Ndugu zangu Watanzania,
Viongozi wa Dini Wameomba na kumsihi Rais Samia awapatie nafasi ya kuwa na uwakilishi Bungeni ili waweze kushiriki vyema katika kutoa michango na mawazo katika utungaji wa sheria zinazogusa masuala ya Imani .
Mimi Lucas Hebel Mwashambwa napinga wazo hilo kukubaliwa na kutekelezwa hapa Nchini. Kiongozi yeyote anayetaka kwenda Bungeni ni vyema akajiunga kwenye chama cha siasa chenye usajili wa kudumu ili apate nafasi ya kugombea Ubunge na kwenda Bungeni kutoa mawazo yake.
Kama ambavyo tumeshuhudia viongozi kama Mheshimiwa Askofu Dkt Josephat Gwajima. Lakini pia Bungeni tumewahi kuwa na marehemu Mama Rwakatale. Lakini pia ikumbukwe ya kuwa zipo sheria mbalimbali Kabla ya kutungwa na kupitishwa kuwa sheria huwa wadau mbalimbali wanapewa nafasi ya kutoa mawazo na maono yao.
Ambapo hata viongozi wa Dini hupewa nafasi na fursa hiyo ya kutoa maoni na mawazo yao na kuzingatiwa vizuri kabisa. Lakini pia inafika wakati viongozi wa Dini hualikwa hadi na Rais kufanya naye mazungumzo na kupata nafasi ya kutoa ushauri wao katika masuala mbalimbali yanayogusa jamii yetu. Hivyo kwa muktadha huo hakuna sheria inayogusa imani au masuala ya kiimani inayoweza kutungwa na kupitishwa kuwa sheria bila kuwapa nafasi viongozi wa Dini kutoa maoni na mawazo yao.
Napinga jambo hili kufanyika kwa sababu hii italeta Taswira tofauti kabisa ,ambapo kila kundi litataka kuwa na uwakilishi wake bungeni .je hizo gharama ni nani atakaye zibeba na kugharamia? Vipi wafugaji nao wakitaka wawe na uwakilishi wao? Vipi wakulima nao wakitaka wawe na uwakilishi wao? Vipi vijana wasio na ajira nao wakitaka wawe na uwakilishi wao? Vipi wajane na yatima wakitaka nao wawe na uwakilishi wao?
Vipi walimu nao wakitaka wawe na uwakilishi wao? Vipi bodaboda nao wakitaka wawe na uwakilishi wao? Vipi madereva malori wakitaka wawe na uwakilishi wao? Vipi wanavyuo wakitaka nao wawe na uwakilishi wao? Vipi waganga wa tiba asili? Vipi machifu nao wakitaka wawe na uwakilishi wao Bungeni?
Ikumbukwe kila kundi litataka liwe na uwakilishi wake ili kulinda,kutetea ,kupigania na kuzungumzia maslahi yake. Je kama Taifa tutakuwa tunakwenda wapi? Hizo gharama kwa Nchi kama Tanzania yenye kuhitaji kila aina ya senti itatoa wapi? Je viongozi wa Dini hawana nafasi ya kutoa mawazo yao mpaka watake waende Bungeni? Tena kwa viti maalumu na kuteuana tu?
Hizo pesa za kuwalipa hao viongozi wa Dini wenye uwezo wa kuonana na Rais wakiomba nafasi zitatoka wapi? si bora tupewe vijana tupate kupata mitaji ya kutusaidia? Kwanini viongozi wa Dini wanataka kutubebesha mzigo wa kodi kwa ajili ya kuwahudumia kupitia kodi zetu? Kwanini hawana huruma na kutuonea huruma wananchi wanyonge? Kwani hao viongozi wa Dini hawaoni kuna vijana hawana ajira mitaani? Kwanini wasiiache serikali itafute pesa ili iongeze wigo wa kuwapatia ajira vijana hawa ambao wapo Mitaani na walisoma kwa kuuza mashamba au ardhi , mifugo n.k.?
Serikali yetu haina Dini ila watu wake wana Dini. Kiongozi yeyote wa Dini anayetaka na kutamani kuingia Bungeni kutoa mawazo yake kuhusu masuala ya imani. Naomba akachukue Fomu agombee Ubunge tu jimboni.
Watanzania tujikite kwenye mambo yanayoweza kupunguza gharama za uendeshaji na utumiaji wa kodi ya mtanzania na siyo kuleta mambo yanayoongeza matumizi ya kodi ya mtanzania bila sababu ya Msingi. Leo Taifa kubwa kama Marekani lina punguza matumizi kwa baadhi ya mambo. Halafu sisi viongozi wetu wa Dini wanapendekeza vitu vitakavyoongeza gharama na matumizi ya kodi kwa mambo yenye mbadala wake..
Naomba tuoneane huruma ndugu zanguni watanzania. nawaheshimuni sana viongozi wote wa Dini na naomba nanyi muwe na huruma nasi hususani sisi vijana. Pendekezeni mambo yenye kugusa Maisha ya wengi na yenye kuwapa tabasamu,furaha na matumaini watu badala kupendekeza mambo yenye kuibua hisia na masononeko .
Kazi iendelee, Mama Ametufikia na kuwafikia watanzania kwa utumishi wake uliotukuka wa kugusa Maisha ya watanzania wanyonge wasio na Sauti.
Lucas Hebel Mwashambwa, Mama ANATOSHA kuendelea kuliongoza Taifa letu kwa muhula wa pili.