Robert Heriel Mtibeli
JF-Expert Member
- Mar 24, 2018
- 34,072
- 79,451
UKWENI PAMOTO JAMANI, YAMENIKUTA.
Na, Robert Heriel.
Nimeanza mwaka vibaya jamani. Wapi naficha uso wangu. wapi nauliza? Kama ningejua mambo yenyewe yapo hivi walahi wabinlahi nisingepeleka pua yangu. Ona sasa. Oneni jamani yamenifika hapa(puani). Nimekuwa kama kinyago cha mpabure, aibu naona mimi Taikon wa Makanya, Looh!
Niite Taikon wa Fasihi, mchumbia wari wa dot.com.
Kwa siri kubwa niliondoka moja kwa moja kuelekea ukweni baada ya kuwasiliana na Mchumba wangu, Binti Chamdeko. Alishawaambia wazazi wake kuwa nitaenda kujitambulisha na kwa mara ya kwanza kujionyesha kuwa mimi ndio namchukua binti yao.
Basi Taikon huyo, nikapanda Mabasi yanayoelekea katika mji wanaoishi wazazi wa mchumba wangu, Chamdeko bin Kipepeo. Nikiwa ndani ya gari niliendelea kuchat na mchumba wangu huku muda mwingi akionyesha furaha yake kwangu. Tulifurahia mno chating zetu. Baada ya masaa tisa nilikuwa nimefika mji wa kikweni. Hofu nisiyoijua ilinivamia vaaapu! Looh! Nisingejiongopea jinsi nilivyokuwa na hofu, niliogopa sana asikuambie mtu.
Nikashuka ndani ya Basi pale kituoni, tayari shemeji yangu alikuja na pikipiki kunipokea. Tulisalimiana, kisha nikapanda kwenye pikipiki nikiwa na Kiroba cha mchele na kidumu cha lita tano za mafuta. Hapo hofu iliongezeka ungedhani naenda kunyongwa. Kitambo kidogo pikipiki ilisimama, tulikuwa tumeshafika. Mapigo ya moyo yalizidi kupiga, nilihisi kuchanganyikiwa. Sikumbuki ni lini niliwahi kuwa katika hali ile . Doooh! Kasheshe kweli.
Nilipokelewa kama Mfalme, vifijo na vigelegele vilisikika. Kina mama na mabinti walishangilia baada ya mimi kuingia katika mlango wa sebule wa nyumba ile. Kila mmoja alihakikisha namshika mkono wake, ilikuwa kama watu wanaonigombania waushike mkono wangu. Hapo nikajiona mtu mashuhuri mwenye kuheshimika. Nikakumbuka jinsi watu mjini wanapogombaniaga kushika mikono ya wasanii wawapo kwenye majukwaa ya kutumbuiza. Sasa nami leo mkono wangu umegeuka gombani goli hapa ukweni. Hii ilifanya hofu yangu ipungue.
Hatimaye nilikaa, na hali ilitulia kila mmoja akiwa amechukua nafasi yake. Wakwe zangu walikaa kwenye kochi moja, mashemeji, na ndugu wakubwa walikaa kwenye viti na wengine kwenye Mkeka wa Ukili. Wote macho yao yalikuwa kwangu mithili ya wacheza bao la kete. Nami nilijitahidi nisimuone yeyote ingawaje ni kama nilikuwa nawaona wote kwa pamoja.
" Karibu sana Mr. Taikon"
Kikao kilifunguliwa rasmi na sauti ya kiume.
" Mimi ni Mjomba wake na Chamdeko, naitwa RUDISHA USASA"
Alijitambulisha, kisha akawatambulisha na wote waliokuwa mule ndani ikiwa ni pamoja na Mama yake Chamdeko, Baba na mashangazi zake.
Baada ya utambulisho waliniuliza maswali ya hapa na pale ya kawaida lakini swali ambalo lilikuwa gumu lililonifanya nibabaike lilikuwa hili:
" Unajishughulisha na nini Taikon? Mtoto wetu asijelala njaa"
Anko RUDISHA USASA aliongea akiwa kama anatania akicheka lakini cheko lake halikuwa halisi. Hakika hapo niliona maruwe ruwe ungedhani nimewekewa madawa ya kulevya. Kijasho chepesi kilipenya kwenye makwapa yangu na kulowanisha kiwalo changu.
Sina kazi mimi jamani, sina makazi maalumu mimi. Yote hayo yalinifanya nisijiamini ukweni. Ilinibidi nifoji na kupiga force king ili nipate kibali cha kumuoa binti Chamdeko umbo jupita.
