Ulevi ni nini, mtu afanye nini ili aache ulevi?

Gelion Kayombo

Senior Member
Feb 17, 2018
149
193
Watu wengi ni walevi siyo kwa sababu wanapenda ulevi. Ukikutana na walevi, baadhi yao utakuta wanasema “Natamani sana kuacha ulevi ila sasa kila nikijaribu kuacha nashindwa.” Watu wanaosema hivyo ujue tayari wameshakuwa watumwa wa ulevi na kwamba mara nyingi au mara kadhaa wamejaribu kuacha tabia hiyo lakini wameshindwa kuacha.

Kuwa mtumwa wa ulevi ni jambo linaloumiza sana. Nina ndugu zangu amabo ni walevi haswa, kwa hiyo ninapozungumzia kuhusu ulevi najua kwa sababu nimeishi na walevi.

Ulevi siyo tu kunywa pombe sana. Ulevi upo wa aina nyingi ingawa watu wengi wakisikia neno ulevi, wazo linalowajia kichwani ni unywaji wa pombe. Ni kawaida watu kuwa na mtazamo wa kuwa mlevi ni yule anayekunywa pombe tu kwa sababu ni mazingira na utamaduni ndiyo unafanya wawe hivyo. Siyo kosa lao na hatuwezi kuwalaumu.

"Mazingira ni muhimu kuliko urithi", Carl Menger alikuwa sahihi kabisa, kwamba mazingira ndiyo yanayomfanya awe kadri anavyo kuwa na siyo vitu unavyorithi.

Ulevi wa mapenzi (uchizi mapenzi) ni ulevi kama ulivyo ulevi mwingine wa kunywa pombe. Ni ulevi kama ulivyo ulevi mwingine kwa sababu watu hawa wote wameshindwa kudhibiti akili zao kwenye utumiaji wa vitu hivyo. Kadhalika mtu anayevuta sigara ni mlevi kama alivyo mlevi wa mapenzi na mlevi wa pombe.

Watumiaji wa madawa ya kulevya kama heroin, cocaine na bangi ni walevi sawa na walevi wengine na wote wameshindwa kudhibiti ulevi wao. Pia kuna ulevi mkubwa wa ulaji wa vyakula na unywaji wa vinywaji laini ambao watu wengi huwa hawahesabu kama ni moja ya ulevi.

Kuna ulevi wa kutumia mitandao ya kijamii au intaneti. Kuna vitu ambavyo huwezi kufanya mpaka ufanye kitu fulani. Mfano mtu hawezi kulala mpaka aingie mtandaoni kuperuzi. Wote huu ni ulevi.

Ulevi nini? Ulevi ni tabia au hali ya mtu kushindwa kukaa kwa kipindi cha muda fulani bila kutumia kitu fulani na asipotumia kitu hicho, matokeo yake ni kujisikia vibaya mpaka atumie kitu hicho. Ile hali ya kujisikia vibaya huondoka kwake kwa muda.

Kuna watu hawawezi kukaa na kumaliza wiki, mwezi na hata miezi bila kufanya mapenzi (sex). Huu ndiyo ulevi wenyewe ninaozungumzia hapa. Wengine hawawezi kukaa na kumaliza masaa, siku, wiki, mwezi na miezi bila kuvuta sigara huku wakijua au kwa kutokujua sigara wanayovuta inaenda kuharibu sehemu ya ubongo/mwili.

Kadhalika kuna watu hawawezi kukaa na kumaliza wiki hata mwezi bila kutumia vyakula kama chipsi, na vinywaji kama soda na juisi. Huu wote ni moja ya ulevi na yeyote asiyweza kukaa kwa kipindi cha muda fulani bila kutumia vitu hivi na vinginevyo ni mlevi kama walivyo walevi wengine. Wote wameshindwa kuendesha akili zao wanavyo taka wao ziende badala yake akili zao zinawaendesha wao zinavyotaka waende.

Ulevi ni kitu ambacho kinajengwa kwenye akili za watu na si kingine. Au ulevi ni tabia ambayo akili ya mtu imehifadhi kwa muda mrefu na hivyo imezoea tabia hiyo. Kwa sababu akili imezoea tabia hiyo basi kinachofanyika ni kila siku akili kutaka mtumiaji atumie kitu anachopenda.

Na kama asipotumia kitu hicho, kitu ambacho akili inapenda basi akili haitafurahia, kama akili haitafurahia, matokeo yake mtu huyo atajisikia vibaya. Kwa hiyo ulevi wa mtu upo kwenye akili yake na kama anataka kuundoa ulevi huo, mlevi atatakiwa ajue jinsi akili yake inavyofanya kazi. Pasipo kujua jinsi akili inavyo fanya kazi basi hataweza kuachana na ulevi na kujenga tabia mpya ambayo itamfanya aachane na ulevi unaomsumbua.

Akili ya binadamu ni ya tabia. Mtu akifanya jambo kwa muda fulani akili ikapenda basi akili hufanya juu chini kurasimisha jambo hilo liwe sehemu ya tabia ya mtu. Na akili ikisharasimisha jambo hilo na kuwa tabia, tabia hiyo mpya huanza kumwendesha mtu. Kwa lugha nyingine tabia ya mtu hugeuka na kuwa ulevi.

Kuna ulevi mzuri na ulevi mbaya. Kwa maelezo haya tuone sasa mtu anawezaje kuacha ulevi (addiction)?

Mtu anaweza kuacha ulevi (addiction) kwa kutofanya au kutotumia kitu ambacho kimegeuka kuwa ulevi kwake. Kwa mfano kama mtu aliyezoea kuvuta sigara kila siku, anaweza kuacha tabia ya kuvuta sigara kwa kufanya maamuzi yakuacha kuvuta sigara. Kama mtu aliyezoea kuvuta siku atakaa saa, siku na hata wiki bila kuvuta sigara atateseka. Kwa sababu akili yake haijazoea mtu kukaa kwa kipindi fulani bila kuvuta sigara, kwa hiyo akili inakuwa inakataa mtu kuacha kuvuta sigara.

Mateso yatamjia kama kiu, lakini kama mlevi ataamua kujikaza na kung'ang'ania maamuzi ya kuacha kuvuta sigara kwa kipindi cha muda fulani, tuseme miezi 2-3 akili yake itazoea hali hiyo mpya na hatateseka tena juu ya ulevi wake. Ingawa hii haimanishi kuwa tabia hiyo imefutika kwenye ubongo wake.

Tabia hiyo bado ipo, ni nguvu na uwezo wa mtu kung'ang'ania maamuzi yake ambayo alishayafanya. Na kama atakaa miezi 6 bila kutumia ulevi huo basi ataweza kujenga tabia mpya ambayo itaweza kudumu maishani mwake. Ingawa pia atahitaji kujiepusha na mazingira yatakayo mfanya arudi kwenye tabia ya ulevi.

Hivi ndivyo mtu anavyoweza kuacha tabia ya ulevi wowote ule. Mada hili (ulevi) haifungwi kwenye sehemu nilizogusia peleke bali hata maeneo mengine ambayo sijagusia.

Asante kwa kusoma chapisho hili. Imeandikwa na Gelion Kayombo.
 
Ulevi ni suala la Kisaikoloji zaidi kuacha ni hadi uJifunze zaidi mbinu za kubalance saikolojia yako.
 
Back
Top Bottom