Mohamed Said
JF-Expert Member
- Nov 2, 2008
- 21,801
- 31,811
|
Maandamano ya Waislam Dhidi ya NECTA Chini ya Dr. Joyce Ndalichako |
Kwa muda mrefu sasa, kumekuwa na maswali mengi wakijiuliza Waislamu, moja likiwa inakuwaje katika maeneo yenye Waislamu wengi ambapo idadi ya wanafunzi Waislamu inakuwa zaidi ya asilimia 70, lakini wanapochaguliwa kwenda sekondari, idadi ya watoto wa Kiislamu huporomoka na kuwa chini ya asilimia 20.
Swali na kitendawili hiki kimekuwepo kwa muda mrefu bila kupatiwa majibu. Hata lilipofikishwa Bungeni mwaka 1999 na aliyekuwa Mbunge wa Kigamboni, Mzee Kitwana Selemani Kondo, bado halikupatiwa jibu.
Akihoji juu hali hiyo, Mzee Kitwana Kondo alitoa mfano jinsi hali ilivyokuwa katika shule ya Pembamnazi iliyokuwa na Waislamu watupu na kwa miaka mingi mfululizo kulikuwa hakuna hata mtoto mmoja aliyekuwa akichaguliwa kwenda sekondari kutoka katika shule hiyo. Aidha alisema kuwa, katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, takwimu zinaonyesha kuwa idadi ya watoto wa Kiislamu katika shule za msingi ilikuwa zaidi ya asilimia 70 lakini inapokuja kuchaguliwa kwenda sekondari, idadi ya Waislamu iliporomoka na kuwa chini ya asilimia 20.
Akizungumza Bungeni tarehe 2 Februari, 1999 alisema kuwa katika watoto waliofanya mtihani wa darasa la saba mwaka 1998, idadi ya Waislamu ilikuwa asilimia 71 na Wakristo 29%. Hata hivyo akasema, ilipotoka orodha ya waliochaguliwa kwenda sekondari, idadi ya Wakristo ikawa asilimia 79 (79%) na Waislamu 21%.
Je, hiyo ilikuwa na maana kuwa watoto wa Kiislamu kwa asili yao hawana akili? Alitaka kujua Mzee Kitwana Kondo. Lakini hakuweza kupata jibu.
Mheshimiwa Waziri,
Ni wazi kuwa Waziri wa Elimu au Waziri Mkuu ambaye ndiye msimamizi wa mambo ya serikali Bungeni asingeweza kutoa majibu ya uhakika kwa sababu swali lilihitaji kufanyika uchunguzi huru wa kina na makini kwanza.
Mheshimiwa Waziri,
Mwaka 1987 aliyekuwa Waziri wa Elimu, Profesa Kighoma Ali Malima, aliweka utaratibu mpya wa ufanyaji wa mtihani wa darasa la saba ambapo namba zilitumika toka kufanya mtihani, kusahihisha na kuchagua wanafunzi wa kwenda kidato cha kwanza. Namba zilivishwa majina baada ya taratibu zote hizo kukamilika. Mwaka huo idadi ya watoto wa Kiislamu waliokwenda kidato cha kwanza iliongezeka kwa asilimia 40 ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Hata hivyo, mara aliondolewa Waziri Malima katika wizara hiyo na utaratibu wa zamani ukarejeshwa ambapo yalikuwa yakichaguliwa majina na idadi ya Waislamu ikaporomoka na kurudi chini ya asilimia 20.
Mheshimiwa Waziri,
Hali kama hii hapana shaka inazua maswali mengi ambayo yanahitaji majibu na majibu hayo hayawezi kupatikana bila ya kufanyika uchunguzi.
Labda tuongeze mifano ili kuliweka wazi zaidi jambo hili. Mwaka 1983 mwanafunzi aliyekuwa akiitwa Kopa Abdallah akisoma katika shule ya msingi Kichangani, Kilosa, alikosa kuchaguliwa kwenda sekondari. Yeye binafsi, wazazi wake na hata walimu wake hawakuamini matokeo yale kutokana na alivyokuwa akifanya vizuri kuliko wanafunzi wote. Baadae ilikuja kugundulika kuwa nafasi yake alipewa mwanafunzi aliyekuwa akiitwa Antoni Samirani ambaye alikuwa na uwezo mdogo sana ikilinganiswa na Abdallah. Kilichofanyika ni kuwa jina la Abdallah lilifichwa na baadae Antoni akapewa jina hilo kimya kimya na kwenda kusoma sekondari akitumia jina Abdallah wakati yeye ni Antoni.
Taarifa zinasema kuwa Kopa Abdallah alipogundua hakuweza kufanya kitu akaishia kuwa dereva.
Hali kama hiyo ilimkuta pia Adam Ramadhani aliyekuwa akisoma shule ya msingi Rutihinda jijini Dar es Salaam na kumaliza darasa la saba mwaka 1999. Yalipotoka matokeo ya mtihani wa darasa la saba na kuonekana kuwa Adam hakuchaguliwa, baba yake hakuamini kuwa mtoto wake anaweza kufeli kutokana na uwezo aliokuwa nao na zaidi akitizama walivyochaguliwa watoto ambao Adam alikuwa mwalimu wao shuleni na mitaani.
