Umuhimu wa Taasisi Imara: Tunahitaji Baraza la Taifa la Ushauri wa Kiuchumi kwa Rais

Mipangomingi

JF-Expert Member
Mar 16, 2011
2,712
2,000
Tarehe 9 Desemba 2016, Tanganyika ilitimiza miaka 55 ya Uhuru wake uliopatikana mnamo tarehe kama hiyo mwaka 1961. Aidha, miezi michache ijayo tutatimiza miaka 53 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliofanya taifa letu kuitwa TAN (Tanganyika)-ZAN(Zanzibar)-IA (Ni kibwagizo katika muundo wa lugha ya kiswahili uliotokana na lugha ya Kiarabu wajuzi wa lugha hizo wanaelewa). Katika kipindi chote hicho hadi hivi sasa, Tanzania imeuwa chini ya Marais watano katika awamu tofauti. Hata hivyo, katika kipindi cha miaka hamsini, bado nchi imo katika umaskini mkubwa tukiachwa mbali na nchi kadhaa za Asia ambazo tuliokua nao kundi moja katika miaka ya 1960. Si lengo langu kueleza historia ya taifa letu, la hasha.

Duniani kote, agenda kuu inayotawala, hata katika kuchagua viongozi ni ujenzi wa UCHUMI imara utakaotoa fursa kwa wananchi wake kujiongezea kipato na hatimaye kukidhi mahitaji yao ya kila siku pamoja na vizazi vijavyo. Nasi kama sehemu ya dunia, hatupo nyuma ya agenda hii; awamu zote tano zimetumia na zimejinadi kujenga uchumi utakaotoa fursa kwa wa Tanzania. Hata hivyo, ndoto hii haijatimia na Taifa letu limeendelea kuwa miongoni mwa mataifa masikini duniani. Miaka 55 tumeshindwa kujibu swali la kwa vipi tutaondokana na Umasikini.

Rais wa Awamu ya Kwanza, Malimu Nyerere aliwahi kusema kuwa ili tuendelee tunahitaji vitu vinne; ambavyo ni WATU, ARDHI, SIASA SAFI na UONGOZI BORA. Maendeleo ya kitafiti katika nyanja ya Uchumi hadi hivi leo, haitofautiani sana na mtizamo huu wa Nyerere juu ya mambo yanayohitajika ili tuendelee. Aidha, kujua tatizo na nyenzo zinazohitajika kutatua tatizo hilo ni hatua muhimu sana katika kutatua tatizo husika. Hata hivyo, hii si kweli kwa Taifa letu. Tumejua tatizo, tumejua nyenzo zinazohitajika ili kuondoa tatizo, tena tunazo (au kwa tusizonazo hazina gaharama kubwa kuzitengeneza) lakini hatutaki kuzitumia nyenzo hizo. Mimi binafsi nimesoma mambo haya manne toka nikiwa darasa la nne katika soma maarufu kipindi hicho SIASA.

Wadau wa masuala ya maendeleo wamekuwa wakihoji, Je, katika nchi yetu watu tunao? Jawabu Ndiyo. Je Ardhi tunayo? Jawabu ndiyo. Tena ardhi iliyosheheni kwa maana ya ukubwa, maji, milima, mabonde, mito, madini, gesi, mito, bahari, wanyama, mimea na kila kinachohitajika. Je Siasa safi tunayo? Hili swali kidogo sio jepesi, linaweza kuwa na jawabu ndiyo au siyo kuteemea na swali la Je tuna uongozi bora tunao? Siasa safi na Uongozi bora kwa pamoja yanaunda chombo muhimu kabisa katika kusimamia maendeleo nacho ni TAASISI. Maendeleo yanahitaji taasisi bora na imara. Wachumi wengi wameelezea tofauti za kimaendeleo baina ya nchi na nchi kwa kuangalia Taasisi-muundo wake, namna zinavyofanyakazi, ufanisi wake na uimara wake kwa ujumla. Nchi ikiwa na Taasisi dhaifu au mbovu, bila shaka itakuwa na uchumi dhaifu na mbovu na hatimaye maendeleo dhaifu na mabovu. Hapa ndipo peneye msingi wa mada yangu Umuhimu wa Taaisi Imara, tunahitaji Baraza la Taifa la Ushauri wa Kiuchumi kwa Rais.

