Usinikimbie mume wangu

Usinikimbie mume wangu

Robert Heriel Mtibeli

Platinum Member
Joined
Mar 24, 2018
Posts
40,330
Reaction score
93,413
USINIKIMBIE MUME WANGU.

Na, Robert Heriel

Kadiri siku zilivyokuwa zinasonga ndivyo matumaini yalivyokuwa yanazidi kupotea. Zile ndoto alizokuwa anaziota akiwa Kigoli wa miaka ishirini ziligeuka ukungu katika wakati wa kiangazi. Alikumbuka kipindi akiwa chuo wakati akichukua shahada yake wa kwanza ya usimamizi wa fedha, jinsi alivyoona maisha yake yatakavyokuwa mazuri. Alijua ni kitambo kidogo atakapomaliza chuo angeingia katika maisha ya kushika mabulungutu ya pesa. Lakini kilichotokea Mungu ndiye anajua.

Alijua mpango wa mume wake kutaka kumkimbia baada ya kupewa taarifa na shemeji yake ambaye ni rafiki ya mume wake. Taarifa hiyo ilimuumiza sana. Alifikiri atawezaje kuwalea watoto wake ambao bado walikuwa ni wadogo. Atawezaje kuwalipia ada na kulipa kodi ya nyumba waliyopanga. Hayo yalimfanya ahisi presha ikipanda.

Aliwatazama watoto wake waliokuwa wakicheza mchezo wa NAGE katika ukumbi wa nyumba ile. Alitamani kuwaona siku moja wakiwa na maisha mazuri. Alitamani kuwaona wakienda shule zenye kutoa elimu bora lakini ndio hivyo tena hakuwa na pesa za kuwapeleka katika shule hizo zaidi ya kuwapeleka shule za serikali ambazo zilikuwa na changamoto nyingi zikiwemo ukosefu wa vitabu, waalimu wa kutosha hasa hasa wa masomo ya sayansi, ukosefu wa maabara na maktaba. Looh! Umasikini ni kazi sana.

Jioni Mumewe alirudi kutoka katika mihangaiko yake akiwa kabeba mfuko wenye nyanya, samaki na mchele. Sura yake ilionyesha dalili za kuchoka na kukata tamaa. Macho yake yaliiashiria kuwa hata alichokibeba alikuwa amekopa ilimradi tu familia isilale njaa. Aljibwaga kwenye kochi kuu kuu pwaaa! na kushusha pumzi mithili ya Kobe mzee.

Alimsihi mke wake na watoto wamuache apumzike kwani alikuwa amechoka sana. Alipitiwa na usingizi na baada ya kitambo kidogo aliamshwa kwa ajili ya chakula cha jioni.
Siku ilikuwa imeisha na muda wa kulala ulikuwa umefika.

Usiku wa manane mume aliamka, alimtazama mke wake ambaye alikuwa yupo fofofo kwa usingizi. Alizishika shika nyuzi za macho yake huku kimoyo moyo akisema; Nisamehe Mama Coletha, sina jinsi acha niende.

Maneno hayo yalimfanya atoe machozi mazito ya huzuni yalioulowanisha uso wake. Alichukua begi lake na kwenda chumba cha watoto ambapo aliwakuta wakiwa wamelala kwa kukumbatiana kwa upendo. Aliwakaribia na kuwabusu kila mmoja katika mapaji ya nyuso zao. Alijihis maumivu makali kuwaacha watoto wake aliokuwa akiwapenda. Kuna muda alitaka aghairi lakini hiyari ilimshinda. Aliwafunika vizuri na shuka na kisha akapiga ishara ya msalaba na kuondoka.

Mama Coletha alizinduka kama nusu saa baada ya mume wake kuondoka. Alianza kwa kuita, akaenda chumba cha watoto na kutoka nje kuona kama kama mume wake huenda alikuwa ametoka uwani lakini hakumuona. Alirudi chumbani akiwa analia sana. Usiku wote ulikuwa ni wa kilio. Alijifuta machozi na mashuka mpaka yakalowana tepe tepe. Hakujua atawalisha nini wanawe kesho yake kutokana na sababu kuwa nyumba haikuwa na chakula wala pesa.

