Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 38,822
- 90,227
UPWEKE NI KITANZI CHA ROHO
Na, Robert Heriel
Mheshimu sana mtu uliyenaye kwa wakati huu anayekufanya ufurahi, anayekufanya ucheke, anayefanya moyo wako uwe na amani. Mtu huyo mlinde na kumtunza, mthamini na kumpenda kuliko jambo lolote lile. Mtu huyo ni zaidi ya fedha.
Mtu yeyote yule anayekupa muda wake bila malipo, mkakaa, mkapiga stori, mkaenda na kurudi huku na huko, anayekupa kampani mkiyafurahia maisha mkiwa wote, pia mkiyapitia magumu mkiwa wote, huyo mpende sana.
Wala usimchezee, wala kumdharau, wala kumpuuza. Mtu huyo ni muhimu kuliko jambo lolote lile.
Hapa Duniani, Hakuna jambo la maana na muhimu kama kampani, kampani ndio kila kitu katika maisha. Maisha bila kampani hayana maana yoyote ile. Maisha ni kampani.
Kampani ya kwanza ni Familia, Yaani Mume, Mke na baadaye watoto. Ila kampani kuu ni Mume na Mke. Hakuna kampani zaidi ya hiyo katika dunia hii. Mtu yeyote anayeiharibu kampani hii anatafuta kujiharibia amani na furaha ya moyo wake. Hakuna furaha popote duniani kama furaha iliyomo baina ya mume na mke waishio kwa upendo. Hakuna raha popote zaidi ya ndoa yenye upendo, Hakuna na haitakuja kuwapo. Ndoa ndio kampani namba moja hapa duniani.
Upweke wa mwanadamu, huanza mapema zaidi pale mtu anapokosa mume au mke anayempenda. Mume na mke asiyepata upendo katika ndoa yake moyo wake hujeruhiwa na kuathirika kisaikolojia Automatiki. Na hapo bila hiyari yake, UPWEKE huanzia hapo.
Kampani ya kwanza ni Mungu, huyu ndiye rafiki namba moja, lakini rafiki huyu kwa sasa hayupo Physical hivyo hakuna ubishi kuwa kampani yake haijitoshelezi na ndio maana kwa kujua hilo akamuumba Mwanamke awe msaidizi (Kampani) wa kuishi na mwanaume. Kampani namba mbili hapa duniani ni MKE UMPENDAYE, au MUME UMPENDAYE,. Hii ndio kampani namba mbili.
Mwanamke au mwanaume anapokosa mwenza wa maisha anayempenda kivyovyote lazima awe mpweke, lazima moyo wake ukose furaha, lazima aishi maisha ya kutia huruma, kusikitisha na maisha ya uasi. Maisha bila upendo husababisha uasi. Ndoa bila upendo husababisha uasi.
Kuna watu hawajapata elimu hii, vijana wa siku hizi hutafuta maisha mazuri yenye ukwasi wakifikiri huko ndiko watapata furaha. Hakuna furaha bila mke mzuri unayempenda, hakuna furaha bila mume mzuri unayempenda, hakuna nasema, hakuna na hayatakuwapo.
Kijana huanza kujihisi mpweke hata kama anawazazi pale anapopevuka na kukomaa kimwili, kiakili na kihisia. Hapa kama ni kijana wa kiume atahitaji kuoa na kama ni mwanamke atahitaji kuolewa. Wakati huu ndio wakati muhimu kwa kijana kuwa makini kuliko nyakati zote.
Ni wakati ambao hapaswi kupuuzia kila hatua yake anayoipiga.
Huwa nasemaga, kuna mambo ya kupuuzia lakini huwezi kupuuzia moyo wako, huwezi kupuuzia upendo wako. Mtu asikudanganye, maisha ni mapenzi, maisha ni mume na mke.
Tena mume unayempenda na anayekupenda, mtu asijekukudanganya kuwa tafuta mwanaume mwenye fedha ndio utafurahi, au tafuta mwanamke mwenye matako au sura nzuri ndio utafurahi. Maisha utayafurahia ukiwa na mwanamke unayempenda.
Maisha bila mwenza unayempenda, utaishi kwa upweke mkubwa sana. Hata upewe majumba na magari yote duniani kama huna mwenza anayekupenda ni kazi bure, huna utakalolifurahia, kwani furaha uipatayo haitadumu.
Mke au mume umpendaye atakupa furaha idumuyo. Mkipendana mtafurahi daima.
Mkipendana mtashiba pasipo kula
Mtaburudika makoo yenu pasipo mvinyo
Mtacheza pasipo muziki
Mtacheka na kutabasamu hata nyakati za taabu.
Mtakumbatiana na kuvutana wakati wa taabu.
Mtapongezana wakati wengine wakiwazomea.