Wanahistoria wa Kiuchumi wanatufundisha kuwa nchi zilizopata maendeleo ya haraka miongoni mwa zile zilizotawaliwa na nchi za Ulaya ni nchi ambazo kwa makusudi zilikuwa na Taasisi imara zilizoanzishishwa na wakoloni katika kipindi hicho. Watafiti nguli katika tasnia ya Uchumi, Acemoglu, Johnson na Robinson (AJR) katika utafiti wao waliouita ""Colonial Origins of Comparative Development" wanasema kuwa nchi ambazo wazungu hawakauthirika na vifo vilivyotokana na mardhi ya jiografia ya maeneo hayo, ziliwashawishi kuweka makazi ya kudumu na hatimaye kuanzisha taasisi imara zilizokuwa na nguvu ya kusimamia na kujenga maendeleo ya maeneo hayo. Taasisi hizi imara zimeendelea kuwa imara hadi leo na nchi hizo zimeendelea kuwa tajiri hadi leo. Katika kundi hili, zipo nchi za Marekani ya Kaskazi, Canada, Australia na New Zealand. Nchi hizi ni tajiri na zina taasisi imara hadi leo. Aidha, AJR wanaendelea kusema, nchi ambazo zilikuwa na matukio ya wakoloni kufariki kwa wingi kutokana sababu ya maradhi ya kijiografia, Wakoloni hawakuwa na mpango wa kuishi na badala yake wakaanzisha taasisi dhaifu, mbovu na nyonyaji (exploitive institutions). Katika kundi hili ndipo kuna nchi nyingi za Afrika, Asia na Marekani ya Kusini.

Tafiti hizi zinatufundisha jambo moja la msingi. SIASA yetu na UONGOZI wetu umejengeka kutokana na asili ya taasisi zilizoanzishwa na wakoloni ambazo kwa makusudi zilikuwana na nia ya kuhakikisha maeneo hayo hayaendelei na yanaendelea kuwa nyonywaji. Hivyo ili tuendelee na kwa mujibu wa Nyerere, jukumu moja kubwa tulilo nalo kama Taifa ni kujenga TAASISI imara zenye malengo tofauti na taaisisi tulizozirithi kwa wakoloni. Kitabu cha "Why Nations Fail" kilichoandikwa na Robinson na Acemoglu tena wanasisiiza juu ya umuhimu wa mfumo wa Kitaasisi katika kuleta maendeleo. Nchi za Asia, walibaini hili mapema hata muundo wa taaisi zao ni copy and paste kutoka nchi zilizoendelea; kama kuna tofauti basi ni chache sana. Japan, Korea Kusini, singapore, Taiwan, Hong Kong na Malaysia ni mfano halisi wa nchi zilizopata mafanikio baada ya kufanya mabadiliko makubwa ya muundo wa taasisi zao. Mfumo wa Taasisi za Kimagharibi umejikita katika uzalendo, bidii, utu, huruma, na kuheshimu mawazo hata ya anayeonekana mwendawazimu au fataani. Mataifa haya hayaruhusu kabisa raia kufanywa daraja la pili na mamlaka ziwe za ndani au nje; na walio katika mamlaka wamejengeka katika nidhamu ya juu sana juu ya raia wao.

