Umeme Stieglers: Mlango wa kukia dira ya maendeleo

elivina shambuni

JF-Expert Member
May 31, 2018
461
295
1566569468847.png


DIRA ya maendeleo ya Tanzania inaelekeza kuifanya kuwa nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025. Ili kutekeleza dira hii, mkazo umewekwa katika ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo, kukuza sekta ya kilimo na uwepo wa nishati ya umeme wa uhakika ili kuwezesha kuendesha shughuli za viwandani. Moja ya miundomsingi ya maendeleo ni nishati ya na katika kutimiza azma ya kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati nguvu ya umeme ni msingi mkubwa.

Ongezeko la viwanda hapa nchini ni dhahiri linaongeza mahitaji ya nishati hiyo ili kukidhi mahitaji mapya ya uzalishaji viwandani. Safari ya ujenzi wa viwanda inaendelea ambapo wawekezaji wa ndani na n je ya nchi wanaohamasishwa kuja kuwekeza Tanzania katika nyanja mbalimbali kama viwanda vya kusindika samaki na mazao mengine ya baharini, kilimo, ufugaji, elimu na afya.

Uwekezaji una faida nyingi zikiwamo kukuza mitaji ya wawekezaji hasa wa ndani, kutoa ajira, kuongeza mapato ya taifa na kukuza uchumi kwa ujumla. Juhudi za kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda na ya uchumi wa kati haziwezi kufanikiwa ikiwa nishati ya umeme wa uhakika itakosekana. Kutokana na ukweli huu, ndiyo maana serikali ya awamu ya tano ilipokuja na mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere au mwanzoni ‘Stiegler’s Gorge’ uliopo kwenye bonde la Mto Rufiji katikati ya mikoa ya Pwani na sehemu nyingine Morogoro kila mpenda maendeleo aliunga mkono.


Mradi huo una uwezo wa kuzalisha umeme wa Megawati 2,115 ambazo zitaongeza umeme unaopatikana nchini kufikia takribani megawati 4,000. Kukamilika na kuanza kutumika mradi huo wa umeme kutatoa nafasi ya kukidhi mahitaji ya nishati ya umeme wa kutumika viwandani, katika shughuli mbalimbali za uzalishaji mali pamoja na matumizi ya majumbani.

Megawati 2,115 ni umeme mwingi ambao unazidi kuipaisha Tanzania kwa kuwa na kiwango kikubwa cha umeme nchini. Hivyo basi, kukamilika kwa mradi huu kunatoa nafasi kwa viwanda vingi kupata umeme wa uhakika na wa gharama nafuu. Viwanda vikipata umeme wa uhakika na wa gharama nafuu bidhaa zinazozalishwa viwandani zinashuka bei na kuuzwa kwa gharama nafuu na hivyo wananchi kumudu kuzinunua bidhaa zinazozalishwa viwandani.

Kukatika kwa umeme kumekuwa kikwazo cha uzalishaji wa uhakika wa bidhaa mbalimbali viwandani na pia utoaji huduma hivyo mradi wa umeme wa Julius Nyerere unakuwa tiba ya kukatikakatika kwa umeme ulioathiri shughuli za uzalishaji viwandani. Wamiliki na wawekezaji wa viwanda wanapotumia umeme mbadala kama wa jenereta katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji huduma, huingia katika hasara kutokana na kutumia fedha nyingi kwa ajili ya ununuzi wa mafuta ya kuendeshea jenereta hizo na kusababisha ongezeko la bei ya kile wanachozalisha. Kutokana na mwarobaini wa ujenzi wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere, tatizo la upungufu wa umeme na kuongezeka bei ya bidhaa mara kwa mara, kutapungua kwa asilimia kubwa.

Wawekezaji waliokuwa na hofu ya kuwekeza katika viwanda kutokana na changamoto ya nishati ya umeme wa uhakika, hawatakuwa na hofu hiyo tena mradi pindi mradi huu utakapokamilika. Kwahiyo, wawekezaji watakuwa na uhakika wa kukuza mitaji yao kwani watakuwa na uhakika wa kuzalisha bidhaa zao pasipo kutumia mitaji yao kwa nishati mbadala.

Wawekezaji watavutiwa kuwekeza Tanzania kutokana na uhakika wa kuuziwa umeme kwa gharama nafuu kutokana na uzalishai wa Megawati 2115 kutoka Mto Rufiji. Upatikanaji wa umeme wa uhakika utachochea shughuli za viwandani kufanyika kwa saa 24. Hakutakuwa na sababu ya viwanda kufanya kazi saa chache ama kufungwa kwa kukosa umeme wa uhakika na wenye kutosheleza mahitaji ya kufanya kazi mfululizo. Katika mchango wa viwanda kuchagiza ukuaji wa uchumi, wamiliki wa viwanda watalazimika kuongeza idadi ya wafanyakazi ili wakidhi mahitaji ya uzalishaji unaoweza kuhitaji watu kufanya kazi saa 24.

Wakulima wataongeza uzalishaji ili kulisha mahitaji ya viwanda kwa kutoa malighafi muhimu zinazohitajika katika uzalishaji. Vilevile, serikali itapata mapato kupitia kodi zitakazolipwa na wamiliki wa viwanda na wafanyakazi wake. Uzalishaji wa megawati 2,115 utatoa nafasi kwa serikali kuuza nishati hiyo katika nchi za jirani zikiwamo za Afrika Kusini na Mashariki zenye mahitaji ya umeme kwa ajili ya kupunguza upungufu.

Fedha zitakazopatikana kutokana na mauzo ya nishati ya umeme zitatumika katika ujenzi wa miradi mbalimbali vikiwamo viwanda vyingine. Pia fedha hizo zitasaidia kuinua sekta nyingine muhimu kama kilimo, miundombinu, elimu, afya, maji, uvuvi na ufugaji ambazo ni sekta nyeti katika kuendeleza maendeleo ya viwanda hapa nchini.

Muhimu ni mkandarasi wa mradi huu kufanya kazi kwa mujibu wa makubaliano ili mradi uweze kukamilika kwa wakati na hatimaye nchi ianze kunufaika na matunda yake hasa sekta ya viwanda. Mradi wa umeme wa Julius Nyerere ambao ni tiba mbadala wa mahitaji ya nishati ya umeme kwa maendeleo ya kiuchumi na ya kijamii unafungua milango ya kuifanya Tanzania kuwa taifa la nishati ya uhakika barani Afrika.
 
Back
Top Bottom