[h=2][/h]JUMATANO, 14 MACHI 2012 07:27 NA KULWA MZEE, DAR ES SALAAM
SHAHIDI wa nne katika kesi ya kupinga matokeo ya ubunge, Jimbo la Segerea, Bazil Ngoholope, jana aliieleza Mahakama kuwa, kilichomsukuma kufika hapo ni kutetea maslahi ya wananchi ili wananchi waongozwe na mgombea waliyemchagua.
Ngoholope aliyasema hayo Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, alipokuwa akitoa ushahidi mbele ya Jaji, Profesa Ibrahimu Juma, huku akiongozwa na Wakili wa Mpendazoe, Peter Kibatara.
Alidai kuwa, alitaka kupinga matokeo ya udiwani wa Kata ya Vingunguti, ambako alikuwa amegombea kupitia Chadema, lakini hakufanya hivyo kwa sababu ya matatizo ya kifamilia.
Mimi nasema ukweli na Mpendazoe kasema kweli, matokeo niliyokusanya katika vituo yalionyesha tulishinda, sijui Diwani wa Vingunguti alitangazwa vipi wakati vituo saba matokeo yake hayakujumlishwa.
Matokeo ya udiwani hayakutangazwa katika kata, hali iliyowafanya wananchi kurundikana katika ofisi za kata hadi walipotawanywa kwa risasi za moto na askari polisi.
Nilijua zilikuwa risasi za moto kwa sababu nilimsikia askari mmoja nadhani ni kiongozi wao akiwaonya wasitumie risasi za moto, walimjibu wee mzee vipi, hatuwezi kuacha kutumia, wananchi hawa wengi wanaweza kufanya lolote, alidai Ngoholope.
Shahidi huyo alimaliza kutoa ushahidi wake na shahidi wa tano ambaye ni Mwangalizi wa Uchaguzi kutoka Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Christina Kanani, alipanda kizimbani kuendelea na ushahidi.
Wakati wa ushahidi wake, alidai alikuwa katika Ukumbi wa Arnatoglo, Mnazi Mmoja kwa siku tatu na matokeo yaliyokuwa yakisababisha vurugu yalikuwa ya Jimbo la Segerea, ambapo alikamatwa mama mmoja akiwa na fomu za kupigia kura za jimbo hilo na mwingine alikutwa na mihuri.
Shahidi huyo alidai kuwa, akiwa ndani katika ukumbi wa kufanyia majumuisho ya kura za ubunge na urais, hakumuona mkurugenzi wa uchaguzi akitangaza matokeo ya mgombea kwa kituo kimoja kimoja.
Matokeo yalitangazwa nje uwanjani saa nane usiku, yalikuwa ya jumla na yalitangazwa kwa dakika tano tu, alidai.
Shahidi huyo alimaliza kutoa ushahidi wake na kesi iliahirishwa hadi leo. Katika kesi hiyo, Mpendazoe anapinga matokeo yaliyompa ushindi Mbunge wa Segerea, Dk. Makongoro Mahanga.