Uongozi, ajira na kiwewe cha 'familianaizesheni'

Jesse

New Member
Nov 21, 2007
1
0
Baada ya kusoma makala ya ndugu Johnson Mbwambo (iko hapo chini) nimeona sina budi kuchangia kidogo katika mjadala huu.

Bw Mbwambo ametumia maneno ya kimzaa "undugunization" na "familianization" lakini maneno haya na uchambuzi wake una maana kubwa sana kwa nchi yetu. Tanzania imetumbukia na inaendelea kutumbukia katika janga la 'NEPOTISM'.

Japo mwandishi anaeleza kuwa utamaduni wa kurithisha watoto au wake uko katika nchi nyingine hata Marekani na kutoa hoja kuwa nchi hizo zimeweka utaratibu ambao anauita wa "check and balance", ambao humfanye anayepata madaraka hata kama ni kwa njia hiyo kuwajibika; ukifuatlia siasa za Marekani utaona kuwa Wamarekani wameeanza kuwa na wasiwasi na utamaduni huo ambao unakua kila kukicha.

Kwa mfano, sababu moja kubwa ambayo inaweza kumfanya Hillary Clinton aukose urais wa Marekani ni wasiwasi wa kile wanachoita "Bush-Clinton dynasty".

Wanasema kuwa ikiwa Bi. Clinton atachaguliwa kuwa raisi the two dynasties- the Bush and Clinton families zitaendelea kudominate siasa za Marekani kwa miaka 28 sasa, jambo ambalo wachunguzi wa kisiasa wanaona halifai na litaleta picha mbaya kwa nchi nyingine duniani hata kama Marekani inatamba kuwa ina demokrsia imara kuliko nchi zote.

Wachambuzi hao wanauliza ni kivipi Marekani inaweza kumwambia Raisi Mubarak wa Misri kuwa usiachie madaraka kwa mtoto wako bali kwa mtu mwingine, au Marekani inawezeje kuwa na sauti kwa nchi kam vile Syria, Korea Kaskazini na nyingi nyinginezo kuhusu kuachiana madaraka kama yenyewe inafanya hivyo hata kama ni kwa njia ya kura?

Kwa hiyo utaona kuwa hata Marekani pia wananchi wameshashtukia siasa za kuachaina madaraka. Kama wao ndo hivi, seuze sisi? Sasa ngoja nieleze kwanini nauungana na mwandishi kupinga mwelekeo unaojitokeza katika nchi yetu, Tanzania.

Tulipopata uhuru Serikali yetu ilifanikiwa kuondoa umwinyi, uchifu n.k ambao nauita "dynasticism" na kujaribu kuleta dhana ya uwezo kuwa ndio kigezo au sifa ya kupata uongozi au kazi , hapa nitaita "meritocracy".

Kuanzia serikali ya awamu ya pili tunaona mambo yanaanza kubadilika. Ukiuliza kwanini ndugu wa viongozi ndio wanapata madaraka katika ofisi za Serikali kama vile Benki Kuu au sehemu zinazofanana na hizo (usisahau TRA) utaambiwa hawakuingia kwa kujuana bali kwakuwa wanasifa (merit).

Wale wanaochaguliwa kwa mfano katika Halamshauri Kuu ya CCM, au Mkutano Mkuu au katika Bunge jibu ni kuwa wamepambana katika kura sawa na wengine na wakashinda, tatizo ni nini? Ukiendelea kuuliza unaweza kuaambiwa "una wivu wa kike". (Samahani).

Wengi wa Watanzania wanaonekana kuwa 'wilfully blind', yaani wamefunga macho hawataki kuuliza mbona watoto, wake, na ndugu wa viongozi kwa ujumla wameanza kujipenyeza katika siasa? Wanasiasa ni wajanja sana, walianzia katika kuwapa watoto wao nafasi katika ofisi zenye maslahi.

Wakaona hakuna mtu anapiga kelele, hakuna mtu anafanya utafiti kujua au kujiuliza kwanini wako huko. Sasa wameamua kujitokeza wazi wazi na kuanza kuwaambia watoto wao au wake zao 'ukigombea nafasi fulani utapata maana nitakupigia debe'.

