Umma uepuke tabia ya kuchukua sheria mkononi | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Umma uepuke tabia ya kuchukua sheria mkononi

Discussion in 'Jukwaa la Sheria (The Law Forum)' started by MziziMkavu, Sep 7, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Sep 7, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,616
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Maoni ya katuni  Miongozi mwa majanga yanayoikabili taifa kwa sasa ni kuporomoka kwa maadili katika jamii; kila mahali hali ni mbaya katika kutii na kuheshimu sheria, kanuni na taratibu.
  Ni kwa msingi huo wimbi la wananchi kujichukulia sheria mkononi haliwezi kutazamwa nje ya janga hilo, kuporomoka kwa maadili. Wananchi wamekuwa na visingizio kwamba

  wanajichukulia sheria mkononi kwa madai kwamba kila wanapowakamata wahalifu na kuwafikisha vituo vya polisi, kesho yake wanakutana na watuhimiwa wao mitaani, tena wakiendesha vitendo vile vile walivyokamatwa kwavyo.

  Ukisikiliza ripoti za uhalifu za makamanda wa polisi wa mikoa yote nchini, hasa Tanzania Bara, kuhusu uhalifu kwenye maeneo yao ya utawala ni nadra sana kupita siku bila kusikia habari ya wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira kuua watuhumiwa wa uhalifu; vibaka au majambazi. Imekuwa ni kawaida!

  Kwa mfano, wiki iliyopita vituo vya televisheni nchini vilionyesha wazi mauaji ya kikatili yaliyofanywa na wakazi wa eneo la Magomeni katika bonde la Jangwani kwa kile kilichodaiwa ni kibaka ambaye amezidi kuwasumbua katika eneo lao. Taarifa zilisema kwamba wananchi hao walimkamata kijana huyo wakampiga kisha kumteketeza kwa moto; hawa wamekuwa wakiripotiwa kama wananchi wenye hasira kali.

  Jana katika ukurasa wa tano wa gazeti hili kulikuwa na habari iliyojikita katika wimbi hilo la kujichukulia sheria mkononi; askari wa kikosi cha Zima Moto katika Halmashauri ya Songea, Frick Ihagula, aliuawa na wananchi wanaodaiwa kuwa na hasira kisha kuuteketeza mwili wake kwa moto baada ya kumtuhumu kwamba ni mwizi.
  Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma alisema kwamba tukio hilo lilitokea katika mtaa wa Mjimwema, Songea na kwamba watu 12 walikuwa wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya mauaji hayo.

  Ushuhuda umetolewa na watu mbalimbali kuwa marehemu Ihagula hakuwa na tabia ya wizi, si kazini kwake wala kwenye jamii aliyokuwa akiishi, zaidi sana anadaiwa kuwa alikuwa mwalimu wa kwaya katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Mathias Kalemba la Jimbo Kuu la Songea, kwa maana hiyo aliishi kwa ushuhuda wa uadilifu.

  Ni kwa maana hiyo kuna hisia nzito kwamba kwa sababu zozote zinazoweza kutolewa juu ya kutuhumiwa kwa marehemu, kuna asilimia kubwa kwamba alishukiwa kimakosa.
  Hakuna jamii yoyote ya binadamu duniani inayojiruhusu kuishi kwa mfumo wa watu kujichukuliwa sheria mkononi na kisha ikapona; mfumo huo ni hatari, huchochea visasi, hupandikiza mifarakano lakini kibaya zaidi wengi hutumia kuwakomoa wale wenye nongwa nao.

  Tumesikia mara kadhaa wapenzi waliogombana na mwanamke kumpigia kelele za mwizi mpeziwe kwa kuwa tu wamekorofishana, wapo waliopoteza maisha kwa sababu ya chuki za namna hiyo, lakini wapo walioponea tundu la sindano kwa sababu majirani wa wapenzi hao walikuwa makini kiasi cha kutambua mtuhumiwa wa kuzushiwa.

  Tunasema bila kumungÂ’unya maneno kwamba umma kujichukua sheria mkononi hauwezi kuwa mfumo wa kujihakikishia haki hata siku moja, ni mfumo hatari ambao hakika utaangamiza jamii.
  Ndiyo maana sisi tumekuwa mstari wa mbele si tu kulaani wananchi wanaojichukulia sheria mkononi kwa sababu yoyote ile, iwe kwa kuwa polisi hawawajibiki vizuri au iwe kwa kuwa vibaka hawaishi mitaani; lakini pia tumekuwa mara zote tukisimama na kulaani hata vitendo vya polisi kujichukulia sheria mokononi pia kwa kuua watuhumiwa.

  Tumekuwa tukifanya hivyo kwa sababu tunatambua katika mfumo wa maisha wa namna hiyo si rahisi haki kutendeka, wenye nia zao ovu watazitumbukiza katika mfumo huo ili kufikia malengo yao mabaya ya kuwaadhibu wabaya wao.
  Tunaomba jamii itambue kwamba utaratibu wa kujichukulia sheria mkononi hauwezi kuvusha jamii yoyote, ni mfumo ambao mwisho wa siku utaleta maafa kwa watu wasiokuwa na hatia kama haya tulioshuhudia Songea kwa askari wa Kikosi cha Zima Moto.

  Tunahamasisha jamii kukataa hali hii, na itambue kwamba kila mtuhumiwa hata awe ni wa uhalifu wa aina gani ana haki ya kujitetea mbele ya vyombo vya sheria, kabla hajaadhibiwa na vyombo vyenye mamlaka ya kutoa adhabu.  CHANZO: NIPASHE
   
 2. pmwasyoke

  pmwasyoke JF-Expert Member

  #2
  Sep 7, 2010
  Joined: May 27, 2010
  Messages: 3,584
  Likes Received: 189
  Trophy Points: 160
  Serikali inastahili lawama kubwa kwa hili. Ni adimu kusikia imewawajibisha hao wanaochukua sheria mkononi.
   
 3. P

  Percival JF-Expert Member

  #3
  Sep 7, 2010
  Joined: Mar 23, 2010
  Messages: 2,567
  Likes Received: 617
  Trophy Points: 280
  Haya yote yanatokea sababu ya vyombo vya usalama hasa polisi kushirikiana na wezi na maharamia. Wanakula pamoja hao na wananchi wamechoka na ufisadi huu.
   
Loading...