Wakala wa kuzimu aliyetumwa na mafia

SteveMollel

JF-Expert Member
Jul 12, 2015
8,451
23,780
WAKALA WA KUZIMU ALIYETUMWA NA MAFIA

Kuna mambo ambayo tumezoea kuyaona kwenye filamu, tukaishia kufurahia, kusimuliana na kukumbushana.

Mambo haya wakati tunasimuliana huwa tunaamini yapo tu kwenye ulimwengu wa tungo, wa kufikirika, na ki uhalisia hayawezi kutokea.

Ati kupambana na jini kama vile alivyofanya Arnold Schwarzenegger kwenye movie ya Predator (1987)? Meli kutwaliwa na roho ya kizimu kama tuonyeshwavyo kwenye movie ya Ghost ship (2002)? Ama yale mauaji ya Freddy Krueger ndani ya movie ya The Nightmare On Elm Street (1984)?

Huwa tunafurahia tu, na hata pale wengine wanapojaribu kuzichukulia movie hizo serious kwa kuhofia, huwa tunawakumbusha:

“Hiyo move tu!” tukihusanisha na dhana ya uongo, hivyo hamna haja wala sababu ya kuhofu.

Ama pengine basi tukitafuta ahueni ya kutoogopa kwa kusemea vifuani punde tunapohisi tumemezwa na woga baada ya kutazama movie ya kutisha.

“Ile ni movie tu, uongo ule na midoli!” angalau tupate usingizi.

Lakini hapa hapa duniani, kuna watu ambao wamewahi kushuhudia hizo ‘movie’ zikitendeka mbele ya macho yao.

Hawakuhadithiwa, bali waliona kwa macho na wakasikia kwa masikio yao wenyewe. Yale mambo ambayo ulizoea kuyaona kwenye movie tu, wao wakakumbana nayo, kwao ikawa ni uhalisia!

Ile hofu unayoipata wewe ukiwa nyuma ya kioo cha televisheni, wao wakaipata maradufu wakiwa ndani ya eneo la tukio. Hakukuwa na director, taa wala kamera. Ni wao tu mbele ya adui! – adui ambaye unadhani anaishi kwenye mkanda wa filamu pekee.
374dde0cc175132f694b9d96e1660b4d.jpg

MAREKANI: NEW ORLEANS, LOUISIANA.
...MWEZI WA TANO, 1918 MPAKA MWEZI WA KUMI, 1919.

Mbali na Kimbunga Louisiana kilichotokea mnamo mwaka 1901 na kusababisha mafuriko makubwa ndani ya jiji la New Orleans, baada tu ya miaka nane kimbunga kingine kilikita jiji na kuacha msiba , majonzi na uharibifu mkubwa, kikienda kwa jina la Grand Isle, upepo wake ukikimbia kwa kilomita 195 kwa lisaa!

Kama vile haitoshi, miaka sita tena mbele, kimbunga kingine kinafyagia jiji hili pasi na huruma, hiki kikimbia kilomita 230 kwa lisaa! Kikibatiza nyumba kuwa maghofu na kuingizia hasara nchi ya Marekani kiasi cha dola milioni kumi na tatu kwa kipindi hicho.

Hizi ndizo zilikuwa habari mbaya kabisa kuwahi kulikumba jiji hili katika karne ya ishirini (1900’s – 1940’s), zikiwapa watu presha na hekaheka haswa, wakipiga simu na kutuma ujumbe huku na huko kuulizia wapendwa wao kama wapo hai.

Lakini inapopita tena miaka mitatu, watu wa jiji hili wanapewa sababu nyingine ya kuhofia. Na mara hii haikuwa tena asili (nature) ndiyo iliyowasulubu, bali binadamu. Binadamu ambaye alikuwa kivuli kwa wanausalama, akigamba anaweza fanya uhalifu popote pale, na kwa muda anaotaka!

Ni nani huyu?

Ndani ya mwezi wa tano mwaka 1918, mwanaume wa kutisha zaidi jiji la New Orleans kupata kumshuhudia anawasili. Ujio wake unaanzisha hofu pana ndani ya jiji iliyodumu kwa muda wa mwaka na nusu.