"Mimi nipo Mamlaka ya anga, pale Dar es Salaam. Ni mkuu wa mawasiliano. Naishi, Mikocheni B"
Nilijibu nikiikaza sauti ifanane na kile nilichokuwa nakisema. Ghafla bin vuu nilishangaa kusikia vigelele Alulululuuuuu! ikafuatiwa na makofi ya nguvu huku wanakikao wote wakionyesha uchangamfu tofauti na hapo awali. Mimi pekee yangu ndiye nilikuwa sijachangamka na niliweka uso wa taadhima na kukunja ndita za heshima kwenye paji la sura yangu.
Wakiwa wanashangilia niliona kiroba changu cha mchele na kidumu cha lita tano nilivyovileta vikipitishwa na mmoja wa vijana wa mule ndani.
Kitambo kidogo kilipita tukiwa tunazungumza, punde niliona sahani zenye vyakula zikiletwa na kuwekwa kwenye meza. Macho yangu yalisimama ilipo sahani iliyokuwa imejaa kuliko zote. Nilijiuliza mbona sahani ile ilikuwa imejaa kuliko zingine. Akili yangu ikaniambia huenda sahani ile ni Baba Mkwe. Kimoyo moyo nikasema Baba Mkwe anafukia duuuh!
Basi Dada mkubwa alianza kwa kuwatengea Baba, na Mama lakini kilichonishtua hakuichukua ile sahani iliyojaa kuliko kawaida. Hapo ikabidi nisubiri nione kijeba anayeweza kufukia msosi wote ule. Niliapa nikimjua nitamheshimu na kumsalimia shikamoo pale pale hata kama ni ukweni.
Katika hali isiyotarajiwa nilishangaa Dada mkubwa ambaye ni shemeji akiniletea kile chakula. Looh! Wakati akikileta niliwaona watu wote mule sebuleni wakinitazama usoni. Nilimtazama Baba Mkwe, yeye akasema:
" Karibu chakula Mr. Taikon"
Sikuwa na jinsi zaidi ya kupokea. Nikaanza kula huku nikipiga stori mbili tatu Ndani ya dakika tano wenzangu walishaanza kumaliza chakula. Mimi bado hata nusu sijasogeza. Mzigo ulikuwa mkubwa mno. Nilitamani nimuite Mchumba wangu Chamdeko lakini desturi haikuruhusu mpaka jioni saa kumi na moja. Kumbuka tokea nifike sijamuona Chamdeko wangu
Sahani zilianza kuondolewa mimi bado nikihangaika na chakula kisichoisha. Hatimaye yalinishinda nikasema nimeshiba. Kaul hiyo iliwafanya watu wote waonyeshe nyuso za kushangaa.
"Umeshiba kweli Mkwe?"
Baba Mkwe aliuliza.
"Ndio nimeshiba Baba, Ahsanteni sana ndugu zangu"
Nilishukuru nikikabidhi sahani.
Tulimaliza huku nikicheua kachumbari na soda. Tulipiga stori mpaka ilipohitimu kumi na moja jioni. Hapo nikaitwa nje na shemeji.
"Mr. Taikon embu kamsikilize shemeji yako"
Baba mkwe alisema, nami bila kupoteza muda nikatoka nje alipo shemeji.
"Nambie shemeji!"
Niliongea nikimkaribia.
" fresh ndugu, shukrani sana"
"Kwa lipi shemeji?"
"Kwa kuja kutupa heshima katika nyumba yetu"
"Aah! Shemeji bhana. Mimi ndio napaswa niwashukuru?
Basi wote tukacheka, lakini kicheko kiliyeyuka kama mshumaa baada ya kuona shemeji kaninyooshea shoka la kuni.
" Shemeji tusaidie kupasua kuni za jioni"
Aliongea akinikabdhi shoka. Niliduwaa, iweje mgeni apewe shoka ati apasue kuni. Hii inawezekana vipi jamani. Niliwaza moyoni. Lakini sikuwa na jinsi zaidi ya kupokea lile shoka. Nilijua huenda wananipima. Shemeji aliondoka na kurudi ndani mimi nikiwa nimebaki nimesimama na shoka mkononi.
Niligeuka upande wa nyumba lilipo dirisha lakini sikuona mtu. Nikaanza kupasua.
Paaa! Paa! Holaa. Pwaaa! Holaa. Masikini kila nilipopiga ukuni na shoka liliteleza na kuniyumbisha na kutaka kunikata. Nilipiga mashoka kumi bila bila. Nilikuwa hoi bin taabani. Jasho likinitoka tadhani nipo chumba cha kuoka mikate.
Nilichungulia dirishani kuona kama kuna mtu anayeniona. Nilishtuka kuona pazia likifungwa kumaanisha kuna watu walikuwa wakinichungulia pale dirishani. Nilijisikia aibu sana. Ile ilikuwa zaidi ya fedheha. Kama nitashindwa kupasua kuni tena ukweni ingetoa tafsiri na picha mbaya kuwa mimi sio mume bora kwa mtoto wao.