Mtalia wakati wa magumu kwa pamoja mkifutana machozi
Mtachuma mali na kuzitumia pamoja bila ubinafsi kwani ninyi ni wamoja.
Lakini kama hamtapendana, basi Upweke utawamaliza.
Mtaishi pamoja lakini hamtakuwa pamoja
Mtachuma mali pamoja lakini hamtatumia pamoja
Mmoja atatafuta mali zaidi na mwingine atatumia zaidi.
Mmoja atakuwa na uhalali wa kuzitumia mali kuliko mwingine.
Mtakuwa wapweke siku zote
Mtachekeana usoni lakini moyoni mnang'ong'ana
Mtafanya mapenzi lakini mmoja wenu hisia zitakuwa kwa mtu wa nje
Mmoja atatamani mwenzake afe mapema ili amuachie uhuru wa maisha
Mmoja atamuua mwenzake ili awe huru na watoto wake na hata mwenzake atakapokufa bado atabaki Mkiwa na mpweke
Mwanamke bila mwanaume ampendaye siku zote atabaki mkiwa
Mwanaume bila mwanamke ampendaye siku zote atabaki mkiwa.
Hakuna upweke kama kukosa mume/mke unayempenda.
Hakuna pigo kama kufiwa na mume/mke unayempenda. Hiyo siku itakuwa siku mbaya kabisa kuwahi kutokea, utasema ni bora angekufa Mwanao, au angekufa mzazi lakini kifo cha mwenza umpendae si lelemama.
Mke au mume sio kufa tuu, hata akuache aende kuoa au kuolewa na mtu mwingine utahisi dunia umeibeba. Mwenzi umpendaye ni kitanzi cha roho. Huyo ndio ukiwa wako siku akiondoka, huyo ndio upweke wako siku akikuacha.
Mpende sana na kumlinda mtu uliyenaye karibu, huyo akupaye raha. Mlinde sana mumeo, mpende sana Mkeo.
Hata siku moja usije ukauza furaha yako kwa wanawake wa nje, usijeiondoa furaha yako kwa mwanaume wa nje.
Mpe mumeo haki zake, mpe mkeo haki zake. Tendeaneni kwa raha siku zote wala asitokee mmoja wenu akataka kuvunja penzi lenu. Upweke unaua kuliko jambo lolote.
Asikudanganye mtu kuwa wanaume au wanawake wamejaa kuwa utaoa au kuolewa na mtu mwingine. Kama unapendwa linda penzi hilo. Mapenzi ya moyoni hayana mbadala, mapenzi haya vipuri(Spares) kwamba utabadilisha mtu mwingine.
Kupenda hakuna replacement labda kutamani.
Moyo umeumbwa kwa mtu mmoja tuu, ukishampata usilete mchezo, utakufa kwa kihoro.
Watu wazima wote watanielewa nazungumzia nini hapa. Mtu aliyeolewa au kuoa mtu asiyempenda huishi bora liende, huishi kwa mazoea tuu. Haoni umuhimu wa mkewe au mumewe.
Kosa kubwa la kuoa mke au kuolewa na mume usiyempenda utaanza kuziona mapema sana baada ya kuzaa mtoto wa kwanza. Athari zaidi utaziona ukishafikisha umri wa miaka 45. Kama ni mwanamke utakubali kuolewa na mwanaume asiyekupenda basi tegemea kuongezewa Mke miaka hiyo, Ogopa kuolewa na mwanaume anayekupenda uzuri wako, ogopa kuoa mwanamke anayekupenda kwa sababu ya U-HB wako wako pesa zako, huyo ataku-cost dakika za lalasalama.
Mwanaume ukiringia pesa zako na kuziitumia kama fimbo kumpata mwanamke unayempenda alafu yeye hakupendi basi tambua unajitengezea mazingira ya kutapeliwa pesa zako uzeeni na mali zako.
Kile unachotanguliza ndicho kitakacho kuumiza siku ya mwisho. Lakini ukitanguliza upendo hakuna maumivu.
Upweke mwingine ni kukosa wazazi, hasa Mama. Huu hujitokeza zaidi kwa mtu aliyechini ya umri wa miaka arobaini. Maisha bila Mama ni magumu sana kwa mtu aliyechini ya miaka arobaini, ila maisha bila mke au mume anayekupenda ni magumu zaidi maradufu.
Wale watu wako wa karibu wanaokupa furaha waheshimu sana. Wapende na usiwaumiza nyoyo zao.
Mpende Mkeo
Mpende Mumeo
Mlinde Mkeo
Mlinde Mumeo
Taikon Nimemaliza, mwenye swali anaweza kuuliza.
Ulikuwa nami;
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0693322300
Kwa sasa, Morogoro