watakaookoa, biashara zitakazokua na shughuli za kiuchumi zitakazochochewa.

Huo ndiyo mtazamo wa Utilitarianism: kupima matokeo ya uamuzi kwa kuangalia manufaa yake kwa jamii kwa ujumla.

Lakini hapa ndipo tunapokutana na changamoto kubwa ya falsafa hii. Je, inawezekana uamuzi ukawanufaisha watu wengi huku ukimuumiza au kumnyima haki mtu mmoja?

Je, kwa sababu wengi wamefurahi, basi kila kilichofanyika ni sahihi?

2. DEONTOLOGY: WAJIBU NA KANUNI ZA MAADILI

Nadharia hii inahusishwa na mwanafalsafa Immanuel Kant. Kant alitoa mtazamo tofauti na ule wa Bentham.

Wakati Utilitarianism inapima ubora wa tendo kwa kuangalia matokeo yake, Deontology inapima usahihi wa tendo kwa kuzingatia wajibu, kanuni na misingi ya maadili.

Kwa mujibu wa Kant, tendo jema linapaswa kufanywa kwa sababu ni wajibu wa kimaadili, si kwa sababu tu litaleta matokeo mazuri.

Kwa mtazamo huu, kuna matendo ambayo hayawezi kuwa sahihi kimaadili hata kama yanaweza kuwanufaisha watu wengi.

Kwa mfano, fikiria mtu asiye na hatia anahukumiwa ili kuzuia machafuko katika jamii na kuwafurahisha wananchi wengi wanaotaka kuona mtu akiadhibiwa.

Kwa mtazamo wa Utilitarianism uliokithiri, mtu anaweza kujaribu kutetea uamuzi huo kwa hoja kwamba umeleta utulivu kwa wengi.

Lakini Deontology inapinga mantiki hiyo. Huwezi kumwadhibu mtu asiye na hatia kwa kisingizio cha kuleta furaha kwa wengi. Haki, wajibu na utu wa binadamu haviwezi kutupwa pembeni kwa sababu tu matokeo fulani yanawafurahisha watu wengi.

Hapa tunajifunza jambo muhimu sana: Si kila jambo linalokubalika na wengi ni sahihi, na si kila jambo linalowafurahisha wengi ni la haki.

3. JUSTICE AS FAIRNESS: HAKI KAMA USAWA NA UADILIFU

Nadharia hii iliasisiwa na mwanafalsafa John Rawls.

Rawls alisisitiza kwamba jamii yenye haki lazima ijengwe katika misingi ya usawa, uhuru wa msingi na taasisi zinazotenda haki kwa watu wote.

Hoja yake kubwa ni kwamba haki za msingi za mtu haziwezi kutolewa kafara kwa ajili ya kuongeza manufaa ya jumla ya jamii.

Katika kitabu chake A Theory of Justice, Rawls anasisitiza:

"Justice is the first virtue of social institutions."

Yaani, haki ndiyo sifa ya kwanza ya taasisi za kijamii.

Rawls alitumia dhana ya Veil of Ignorance (Pazia la Kutojua) kueleza namna tunavyopaswa kufikiria tunapotengeneza mfumo wa haki.

Anatuambia tufikirie tunatengeneza kanuni za kuongoza jamii bila kujua nafasi tutakayokuwa nayo katika jamii hiyo. Hatujui kama tutakuwa matajiri au maskini, viongozi au wananchi wa kawaida, wenye nguvu au wasio na uwezo wa kujitetea.

Je, katika mazingira hayo tungetengeneza mfumo unaoruhusu haki za baadhi ya watu kukanyagwa kwa sababu tu wengine ni wengi?

Bila shaka, tungehitaji mfumo unaolinda haki za kila mtu, hasa wale walio katika mazingira magumu.

Hii ndiyo hoja ya Rawls: mfumo wa haki haupaswi kupimwa kwa kuangalia furaha ya walio wengi pekee, bali pia namna unavyowatendea wale ambao hawana nguvu ya kushawishi maamuzi ya jamii.

TUILETE FALSAFA HII KATIKA TUKIO LA KIMARA

Sasa tuje katika jambo lililotokea jana Kimara.

Mkuu wa Wilaya ni mwakilishi wa Serikali katika Wilaya yake. TANROADS ni Wakala wa Serikali ulio chini ya Wizara ya Ujenzi, wenye majukumu ya usimamizi na maendeleo ya mtandao wa barabara kuu na za mikoa.