Na hata wakati mwingine kupiga debe hakuhitajiki kwakuwa JINA linaonekana. Mpiga kura hana kujiuliza kuwa huyu ni nani tena maana jina linajionyesha. Sana sana mpiga kura atauliza 'hivi huyu' ni mke wake, au dada yake au mtoto wake nk.

Akipata jibu kama alikuwa hamjui kuwa ni nani yake anadondosha kura yake kuonyesha support yake kwa rais, au waziri mkuu au waziri. Hili ni gonjwa ambalo limeanza kuitafuna nchi yetu. Ngoja tujiulize kidogo, ni Watanzania wangapi wanaochagua mtu ambaye hawajawahi kumsikia?

Kwa mfano, professor mmoja ajitokeze pale mlimani aseme anagombea nafasi ya Udiwani kata ya Manzese, au Tandale au hata Ubungo. Kama alikuwa ni mwanachama tu ambae alikuwa hajulikani na watu hata kama angekuwa na sera nzuri na mikakati gani hawezi kuchaguliwa.

Mara nyingi ndivyo siasa zinavyokwenda nchi yoyote ile. Pamoja na mikakati yako na mipango na uwezo mkubwa ulio nao, huwezi kuchaguliwa kama hujulikani.

Hapa nataka kueleza kuwa zana ya "Meritocracy" ambao viongozi wetu wanataka kujikinga nayo wanapowaweka watoto na ndugu zao katika nafasi haina msingi wowote ule.

Uzoefu unaonyesha kuwa mtu anayefahamika aidha yeye mwenyewe au kupitia kwa baba yake, mama yake, dada yake, babu yake au lololte linaloishia na 'yake' anakuwa na nafasi kubwa ya kushinda.

Hii haiwezi kutafsiriwa kuwa mtu huyo amecahguliwa kwa sifa, hata kama kweli anazo sifa bali atakuwa amechaguliwa kwa kujulikana.

Sasa mwananchi wa kawaida ambae hajulikani lakini anao uwezo mkubwa kumshinda huyo anayejulikana atapataje nafasi?

Nchi zote duniani uzoefu unaonyesha kuwa watu hupenda kuchagua kile wanachokijua au walichowahi kukiona. Watu huvutiwa na "brand names", sio kwasababu wanaamini kuwa mtu huyo ni bora ila kwakuwa wamezoea hilo jina. Wanaweza kukataa tu ikiwa wanazo sababu kubwa sana ambazo zinawafanya wampinge mtu huyo.

Na hii inatokea hasa katika nchi ambazo ufahamu na ufuatiliaji wa uendeshaji wa nchi ni mkubwa kwa wananchi walio wengi. Haiingii akilini kusema kuwa mtoto au mke wa raisi, hasa katika nchi zenye demokrasia changa kama yetu, amechaguliwa katika nafasi ya ungozi kwakuwa ana uwezo.

Kwanini hakugombea kabla? Jibu ni rahisi. Anajua kuwa kwa kutumia jina la baba yake au mke wake au mume wake atachaguliwa tu. Labda tutoe mfano mwingine hapa.

Gavana wa Benki anateuliwa na raisi. Mtoto wa rais au wa waziri mkuu au kiongozi mkubwa wa serikali anakuja kuomba kazi unategemea Gavana atamkatalia kuwa hana vigezo hata kama hakuja na memo? Lazima atamchukua kwakuwa na yeye anataka kulinda kazi yake.

Anataka kumfurahisha bosi wake. Sasa ikiwa huyo mwomba kazi kaja na kimemo au Gavana kapigiwa simu kabla kijana hajafika, hapo ndio panakuwa pabaya zaidi. Mimi huwa siamini kuwa kelele zinazopigwa na viongozi wetu kuwa rushwa ni adui zina maana yoyote.

Mifano tuliyoiona hapo juu yote ni ya rushwa iliyojificha. Kama Gavana au Mkurugenzi wa TRA amemuajiri mtoto wa mkubwa kutokana na kujuana "nepotism", unategemea ataogopa kula rushwa? Nani atamkemea? Gurudumu linaendelea kuzunguka pale pale.

