| Sina lengo la kutafuta umaarufu kwa kumzungumzia mtu ambaye kwa sasa anaonekana kuwa maarufu zaidi nchini Tanzania. Ana mvuto wa pekee na kajijengea heshima kubwa katika jamii. Anakubalika kila eneo. Bara na Visiwani; Wakristo na Waislamu, Wenye kumcha Mungu na Wapagani; Wazee na Vijana; Wanaume na Wanawake wote wanamkubali. |
Kinachonisukuma kuandika waraka huu; ni kuikumbusha jamii na Ndg. Lowassa kuwa Mungu ametujalia kumpata mtu ambaye anaweza kutumika vizuri katika kuleta mtangamano wa Kitaifa. Kwa karama yake ya kukubalika, binafsi, naona ni mtu sahihi wa kufanya usuluhishi yaani MEDIATION. Mwl. J.K. Nyerere alijaliwa kipawa hiki na alitumika kufanya usuluhishi wa ndani na nje ya nchi. Amefariki akiwa ni mpatanishi wa mgogoro wa Burundi. Ninaiona karama hiyo kwa Lowassa. Kwangu mimi hii ni hazina kubwa ambayo hatuna budi kuitumia kwa manufaa ya taifa letu.
Ninatambua wale ambao wanawaza siasa katika kila jambo wanaweza kuja na kejeli nyingi juu ya hiki, lakini ningependa mnipe mbadala wa Lowassa katika kukubalika katika jamii. Je, ni Pinda, Ben, Mzee Ruksa, JK, Salim, Mzee Wassira, au Warioba??? Kwangu mimi, Lowassa ndiye mtu pekee kwa sasa ambaye anaweza kuwaambia watu wenye jazba, tulieni na wakatulia, wenye silaha mikononi kuwa wekeni chini na watu wakaheshimu; anaweza kuwaambia wanaopigana tulieni na watu wakatii.
Baada ya maisha ya siasa, sasa ni wakati muafaka sana kwa Mzee Lowassa ukawatumikia Watanzania kwa njia hii ambayo kwangu mimi naona ina thawabu kubwa sana mbele za Mungu. Tuna migogoro ya muda mrefu hapa nchini mf. Wakulima na Wafugaji, Wachimbaji wa madini na Wawekezaji, misuguano ya kidini ya chini kwa chini nk. Migogoro hii kwa upande mwingine haihitaji mabavu au mkono wa Serikali bali watu wenye busara zao kama Ndg. Lowassa. Kama hili halitoshi, familia ya Lowassa imebahatika kuwa na Mama mwenye mvuto na ushawishi kuliko wanawake pengine wote kwa sasa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Anajiheshimu, ana busara na anakubalika mno mno. Hii ni nyongeza kwa Mzee Lowassa katika kukamilisha kazi ambayo naiona imebaki katika kipindi cha maisha yake. Neno la Mungu linasema Heri Wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu!!
| Mwenyezi Mungu akupe jicho la pekee Mzee Lowassa ili uweze kutumika kwa namna mpya na yenye manufaa makubwa kwa Taifa, Bara la Afrika na Dunia kwa ujumla. Mungu akuzidishie maisha marefu na wote wenye kuwaza na kupanga mabaya dhidi yako washindwe. |