MpendaNchi1
Member
- Sep 25, 2021
- 7
- 4
Nianze tahadhari hii fupi kwa misemo ya kifalsafa ili kuwapa mwaliko wa kufikiri kizazi cha “hi inakuwaje”, “ni aje”, “wari”, “ugari”, “lisaa limoja”, “Arsenal imepata matokeo” (yepi, chanya au hasi?) “Pacome na Chama wamepata majeruhi” (badala ya majeraha). Kizazi kinachozungumza lugha chambilecho, marehemu Sudi Andanenga, sauti ya kiza, lugha "Inayotobangwa" kiasi cha kuishiwa hamu ya kuisikiliza. Mahala pa “L” inawekwa “R” na kinyume chake. Nakadhalika, nakadhalika.
Kizazi kinachoshinda mitandaoni kutukana, kujitukana, kushindana katika utovu wa adabu na nidhamu, kuvunja heshima za watu na zao wenyewe kwa makusudi au bila kujitambua. Kizazi kisichojua siri, lipi la kusemwa wapi, la hadharani lisemwe au litamkwe vipi. Kizazi kisichojua staha ya lugha wala stara ya mavazi na haiba. Kizazi kilichopotoka kwenye usanii na sanaa, kuwehuka kisiasa na uhayawani wa kijamii. Kizazi kisichojua kumbi na mkole. Kizazi chenye ufaulu mkubwa darasani, alama sifuri mitaani.
Mwanafalsafa wa Kigiriki, Aristotle, alisema: “Kwa vigezo vyote vya sanaa, jambo liwezekanalo lakini lisilo na uwezekano ndilo lifaalo, kuliko lile lenye uwezekano lakini lisilowezekana.” Mwanafalsafa mwingine, Jean Paul Sartre, alisema: “Hata kuamua kutokuchagua pia ni kuchagua.” Na msemo mwingine wa kutafakari unasema: “Leo ni jana ya kesho.” Ni misemo ya kifalsafa yenye kufikirisha. Ni misemo inayojenga jengo la ufikiri lenye madirisha na milango ya vifikirishi.
Tanzania imepata fursa kubwa kupitia mitandao ya kijamii, ambapo sauti ya vijana inasikika haraka zaidi kuliko hapo awali.
Hii ni hatua chanya kwa demokrasia, kwa sababu kizazi kipya sasa kinashiriki moja kwa moja katika majadiliano ya kitaifa. Lakini pamoja na fursa hiyo, kuna ishara zinazoonyesha kupungua kwa ubora wa mijadala yetu ya hadharani.
Baadhi ya vijana wanaoposti kuhusu siasa, posts zao haziakisi uwezo wa kufikiri wala kutafakari, sikwambii tafakuri jadidi au tunduizi. Bali huonekana kukimbia kutoa hukumu hasi dhidi ya matukio, mitazamo, hali na kauli wasizokubaliana nazo, au kushawishika na saikolojia ya magenge. Hawako tayari kusoma kwa umakini au kuelewa muktadha wa jambo.
Matokeo yake ni maandishi yanayorudia hoja za wengine, fujo na kelele mitandaoni, na tuhuma na shutuma zinazokosa ushahidi, wakati mwingine zikichochea chuki za kulazimishwa katika jamii kwa malengo binafsi au ya wale wanaowatuma.
Hali hii haileti mabadiliko, bali inaongeza mgawanyiko kati ya wananchi wenye maoni tofauti. Mojawapo ya sababu za tatizo hili ni kukosa utamaduni wa kusoma kwa kina.
Elimu ya leo inapaswa kuwapa wanafunzi nafasi ya kuchambua, kuhoji, na kujenga hoja zao wenyewe. Tunapopata kizazi kinachopita mitihani lakini hakijafundishwa kutafakari, tunapata mitandao iliyojaa kelele bila maudhui.
Ubora wa lugha pia unaathirika, kwani Kiswahili na Kiingereza vinatumika hovyo, kwa makosa ya msingi ya mtiriko, herufi, sarufi na matumizi.
Lugha ni chombo cha mawazo. Unapoandika, unatafsiri uwezo wako wa kufikiri kupitia maandiko. Ukiitumia vibaya kalamu au kidole chako, mawazo yako hayafiki kwa watu kwa ufasaha, kwa sababu unatafsiri ujinga wako kwa jamii au jumuiya.
Taifa linalotegemea viongozi wa baadaye wasioweza kuandika na kuzungumza kwa mantiki lina hatari kubwa.
Changamoto nyingine ni utamaduni wa kuposti ili kupata wahabiki na wafuasi, si ili kuelimisha.
Posti zinazochochea hisia kali zenye kejeli na matusi hupata “likes” na shares zaidi kuliko zile zenye uchambuzi wa kina.
Hii inawapa vijana motisha isiyo sahihi ya kutafuta umaarufu kwa gharama ya ukweli na adabu. Mitandao si vijiwe vya udaku wala uwanja wa vita, bali ni jukwaa la kujenga uelewa na kutafuta ufumbuzi.
Tunapodhalilisha taasisi zetu hadharani, hatudhalilishi viongozi tu, bali tunaharibu taswira ya nchi yetu mbele ya dunia na jumuiya ya kimataifa.
Mataifa mengine yanatusoma kupitia tunachoandika, kwa hivyo tuoneshe kuwa tuna akili na nidhamu. Kukosoa ni haki, lakini ukosoaji bora ni ule unaolenga kuboresha, si kubomoa.
Kama kizazi, tuna wajibu wa kubadili mwelekeo huu kwa kusoma zaidi, kufikiri zaidi, na kuandika kwa heshima.
Kabla ya kubonyeza “posti”, simama kwa dakika moja ujiulize kama maneno yako yanajenga au yanabomoa. Hoja yenye nguvu haitaji matusi, inahitaji ukweli, ushahidi, na lugha safi. Tumia mitandao kama darasa lako la hadharani, ambapo unaweza kujifunza na kufundisha kwa wakati mmoja.
Kumbuka kuwa kila neno unaloandika linafuatana na jina lako na taswira ya taifa lako. Unapochagua kejeli na matusi, unapoteza nafasi ya kushawishi na kujenga uaminifu. Dunia ya kidijitali haisahau, na maandishi ya leo yanaweza kukufuatia kesho unapopata nafasi ya uongozi.
Gen Z wa Tanzania, chagueni kuwa kizazi cha hoja na sio kelele. Soma zaidi, tafakari zaidi, andika kwa heshima. Heshima kwa lugha, heshima kwa nchi, na heshima kwa nafsi yako ndio msingi wa mabadiliko unayotaka kuyaona.
Mhitimu 2025
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
Pia soma: Kizazi cha Mabadiliko si Gen Z, ni Millennials hawa ndo waliona Ahadi, Kashfa na Mfumo kwa Macho Yao