Ujio wake unawafanya wakazi wa New Orleans kutega masikio na kusikiliza kila aina ya sauti nyakati za usiku, kuwa makini na kila kivuli, na kufungua magazeti asubuhi kwa mikono inayotetemeka.

Mwanaume huyu alikuwa ni muuaji aliyekuwa anatumia shoka kumaliza wahanga, tena akiua pasipo hata tembe ya huruma. Alifanya kila mtu ndani ya New Orleans kujihisi hayupo salama. Mpaka leo hii, hakuwahi kuja kujulikana alikuwa ni nani, imebakia kitendawili.

Wengi wanaamini hakuwa binadamu kabisa, bali roho iliyokuwa na uwezo wa kutokea na kupotea. Wengineo pia wakiamini alikuwa muuaji wa mpangilio aliyekuwa anakata watu vichwa kipindi wakiwa usingizini.

Hakuna aliyekuwa na jibu moja.

MAUAJI YA KWANZA: NA UJUMBE UNAACHWA KWA AJILI YA KUWAKUMBUSHA POLISI.

Tarehe 23, mwezi wa tano, 1918, muuza duka na vitu vidogovidogo vya nyumbani mwenye asili ya Italia, Joseph Maggio, na mkewe walikatwa katwa na shoka wakiwa wamejilaza kwenye apartment iliyo juu ya duka lao, Maggio grocery store.
mail334.jpg

Kwa mujibu wa uchunguzi, polisi wakagundua kibanzi cha mlango wa nyuma wa nyumba kilikuwa kimeng’olewa na hivyo kumpa mwanya muuaji kuzama ndani na kutimiza haja yake.

Silaha iliyotumika kwa ajili ya mauaji, shoka, ilipatikana ndani ya jengo, bado ikiwa na damu ya Maggio. Ndani hakuna chochote kilichoibwa, ikiwemo vito vya thamani na pesa ilhali vilikuwa wazi mahali pa kuonekana.

Wapelelezi wakazama kazini, na watuhumiwa kadhaa wakakamatwa kwa ajili ya mahojiano, lakini wote wakaachiwa kutokana na uhaba wa ushahidi. Kielelezo (clue) pekee kalichopatikana kilikuwa ni ujumbe uliokuwa umeandikwa na chaki karibu na nyumba ya wahanga, ukisomeka:

“Mrs Joseph Maggio atazingatiwa usiku, kama Mrs Toney.”

UJUMBE HUU KUMAANISHA NINI?

Wapelelzi walianza kufukunyua na kuchimba taarifa kwenye mafaili yao kuona kama kuna tukio lolote huko nyuma linalohusiana na kiifo cha Maggio, na kwa mshangao wakagundua mauaji matatu na mashambulizi kadhaa dhidi ya wauzaji wenye asili ya Italia yalishawahi kufanyika huko mwaka 1911.

Mauaji yalifanana na ya Maggio ambapo muuaji alitumia shoka, lakini pia akitumia kibanzi cha mlango wa nyuma ya nyumba kuingilia ndani.

Tazama kibanzi (panel) cha mlango.
doors-and-windows-5-638.jpg


Mauaji haya ya mwaka 1911 yalidhaniwa na kuhusishwa na kundi la Mafia, ambalo lilikuwa limelenga polisi na watu wenye asili ya Italia.

Kwahiyo basi ujumbe huu uliwasahihisha polisi ya kwamba mauaji ya Maggio hayakuwa ya kwanza, bali ya pili! Warekebishe hilo kwenye data zao ili sasa waende pamoja kwenye mazoezi yafuatayo.

MASHAMBULIZI YAKAENDELEA… (MKE ANAMTUHUMU MUME KUWA MUUAJI)

Karibia ikitimia mwezi baada ya kifo cha Maggio na mkewe, Louis Bossumer, muuzaji duka mwenye asili ya Italia anayeishi nyuma ya duka lake na mkewe, Annie Harriet, wakagundulikana na kukutwa na majirani zao wakiwa kwenye dimbwi la damu. Bossumer alikuwa amejeruhiwa vibaya mno lakini hakuwa amekufa. Pembeni yake pia, Annie, alikuwa amejeruhiwa sana, ila akiwa hai.