Kwa walioshuhudia uongozi wa awamu ya kwanza wa Mwalimu Nyerere, hawatoshangaa neno "HAAMBILIKI". Hili neno liltumiwa na watu wakimrejea Nyerere kuwa hashauriki, hataki kusikiliza ushauri wa washauri zake. Hivyo haambiliki. Lakini kwa walioshuhudia uongozi wa awamu ya pili wa Alhaji Mwinyi, watakumbuka kuwa Alhaji Mwinyi alituhumiwa kupokea ushauri kutoka kwa "Mke wake". Mwalimu alitumia fasihi kueleza hili na wachambuzi wakatafsiri katika namna hiyo. Aidha, awamu ya Tatu ya Mzee Mkapa, kauli ilibadilika na kusema kuwa hataki kusikiliza ushauri wa wataalamu wake juu ya mambo ya Kiuchumi. Kwamba yeye ni mbabe. Miaka 10 ya Mkapa ilipita ikaja ya Kikwete. Kwa mara nyingine watanzania wakawa wanaona matumaini yao ya kiuchumi hayatimii. Lakini safari hii, sio kwamba Mzee Kikwete alikuwa haambili. La hasha, wanasema alikuwa akipotoshwa na washauri wake. Yaani washauri wake walikuwa wakimshauri vibaya. Mimi binafsi sijaweza kujua ni akina nani hao waliokuwa washauri wake? Lakini Kikwete aliwahi kunukuliwa na msemo mmoja maarufu sana, ambao mimi binafsi naukubali. Akili za mbayuwayu; akili za kuambiwa changanya na za kwako. Sijajua kwanini kiongozi huyu aliamua kuja na usemi huu hapo baadaye. Labda inawezekana ulitokana na hiyo dhana waliyoijenga wananchi kuwa alikuwa akipotoshwa na washauri wake.

Miaka 10 ya Mzee Kikwete ikapita ikaanza miaka mingine (labda 10) ya Dkt. Magufuli. Magufuli anajulikana toka mwanzo kuwa ni mtu anayependa kusimamia jambo liende hivyo hivyo kama lilivyo. Wataalam wanasema watu wa namna hiyo wana faida na hasara yake. Faida na hasara yake inategemea na vipaumbele, mipango na mikakati ya kitaifa itakoyoandaliwa, kukubalika na kupitishwa. Ikiwa mizuri na hivyo kuleta matokeo chanya, basi matokeo haya pia huwa kwa asilimi 100. Lakini pia mipango hiyo ikiwa mibovu, hasara pia inakuwa mbaya kwa asilimia 100%. Hata hivyo, uongozi (hasa wa ngazi ya juu tena wa kisiasa sio siku zote ni "by dejeure" wakati mwingine ni "by de facto". Katika hali ya kiongozi wa namna hii, utaona kwamba namna pekee ya ku-win ni kuwa na mfumo imara wa kitaasisi ulio shirikishi ambapo mipango na mikakati ya kitaifa ni shirikishi, inaandaliwa kwa ufanisi wa hali ya juu ikiwa pamoja na kuwepo kwa Taasisi imara inayomshauri Rais juu ya masuala ya Kiuchumi.

Nimesema hapo juu, UCHUMI ndiyo agenda kuu ya nchi yoyote duniani kwa watu wake. Lakini uchumi ni fani ya kitaaluma, tena ni fani tete, kwani ndiyo fani inayohusika na mgawanyo na mpangilio wa nyenzo za uzalishaji kwa ajili ya kuongeza uzalishaji, kukuza uchumi, na hatimaye kufikia maendeleo ya nchi na watu. Changamoto iliyopo hapa kama nchi ambayo nchi nyingi pia wanayo, Katiba yetu haitulazimishi kuchagua "mtendaji mkuu" na muamuzi wa mwisho wa mgawanyo na mpangilio wa njia kuu za uzalishia kuwa MCHUMI kitaaluma. Anaweza kuwa yeyote, kama inavyodhirika kwa baadhi ya viongozi wetu baadhi yao kutokuwa wachumi. Taifa la Marekani liliona mapema changamoto hii. Hivyo katika kukabiliana na Taifa lao kujiepusha na maamuzi ya Kiuchumi yanayotokana na Rais ambaye si mchumi ni kuunda Baraza la Taifa la Ushauri wa Kiuchumi kwa Rais hapo mwaka 1946. Kabla ya Baraza hili, Rais alikuwa akishauriwa na Ofisi ya Utendaji ya Rais "Executive Office of the President's of the United States".

