Utandawazi: Ukweli upaswao kujulikana | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Utandawazi: Ukweli upaswao kujulikana

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Yona F. Maro, Dec 22, 2008.

 1. Yona F. Maro

  Yona F. Maro R I P

  #1
  Dec 22, 2008
  Joined: Nov 2, 2006
  Messages: 4,237
  Likes Received: 33
  Trophy Points: 0
  UTANDAWAZI kwa jina jipya la 'globalization' pengine ni dhana mpya kwa jina lakini si kitu kipya hapa duniani. Dhana hiyo kwa leo imejaa hadaa inayowaaminisha baadhi ya watu kuwa utandawazi ni kitu chema. Haijawahi kuwa hivyo na haitawahi kuwa vivyo.

  Hii ni kutokana na ukweli kuwa utandawazi au Kiswahili chepesi mfumo unaoruhusu wachache kuhalalisha kunyonya wengi kama ni kitu kisichoepukika na kwamba hiyo ndiyo hatima ya mwanadamu.

  Isingewezekana mfumo huo kuitwa jina baya la 'exploitation' na ndiyo maana likachaguliwa jina la 'globalization' kuficha ule unyama wa kibinadamu uliomo ndani ya dhana hiyo.

  Kihistoria hili linatokana wakati mwingine na ile imani kwa baadhi ya watu kuwa kuna watu waliojaliwa na waliolaaniwa hapa duniani, na kwamba wale waliobarikiwa wanastahili kuwa na kila neema na bahati njema, na wale waliolaaniwa hawastahili baraka bali nuksi, mikosi na fadhaa katika maisha yao - tangu wanapozaliwa hadi kaburini.

  Hata hivyo, ushahidi kutokana na imani mpya hivi sasa zilizojipambanua na zile imani za kale ni kinyume cha hayo.
  Imani hizi zinathibitisha kuwa Mwenyezi Mungu yuko kwa ajili ya wote, matajiri na masikini, wanyonge na wenye nguvu, wazuri na wabaya.

  Mifano kutoka nchi zenye kufuata mfumo wa kisiasa na kiuchumi wa sosho-demokrasia umedhihirisha pia kuwa si lazima kuwe na unyonyaji mkubwa ili pawepo na maendeleo ya kweli na manufaa ya wengi katika jamii.

  Imedhihirishwa kuwa watu wanaweza kuruhusiwa kutajirika kiasi watakacho lakini vilevile masikini wasilazimike kuwa masikini zaidi ili kuruhusu matajiri wawe matajiri zaidi.
  Amani na utulivu katika nchi hizo ni kwa kiwango cha juu kabisa ukilinganisha na nchi zinazofuata ubepari wa kufa au kupona.

  Utandawazi umekuwepo kwa miaka elfu kadhaa kwa majina tofauti. Ingawa tunauzungumzia utandawazi huu ambao kwa hakika tafsiri yake rahisi ni unyonyaji uliokubalika kati ya wanyonyaji na wanyonywaji katika ngazi ya kimataifa, ieleweke kuwa kuna utandawazi au unyonyaji na unyonywaji wa ndani kama vile kulivyo na huo wa nje.

  Na ushahidi upo wa kutosha kuwa ni wale tu wanaopambana na kuupunguza kwa kiasi cha chini kabisa unyonyaji na unyonywaji wa ndani, yaani, utandawazi wa ndani, ndio wanaoweza kuhimili vishindo vya kupambana na utandawazi wa nje kwani tayari wanakuwa na silaha na uzoefu wa kutosha kufanya hivyo.

  Utandawazi hauwezi kuwa utandawazi kama si mfumo wa kiuchumi iwe ndani au nje ya nchi unaohalalisha tofauti za kipato au utajiri kati ya watu. Nia kuu ya utandawazi ni kuwatawala wale wasio nacho ikiwa ndani au nje ya nchi, ili waamini na waishi kwa kuamini kuwa tofauti za kiukwasi ni halali, na kwamba matajiri lazima wawepo kama ilivyo lazima pia kuwepo kwa masikini.

  Utandawazi haumlindi masikini dhidi ya tajiri kutajirika zaidi na yeye kufukarika zaidi bali unamlinda tajiri asipoteze utajiri wake au mali na maisha yake yasiwe hatarini kwa kijicho na wivu wa masikini.

  Ndiyo maana kuanzia mwanzo utandawazi kama mfumo wa kisiasa uwe wa kitaifa au wa kimataifa unakuwa umeshindwa kabla haujaanza, kwani kiasili hakuna binadamu anayezaliwa tajiri au masikini lakini ni mazingira yanayomfanya awe ama na maisha mazuri au maisha mabaya.