Katika kufuatilia suala hilo wizarani, ilikuwa aibu kwa wizara baada ya kuonekana kuwa walichaguliwa watoto wa Kikristo wenye alama za chini kabisa huku akiachwa Adam Ramadhani aliyekuwa na alama za juu kuliko wote.
Mheshimiwa Waziri,
Mifano kama hii ni mingi mno na ipo katika ngazi zote kwa maana kutoka elimu ya msingi kwenda sekondari, kutoka kidato cha nne kwenda kidato cha tano na kutoka kidato cha sita kwenda Chuo Kikuu. Kwamba hata kutoka kidato cha nne kwenda kidato cha tano, wapo watu waliopata kushuhudia majina ya wanafunzi wa Kiislamu yakiwekwa pembeni japo walikuwa na sifa za kuchaguliwa.
Mheshimiwa Waziri,
Ukiacha hujuma katika kuwaacha wanafunzi Waislamu wenye sifa kuendelea na masomo, matatizo huanzia kwenye kuamua nani amefaulu na nani kafeli. Tuhuma zilizopo ni kuwa wapo wanafunzi wanapewa madaraja ya juu wakati alama zao ni za chini na wapo wanaopewa madaraja ya chini wakati alama zao ni za juu. Na hii ni kwa masomo yote.
Mheshimiwa Waziri,
Kumekuwa na utamaduni katika nchi hii wa kukataa ukweli. Kufuatia uchunguzi uliofanywa na Kamati za Bunge, tumeshuhudia wizi na ufisadi wa kutisha ukifichuliwa Bungeni hivi karibuni hali iliyopelekea mpaka Mheshimiwa Rais kubadili Baraza lake la Mawaziri.
Sasa baada ya kuyasema yote hayo, tunasema kuwa Baraza la Mitihani la Tanzania, limekuwa likilalamikiwa kwa zaidi ya miaka 30, lakini malalamiko hayo yamekuwa yakipokewa kwa sikio la uziwi. Imefikia mahali tunasema kuwa hatuna tena imani na Baraza hilo.
Mheshimiwa Waziri,
Ili kupata ukweli wa malalamiko na shutuma hizi, na ili kujibu lile swali juu ya watoto wa Kiislamu ambalo halikupata jibu Bungeni, tunaitaka serikali kufanya yafuatayo:
- Tume huru iundwe kuchunguza Baraza la Mitihani la Tanzania na utendaji wake kazi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.
- Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani (NECTA) ajiuzulu mara moja ili kulinda heshima ya serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzaani na Baraza la Mitihani. Watendaji wakuu wa kitengo cha mitihani na wanaohusika na mfumo wa Kumputa ya Baraza la Mitihani nao wawajibishwe mara moja.
- Hatua za kisheria na kibinadamu zichukuliwe dhidi ya watumishi wa Baraza la Mitihani watakaothibitika kuhusika na kashfa hii.
- Muundo wa Baraza la Mitihani uzingatie uwiano wa kidini, kitendo cha chombo nyeti kama hiki kujazana watu wa dini moja kunaliondolea Baraza la Mitihani sura ya kitaifa, kwani takwimu zinaonyesha Makatibu Wakuu Watendaji na Manaibu Katibu Wakuu wamekuwa Wakristo na Wenyeviti wa Baraza hilo ni Wakristo tangu lilipoanzishwa mwaka 1973, mpaka hii leo na takwimu tunazo.
Mheshimiwa Waziri,
Tunaomba ieleweke kuwa tunachotaka ni kupatikana haki na kufanyika uadilifu kwa watu wote. Hatudai wala hatutaki upendeleo kwa Waislamu na wala hatutaki kuona mtu yeyote anaonewa au kuporwa haki yake, awe Mwislamu au mtu wa dini nyingine.
Tunachoamini ni kuwa kama Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi haina cha kuficha, basi itaunda Tume hiyo kwa haraka na kuhakikisha kuwa ni Tume ya kuaminika itakayofanya kazi yake kwa umakini, kwa kina na kwa uadilifu wa hali ya juu kabisa.
Lakini kama Wizara yako itaona kuwa haiwezi kuunda Tume ya uchunguzi, tunacho kuhakikishia ni kuwa sisi tutafanya kila liwezekanalo na kwa namna yoyote kuhakikisha kuwa Tume hiyo inaundwa. Na ikigundulika kuwa kuna hujuma zinafanyika katika utendaji wa Baraza, basi itabidi uwajibikaji uanze kwenye Wizara kabla ya kuwawajibisha watendaji wa Baraza la Mitihani.
Ni imani yetu kuwa utayapokea madai ya Waislamu na kuyafanyia kazi kwa umakini na kwa haraka ili kujenga mustakbali mwema wa nchi hii na watu wake.
Tunaomba kuwasilisha,
Mwenyekiti,
Baraza Kuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu
Juni 8, 2012