Hapa tunakutana na taasisi mbili za Serikali zenye majukumu tofauti, lakini zinazopaswa kushirikiana katika kutekeleza sera na mipango ya Serikali.

Swali langu ni hili: Je, katika tukio la jana Kimara, nani alipaswa kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa sheria na mamlaka aliyopewa?

Je, Mkuu wa Wilaya alitenda kwa kuzingatia mipaka ya mamlaka yake? Je, TANROADS ilitekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, taratibu na mamlaka yake?

Tusichanganye mamlaka ya kisiasa na mamlaka ya kisheria. Kuwa mwakilishi wa Serikali hakumaanishi kwamba kila kiongozi ana mamlaka ya kuingilia au kusimamisha majukumu ya kila taasisi ya Serikali bila kuzingatia sheria.

Vivyo hivyo, kuwa wakala wa Serikali hakumaanishi kwamba taasisi inaweza kufanya kazi bila kushirikiana na viongozi wengine wa Serikali na kuzingatia utaratibu wa kiutawala.

Serikali ni moja, lakini majukumu ya taasisi zake yamegawanywa kwa mujibu wa sheria. Ushirikiano wa taasisi hizo haupaswi kuondoa mipaka ya mamlaka iliyowekwa kisheria.

Kwa kutumia nadharia hizi tatu, tunaweza kutafakari tukio hili kwa namna ifuatayo:

Bentham – Utilitarianism: Je, hatua iliyochukuliwa Kimara imeleta manufaa gani kwa wananchi wengi zaidi? Je, imeongeza ustawi wa jamii au imezalisha usumbufu?

Kant – Deontology: Je, kila mhusika ametekeleza wajibu wake kwa kuzingatia sheria, kanuni na mipaka ya mamlaka yake? Je, hatua zilizochukuliwa zilikuwa sahihi kimaadili na kiutendaji hata bila kuangalia nani amefurahi?

Rawls – Justice as Fairness: Je, uamuzi uliofanyika umetenda haki kwa kila upande? Je, haki za wananchi na watu wengine walioathiriwa zimezingatiwi kwa usawa.

TUSIMAMIE SIASA AU SHERIA?

Ninachojaribu kusema ni kwamba siasa na Sheria zinaweza kukutana katika utawala wa nchi, lakini siasa hazipaswi kuwa mbadala wa Sheria.

Viongozi wanaweza kuwa na nia njema, wananchi wanaweza kuwa na matarajio makubwa na maamuzi yanaweza kuungwa mkono na wengi. Lakini hayo yote hayafuti wajibu wa kufuata Sheria.

Demokrasia si ruhusa ya walio wengi kufanya kila wanachotaka. Demokrasia inayojengwa juu ya utawala wa Sheria lazima iheshimu pia haki za wale ambao hawana idadi kubwa ya kuwaunga mkono.

Ndiyo maana tunapaswa kutofautisha kati ya kile ambacho wananchi wanataka, kile ambacho Serikali inaona kina manufaa na kile ambacho Sheria inaruhusu.

Nina maswali matatu ya kuhitimisha:

1. Je, Sheria inapaswa kutafuta furaha ya wengi au kulinda haki za kila mtu, hata pale ambapo kufanya hivyo hakuwapendezi wengi?
2. Je, kiongozi anapochukua uamuzi unaopendwa na wananchi lakini unaotia mashaka kuhusu mipaka ya mamlaka yake, tunapaswa kuupima kwa umaarufu wake au uhalali wake kisheria?
3. Je, katika tukio la Kimara tunajadili ushindi wa mamlaka ya kisiasa au tunajadili namna taasisi za Serikali zinavyopaswa kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria?

Kwangu mimi, mjadala huu haupaswi kuishia katika nani ameshinda hoja kisiasa. Unapaswa kutupeleka katika swali kubwa zaidi: Je, tumetengeneza utamaduni wa viongozi kuheshimu Sheria na taasisi za Serikali, au bado tunapima usahihi wa maamuzi kwa kuangalia nani aliyatoa?

TUSIMAMIE UTAWALA WA SHERIA (RULE OF LAW), SI UTAWALA WA HISIA AU MATAMANIO YA WENGI (RULE OF POPULARITY).
 
Back
Top Bottom