Wote walikuwa wamejeruhiwa na shoka ambalo liliachwa pembeni ya Bossumer likiwa limetota damu. Kibanzi cha mlango wa jikoni kilikuwa kimetolewa, na hakukuwa na chochote kilichoibwa.

Baada ya kushambuliwa, upande mmoja wa uso wa bibie Annie ulipooza, akafanyiwa upasuaji kuurekebisha. Siku mbili kabla hajafa, akawaambia polisi kwamba anamtuhumu Louis Bossumer ndiye aliyemshambulia.

Hivyo Bossumer akashtakiwa kwa mauaji na akahudumu miezi tisa jela kabla ya kuja kutolewa mwaka 1919, mwezi wa tano baada ya kesi kusikilizwa kwa dakika kumi tu na mwanaume huyo kuthibitika hana makosa, akaachiwa.

Baadae ndani ya mwaka huohuo, mwezi wa nane.

Tarehe 5, mashambulizi yakaendelea kwa Mrs. Edward Schneider ambaye alikuwa mjamzito wa mimba ya miezi nane. Mwanamke huyu alikuwa kwenye kitanda akilala alipoamka na kumuona mtu mweusi amesimama na kumtazama kando kidogo ya kitanda akiwa amebebelea shoka.
6c8ebb27c93125515a32655fe3a2fa8b.jpg

Akakatwa katwa mara kadhaa!

Muda mfupi baada ya usiku wa manane mume wake alirejea nyumbani na kumkuta mkewe akiwa ametapakaa na kutota damu. Ngozi ya kichwa chake ilikuwa wazi.

Lakini kwa kheri, mwanamke huyu akadumu mpaka kujifungua mwanaye siku mbili mbele baada ya shambulizi.

Mwanaume mmoja akakamatwa kwa kuhisiwa kuhusika na tukio, ila baadae akaja kuachiwa baada ya kuonekana hamna vielelezo wala ushahidi wa kumshikilia.

MUUAJI ANAONEKANA!

Zikapita siku tano tu, tukio lingine likajiri kwa muuza duka mwingine, mwanaume aitwaye Joseph Ramano ambaye alishambuliwa tarehe 10 mwezi wa nane.

Ramano alikuwa akiishi na wapwa zake wawili ambao walishtuka usiku baada ya kusikia sauti ya kelele kwenye chumba muungano ambamo mjomba wao, bwana Ramano, alikuwa anaishi.

Wapwa hawa wakakimbilia chumbani mwa mjomba mwao wakamkuta Ramano akiwa na jeraha kubwa kichwani, na muuaji akifanya jitihada za kutoroka.

Muuzaji huyu, japo aliumizwa mno, aliweza kutembea mwenyewe mpaka kwenye gari la wagonjwa punde lilipofika, lakini akafa siku mbili mbele baada ya maumivu makali mno ya kichwa.

Wapwa wale wa Ramano wakatoa maelezo kwa polisi juu ya muuaji: alikuwa ni mwenye ngozi nyeusi (dark-skinned), mwili mpana akivalia suti nyeusi na kofia iliyoegamia upande.
the-terrible-axeman-of-new-orleans-art-1.jpg

Taarifa zingine zilikuwa ni zilezile kama za awali, maeneo kuvunjwa pasipo kuibiwa chochote, vibanzi vya mlango kunyofolewa, na wengi wa wahanga wakiwa ni watu wenye asili ya Italia.

Mauaji haya yakatengeneza hofu kubwa ndani ya jiji. Polisi walikuwa wanapokea taarifa toka huku na kule zikinadi kumuona muuaji akinyemelea nyumba jirani, mashoka yakikutwa uani, na milango na madirisha yakivunjwa.

Watu walianza kubeba bunduki ambazo zilikuwa tayari zimekokiwa na wanafamilia wakipeana zamu ya kulinda nyumba nyakati za usiku.

Ripoti moja ilisema muuaji alionekana maeneo fulani akijifanya mwanamke, na ingine akionekana anaruka fensi kuzama ndani ya nyumba.