Kama nchi yetu itaendelea kukumbatia tabia ya 'nepotism' bila kuikemea na kujifanya kuwa hao ndugu wa wakubwa wana uwezo tutaishia katika dimbwi la usultani, umwinyi, uchifu na kuendelea kulindana hata pale ambapo kosa la jinai limefanyika.

Rais atawezaje kumkemea rafiki yake ambaye amwemweka katika nafasi? Rafiki huyo atawaheshimuje na kuwajibika kwa wananchi ambao anajua hawana mchango wowote kupata nafasi aliyonayo?

Mtoto wa maskini mwenye uwezo lini atapata nafasi sawa ya kushiriki katika kuleta mabadiliko katika nchi yake? Ndio maana utaona wananchi wengi wameanza kukata tamaa ya kuleta mabadiliko maana wanaonana kuwa wigo amabao serikali yao na chama kinachoongoza imeshaujenga ni mkubwa sana kiasi kwamba haupenyeki tena.

Kwahiyo aidha wanaamua kujishughulisha na mambo yao wenyewe ambayo hata hivyo hayawezi kuwafikisha mbali maana 'sera za nchi' zitaendelea kuwaandama popote na kwa lolote wanalofanya au wengine wameamua na wao kujaribu kujitumbukiza katika kinyang'anyiro cha siasa ndani ya chama mama na kujaribu 'bahati' yao, wakiamini ule msemo usemao "kama huwezi kumshinda adui yako ungana nae".

Tukifikia hapo nchi itakuwa imekwisha na tutaendelea kuwa watumwa wa nchi nyingine ambazo zimepiga hatua kubwa ya maendeleo.

Nimalizie kwa tahadahari ambayo wachambuzi wa siasa za Marekani wanaitoa hasa katika kampeni zinzoendelea kuwa "America people need to pray for a 'Great Awakening' because another 4 or 8 years of the Bush-Clinton dynasty might turn this once- great constitutional republic into just another banana republic".

Kama wenzetu wameanza kuchukua tahadhari hii japo wanao mfumo mzuri wa ku-control viongozi wao, je sisi watanzania ambao tunaweza kubadili katiba kila kukicha endapo serikali inataka kufanya hivyo? Inabidi tujifunze.Uongozi, ajira na kiwewe cha 'familianaizesheni'

Johnson Mbwambo Novemba 14, 2007

KATIKA toleo lililopita nilijaribu kueleza jinsi ambavyo Watanzania hatujabadilika kifikra, kitabia na kimaadili miaka 46 baada ya Uhuru.

Nilieleza jinsi ambavyo tumeruhusu matatizo yale yale ya miaka ya mwanzo ya Uhuru, tuliyopigana nayo tukayashinda, kurudi tena miaka 46 baadaye na kuitafuna nchi yetu. Leo, napenda kuuendeleza mjadala huo kwa kukita katika moja ya matatizo hayo ya miaka ya 60 ambalo tulilishinda lakini sasa limerudi kwa kishindo - tatizo la ndugunaizesheni au familianaizesheni katika ajira na uongozi.

Wiki iliyopita Chama cha Mapinduzi (CCM) kilikamilisha uchaguzi wake mkuu mjini Dodoma. Hebu soma majina haya ya baadhi ya waliochaguliwa kuingia NEC, na kisha jiulize iwapo yanaashiria kitu chochote? Margaret Sitta, Anna Malecela, Zainab Kawawa, Violet Mzindakaya, Nape Nnauye, Adam Malima, Dk. Hussein Mwinyi.

Kama bado hujaipata picha ninayojaribu kuichora; ongeza majina hayo na yale ya wabunge kadhaa kama vile Rosemary Nyerere, Emmanuel Nchimbi, Janet Kahama, Asha Kigoda na Abdallah Kigoda.

Na kama bado picha hujaipata, ongeza majina ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM ya Makongoro Nyerere, Ridhiwan Kikwete na Salma Kikwete.

Bila shaka picha umeipata! Majina haya yanaashiria kitu kimoja; nacho ni kwamba linapokuja suala la uongozi wa kisiasa; na hasa ndani ya CCM, sasa, tumo kwenye zama za familianaizesheni!

Yaani, tumefika pahala ambapo tuna Spika anayeitwa Samwel Sitta anayeongoza kikao cha Bunge ambacho huhudhuriwa pia na mkewe anayeitwa Margaret Sitta ambaye naye ni waziri na mbunge.