Sisemi kwamba nchi yetu haina mfumo wa kumshauri Rais, au Marekani haikuwa na mfumo wa kumshauri Rais; hapana, sipokuwa mfumo uliopo sasa hauonyeshi ni nani kashauri nini na mshauriwa kashaurika vipi? Kwa mfumo wa Marekani, Baraza hili lina nguvu sana (very authoritative" lakini Rais au Congress hawana ulazima wa kutekeleza ushauri wa Baraza hili. Hata hivyo, utendaji kazi na weledi wa Baraza hilo, ni Mwendawazimu pekee ambaye hatatekeleza ushauri wake, hivyo "by De Facto", Baraza hili ni kama linamlazimisha Rais kufuata ushauri wao ambao unahusu masuala yote ya sera za uchumi wa ndani na wa Kimataifa ikiwa pamoja na kutoa mapendekezo ya viwango vya riba na sheria zote ambazo kwa namna moja au nyingine zitaathiri Uchumi wa Taifa hilo. Baraza hili huwa linaundwa na wajumbe watatu na ni LAZIMA wawe wachumi walioelimika katika fani hiyo. Mmoja kati ya wachumi hao anakuwa Mwenyekiti na Baraza linaundwa na timu ya wataalamu waiosheheni katika fani ya Uchumi na Takwimu. Kwa sasa Mwenyekiti wa Baraza hilo ni Profesa Jason Furman ambaye ni mhitimu wa BA, MA, PhD (Harvard) na MS kutoka Shule ya Uchumi ya London (Londo School of Economics). Wajumbe wengine ni pamoja Sandra Black (UCB, Harvard) na Jay Shambalaugh, nguli wa masuala ya uchumi mpana na wa Kimataifa kutoka chuo cha Calfornia cha mjini Berkeley (UCB).

Baraza hili pamoja na majukumu mengine huwa linaandaa taarifa ya uchumi kwa Rais iliyoshiba vema ikiambatana na ushauri nini kifanyike. Kama nilivyosema hapo juu, itakuwa ni Rais mwendawazimu ambaye labda ni mhitimu wa Sheria (kama Obama) au shahada ya kwanza ya Uchumi (Trump) atakayeweza kupinga ushauri wa timu ya wachumi mahiri watatu wakisaidiwa na wataalam wengine katika fani hiyo kati ya 27-35. Kwa kuwa na Baraza hili ambalo taarifa zake nyingine zinakuwa hadharani ili watu wasome na waone, walau tungeweza kuondoa dhana zote ikiwa Rais, haambiliki, anashauriwa na mkewe, hashauriki, anadanganywa au yeye ndiyo anashauri washauri wake. Lakini pia tungekuwa tunajua ni nani hasa mbaya wetu, tofauti na sasa ambapo wanachi hatujui moja kwa moja ni nani mshauri wa Rais katika masuala ya Kiuchumi na anamshauri kwa kuegemea model ipi ya uchumi.

Napenda kumalizia kwa kusema kuwa, kama tunahitaji kujenga uchumi imara, shirikishi tunahitaji ujenzi wa TAASISI imara tukianza na Baraza la Taifa la Kumshauri Rais mambo ya Kiuchumi ( Council Economic Adivisor to the President of the United Republic of Tanzania). Tukiwa na Baraza hili bila shaka watanzania tutaacha kuwa wabashiri juu ya mfumo wa ushauri wa masuala ya kiuchumi yanachokuliwa na viongozi wetu. Unfortunately, the nature doesn't work the way that we might expect. Some of issues that happen seem like they should not, while other issues that they don't happen seem like they should. Kupanga ni kuamua, tuamue sasa kuunda taasisi makini zitakazoweza kusimamia maendeleo yetu.