MUUAJI ANAPOTEA, ANARUDI NA KISA CHA MWANAMKE MWINGINE KUMTUHUMU MTU KUWA MUUAJI.

Akiwa kama mtu aliyefahamu kuwa jiji sasa limejazwa na hofu na tahadhari mno, muuaji akapotea. Hakutokea ripoti za mauaji ndani ya jiji kwa miezi.

Hofu za watu zilipoa na kurudi kuwa kawaida, shughuli zikaendelea kama kawaida watu wakidhani sasa ni salama. Walitoka na kuacha bunduki zao makabatini, wakapanua midomo kutabasamu na kucheka.

Lakini hali hii haikudumu, muuaji akarejea tena mwezi wa tatu tarehe 10, 1919! Sasa mhanga ikiwa ni familia ya muuzaji duka mwingine mwenye asili ya Italia, bwana Charles Cortimiglia aliyekuwa anaishi na mkewe, Rosie, na binti wa miaka miwili, Mary, katika mji wa Gretna, ukivuka tu mto Mississippi.

Wakati makelele yakisikika kutoka kwenye makazi ya Cortimiglia asubuhi ya mapema, jirani, bwana Iorlando Jordano, alikimbilia eneo hilo kutazama. Huku akakuta watu watatu wameshambuliwa.

Rosie, mke wa Cortimiglia, alishtuka usingizi baada ya kusikia mumewe akipambana na mtu mkubwa aliyeshikilia shoka. Mume wake alipodondoka chini kwa kuzidiwa, muuaji akamtazama yeye, Rosie akamdaka mwanaye, Mary, na kuomba wabakiziwe uhai.
ed343a89d33502d207d7505d52c36d84.jpg

Pasipo kujali, muuaji akashusha shoka kwa mama na mtoto wake. Pale majirani walipowasili, wakamkuta Cortimiglia akiwa amelala kwenye dimbwi la damu sakafuni, Rosie akisimama mlangoni na jeraha kubwa kichwani, akimbebelea mwanaye aliyekuwa amekufa.

Waliwahishwa hospitali na wote, mume na mke, wakatibiwa nyufa za fuvu lao la kichwa. Mwanaume akaruhusiwa baada ya siku mbili wakati mke akibakia chini ya uangalizi wa madaktari.

Akiwa anapata fahamu zake kamili, Rosie akasema shambulizi lilifanywa na jirani yao, Iorlando Jordano, na mtoto wake wa kiume mwenye miaka 18, Frank. Japokuwa Iorlando, mwanaume wa miaka 69, alikuwa ni mwenye afya mgogoro ya kuweza kutenda hilo jambo, na mtoto wake, Frank, alikuwa mnene mno kupita kwenye tobo la mlango, walikamatwa kwa ajili ya mahojiano.

Ingawa Cortimiglia alikana kuhusika kwa majirani hao, ajabu walishikiliwa na walikuwa wanaelekea kuhukumiwa kwa Frank kupewa adhabu ya kunyongwa na mzee Iorlando kumalizia maisha yake jela.

Cortimiglia akampa talaka mkewe kutokana na tuhuma hizo. Baada ya mwaka Rosie akabatilisha maneno yake kwa kusema aliwatuhumu kimakosa majirani zake kwasababu ya wivu!

Kutokana na tuhuma zake ndizo zilikuwa kijiushahidi pekee, watuhuhumiwa wakaachiliwa muda mfupi mbeleni.

Kutokana na hichi kilichotokea kwa familia ya Cortimglia, jiji la New Orleans likajazwa tena hofu na watu wakaanza kukobeka tena silaha mikononi. Polisi walisema wanaamini kabisa uhalifu wote huu ulifanywa na mtu mmoja,

“Mwehu mwenye kiu ya damu, akijazwa na hamu ya kuchinja binadamu!
889b1589e13cb348123c71bb9b70a1a3.jpg

MUUAJI ANATUMA BARUA: ANATOA MASHARTI KWA WATU KUWA HAI.

Mambo yakaendelea kutokuwa mambo, mtu aliyetuhumiwa kuwa ndiye muuaji alipotuma barua kwenye shirika la magazeti la Times-Picayune tarehe 14, mwezi wa tano, 1919 akiahidi kushambulia tena!