Nilianza kulipasua lile gogo kwa hasira bila akili. Ni kama nilikuwa nimewehuka. Looh! Niliishia kuchoka na kutweta kama swala aliyekoswa koswa na mamba.
Punde Mama Mkwe alitoka,
" Jamani nani amempa mgeni kazi ya kupasua kuni?"
Mama alisema kwa sauti, Mimi nilijifaraguza kumwambia wala asijali kwani hata mimi naweza kupasua kuni.
" Hapana mwanangu, embu leta hapa hilo shoka. Hawa watoto kweli wanaakili?"
Mama mkwe alichukua shoka mimi nikisogea pembeni nisijue niende ndani au nibaki pale pale nje.
Mama Mkwe alianza kupasua lile gogo. Alipiga shoka mara tatu gogo likapasuka. Looh! Nilisikia aibu sana. Mama Mkwe kanidhalilisha.
Nilijisikia vibaya sana, nilitamani nikimbie lakini vitu vyangu vilikuwa ndani. Simu, viatu na begi langu vyote vilikuwa ndani. Yaani Daah! Mwaka umeanza vibaya huu.
Basi nikaingia ndani, macho yao yakinitazama nami kwa aibu kama niliyetafsiri muangalio ule nikawa naangalia chini kama niliyefumaniwa na mke wa mtu. Nikakaa.
" Mwanangu, hivi utaweza kuishi na mwanangu kweli?"
Mzee aliongea.
"Ndio Baba, nitaweza"
"Mhh! Kwa chakula kile ulichokula utapata wapi nguvu za kutafuta pesa mwanangu? Kwa chakula kile ulichokula si utamlaza binti yangu njaa wewe? Kwa chakula kile utaweza hata kumpa haki yake ya ndoa akaridhika kweli? Ati, embu nambie utaweza kumfikisha kweli mwanangu? Au unataka mwanangu baada ya miezi atuleletee malalamiko kuwa humridhishi? Eeeh!"
Baba aliongea hapo nikabaki kimya. Kilichonifanya niwe kimya ni ile hali ya kushindwa kupasua kile kigogo mbaya zaidi Mama mkwe akaja akakipasua. Looh!
" Najua binti yangu anakupenda. Nami nitakukabidhi. Lakini nakusihi kuanzia leo hii kula msosi kama mwanaume, kula msosi wa haja ili upate nguvu. Si unaona umeshindwa hata kupasua kile kigogo. Mwanaume hupaswi kuwa hivyo. Mwanaume sharti ule chakula kingi ili upate nguvu na akili ya kutafuta pesa ya familia. Usiwe kama vijana siku hizi. Kula mwanangu. Sawa Taikon"
Baba alimaliza kuongea nami nikamuitikia kwa kutingisha kichwa.
Moyoni niliapa kuwa nikitoka hapo sitarudi. Nilikuwa nampango wa kulala lakini nilisitisha mara moja kwa aibu niliyoipata. Sikutaka kuendelea kukaa hapo kwani nilijua naweza patwa na aibu kubwa nyingine. Lakini tayari ilikuwa jioni hivyo sikuwa na jinsi zaidi ya kulala.
Muda wa kulala ulifika, nikapewa chumba ambacho nililala na shemeji yangu, mdogo wake na Chamdeko mwenye miaka kumi. Kitandani usingizi ulikataa kata kata kuja. Nilikumbuka aibu ya mchana nikaishia kusonya nikisikitika. Punde si punde nilishtuka kusikia sauti chini ya sakafu. Kuchungulia nilikutana na nyoka mwekundu akitambaa sakafuni.
Nilipiga kelele mpaka shemeji yangu niliyelala naye akaamka.
Wote tulikuwa tunakimbilia kwenye kona tukipiga makelele tukisema Nyoka! Nyoka!
Punde Watu waliamka na kuja chumbani kwetu. Wakamuua.
Ilikuwa aibu nyingine, Baba Mkwe alinikata jicho la dharau kisha akaondoka. Nilijisikia vibaya sana. Nilijidharau kwa kushindwa kumuua nyoka ukweni. Nikakumbuka swali la Mkwe wangu: Utaweza kuishi na Binti yangu.
Kimoyo moyo nilikiri bado sijakamilika kuitwa mwanaume.
Kesho yake niliaga kurudi home, Chamdeko naye akasema atakuja apaone nyumbani siku tatu zijazo. Tukaagana huku walionisindikiza wakionionea huruma kwa aibu niliyoipata.
Siku tatu zilizofuata Binti chamdeko alikuja nyumbani. Alifanyaje. Tusubiri kipande chake kinakuja.
Robert Heriel
Taikon wa Fasihi
0711345431 au 0693322300.