Viongozi wa dini tuwaambie ukweli watawala

Danos

Member
Dec 21, 2013
88
100
Naomba kuwasilisha maoni yangu kwa viongozi wetu wapendwa katika imani mbalimbali za kidini.

Baadhi ya viongozi wa dini wamekuwa wakitumia upande mmoja tu wa Neno la Mungu kuelezea kuhusu umuhimu wa kuheshimu mamlaka zilizopo kwa kuwa zimetoka kwa Mungu na zimeruhusiwa na yeye kuwepo.

Nikinukuu mstari huo wa Biblia ambao hupenda kuutumia, unatoka kwenye Warumi 13:1

"Kila mtu hana budi kutii serikali inayotawala. Kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na serikali zote zilizopo zimewekwa na Mungu" (Biblia Takatifu).

Ninaunga mkono kabisa jambo hili. Ni hakika kila utawala umeruhusiwa na Mungu kuwepo, kwa ajili ya kusudi la Mungu huyo aliyeruhusu utawala huo kuwepo. Hivyo ni wajibu wa kila raia kuheshimu watawala.

Ukweli ambao sasa viongozi wengi wa dini hawawaambii watawala hao ni kuwa wanawajibika mbele za Mungu huyo aliyewapa hayo madaraka (they are responsible). Ipo siku watatoa hesabu mbele za huyo Mungu aliyewapa hayo madaraka ni kwa jinsi gani waliyatumia madaraka hayo kutekeleza kusudi la Mungu.

Pale watawala wanapokosea haipaswi viongozi wa dini kusifia tu kila jambo, ni muda wa kuwatahadharisha na kuwaeleza wajirekebishe kwa kuwa Mungu aliyewaweka hapo atawahukumu pia siku moja.

Nikitumia kitabu cha Biblia tunaona kuna tawala na wafalme waliruhusiwa/waliwekwa na Mungu kwa ajili ya kusudi lake. Baadhi yao walifanya vibaya na mwisho wa siku walihukumiwa na huyo huyo Mungu. Kwa mfano:

I. Mfalme wa Ashuru aitwaye Senakeribu aliwekwa na Mungu kwa lengo la kupeleka hukumu dhidi ya falme nyingine zilizokuwa ovu. Alifanikiwa sana, lakini alipokuja kumdharau Mungu hapo ndipo alipoangamia (Isaya 37).

2. Mfalme Uzia huyu naye alianza vema kabisa kutawala na alifanya vizuri. Lakini alipokuwa na nguvu na umaarufu, moyo wake ulitukuka na akamdharau Mungu. Alitaka kuchukua nafasi ya makuhani ambayo haikuwa yake na Mungu alimpiga kwa ukoma na akafa akiwa na ukoma katengwa kabisa (2 Nyakati 26:16-23).

3. Mfalme Nebukadneza. Huyu naye aliwekwa na Mungu na alikuwa ni mfalme Mkuu sana wa Babeli. Lakini moyo wake ulipotukuka na kujiinua juu kuliko Mungu na kutaka yeye ndiyo aabudiwe na kutukuzwa, Mungu alimshusha. Anapewa adhabu ya miaka saba kula majani kama ng'ombe, na kuishi maporini kama wanyama mpaka alipotambua kuwa Mungu ndiye mtawala mkuu juu ya ulimwengu wote (Danieli 4).

4. Mfalme Herode katika Agano Jipya alipojaribu kutaka kutwaa sifa na utukufu wa Mungu, basi Mungu alimpiga Herode na kufa (Matendo ya Mitume 12:21-22).

Hii ni mifano michache Kati ya Mingi ya watawala walioruhusiwa kuwepo madarakani na Mungu, lakini waliwajibika mbele za Mungu huyo.

Ushauri wangu ni huu, tusiwe kama mafarisayo ambao tatizo lao kuu lilikuwa ni unafiki na hata Bwana Yesu aliwakemea sana kwa tabia hiyo ya unafiki (Mathayo 23). Unafiki na kujipendekeza ndicho kitu ambacho walikuwa nacho hawa viongozi wa dini. Hawakuhubiri kweli kamili na hata kuiishi hiyo kweli.