Tumefika pahala ambapo (kwa mfano) kaka na dada - Abdallah Kigoda na Asha Kigoda wote wanaketi katika bunge hilo hilo moja. Lakini pia tumefika pahala ambapo mama na mwana - Ridhiwan Kikwete na Salma Kikwete wote ni wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho hicho kimoja!

Tumefika pahala ambapo U-First Lady pekee hautoshi na unabidi kuongezewa nguvu na ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM. Nalo pia hilo halitoshi na inabidi mtoto naye aingizwe humo akiwa mjumbe wa NEC !

Wako Watanzania kadhaa waliopata kuhoji busara ya Ridhiwan Kikwete kuwania ujumbe wa NEC miezi michache tu baada ya baba yake kuwa Rais. Walihoji iwapo, ghafla, mtoto huyo wa Rais 'aligundua' siasa na ghafla akatamani kuwa mjumbe wa NEC au iwapo 'ugunduzi' huo aliufanya baada ya baba yake kuwa Rais na Mwenyekiti wa CCM!

Watanzania hao, hata hivyo, walijibiwa haraka na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kwamba hawana hoja na akawauliza: "Mnashangaa vipi mtoto wa dereva kuwa dereva?"

Kwa mantiki ya Makamba, hata sisi tuliozaliwa na baba na mama ambao ni wakulima (peasants na sio farmers!) tulipaswa kuishia kuwa wakulima.

Lakini Makamba hatarajiwi kusema vinginevyo; kwa sababu hata yeye mwenyewe alijaribu kumsukuma binti yake kugombea uongozi wa CCM mkoa wa Tanga, lakini akajitoa dakika za mwsisho. Nina hakika nia ya Makamba kumwona binti yake anaingia ndani ya duara la viongozi wa CCM bado iko pale pale.

Ni muhimu kulijadili suala hili la familianaizesheni katika uongozi kwa mapana na marefu. Swali la kujiuliza ni je: Haya ni maendeleo ya kujivunia katika uongozi wa kisiasa au ni kitu kinachoashiria kasoro fulani itakayoleta matatizo huko mbele ya safari?

Swali hili ni gumu na halina jibu jepesi. Ni gumu kwa sababu ndani ya orodha hiyo wako ambao kupanda kwao chati haraka katika uongozi wa kisiasa ni stahili yao (merit), lakini ni dhahiri wengine 'wamebebwa' na uzito wa majina ya familia zao katika siasa za Tanzania.

Nimetoa mfano wa fani ya siasa tu, lakini ukweli ni kwamba tatizo hili la familianaizesheni lipo pia katika nyanja nyingine za uongozi.

Kwa hakika, tatizo hili limeanza, kidogo kidogo, kuota mizizi nchini. Lilianzia ngazi za juu na lilipokubalika huko likaanza kushuka ngazi za chini hadi kwenye uongozi wa ngazi za vijiji.

Ni saratani inayotafuna nchi yetu kidogo kidogo, na sote tunaonekana kuinyamazia kwa kuliona jambo hilo kuwa ni la kawaida.

Ukilizungumzia suala hili kwa baadhi ya watu, watakupa mfano wa Marekani ambako kuna koo za watawala za kina Bush na kina Kennedy.

Watakupa mfano hata wa Bill Clinton na Hillary Clinton au wa Indira Gandhi na Rajiv Gandhi.
Lakini tujiulize: Je mfumo wetu wa utawala umeimarika kiasi cha kukumbatia tamaduni hizo za nje? Je, tuna mfumo madhubuti wa check and balances kama wa wenzetu hao?

Je, uadilifu wetu katika uongozi unafikia wa hao wenzetu? Mimi nadhani, kidemokrasia, tunatofautiana mno na wenzetu hao kiasi kwamba hatuwezi kuziiga moja kwa moja baadhi ya taratibu zao, na bado zisituletee matatizo.

Kwa mfano, kiongozi Marekani akipatikana na hatia ya kukwepa kodi anaweza hata kujitia kitanzi kwa aibu. Kwa hakika, mwanzoni mwa mwaka huu kuna waziri mmoja Japan alijiua baada ya kupatikana na hatia ya ufisadi.

