SoC01 Vyuo Vikuu, tuzalishieni wasomi na siyo wasomaji

Stories of Change - 2021 Competition

Gnyaisa

Member
Jul 13, 2021
23
24
Tofauti kubwa iliyopo kati ya “MSOMAJI” na ‘MSOMI” ni kwamba mmoja husoma au kutamka kile kilichoandikwa “mbele” yake na mwingine husoma au kutamka kile kilichoandikwa “ndani” yake. Kwa lugha nyepesi tunaweza kusema mmoja huamini sana katika kile anachokiona kwa muonekano wa nje na kisha kuridhika ilhali mwingine huamini sana katika kile anachokiwaza na kisha kijibidiisha ili kukifanya kitokee katika ulimwengu wa uhalisia.

Lengo la taasisi yoyote ya Elimu ya Juu kwa maana ya Vyuo Vikuu ni kubadili fikra za mtu kutoka katika kuamini kile anachokiona na kuridhika nacho (MSOMAJI) kwenda katika kuamini kile anachokiwaza na kukifanya kitokee (MSOMI). Bahati mbaya idadi kubwa ya Vyuo tulivyonavyo nchini vimepoteza lengo hili na kuanza kufanya kinyume chake!

Leo hii ni jambo la kawaida kwa kijana aliyekuwa na ubunifu mkubwa katika masuala ya teknolojia pindi alipokuwa shule ya sekondari kujikuta hawezi kufanya lolote mara tu baada ya kuhitimu elimu yake ya Chuo Kikuu! Badala ya kuwa matanuru ya kunoa vipaji na kuzalisha wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali, vyuo vingi nchini vimegeuka kuwa mahandaki ya kubutusha makali ya akili za vijana. Kijana aliyehitimu elimu ya msingi kwa ufaulu wa juu mathalani katika masomo ya sayansi na kuchaguliwa kujiunga na shule ya vipaji maalumu ya Ilboru au Mzumbe hujikuta akishindwa kufanya lolote pindi aingiapo na kumaliza Chuo Kikuu!

Vyuo vingi nchini vimejikita katika kutoa nadharia pekee bila mafunzo kwa vitendo na hatimaye kuzalisha tabaka la vijana wanaoamini zaidi katika vyeti na ufaulu wa darasani kuliko uwezo wa kutenda na kuzalisha kile wanachokiamini. Leo hii ni jambo la kawaida kukutana na mhitimu wa Chuo Kikuu ambaye vyeti vyake vinaonesha ufaulu mkubwa katika masuala ya Kompyuta lakini hajui jinsi ya kufungua akaunti ya barua pepe!

Inashangaza sana kuona vyuo vinavyotoa mafunzo ya afya kama vile Chuo Kikuu cha Muhimbili au Chuo Kikuu cha Bugando vinakuwa na wahadhiri ambao pia ni madaktari katika mahospitali yanayopatikana hapo Vyuoni au mahali pengine lakini wahadhiri katika fani nyingine kama za sheria au ujasiriamali wakiwa hawajawahi kusimamia kesi yoyote mahakamani au kumiliki duka, achilia mbali kampuni ya uwakili au ujasiriamali! Mhadhiri huyu katika fani ya ujasiriamali hategemewi kuzalisha mjasiriamali nguli mwenye uwezo wa kubadili aiskrimu iliyokuwa ikifungwa kwenye nailoni chafu na kuuzwa kwa watoto wa shule za msingi kuwa aiskrimu iliyotengenezwa kwa ubora na kuuzwa katika maduka makubwa ya kisasa ya vyakula. Hatutegemei mhadhiri huyu azalishe mfanyabiashara mashuhuri mwenye kuona kuwa ukosefu wa maji katika jiji la Dar es Salaam ni fursa ya utajiri. Tegemeo pekee kwa wasomi watakaozalishwa na mhadhiri wa aina hii ni kuona wakiishinikiza serikali iwatimue kazi watendaji wa Mamlaka ya maji (DAWASCO) kwa kushindwa kufanya kazi.

Kama sifa kuu ya kuanzisha Chuo cha Afya nchini ni kwa Chuo hicho kuhakikisha kinakuwa na hospitali au kituo cha Afya kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo, iweje sifa hiyohiyo isitumike kwa Chuo cha Sayansi na Teknolojia kuwa na kiatamizi cha teknolojia (incubator) kwa ajili ya kuchochea ubunifu wa wasomi wetu?

Kila mwaka Vyuo Vikuu nchini vinazalisha maelfu ya wataalamu wasio na uwezo wa kujitegemea na hatimaye kuliendeleza taifa kwa kasi iliyokusudiwa kutokana na kukosa uwezo wa kubadili mawazo na ubunifu walionao kuwa bidhaa zenye kuuzika kwa faida licha ya kutumia zaidi ya muongo mmoja na nusu wakiwa mashuleni.

Kwa msomi aliyepikwa vema na kisha kujitambua, huwezi kumkuta akinung’unika au kulalamika juu ya matatizo mbalimbali yanayoikabili jamii inayomzunguka. Huyu ni mtu aliyejengewa uwezo wa kubadili matatizo hayo kuwa changamoto na kisha kuzitazama changamoto hizo kwa jicho la FURSA zenye kuzalisha mali na ajira. Kwa msomi huyu fedha sio tafsiri sahihi ya neno “Mtaji” na hivyo ukosefu wa fedha sio sababu ya yeye kushindwa kujiajiri. Anaamini “mtaji’ ni wazo lililopikwa vema na kisha kufanyiwa utafiti wa kina wa masoko na jinsi ya utekelezaji wake.

Ni wakati sasa kwa Vyuo vyetu kuacha kushindana kujenga majengo mazuri na yenye kuvutia macho na kuanza kutoa elimu bora na yenye kuvutia fikra za ubunifu na weledi kwa vijana wetu. Vyuo vyetu viache kuzalisha “wasomaji” wanaohusudu ajira zenye malipo makubwa, viti vya kuzunguka na ofisi za viyoyozi na kuanza kuzalisha “wasomi” wenye mtazamo chanya na uwezo wa kubadili upepo wa Singida kuwa nishati ya umeme.
 
Back
Top Bottom