Barua hii ilizua hofu, lakini pia ikasababisha watu kuwa wehu kwa kutimiza kile kilichomo ndani.

Barua ilisomeka kama ifuatavyo.

Jehanamu, March 13, 1919

Wapendwa viumbe:

Hawajawahi kunikamata na kamwe hatafanikiwa. Hawajawi kuniona, kwakuwa sionekani … mimi sio binadamu, bali roho na jinni kutoka jehanam. Mimi ndiye yule ambaye watu na polisi wenu wajinga wanamuita mtu wa shoka (Axeman).

Ninapotaka, nitakuja na kuwadai wahanga. Mimi mwenyewe ndiye najua watakuwa ni wakina nani. Sitaacha ushahidi wowote isipokuwa shoka langu lenye damu na ubongo wa ambaye nimempeleka jehanam kunipa kampani.

Kama mnapenda mnaweza mkawaambia polisi wawe makini wasiniudhi … ila sidhani kama nina haja ya kuwaonya, naamini kabisa polisi watanikwepa kama walivyonikwepa huko nyuma. Wana hekima na wanajua namna gani ya kukaa mbali na madhara.

Pasipo mashaka, nyie watu Orleans mnadhani mimi ni muuaji katili, ambalo kiuhalisia ni kweli, lakini naweza kuwa zaidi ya hapo nikiamua. Kama nikipenda naweza kuwatembelea kila usiku, nikachinja raia bora kwasababu nina mahusiano ya karibu na malaika wa kifo.

Sasa basi kuwa wazi, saa sita na robo usiku (muda wa dunia) Jumanne ijayo (March 19, 1919), nitakatiza jiji la New Orleans. Kwa huruma yangu ndogo, nitawahitaji mfanye jambo fulani dogo. Hili hapa:

Mimi ni mpenzi sana wa muziki wa Jazz, na ninaapa kwa mashetani wote wa maeneo haya, yeyote yule atapona endapo akiwa anapiga muziki wa jazz kwa muda ambao nimeutaja.

Kama kila mtu ana bendi ya Jazz, ni sawa, basi ni bora kwake. Lakini jambo moja ambalo la uhakika ni kwamba baadhi yenu ambao mtakuwa hamu – jazz siku ya Jumanne usiku, atapata shoka.

… Nimekuwa na nitakuwa roho mbaya kabisa kuwahi kutokea …

Mtu wa shoka (The Axeman).

--- Mwisho wa barua - - -

Kwahiyo basi kwa mujibu wa muuaji, mtu yeyote ambaye atakuwa hasikilizi Jazz, March 19, atakumbana na shoka!

Barua hii ikachapishwa kwenye gazeti na kusambaa. Na kweli, siku ya tarehe 19 March, muziki wa Jazz ukateka jiji la New Orleans. Kuanzia majumbani, katikati ya jiji, kumbi za starehe, kote huko muziki ukawa ni mmoja tu: Jazz!
293161ef1aab94513b618f00d57245e0.jpg

Na hakuna aliyekufa!

Kwa majuma kadhaa kukawa kimya na salama, lakini bado watu waliishi kwa hofu.

MAUAJI YAKAENDELEA NA HATIMAYE YANAKOMA.

Tarehe 10, August 1919, muuza duka mwingine aitwaye Steve Boca akavamiwa na muuaji wa shoka. Alijeruhiwa lakini akafanikiwa kuishi. Kama kawaida hakuna kilichoibiwa, na kibanzi cha mlango wa nyuma kilikuwa kimenyofolewa.

Mchezo ukaendelea pia kwa muuza madawa ya binadamu William Carson ambaye yeye alifanikiwa kuepuka kifo kwa kumrushia risasi muuaji huyu aliyepotea.

Mtu mwingine aliyefatia ni mwanamke aitwaye Sarah Laumann na wa mwisho kukumbana na sekeseke la mtu huyu wa shoka alikuwa ni Mike Pepitone, yeye hakuishia kujeruhiwa bali alikufa kabisa na kuacha mjane na watoto sita.