Hapa kwetu kujiuzulu wadhifa kwa kosa kama hilo ni shida; achilia mbali kujiua. Hapa kwetu mkwepa kodi anaonekana ni shujaa, na wakati mwingine anapewa hata uongozi wa kisiasa; wakati kwa wenzetu anachukuliwa kama msaliti mkubwa.

Kwa hiyo tusipuuze tu haraka hoja hii ya familianaizesheni ya uongozi kwa kutoa tu mifano hiyo ya nje.
Hii ni saratani itakayofikisha nchi yetu pabaya; maana tayari tumekwisha kufika mahali ambapo mtu akishakupata uongozi, basi, atafanya juu chini kumsaidia mwanawe, mpwawe, mume, mke, dada, mjomba, shangazi au binamu, kupata ajira mahali ambako yeye ni bosi.

Na kama yeye ni kiongozi katika fani ya siasa; vivyo hivyo atahakikisha 'anamsukuma' mbele mwanawe, mpwawe, mume, mke, dada, mjomba, shangazi au binamu, ili naye hatimaye aingie katika duara la viongozi wa siasa, si hoja ni ngazi ya kijiji, wilaya, mkoa au taifa.

Na matokeo ya familianaizesheni hii ni picha hiyo niliyojaribu kuichora mwanzoni kabisa ambapo mtu na mkewe wanaweza wote kuketi katika baraza moja la mawaziri au katika bunge moja au katika NEC moja, na mara nyingine wanaweza hata kujikuta wameketi katika kamati moja au bodi moja.

Kwa wenye merit tatizo si kubwa, japo dhana hii nayo ina utata kama nitakavyojaribu kueleza baadaye. Lakini tatizo hasa lipo kwa hao 'wanaosukumwa' au 'kubebwa' na mwanafamilia au wanafamilia, kwa kuwa tu wao ni viongozi na wana majina mazito. Hili ni jambo lenye hatari kubwa zaidi katika maendeleo ya nchi.

Imefika mahali ambapo ukichaguliwa kuwa meneja wa mradi fulani kijijini, basi, bila haya, utahakikisha unamweka mwanao kuwa mweka hazina; hata kama hana ujuzi wala uzoefu wa kazi hiyo.

Ukichaguliwa na wanakijiji wenzako kuwa mgawa-maji mkuu wa kijiji, kwa sababu labda zamani ulipata kuwa ofisa wa maji wa wilaya, basi, bila haya, utamteua kaka yako kuwa mgawa-maji mkuu msaidizi japo sifa yake kubwa kijijini ni ufundi baiskeli!

Picha ni hiyo hiyo ngazi ya wilaya, mkoa na taifa. Ukiteuliwa kuwa waziri au ukiwa na wadhifa wowote mkubwa ndani ya chama tawala cha CCM, basi, bila haya, utahakikisha mwanao anaajiriwa katika mashirika makubwa yanayolipa mishahara minono kama vile Benki Kuu ya Tanzania.

Nimeambiwa (kwa mfano), tena kwa kutajiwa majina, kwamba Benki Kuu ya Tanzania ndiyo inayoongoza kwa kuajiri watoto wengi wa vigogo nchini; huku baadhi yao wakiwa hawana hata sifa au uzoefu wa kazi walizoajiriwa kuzifanya.

Ni dhahiri waathirika wakubwa wa utamaduni huu mbaya wa familianaizesheni za ajira na uongozi, ni watoto wa walalahoi na hasa wakulima vijijini.

Huko tuendako itakuwa vigumu kwa mtoto wa mkulima kuajiriwa kwenye asasi kubwa za kibiashara kama Benki Kuu, hata kama wana bongo zinazochemka kiasi gani!

Kuwa na bongo tu zinazochemka hakutatosha; kwani watahitaji pia kuwa na 'Godfather' wa kuwaunganishia ajira hizo. Na katika mazingira yetu, mtoto wa mkulima atampata wapi 'Godfather' wa kumfanyia kazi hiyo? Amezaliwa katika familia masikini na hivyo atakufa masikini!

Mwanzoni nilieleza kwamba wapo wanaoupata uongozi wa kisiasa au ajira hizo kwa merits; lakini nikagusia pia kwamba dhana hii nayo ina utata.

