Benjamini Netanyahu
JF-Expert Member
- Aug 7, 2014
- 92,382
- 112,023
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro, akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuhusu hali ya usalama nchini na suala la mauaji ya wananchi mkoani Pwani.Kulia ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya jinai (DCI), Robert Boaz na Kamishna wa Polisi Jamii, Musa Ali Musa. PICHA NA LOVENESS BERNARD
Kulwa Karedia na Nora Damian-Dar es Salaam
SIKU moja baada kuwapo taarifa za kufumuliwa kwa Jeshi la Polisi, kishindo cha mkuu wa jeshi hilo (IGP), Simon Sirro, kimeanza kutikisa.
Hatua hiyo, imekuja baada ya MTANZANIA katika toleo lake la jana, kuripoti kwa kina kuwa IGP Sirro amedhamiria kufanya mabadiliko makubwa ya makamanda wa polisi wa mikoa, wakuu wa upelelezi wa mikoa na wakuu wa polisi wa wilaya, ikiwa ni ahadi yake ya kurejesha nidhamu ya utendaji ndani ya jeshi hilo.
Kutokana na hali hiyo IGP Sirro juzi alilazimika kufanya mabadiliko ndani ya Kitengo cha Udanganyifu ‘Fraud’ kwa kuwaondoa viongozi wake kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo rushwa.
Hiyo inakuwa ni hatua yake ya kwanza baada ya kuwapo kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu kitengo hicho ambapo viongozi wake walikuwa wamegubikwa na malalamiko ikiwemo matumizi mabaya ya madaraka.
Kutokana na taarifa hizo MTANZANIA ilimtafuta IGP Sirro, ambaye alithibitisha kufanya mabadiliko hayo kwenye kitengo hicho kwa kusema kuwa ni ya kawaida yakiwa na lengo la kukisuka upya kitengo hicho.
“Ni kweli nimefanya mabadiliko kwenye kitengo hiki, haya ni ya kawaida tu ndugu yangu, tumejipanga kurudisha nidhamu ya utendaji,” alisema IGP Sirro.
Alipoulizwa sababu ya mabadiliko hayo, alikataa kutaja sababu, japo gazeti hili lina taarifa za uhakika kuwa wameondolewa kutokana na kutuhumiwa kwa matumizi mabaya ya ofisi, ubadhirifu na kushamiri kwa vitendo vya rushwa katika kitengo hicho.
Katika mabadiliko hayo, amemwondoa Mkuu wa kitengo hicho Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Joseph Konyo na msaidizi wake, Kamishna Selemani Nyakuringa.
Alisema katika kujaza nafasi hiyo amemteua Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Deodatus Mataba kukaimu nafasi ya Konyo.
Habari za ndani zinasema kitengo hicho kimekuwa kikilalamikiwa na watu wa kada mbalimbali hasa wafanyabiashara wakubwa wanaodaiwa kubambikiziwa kesi na kuombwa rushwa.
“Mabadiliko haya ya afande IGP yamekuja wakati mzuri mno, maana sisi askari wa chini tumekuwa kama watazamaji tu… wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wanaonewa,” alisema ofisa wa jeshi hilo ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini.
“Huwezi amini kwa muda mrefu afande Konyo amekuwa pale, lakini kumekuwapo na malalamiko mengi, tunaamini kuingia kwa afande Mataba kwenye kitengo hiki kunaweza kurudisha imani kubwa kwetu askari wa ngazi za chini na wananchi kwa ujumla.
“Nadhani afande IGP amezingatia malalamiko yaliyopo japo ameingia ofisini jana (juzi) tu…hawa watapangiwa kazi nyingine kama nilivyosikia,” alisema.
AWAITA MAKAMANDA
Katika hatua nyingine, IGP Sirro amewaita makamanda wa polisi wa mikoa yote kuja Dar es Salaam kwa ajili ya kikao maalumu ambacho kitafanyika kesho kuanzia saa moja na nusu asubuhi.
“Nimewaita makamanda wote wa mikoa waje Dar es Salaam kwa ajili ya kuzungumza nao…siwezi kusema nini tutauzungumza maana hayo ni mambo yetu ya ndani,” alisema IGP Sirro.
Kwa mara ya kwanza IGP Sirro amewaagiza makamanda wapande magari kwa kanda, badala ya kila kamanda kutumia gari lake ili kubana matumizi.
“Kwa mara kwanza afande IGP ameagiza makamanda waje kwa kupitia kutokana na ukaribu wa mikoa au kanda ili kupunguza gharama za matumizi ya mafuta na na malipo ya maderava (allowance),” alisema ofisa mmoja wa jeshi hilo.
ATUMA SALAMU
Katika hatua nyingine, IGP Sirro, ametuma salamu kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu na kusema kuwa anayefanya ubaya atajibiwa kwa ubaya.
Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya jeshi hilo jana, alisema licha ya nchi kuwa shwari, yapo matukio machache ambayo yanahitaji nguvu ya pamoja kuyashughulikia.
Aliyataja baadhi ya matukio hayo, kuwa ni mauaji ya wananchi ambayo yamekuwa yakitokea mkoani Pwani, wananchi kujichukulia sheria mkononi, bodaboda kutotii sheria za usalama barabarani na kujihusisha na vitendo vya uhalifu na vitendo vya rushwa.
Alisema kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa kikundi cha wahalifu wanaojihusisha na mauaji mkoani Pwani, atazawadiwa Sh milioni 10.
