Uwe na maisha mema

Amani Dimile

JF-Expert Member
Jul 27, 2022
243
395
Niliandika maandishi haya nikiwa kwenye dimbwi kubwa la majonzi na huzuni, mboni zangu zikiwa zimelegea tepe kwa vundo kubwa la machozi yaliyokuwa yakitiririka muda mrefu shavuni mwangu.

Akili yangu ilikuwa imesimama kama ndama aliyeachwa njia panda na mamaye asijue la kufanya. Kichwa changu nilichokitegemea kwenye kufikiri jibu sahihi la kufanya ndio hicho hicho kilikuwa kimejaa kumbukumbu zako nyingi huku nikijitahidi kujiaminisha kwamba nitakusahau.

Ukweli ni kwamba, kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho, lakini shida ni kwamba si kila mwisho unaendana na mwanzo. Safari ya mapenzi yetu ilikuwa nzuri iliyofana, iliburudisha sana moyo wangu na kunifanya nijione kiumbe bora kuliko wote katika dunia hii.

Lakini ghafla upepo wa kusi ulikuja na kuzima tumaini langu lililokuwa limewaka mithili ya kibatari. Mapenzi yakaniacha chali, nikiwa sina hali mpungufu mwanaamali nisie na fedha wala mali.

Nenda, nenda tu mpendwa huenda hukujua ni jinsi gani nilikuwa nikilia kwa ajili yako. Huenda hukuwahi kuthamini hata theluthi ya pendo langu kwako. Hukuwahi kutambua ni jinsi gani nilijitahidi kuzitimiza ahadi zote nilizoziahidi mbele yako.

Hukuweza kusubiri hata kidogo, hukuweza kuamini hisia za awali nilizozionyesha mbele yako, nasikitika kuona wajanja wa mjini wamepofusha mboni zako tamaa imekutawala na kuongoza maisha yako bila kujali shimo la majuto hutumbukia yeyote atangulizae tamaa kuliko hali halisi aliyonayo. Umekuwa mtu mwingine kabisa, si yule tena aliyekuwa na kiu ya mafanikio bali umekuwa na kiu ya kulala na waliofanikiwa.

Ushauri wangu ni kwamba kuwa makini sana na maisha uliyochagua kuishi, hapa mjini unaweza ukapata mpenzi mpya lakini huwezi kupata afya mpya. Hapa mjini mapenzi yanapimwa kwa kilo kutokana tu na mfuko wako, lakini unapewa na magonjwa kama kifungashio. Angalia, maisha ya wale waliokata tamaa yasipoteze matumaini yako ya uhai, mwisho wa siku msaada pekee utakaopewa ni "pole".

Usipotumia akili zako kuuongoza wako mwili, zitakazoumia ni sehemu zako za siri. Kuwa makini, kifo humsubiri yeyote asiefuta ushauri wa waliomtangulia hapo awali.

Ahsante sana kwa kunisikiliza, ni mimi mpenzi wako wa zamani.

Amani Dimile

Sent from my TECNO KE5 using JamiiForums mobile app
 
Back
Top Bottom