Wagonjwa 600 wa Saratani ya kinywa kwa mwaka

John Haramba

JF-Expert Member
Feb 4, 2022
365
1,373
Mratibu wa Afya ya Kinywa na Meno Taifa kutoka Wizara ya Afya, Dk. Baraka Nzobo amesema kwa mwaka 2021, takriban wagonjwa 600 waligundulika kuwa na saratani za kinywa na meno.

Dk. Nzobo alibainisha hali hiyo Septemba 7, 2022, Mkoani Dar es Salaam katika mahojiano na Nipashe wakati wa Kongamano la Vijana la siku tatu lililoanza juzi, likilenga masuala ya uongozi katika afya ya kinywa na meno na kuwakutanisha washiriki 26 kutoka nchi za Malawi, Rwanda, Tanzania na Zambia.

Kongamano hilo limeandaliwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, MC-Tanzania lenye maono kwa jamii ya Tanzania kuishi bila magonjwa ya kinywa na meno na MCW Global la Marekani linalotaka kufikia viwango vya juu vya elimu, afya bora na usalama wa kiuchumi ulimwenguni.

Dk. Nzobo alitaja vyanzo vikubwa vinavyosababisha saratani ya kinywa na meno ni matumizi ya bidhaa za tumbaku ikiwamo uvutaji wa sigara na unywaji wa pombe uliopitiliza.

“Matibabu ya saratani ni kama kawaida, atafika hospitalini atachukuliwa kipimo, hii itajulikana ni saratani ya aina fulani. Matibabu kuna mionzi, kuna kufanyiwa upasuaji au atapewa dawa za dripu au kumeza, atapona lakini endapo mtu atachelewa athari yake ni rahisi kusambaa kwenye mapafu,” alisema.

Kuhusu kongamano hilo, alisema wamekutana washiriki kutoka nchi mbalimbali kuangalia shida zinazokabili sekta ya kinywa na meno ili kuzitatua.

“Wataalamu wa kinywa na meno ni wachache, tunahitaji madaktari bingwa angalau 171 lakini mpaka sasa waliopo ni 70 na kati yao, madaktari bingwa 68 wapo hospitali za Dar es Salaam na mmoja Mkoa wa Morogoro na mwingine Dodoma," alifafanua.

Alisema ili kupata madaktari bingwa, uzalishaji wake kwa ngazi ya shahada unatakiwa uwe mkubwa na kwa bahati mbaya awali kulikuwa na chuo kimoja kinachowazalisha na mwaka huu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Kitivo cha Mbeya kimeanza kuchukua wanafunzi ngazi hiyo.

“Tunaomba wazazi na walezi wawatie moyo vijana wao kwamba nchi inahitaji madaktari wa kinywa na meno wengi na eneo hili bado halijatumika vizuri, ni eneo ambalo mwanafunzi akiomba, anapata mkopo,” alisisitiza.

Pia alisema kada ya matabibu meno ambao wanaohitajika ni 2,500 na kupitia kibali kilichotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan mwaka huu, zaidi ya matabibu meno 150 wameajiriwa kwenye vituo vya serikali na kufanya jumla yao kwa sasa kufikia 404.

Alisema baada ya ajira hizo kutolewa, hakuna wengine ambao wamebaki na sasa vituo binafsi vina uhitaji wa watalaamu hao.

Pia alisema kati ya vituo 9,726 vinavyotoa huduma ya afya, 597 ndivyo vinavyotoa huduma ya tiba ya kinywa na meno, sawa na asilimia 6.7.

Dk. Nzobo alitaja kikwazo kingine ni uhaba wa dawa na vifaa tiba vya meno hasa kutoka Bohari ya Dawa (MSD).

“Kwa sasa msimamo wa wizara, hatutaki kuwa na taifa la vibogoyo, tunataka Watanzania wabaki na meno yao. Mtu atatibiwa jino linabaki, hii inaboresha afya ya mwili, uking’oa meno kuna baadhi ya vyakula hutaweza kula, wale waliong’olewa meno mengi, ipo huduma ya meno bandia, ambao bado tunakataa vibogoyo,” alisema.

Dk. Nzobo alisema huduma hiyo ilikuwapo muda mrefu na watalaamu wa afya ya kinywa na meno wanaifahamu, hivyo katika kuwabana wasiendelee, upo mfumo wa taarifa ambapo mtu akiziba meno ya watu wengi, utatoa alama ya kijani yenye maana nzuri.

“Ukiziba wengi kidogo utakupa alama njano kama utaziba wachache utakuwa umeng’oa wengi mfumo utakupa alama nyekundu, maana yake wewe ni hatari hufai.

“Mfumo huu umeanza kufanya kazi Januari mwaka huu na tayari baadhi ya maeneo watalaamu wameanza kubadilika na matokeo ni mazuri hasa hospitali binafsi. Mfumo unawapima wataalamu wa hospitali za serikali na binafsi,” alisema.

Rais wa Chama cha Afya ya Kinywa na Meno Tanzania, Dk. Deogratius Kilasara, alisema mkutano huo ni wa kwanza na wa aina yake kufanyika Tanzania na Afrika uliolenga afya ya kinywa na meno.

“Tumekutanisha vijana kutoka Tanzania, Rwanda Zambia, Malawi, Zimbabwe, Cosovo na Marekani. Mambo ya kinywa na meno siyo kwa Tanzania tu, kwa nchi nyingi ni kitu ambacho hakipewi msukumo wa mambo ya sera za nchi mbalimbali,” alisema.

Meneja wa MC-Tanzania, Venance Ngungo ameisema lengo la kongamano hilo MCW Global ni kuboresho masuala ya uongozi katika afya ya kinywa na meno kwa wataalamu wa afya ya kinywa na meno kwa vijana wa Afrika Mashariki na Kusini.


Source: Nipashe

Pia soma: Ngono ya kinywa inaweza ambukiza Saratani ya Koo
 
Back
Top Bottom