Baada ya hapo muuaji huyu akapotea ndani ya jiji. Haikueleweka jambo gani limemtokea na kumfanya apotee na kukoma kuua.

Lakini, mtuhumiwa mmoja, Joseph Momfre, mwanaume mwenye asili ya Italia, alipigwa risasi na kuuawa mwaka uliofuata. Muuaji wake alikuwa ni mjane wa Mike Pipetone, mwanaume wa mwisho kuuawa na muuaji wa shoka.

Mjane huyo alimtuhumu Momfre kuwa ndiye mwanaume aliyekuwa nyuma ya mauaji. Lakini muunganiko kati ya Momfre na muuaji wa shoka haukuwahi kuthibitishwa, japokuwa mauaji yalikoma tangu Momfre alipoenda mbali na mji.

LAKINI KUNA MASWALI KADHAA:

Kwanini muuaji wa shoka alikuwa anavutiwa kuua watu wenye asili ya Italia? Tena wauza maduka? Na ni kisasi ama chuki gani zilikuwa zinampelekesha kiasi cha kufanya unyama huu?

Maswali haya yalikuwa na taarifa finyu mno mpaka miezi michache iliyopita ambapo Makala ndefu iliyochapishwa kwenye jarida binafsi likielezea historia ya jamii ya Mafia.

Makala hiyo kwa kina ilielezea kuamka na kukua kwa kundi la Mafia huko Los Angeles, ikajikuta ikitoa taarifa fulani nyeti kumhusu muuaji wa shoka.

Makala hiyo ilienda kwa jina la “Richard Warner ‘Mkuu wa kwanza wa kimafia Los Angeles?’ Mikasa ya Vito Di Giorgio.”

Ndani ya Makala hiyo kulikuwa kuna mapendekezo kadhaa kwamba mtu wa shoka alikuwa ana maunganiko wa moja kwa moja na kundi la Mafia (lenye mahusiano na jamii ya Sicily huko Italia).

New Orleans ulikuwa ndiyo jiji la kwanza Marekani kuwa na familia ya Mafia inayojitegemea, na mapema katika karne ya ishirini, familia ya Mafia wa New York na New Orleans walikuwa wanatumia maduka kama mahali pa kufichia na kuasisi harakati zao za kihalifu, haswa unyang’anyi.

Hivyo basi kwa mujibu wa Makala hiyo iliyokuwa imefanyiwa utafiti wa kina na mwandishi wake bwana Warner, mashambulizi ya wauza duka wa ki Italiayaliyokuwa yanafanywa na mtu wa shoka yalikuwa ni matunda ya vita ndogo ndogo zilizokuwa zinapiganwa na Mafiosi wa jiji.

Kwahiyo kumbe Mtu wa shoka (The Axe-man), alikuwa ni ‘wakala wa kuzimu’ aliyetumwa na kundi la Mafia kutisha, kuteketeza, na kumaliza visiki!

Mpaka leo hii vyombo vya usalama, wenzetu hao tunaowaita wataalamu wa mambo ya udadisi na upelelezi, hawajahi kusuluhisha wala kutoa majibu rasmi kumhusu muuaji huyu.

Hawamjui haswa ni nani.
9f301b697d3742d1309e48bfa3576d08.jpg

Na hilo basi linazidi kumfanya mtu huyu kuwa maarufu na kuhusishwa na roho za giza. Akipachikwa majina kadha wa kadha ya kuogofya.

MWISHO.

Na SteveMollel.
 
Japokuwa hujaniita mkuu mie nimeshafika na viatu nimevua!


Naomba uwe unanitag mkuu. Sitaki kukosa hizi nondo zako kila unapozituma mzee.
Nisamehe mkuu kwa kusahau kukutag, sijakutendea haki kabisa. Anyway, ntajitahidi sana nikitupia mzigo mwingine uwe wa kwanza kabisa! :cool: :cool: :cool:



Nashukuru sana kwa kuwa follower wangu mkuu! Regards.




☆Steve
 
Nzuri sema huu muda niliosoma sio mzuri. Sitalala leo au la nitamuota huyo axeman
 
Back
Top Bottom