 

iparamasa

JF-Expert Member
Nov 14, 2013
13,445
2,000
Katiba inasema kwamba,Rais anaweza kuomba ushauri,lakini hlazimiki kufuata ushauri wa mtu yeyote,hata umuundie Baraza la kahawa,la chair,la ushauri sijui wa nini.

Wataongea weee
Watashauri weeee

Lakini anaweza kuukataa ushauri huo na akafanya yake tu anayoyajua yeye
 

Mipangomingi

JF-Expert Member
Mar 16, 2011
2,712
2,000
Katiba inasema kwamba,Rais anaweza kuomba ushauri,lakini hlazimiki kufuata ushauri wa mtu yeyote,hata umuundie Baraza la kahawa,la chair,la ushauri sijui wa nini.

Wataongea weee
Watashauri weeee

Lakini anaweza kuukataa ushauri huo na akafanya yake tu anayoyajua yeye
Sidhani kama umeisoma makala yote ndugu iparamasa, nimetoa mfano hata Marekani walikuwa na mfumo kama huu wa kwetu lakini kuwepo kwa Baraza la namna hiyo kumesaidia wananchi kujua ni nani wa kumnyooshea kidole kwa sera mbovu za kiuchumi. Aidha, hata Marekani Rais halazimiki kukubali ushauri wa Baraza pamoja na nguvu ya kisheria iliyounda Baraza hilo, lakini muundo wake na utendaji wake, ni Rais mwendaazimu pekee ndiyo hatakubaliana na ushauri wa Baraza kwa kuwa liko "well equoped". Aidha, kuwepo kwa Baraza hilo, sio optio kwa Rais "kuomba" kushauriwa. Linamlazimisha Rais kushauriwa kwa vyovyote vile.
 

iparamasa

JF-Expert Member
Nov 14, 2013
13,445
2,000
Sidhani kama umeisoma makala yote ndugu iparamasa, nimetoa mfano hata Marekani walikuwa na mfumo kama huu wa kwetu lakini kuwepo kwa Baraza la namna hiyo kumesaidia wananchi kujua ni nani wa kumnyooshea kidole kwa sera mbovu za kiuchumi. Aidha, hata Marekani Rais halazimiki kukubali ushauri wa Baraza pamoja na nguvu ya kisheria iliyounda Baraza hilo, lakini muundo wake na utendaji wake, ni Rais mwendaazimu pekee ndiyo hatakubaliana na ushauri wa Baraza kwa kuwa liko "well equoped". Aidha, kuwepo kwa Baraza hilo, sio optio kwa Rais "kuomba" kushauriwa. Linamlazimisha Rais kushauriwa kwa vyovyote vile.
Ni wazi zuri sana.

Ni vizuri pia senior officials kama hao wasiwe wanaondolewa(kutumbuliwa)kirahisi rahisi.

Wawe na aina fulani ya kinga dhidi ya rais endapo kutatokea mgongano wa kimawazo(they must agree to disagree) katika baadhi ya mambo.

Hii itawafanya wasiwe na hofu ya kutoa ushauri wowote katika jambo la kiuchumi bila woga.

Pia ili tupate wa kumnyooshea kidole sawasawa,taasisi hii iwe inatoa taarifa yake pia bungeni,huko ndiko kuna watu ambao tumewateua wahoji mambo kwa niaba yetu.Hivyo taarifa ya waziri anayehusika na uchumi,italinganishwa na ushauri wa Baraza la ushauri la uchumi na kujua nani katuingiza chaka.

Mambo kama ya Twiga Bancorp,kodi ya miamala na mengineyo,yasingepita bila kutolewa taarifa ya kina bungeni na kujadiliwa
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom