Vevo ni nini? Nani mmiliki?

Vevo ni nini? Nani mmiliki?

Kingsmann

JF-Expert Member
Joined
Oct 4, 2018
Posts
5,533
Reaction score
20,920
Kampuni ya Vevo ilizaliwa mwaka 2009 huko Marekani kwa lengo la kutoa huduma za usambazaji maudhui ya wasanii hasa waimbaji kwa kuambatanisha na matangazo ili waweze kujipatia kipato. Vevo ilianzishwa na makampuni makubwa matatu ya kusimamia wasanii; Universal Music Group, Sony Music Entertainment na EMI,

Watu wengi wamefahamu Vevo kwa kusambaza video za wasanii kupitia YouTube, lakini kampuni hiyo husambaza video za wasanii kupitia majukwaa mengine mengi kama vile Apple TV, Roku, Samsung TV Plus, Amazon Fire TV na Amazon Echo Show, Pluto TV, VEWD, Sky Q, Virgin Media, Unity Media na Now TV miongoni mwa majukwaa mengi.

Wakati VEVO inaanzishwa, fikra kubwa na ya kwanza ilikuwa ni kuunda mfumo wa kipekee na unaojitegemea unaofanana na YouTube ambao ungeweka maudhui ya wasanii, yaani nyimbo peke yake. Mara baada ya kuanzishwa, Vevo waliunda tovuti kama ilivyo YouTube na baadaye simu janja zilipokuja, waliunda programu tumishi iliyokuwa inapatikana kwa njia za simu.

Tovuti ya Vevo na Programu yake tumishi zilidumu kwenye huduma ya kupakia maudhui ya wasanii na kusambaza YouTube na majukwaa mengine kwa miaka tisa tu. Kufikia mwaka 2018, Vevo waliishiwa pumzi ya kuwa na fikra za kujenga jukwaa mbadala la YouTube na wakaamua kusitisha utoaji huduma kupitia programu tumishi na tovuti yao. Hata hivyo waliingia katika makubaliano mapya ambayo yasingeathiri sana yale ya awali, isipokuwa tu wao Vevo wasingeweka maudhui kwenye tovuti yao tena.

Pamoja na kusitisha utoaji huduma kupitia tovuti na programu tumishi yao, bado wameendelea kuwa wasambazaji maudhui ya wasanii kote duniani na kupitia majukwaa tofauti.

Kwanini walishindwa kuwa mbadala wa YouTube?

Si rahisi sana kuwa mbadala wa YouTube au Google, tunaweza kusema hivyo. Pamoja na kuwa wamiliki au wasimamizi wa wasanii karibu wote wakubwa duniani na kuwa na nguvu ya kifedha, makampuni yaliyopo nyuma ya Vevo kama Sony Music Entertainment na Universal Music Group yamekubali ukweli kuwa kuanza kuumba jukwaa lingine linalojitegemea la kuweka video za wasanii si kazi rahisi na ingewagharimu kwa namna nyingi.

Itakumbukwa kwamba, mwaka 2018 YouTube waliunganisha idhaa (channel) za wasanii ambao walikuwa na zaidi ya moja. Kwa mfano, hapa kwetu Tanzania, kulikuwa na idhaa ya Diamond Platnumz na Diamond Platnumz VEVO, Alikiba na Alikiba VEVO, Vanessa Mdee na Vanessa Mdee VEVO ambazo YouTube iliunganisha na kumpatia kila mmoja idhaa moja ambazo leo hii ni Diamond Platnumz, Alikiba na Vanessa Mdee huku zote zikiongezewa alama ya muziki mbele ili zitambulike kama idhaa za waimbaji.

Hatua hiyo na hatua nyingine zilipunguza nguvu ya Vevo, kama mshindani wa YouTube na kuwa mtoa maudhui kwa YouTube. Kwa kifupi, YouTube imeshinda vita na mambo yametokea kama ambavyo walitaka, kuwa na watoa na wauzaji maudhui kwenye jukwaa lao na si washindani.

YouTube inakadriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 40, wastani wa shilingi trilioni 85 za Tanzania. Mwaka 2019 pekee, YouTube iliingiza faida ya dola bilioni 15.15 ambayo ni zaidi ya shilingi za kitanzania trilioni 32. Kwa kulinganisha ni kuwa, Vevo wao wana thamani kiduchu tu ya dola bilioni 1 za kimarekani, sawa na shilingi trilioni 2.2 huku taarifa ya mwisho ya mwaka 2017 ikionesha kuwa walipata faida ya dola milioni 650, sawa na kama shilingi trilioni 1.4 za kitanzania.

1587679430_mLL6PpmpzJ.jpg


Serengeti Post.
 
Back
Top Bottom