Baba Coletha alipanda gari linaloelekea mjini. Alifungua begi lake ambapo ndani yake aliweka pesa ya nauli. Alishangaa kuona mabadiliko katika pesa zake. Pesa zilikuwa zimefungwa na karatasi tofauti na alivyoziweka yeye. Aliifungua ile karatasi na kuona maandishi yaliyosomeka hivi:

USINIKIMBIE MUME WANGU

Habari mume wangu mpenzi!
Nimesikitika kwa hatua uliyochukua lakini nitajiona nisiye na thamani endapo utaisoma barua hii alafu usirudi nyumbani.

Mume wangu, tambua wewe ndiwe mwanaume niliyeapa kuishi naye katika shida na raha. Mwanaume niliyeitunza bikra
yangu kwa ajili yako. Mwanaume niliyeamua kukuzalia watoto. Mwanaume ambaye sikujali hali yako ya umasikini nikakukubali jinsi ulivyo. Mume wangu rudi bado nakuhitaji mpenzi.

Rudi tulee watoto wetu pamoja. Wanahitaji malezi ya mama na Baba. Mimi na watoto tunakupenda mume wangu. Hatujali umasikini wetu bali utu na mapenzi yetu ndio muhimu Mume wangu.

Popote utakapoenda nitakufuata, sitajali taabu na shida mume wangu. Utakapozikwa nami ndipo nitazikwa. Nimeamua kuishi na wewe mpaka kifo kitutenganishe na wala si umasikini, wala si maradhi, na wala si njaa. Rudi mume wangu usinikimbie mkeo.

Mbona Ibrahimu aliondoka na mkewe Sarah baada ya nchi yao kukumbwa na njaa. Yeye hakumuacha mke wake bali aliondoka naye. Nami nataka twende wote. Njaa isiwe sababu ya kunikimbia Mume wangu.

Ni matumaini yangu moyo wangu utaulinda na utarudi nyumbani. Usije nishusha ardhini kwa huzuni na kihoro Mume wangu. Nakupenda sana mume wangu.

Wako akupendaye.
Mama Coletha.
+++++++

Maneno ya barua hiyo yalimchoma sana Baba Coletha. Alipiga makelele kama kichaa; Dereva simamisha gari nishuke.
Watu walimshangaa wakati huo tayari alikuwa amesimama anaelekea ulipo mlango wakutokea. Uso wote ulijawa na machozi huku kifua kikienda mbele na kurudi nyuma kutokana na mapigo ya moyo kudunda kwa kasi.

Alirudi nyumbani yapata saa tatu asubuhi, aliwakuta watoto waliokuwa na njaa. Watoto walimuuliza kuwa alienda wapi akabaki kuwatumbulia macho asijue awajibu vipi.
"Mama kaenda wapi?"
"Ameenda dukani"
Kabla hajamaliza kujibu Mama Coletha alitokea akiwa kabeba mfuko wenye sambusa. Alimkimbilia mume wake na kumkumbatia.

"Usinikimbie Mume wangu, nakupenda sana Baba Coletha"
Yalikuwa maneno mazito yaliyomtoka mama Coletha akiwa amekumbatiana kwa nguvu na mume wake kipenzi. Watoto walikuwa wamesimama wakishangaa tukio hilo la kupendeza.

Sauti ya chai inayochemka jikoni inasikika, Mama Coletha anaenda kuzima Moto na mwisho kuna kuwa kimya chenye Faraja.

Niite Taikon wa Fasihi.

Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
 
Kadiri siku zilivyokuwa zinasonga ndivyo matumaini yalivyokuwa yanazidi kupotea. Zile ndoto alizokuwa anaziota akiwa Kigoli wa miaka ishirini ziligeuka ukungu katika wakati wa kiangazi.

Ni kiangazi cha eneo gani juu ya uso wa nchi, kinachoambatana na ukungu?

ROBERT HERIEL aka taikon wa fasihi, hebu nitanzulie huu utata tafadhali
 
Back
Top Bottom