  Na kwa kuwa binadamu kazi yake ni kupambana na mazingira, haitayumkinika kutokuwa na watu wanaohoji utajiri wa matajiri unatoka wapi na umasikini wa masikini unasababishwa na nini. Majibu ya hili yatakuwa ni mapambano yasiyo na mwisho siku zote na hasa katika zile jamii na nchi zitakazoshindwa kuja na mipango na mikakati inayoeleweka na inayofanya kazi ili kiwango cha chini cha umaskini kiwe ni kile kinachokubalika na jamii na kiwango cha juu cha utajiri pia kiwe ni kile kinachochangia kuhakikisha kuwa masikini hawashuki chini ya mstari fulani unaokubaliwa na jamii.

  Utandawazi hatari zaidi ni ule ambao kikundi cha wanasiasa wa chama fulani (mara nyingi chama tawala) kinakula njama na Serikali, Mahakama, Bunge, Vyombo vya Habari na Vyombo vya Dola, kuhakikisha kuwepo kwao madarakani milele kwa njia za halali na haramu.

  Huu ni utandawazi unaojali na kulinda hali na mali ya wakubwa, kwa maana ya viongozi na matajiri lakini hauna habari na hali ya wafanyakazi, wakulima na masikini wengine katika jamii.

  Huu ni utandawazi mbaya sana ndani ya nchi kwa kuwa si tu unaendeleza unyonyaji bali pia unakubali kuuzwa kwa haki za watu (ikiwemo wizi wa kura - wizi ambao baadhi ya wanasiasa wameuita kuwa mbaya kuliko wizi wa benki); kupitisha sheria zinazowalinda wachache tu katika jamii; kulea uongo na kuubadili kuwa kweli; kutumia Jeshi na Polisi kulinda tu kikundi fulani katika jamii na kuonea na kudhulumu makundi mengine ya watu; na kutenda yote yale ambayo ni sumu kwa haki za binadamu, utawala bora na demokrasia katika nchi.

  Lengo la wanasiasa walioko madarakani linakuwa si kulinda nchi na watu wake, wala si kuendeleza nchi na watu wake, na wala si kuhakikisha nchi inapata kiongozi bora bila kujali anatoka chama gani na ana imani au itikadi gani.

  Lengo la wanasiasa hao linakuwa ni kujilinda wao na chama chao hata kama wananchi wanaumia; kujiendeleza wao na wanaowataka (ikiwemo kuiuza nchi kwa wageni); na msimamo wao unakuwa ni kuwa na kiongozi mradi kiongozi hata kama haifai nchi.

  Nchi yoyote ambayo viongozi wake wanaridhia watu wake kunyonywa ndani ya nchi yao na watu wa nje kamwe haiwezi kupambana na utandawazi.

  Huu ndio ule mfumo wa kisiasa ndani ya nchi, yaani utandawazi wa ndani, unaochangia mara nyingi kuwapo kwa vita ya wenyewe kwa wenyewe baada ya wanasiasa na wafuasi wa vyama visivyo madarakani kuchoshwa na kunyanyaswa, kuibiwa kura na kuporwa haki yao ya kushiriki katika uongozi wa nchi kwa njia ya kidemokrasia.

  Katika miaka elfu kadhaa, huko Asia utandawazi ulikuwepo kwa namna ya falme zilizovamia na kupora mali ya falme nyingine au jamii zilizokuwa hazina tawala madhubuti, zenye nguvu za kijeshi wala uwezo wa kuwazuia wavamizi kutoka nje.

  Utandawazi kama wizi wa mabavu

  Utandawazi kwa hiyo ulikuwa ni wizi wa mabavu - mwenye askari na silaha zaidi akiwapora walio na askari wachache au waliokuwa hawana askari wala silaha.

  Kadhalika hivi ndivyo ilivyokuwa huko Ulaya kwenye zama za Vikings na vituko vyao. Aidha ndivyo ilivyokuwa hapa Afrika ambapo wafalme wa Misri, Ethiopia, Mali, Songhai na Ghana nao walifanya vitu vyao.

  Wakati wa Warumi na Wayunani si Waingereza au Wamarekani waliokuwa na nguvu. Na wala kwa wakati huo hawakuwa hata wakidhaniwa wangekuwepo. Lakini Warumi, mathalani, walijitanua hadi Afrika, Ulaya na kwa kiasi fulani Asia. Hawakuweza kufika tu China, Marekani na Australia.

  Wachina, hata hivyo, kwa upande wao nao katika miaka ya kina Jenghiz Khan walifanya jambo hilo hilo. Wajapani wakati fulani nao waliwageuzia kibao Wachina na Wakorea. Wajapani walitamani kuwa dunia yote yenye watu kama wao ingelikuwa ni nchi na soko lao. Hawakufanikiwa mara ya kwanza kama walivyoshindwa mara ya pili. Mara ya tatu mbinu na mikakati yao ndiyo iliyokuja kuzaa utandawazi wa aina mpya. Huu ndio utandawazi unaotaka kuitawala dunia leo na kesho.