Ili upate uongozi (uwe wa kisiasa au wa sehemu ya kazi) sifa kubwa mbili zinazoangaliwa ni elimu na uzoefu. Sasa mtoto wa masikini atawezaje kupata sifa hizo kama mazingira yaliyopo hayamwezeshi kushindana na watoto wa wakubwa kuzipata sifa hizo mbili kubwa?

Chukua mfano huu wa mtoto wa mkulima na mtoto wa waziri. Mtoto wa waziri ana akili za wastani, lakini mtoto wa mkulima ana ubongo unaochemka kweli kweli.

Wakati mtoto wa waziri atapelekwa Uingereza au Marekani kusoma katika vyuo vikuu vya huko, mtoto wa mkulima, baba yake akijitahidi sana, ataishia sekondari ya serikali ambako kila kitu ni shida - kuanzia waalimu, vitabu, maabara na hata chakula.

Sasa inapotokea nafasi ya kazi katika Benki Kuu na wote wakaiomba nafasi hiyo, ni nani atakayechaguliwa? Bila shaka ni mtoto wa waziri - amesoma Ulaya, ana vyeti vizuri na anazungumza Kiingereza kizuri. Kwa ufupi ataipata kazi hiyo kwa merit.

Lakini je, kama mtoto wa mkulima naye angepelekwa Ulaya kusoma katika vyuo vilevile alivyosomea mwenzake, nani angeipata kazi hiyo? Bila shaka ni mtoto wa mkulima ambaye tangu mwanzo kabisa alionyesha kuwa na ubongo unaochemka.

Ninachojaribu kueleza hapa ni kwamba tusikimbilie tu kuitumia dhana hii ya merits kuhalalisha kuajiriwa au kupata uongozi kwa watoto wa vigogo, na kusahau kwamba kama mazingira yangekuwa mwafaka hata watoto wa masikini wangekuwa na merits hizo.

Ukweli ni kwamba japo baadhi yetu tunatoka katika familia za wakulima masikini vijijini, tuliweza kupata ajira za merits, kwa sababu muasisi wa Taifa hili, Mwalimu Julius Nyerere aliweka mfumo wa utawala uliozingatia na ulioheshimu dhana ya fursa sawa kwa wote; mfumo ambao hivi sasa hauzingatiwi.

Chini ya Mwalimu Nyerere tuliweza kusoma bure na kupata ajira bila kuhitaji kuwa na baba au mjomba ambaye ni kigogo serikalini au chamani.

Enzi hizo, ulichohitaji kufanya ili kusonga mbele na kutimiza ndoto yako ni juhudi tu na ubongo unaofanya kazi vizuri, basi! Leo hii, hata kama unavyo hivyo; kama huna 'Godfather' hufiki mbali. Fursa sawa kwa wote ni dhana iliyokufa na Nyerere!

Lakini kinachosikitisha zaidi ni kwamba magwiji hawa wanaousukuma mbele utamaduni huu wa familianaizesheni katika ajira na uongozi, wao wenyewe wasingefika hapo walipofika kama si mazingira mazuri yaliyowekwa na Mwalimu Nyerere enzi zao; mazingira yaliyotoa fursa sawa ya elimu kwa wote; bila kujali wewe ni mtoto wa chifu au wa tajiri.

Lakini wamemsaliti Nyerere hata kwa hilo! Nina hakika Mwalimu Nyerere angekuwa hai angelipigia hili kelele kama alivyofanya wakati ule wa ndugunaizesheni miaka ile ya mwanzo ya uhuru.

Tafakari.

 
SLAA vs
LISSU vs
NDESAMBURO vs
MBOWE vs JOYCE MUKYA.
Hapo juu jaza mwenyewe , kosa liwe kwa Ridh1 kugombea?
 
demokrasia ilikufa maana hata wajumbe,mkiti wilaya na mkoa walikuwa na hofu maana ni jina la mtoto wa m/kiti wa chama taifa
 
alienda kinyume cha sera ya ujamaa na kujitegemea,maana familia moja kuichota hazina mamilion kwa kazi isiyo ya kusomea angali walikuwapo wengi wengine wenye sifa.hakuna division ya keki ya taifa
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom