Ulinzi na usalama ni wajibu wa kila mwananchi

cheusimangala_

Senior Member
Dec 1, 2018
114
174
Usalama ndio msingi mkubwa wa maendeleo ya jamii katika ngazi zote, na kwa hakika hakuna jamii ambayo itajivuna kupata mwelekeo wa maendeleo kama kwao usalama haupo.

Ndio maana sasa wananchi wengi wanafahamu kuwa ili uzalishaji ufanyike kwa matumaini ya kuwa na maendeleo, lazima ulinzi wa maisha na mali zao kwa kiwango kikubwa utegemee ushiriki wao katika Ulinzi Shirikishi.

Pamoja na dhana ya kuimarisha ulinzi katika ngazi zote, na kushirikisha kila mwananchi katika nafasi yake, bado wapo wahalifu sugu ambao wanatokana na kutotii sheria kwa hiari.

Suala la baadhi ya watu kuwa sugu katika uhalifu, halina uhusiano na dhana ya polisi jamii bali ni matokeo ya kutotaka kutii sheria kwa hiari.

Zipo sheria zilizowekwa kwa mujibu wa Katiba ya nchi, sheria zinazoelekeza nini kisifanyike na wakati gani wananchi wawajibike katika utekelezaji wa maagizo ya msingi yanayotolewa kisheria.

Ni maagizo ambayo mara nyingine utakuta baadhi ya wananchi wanaamua kwa hiari yao kuvunja huku wakijua kuwa wanafanya kinyume cha sheria, hiyo ni moja ya tabia za usugu wa kutotii sheria bila shuruti.

Wakati mmoja akiwa bungeni, aliyekuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima wakati akijibu swali la Mbunge wa Ileje, Aliko Kibona wa CCM, ambaye alitaka kujua sababu za watu kuzidi kuwa sugu katika suala zima la kutotii sheria bila shuruti, Silima alisema usugu katika uhalifu ni matokeo ya kutotaka kutii sheria kwa hiari.

Kuna aina mbili za kutii sheria, moja ni kwa hiari bila shuruti, wakati njia nyingine ni kutii sheria kwa kushurutishwa, aina hii mara nyingi nguvu hulazimika kutumika ingawa pia nguvu hiyo hutegemea mazingira ya uvunjwaji wa sheria husika.

Kutii sheria kwa hiari ni kufuata taratibu zote zilizowekwa kwa mujibu wa kanuni na sheria zinazomiliki jamii, na mara zote sheria hizo ni zile zinazozingatia usalama na ustawi wa jamii.

Wakati wa kufafanua suala la umuhimu wa kuwa na dhana ya Polisi jamii, Silima alisema dhana ya Ulinzi Shirikishi ilianzia Uingereza mwaka 1629, na mwanzilishi wake alikuwa Sir Robert Peel.
Alisema dhana hiyo ilianzishwa ili kupunguza wasiwasi juu ya jamii kuhusu uhalifu na kujenga uhusiano baina ya Polisi na jamii ili kufikia malengo ya Polisi katika ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Alisisitiza kuwa suala la baadhi ya watu kuwa sugu katika uhalifu halina uhusiano na dhana nzima ya Polisi jamii, bali hayo ni matokeo ya kutotaka kutii sheria kwa hiari, na inasemekana kuwa utafiti uliofanywa ndani na nje ya nchi umeonesha kuwa matumizi ya dhana ya Polisi jamii yana matokeo yenye faida nyingi kuliko hasara.

Wajibu wa wananchi katika suala la ulinzi wao unatokana na ukweli kwamba Jeshi la Polisi bado ni dogo ukilinganisha na maeneo makubwa ya nchi hii ambako wananchi wake wametawanyika.
Polisi hawawezi kuwepo kila mahali kwa nyakati zote, matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi na mali zao hutokea mahali popote na kwa wakati wowote, kinachotakiwa kufanyika kwa faida ya wananchi wenyewe ni kutoa ushirikiano mkubwa kwa Jeshi la Polisi, kwa kufichua njama za uhalifu pamoja na kuwatambulisha wahalifu kwa polisi.

Najua hayo yote yanafanyika, lakini tahadhari ambazo zinatakiwa zichukuliwe na wananchi katika kutekeleza majukumu ya kusaidiana na Jeshi la Polisi ni kuepuka kuchukua hatua za adhabu mikononi.

Matukio mengi ya vifo kwa wananchi waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali mitaani hufanywa na wananchi wanaoaminika kuwa na hasira kali, hilo ni kutotii shetia kwa hiari, na pia hali kama hiyo haisaidii Polisi jamii badala yake huongeza jukumu la Polisi kuwa gumu zaidi.

Ni kweli wakati mwingine hawa wavunja sheria wanaochomwa moto mitaani wanakera, na kero nyingine hutokana na watuhumiwa 'kutamba' sana inapotokea wakati mwingine wanakamatwa na kupelekwa polisi, lakini mara utawakuta wameachiwa huru kwa madai ya kukosa ushahidi kwa tuhuma walizo nazo.

Watuhumiwa walioachiwa mara nyingi huanza kufanya manyanyaso kwa waliowatuhumu na kuendelea na uvunjaji wa sheria kwa kufanya makosa mengine, matokeo yake ni kwa wananchi kuamua kuvunja sheria kwa kufanya mauaji.

Silima pia aliwahi kusema kuwa ushiriki kwa jamii kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa njia mbalimbali kumechangia kudhibiti uhalifu kabla na baada ya kutendeka, aidha alisema uanzishwaji wa vikundi vya ulinzi shirikishi kwenye maeneo ya jamii, kumechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza uhalifu.

Nimeamua kuyasema hayo ili tukumbushane na pia tuweze kutambua umuhimu wa kuendelea kupambana na uhalifu, hasa katika maeneo ya makazi yetu ambako kuna vijana wengi ambao baadhi hukaa na kuzurura tu mitaani bila kazi maalum ya kufanya.

Vijana wa aina hiyo ni rahisi kushawishika kufanya uhalifu, ni wajibu wa jamii kukemea ikishirikiana na serikali za mitaa, vijana wengi ndio chimbuko la uhalifu, baadhi tunatambua waliko lakini inaonekana tunawaonea aibu kwa kuogopa kulaumiwa.

Wabwia unga na wavuta bangi tunaishi nao mitaani, lakini tunajifanya hatutambui wafanyalo, tutambue kuwa tusipoziba ufa sasa, hatima yake tutaingia gharama kubwa zaidi, tulisaidie Jeshi la Polisi kwa usalama wetu.
 
Dah hivi hamchoki kutupa majaribu ya kutoa mapovu.

Ulinzi kwa hata kwa "WATU WASIOJULIKANA" ni wajibu wa kila raia? Mbona raia wakiwataja wanaishia kuwekwa rumande na wanaishia kupotezwa (Azory Gwanda na wengine)?

Dada nakushauri ni bora ungeandika "UZI" wa Diamond Vs Kiba au wa "MENINAH" au wa mapenzi tu.

Subiri wanakuja.
 
Wabwia unga na wavuta bangi tunaishi nao mitaani, lakini tunajifanya hatutambui wafanyalo, tutambue kuwa tusipoziba ufa sasa, hatima yake tutaingia gharama kubwa zaidi, tulisaidie Jeshi la Polisi kwa usalama wetu.


Kabla hatujawaonesha hao wa mitaani mbona wale wa stendi za daladala na mabasi makubwa mmewashindwa na wanabwiya kweupeee
 
Back
Top Bottom