MAUAJI PWANI
Alisema hakuna matukio makubwa ya kutisha, lakini changamoto kubwa iliyopo ni mauaji yanayoendelea kuwa yanafanywa na kikundi cha watu wachache wanaofikiri wanaweza kufanya mkoa huo usiwe na amani na utulivu.
“Unapoua kwa silaha unategemea nini…kwa hao wanaofanya ubaya tupeleke tu salamu kwamba ubaya huu tutajibu kwa ubaya kwa mujibu wa sheria.
“Sisi ni wengi wao ni wachache tunaweza na majibu ya Ikwiriri, Kibiti hayatachukua muda mrefu, wale tuliofanya kazi pamoja nafikiri tunafahamiana vizuri.
“Vitendo vizungumze zaidi kuliko maneno, wakubwa zetu walishasema kilichobakia ni kutekeleza.
“Wanaelewa jeshi lilivyo tunapokuwa kwenye oparesheni kwahiyo hawajatuzidi nguvu na wala hawatatuzidi. Wana Mkuranga, Ikwiriri wasubiri majibu ndani ya muda mfupi,” alisema Sirro.
IGP Sirro pia aliwaomba wananchi wa mkoa huo wasiyakimbie maeneo yao na kwamba muda si mrefu atakwenda kuzungumza nao ili wamwelewe.
“Wewe kama si mhalifu kwanini ukimbie, kama kuna mtu ameonewa ajitokeze ili ashughulikiwe kwa sababu maelekezo tunayoyatoa ni kushughulika na uhalifu na wahalifu, tusipoaminiana kazi itakuwa ni ngumu,” alisema.
Kuhusu mauaji dhidi ya polisi, alisema ni ajali kazini na huwa wanayachukulia kama changamoto na kuzidi kujipanga zaidi.
“Unapopambana na uhalifu ni pamoja na wanaotumia silaha na si kwamba tunakufa sisi tu na wao wanakufa. Ndiyo maana huwa najisikia vibaya mtu anapofanya makosa halafu anakataa kukamatwa.
“Watu wanasahau polisi wamepewa wajibu wa kutumia nguvu ya kadiri kuhakikisha kwamba anakukamata,” alisema.
BODABODA
Alisema baadhi yao, wamejiingiza kwenye matukio ya uhalifu na wamekuwa hawazingatii sheria za usalama barabarani.
Alisema baadhi ya bodaboda wamekuwa wakipita kwenye taa nyekundu, kupakia ‘mishikaki’ na kutovaa kofia ngumu hatua ambayo huwasababishia vifo, kujeruhiwa na kupata ulemavu wa kudumu.
Hivyo aliwaagiza makamanda wote wa mikoa kuwakamata na kuwachukulia hatua kali za kisheria wote wasiofuata sheria za usalama barabarani ama kujihusisha na vitendo vya uhalifu.
“Hakuna kikundi cha watu ambao wako juu ya sheria, hivyo mtu yeyote katika shughuli hii ya bodaboda akifanya tofauti ni lazima akamatwe na kufikishwa mahakamani,” alisema.
SHERIA MKONONI
Alisema tabia ya watu kujichukulia sheria mkononi inazidi kukua ambapo kati ya Januari hadi Machi, mwaka huu, yameripotiwa matukio 245 ukilinganisha na matukio 222 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.
“Mtu ameiba kuku halafu mwenye kuku anapiga kelele wananchi wanakuja wanampiga hadi kumuua, je kuku aliyeibwa ana thamani na mtu aliyeuawa?
“Kama amekosa tumkamate na tumpeleke mahakamani na sheria itachukua mkondo wake,” alisema.
RUSHWA
Kuhusu rushwa alisema kumekuwa na malalamiko dhidi ya askari polisi kujihusisha na vitendo vya rushwa, huku pia baadhi ya wananchi wakiwashawishi askari kupokea rushwa kama ngao ya kukwepa kuwajibishwa pindi wanapokuwa wamefanya makosa.
“Hakuna cha msalie mtume kwa askari atakayebainika kujihusisha na vitendo vya rushwa, tukishapata ushahidi tutamfukuza kazi na kumpeleka mahakamani.
“Rushwa ni adui wa haki, nawaomba Watanzania tusiwashawishi askari kupokea rushwa na askari atakayefanikisha kumkamata mtu aliyetaka kumshawishi atazawadiwa kiwango sawa cha thamani ya rushwa aliyoikataa,” alisema Sirro.
DAWA ZA KULEVYA
IGP Sirro, aliwatahadharisha watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kuacha mara moja kwa sababu mwisho wa siku wataishia katika mikono ya sheria.
“Wale ambao kipato chao kilikuwa kinatokana na biashara ya dawa za kulevya nawasihi waachane nayo, kwa sababu kwa sasa hailipi na mwisho wa siku itawafanya waache familia zao,” alisema Sirro.
SAFU MPYA
Kuhusu safu mpya alisema amekaa ndani ya jeshi hilo kwa muda mrefu na kwamba kuna watendaji wazuri, jambo la msingi ni kufanya kazi ambayo itaonekana.
“Nimekaa ndani ya jeshi la polisi muda mrefu tunafahamiana. Polisi, maofisa ni walewale na ni watendaji wazuri, kwahiyo lazima tufanye kazi wananchi wajue kwamba kuna kazi inafanyika na wajue kwamba tuko salama,” alisema.
VIPIGO KWA WAANDISHI
Akizungumzia matukio ya kupigwa kwa waandishi wa habari, IGP Sirro alisema si sahihi kumpiga mwandishi wa habari na akawataka waandishi watakaopigwa kupeleka malalamiko ili hatua za kisheria zichukuliwe
Chanzo: MTanzania