  Huu si utandawazi mwingine, ila ule wa kuigawa dunia kati ya nchi zinazozalisha mali zenye bei kubwa na kuziuzia nchi zisizozalisha bidhaa za namna hiyo lakini zenye kutoa maliasili inayotumika kuzalisha bidhaa zinazorejeshwa kuuzwa kwao kesho na keshokutwa.

  Fumbo gumu la dunia ni lile la kushindwa kutambua kwa nini maliasili iwe na bei rahisi mno ukilinganisha na bidhaa inayozalishwa kutokana na maliasili hiyo. Lakini hii ni mojawapo ya kanuni muhimu katika kuwepo na kuimarika kwa utandawazi duniani. Lazima pawepo na wanaouza ghali na kununua kwa bei rahisi kupita kiasi.

  Vitu kutoka nje vinakuwa ghali si kwa sababu waliozalisha ndio wenye mali ghafi, bali waliozalisha ndio wenye akili. Somo hapa ni kuwa nchi zetu zikiendelea kuwa masoko ya wajinga na washamba wa kutengeneza bidhaa tusitarajie kabisa kunufaika na utandawazi.

  Haiyumkiniki kwa suala na kongoni kuwaomba simba na chui huruma katika kuwararua na kuwageuza kitoweo kila siku iendayo kwa Mungu. Huruma watakayokuwa nayo simba na chui na pengine fisi ni pale watakapokuwa wameshiba na kukinai.

  Nchi isiyo na wasomi na wataalamu wa kutosha wanaoshawishika kwa hali na mali kubaki nyumbani haiwezi kuukabili utandawazi hata kidogo.

  Akili fupi za Waafrika zinawatuma kukubali na kupokea magari, mashine na vifaa mbalimbali vya kisasa kwa upande mmoja, lakini kwa upande mwingine kuwafukuza wataalamu mbalimbali wanaotaka kuhamia bara hili na kuchangia katika maendeleo yake.

  Hii inatokana na ile siasa ya 'soko la wote', ambayo, hukazia maendeleo ya vitu na si watu. Siasa hii ni rutuba tosha kuongeza umasikini na mifarakano katika jamii yoyote ile mara utandawazi unapoingia.

  Huko Marekani, makundi fulani ya Wahindi wekundu nao walikuwa wakiendesha utandawazi wa aina yao hadi walipovamiwa na Waingereza na Wazungu wengine wakati utandawazi unaoitwa ukoloni ulipoingia duniani. Wavamizi hao katika karne ya 17 leo ndio wanaoitwa Wamarekani.

  Hawa ni mchanganyiko wa Wazungu mbalimbali waliokimbia njaa Ulaya na kwenda kuishi Marekani ambako ilibidi wawaangamize Wahindi wekundu ili utandawazi wa Ulaya ufanikishe kile ulichokifuata huko bara la Wahindi wekundu.

  Cha ajabu ni kuwa siku ya siku ilikuja fika na hao Wamarekani wapya wakachoshwa na utandawazi wa Uingereza na mfalme wake. Wakaasi. Wakapigana vita na Mwingereza. Wakashinda. Wakawa huru. Na uhuru kwao ikawa ni kuanza kujenga utandawazi wao wenyewe kwa kila aina ya hila na uzaini ambao ulichangia na unaendelea kuchangia kuiweka dunia katika hatari hii au ile kila kukicha.

  Marekani isije kusahaulika wakati fulani nayo ilikuwa koloni la Uingereza pia. Kilichotokea kati ya Marekani na Uingereza hadi huyo wa mwanzo kutangaza vita dhidi ya Waingereza ni utandawazi ulioelekea kunufaisha upande mmoja kwa kushirkiana na vibaraka wachache upande wa pili.

  Kwa mantiki hiyo hiyo, kinachotokea hivi sasa ni kuwa Marekani na Ulaya kwa upande mmoja zinanufaika na utajiri wa asili na akili za Waafrika wakati Waafrika wenyewe wanafaidika kidogo mno na rasilimali hizo.

  Marekani, Ulaya na nchi nyingine tajiri zimekula njama ya kuwatumia watu wachache katika nchi mbalimbali za kiafrika kuhamisha utajiri wetu kwenda kuwanufaisha wazungu wakati Mwafrika kwa mujibu wa ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Bw. Kofi Annan sasa iko taabani kuliko ilivyokuwa miaka 40 iliyopita.
   
Loading...