Tumia nyenzo za kidigitali kubaini eneo halisi iliporekodiwa video hii. Je, ni kweli imerekodiwa Uyole mkoani Mbeya kama ilivyodaiwa na mtumiaji mmoja wamtandao wa Instagram? anasema "Leo Mapema Uyole Fashion Week Hapa Igawilo"
- Tunachokijua
- Uhakiki na uthibitishaji wa maudhui picha na video ni muhimu ili kudhibiti upotoshaji unaoweza kufanyika kupitia maudhui ya aina hiyo. Hivyo ni muhimu kujifunza namna ya kutumia nyenzo za kidijitali zinazotuwezesha kubaini uhalisia wa picha na video ili kuepuka upotoshaji wakati wote.
Uthibitishaji Picha au video kwa kutumia Google Reverse Image Search ni njia muhimu ya kubaini asili au maelezo zaidi kuhusu video kwa kuchukua picha (screenshot) katika sehemu ya video husika.
JamiiCheck imekuandalia utaratibu wa hatua kwa hatua wa jinsi ya kutumia Nyenzo hii kufanya uhakiki wa picha na video. Rejea kiungo hiki kufuata hatua zote.
Mfano tutumie video hii inaonesha mazingira ya mjini, ikidaiwa kuwa imerekodiwa Uyole mkoani Mbeya ambapo mtumiaji wa mtandao wa Instagram aliandika "Leo Mapema Uyole Fashion Week Hapa Igawilo"
Je, ni kweli imerekodiwa Uyole mkoani Mbeya?
Kwa kutumia nyenzo za kidigitali wadau wa JamiiCheck wameshiriki kuthibitisha video hiyo ambapo wanabainisha kuwa mazingira ya eneo hilo hayafanani na eneo linalotajwa kuwa imerekodiwa. Mfano wadau wameeleza kuwa Uyole hakuna msikiti mkubwa unaofanana na ule unaoonekana katika video.
Ufuatiliaji wa JamiiCheck
JamiiCheck kwa kutumia Google Reverse Image Search imebaini video ya msikiti huo ambayo ilichapishwa katika ukurasa wa TikTok wa Jonathan Koffi Novemba 15, 2025 akibainisha kuwa ni Msikiti Mkuu wa Adjamé nchini Ivory Coast.
Aidha Oktoba 17, 2025 tovuti ya Lavenir.ci ilichapisha taarifa iliyohusu hafla ya makabidhiano baada ya kukamilika kwa ukarabati wa Msikiti Mkuu wa Salam wa Adjamé pamoja na kituo chake cha Kiislamu ilifanyika siku ya Ijumaa, tarehe 17 Oktoba 2025. Rejea picha hii iliyoambatanishwa katika taarifa hiyo inafanana na msikiti ulioonekana katika video.
Aidha kupitia Google Earth inaonesha muonekano wa eneo la msikiti huo sambamba na maeneo jirani ambayo yanaonekana katika video.