Hivyo basi, wapendwa viongozi wa dini tuwe mstari wa mbele kuwaambia watawala ukweli pale wanapoenda nje na mapenzi ya Mungu. Pale wanapofanya mambo mabaya kama vile rushwa, ufisadi, uonevu, kutojali Kilio cha masikini na wale wanaowaongoza, na mengine yasiyofaa kufanywa na viongozi.

Msiogope kulipa gharama maana ninyi ufalme wenu si wa dunia hii, bali ni wa mbinguni.

Wako wapi mashujaa kama kina nabii Musa aliyemkemea Farao? Wako wapi mashujaa kama kina nabii Nathani aliyemkemea mfalme Daudi? Wako wapi mashujaa kama nabii Samweli aliyemkemea mfalme Sauli? Wako wapi mashujaa kama nabii Isaya aliyewakemea viongozi waovu wa Yuda na Israeli? Wako wapi mashujaa kama kina nabii Yeremia aliyewakemea viongozi waovu wa Yuda? Wako wapi mashujaa kama kina Danieli waliokataa maovu? Wako wapi mashujaa kama kina Yohana Mbatizaji aliyemkemea mfalme Herode?

Kikubwa ninachokiona ni hofu ya kutendewa mabaya na watawala hao endapo mtawaambia ukweli. Lakini jueni kuwa na nyinyi pia mtatoa hesabu kwa Mungu kuhusu jambo hilo. Wanapofanya vizuri muwapongeze, na pale wanapokosea muwaambie ukweli msinyamaze kimya.

“Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; Bali mwovu atawalapo, watu huugua. ”
— Mithali 29:2 (Biblia Takatifu)
 
Tatizo sadaka zetu na enyewe ni asali tosha ndio maana wanakaa kimya ..... waumini wao tunaumia sana hadi hukohuko kabisaa saa ii zimekua nyingi sana ndio maana kimya kimetawalwa na viongozi wa dini
 
Nitawazungumzia wa Ukristo. Wanajua Mungu kwa maana ya JEHOVA au NIKO Ambaye NIKO etc ni Wahaki na Kweli yote. Lakini utakuta katika suala la kuombea Viongozi wa tawala za kimwili/ dunia/ Wanasiasa wanaangalia kuwaombea upande mmoja wa baraka tu. Ambavyo si haki mbele za Mungu hata mbele za wanadamu. Viongozi hawa wa wananchi wa kidunia unakuta wako baadhi si wote pengine wachache ni watenda maovu ya kiwemo ya kifisadi yanayo waumiza wanao waongoza ile mbaya lakini huoni kiongozi wa Kikristo anaye stuka. Sana sana utakuta kwenye miongozo yao ya ibada wameweka kuwaombea kijumla jumla tu Viongozi wa kiraia ambao kati yao wako waovu, wanawaombea ulinzi na baraka za Mungu.

Wakati kiuhalisia bila hata kumtangazia mtu maana pengine wanaogopa, basi wangetakiwa angalau wachukue hatua kumlilia Mungu sirini ili awakoe watu wakiwemo waumini wao na maovu ya baadhi ya hawa viongozi. Sala za kufanya kuwa shitaki viongozi waovu na watu waovu wanao waumiza wenzao kwa tamaa tena za dunia hii ambayo maisha yake ni ya kitambotu ziko wazi kwenye Bibla. Mfano ZABURI ya 10 ni Sala nzuri na inayo jitosheleza ya kushughulikia na kumalizana na watenda maovu wote dhidi ya wanyonge wasio na mtetezi.
 
Kuna Viongozi wengine wa Dini ni bora wanyamaze tu maana wakifungua tu midomo yao inakuwa kama ifuatavyo

Imagine unayasema yote haya kwa sinia la Ubwabwa na bahasha ya laki unusu.
 
Hongereni sana TEC kwa waraka mzuri ambao kila mwenye kuona vema ameguswa nao. Mmeonesha njia. Tunangoja na wengine pia wafuate kama vile CCT na CPCT.

By the way huwezi kuzitenganisha dini na siasa kwa mtazamo wa viongozi wa kidini kutoa maoni yao kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu taifa.

Endeleeni mbele kukemea maovu yote katika jamii pasipo kuangalia cheo au status yoyote kwa maana mnawajibika kwa kila mtu.
 
Back
Top Bottom