Ukitaka Kujifunza Waruhusu Watu Waone Usichokiona

Ukitaka Kujifunza Waruhusu Watu Waone Usichokiona

Jielewe

Member
Joined
Jan 10, 2017
Posts
40
Reaction score
62
​
UKIFUATILIA mazungumzo ya wa-Tanzania wengi kwenye mitandao ya kijamii, unaweza kuona namna watu wanavyojinasibu kujua. Mijadala mingi imejaa ‘ujuaji’ unaofanya watu wajigambe, wadhihaki wengine, watukane na wakati mwingine, kadri ya mamlaka yao, watake kulazimisha kile wanachokiona wao ndio kiwe ukweli usiopingika.

Katika makala haya, ninajaribu kuonesha kuwa ili tujenge jamii ya watu wastaabu wanaoheshimiana lazima tuwe tayari kujifunza hata katika mazingira ambayo tunaamini tunajua.

Labda utaniuliza, una maana gani unaposema ‘ujuaji’? Je, kujua ni jambo baya? Nikujibu kabla sijafika mbali. Kujua si jambo baya. Kimsingi ili mwanadamu akabiliane na mazingira yake na awe salama, analazimika kujua mambo kadha wa kadha. Mwanadamu anahitaji kujua wapi anaweza kupata mahitaji yake, nani ni rafiki yake, nani ni adui yake, wapi kuna dalili za hatari na mambo kama hayo ambayo ni msingi wa usalama wake.

Aidha, tunafahamu pia kuwa mbali na kutaka kujua ili kujihakikishia usalama wetu wa kimwili, maarifa yanatuhakikishia usalama wa kisaikolojia. Chukulia pale unapogundua umekosea. Unajisikiaje? Hatupendi kuwa wajinga (wasiojua) ndio maana tunapohisi kuna jambo hatulijui tunajisikia vibaya. Hata pale tunapopata taarifa sahihi zinazothibitisha kuwa tulikuwa tumekosea, bado tunakuwa wagumu kukubali makosa yetu. Maana yake kujua ni hitaji muhimu la kisaikolojia alilonalo mwanadamu.

Shida inakuja pale tunapofikiri tuko sahihi na wengine wote wenye mtazamo tofauti na ule tulionao hawako sahihi. Mawazo kama haya ndiyo ninayoyaita ujuaji. Ujuaji ni ile tabia ya mtu kutaka kuonekana ana ufahamu wa mambo hata kama wakati mwingine yeye mwenyewe anajua hujui.

Mtazamo kama huu ni dalili za upungufu mkubwa wa uelewa. Kwanza, ni kutokana na ukweli kuwa binadamu pamoja na kupenda kufahamu mambo mengi, bado tunafahamu mambo machache mno. Lakini pia, ufahamu wetu kwa asili una tabia ya kutudanganya bila sisi kujua tumedanganyika. Nikupe mfano rahisi.

Ukitazama picha hiyo hapo juu, kwa haraka haraka unaweza kudhani unaona sura ya kijana wa ki-Hindi anayetazama kushoto na nywele zake ndefu amezitimua kwa nyuma. Unachokiona ni kitu sahihi. Hata hivyo, huo si mtazamo pekee kwa picha hiyo.

Ingawa ni kweli umeona uso wa kijana wa ki-Hindi, bado unaweza kuona kitu kingine ukiwa tayari na kuufungua ufahamu wako. Tazama kwa makini kuona kama unaweza kumwona mtu mfupi jamii ya Waeskimo aliyegeukia ubao akiandika kitu kwa mkono wa kulia.

Tazama kwa makini. Nikusaidie kumwona. Uso wa yule kijana wa ki-Hindi sasa utazame kama kichwa cha mtu huyu mfupi aliyejifunika koti lenye manyoya mithili ya koti la ‘Father Christmas’, shingo ya kijana wa ki-Hindi sasa itazame kama miguu ya mtu huyu mfupi, na nywele za kijana wa ki-Hindi sasa zitazame kama ubao wa kuandikia. Je, umemwona? Kama bado, tazama kwa bidii.

Huu ni mfano unaoweza kutusaidia kuelewa namna gani jambo lile lile linaweza kuwa na tafsiri zaidi ya moja kutegemea na kile tunachokitarajia au kutaka kukiona. Ndivyo ilivyo katika maisha. Suala hilo hilo unaloamini liko vile unavyojua linaweza kuwa tafsiri tofauti ikiwa tu utafungua milango ya kujifunza zaidi.

Unapojadiliana na watu, usilazimishe kuwa sahihi hata kama unaamini uko sahihi. Kile unachokiona ni kwa mujibu wa taarifa ulizonazo na imani uliyonayo tayari. Wengine unaofikiri hawako sahihi nao wanaweza kuwa na taarifa tofauti na zile ulizonazo wewe. Ukilazimisha waone kile tu unachokiona wewe unakosea.

Kama nilivyotangulia kusema, tunalazimisha kuwa sahihi kuliko wenzetu kwa sababu tunafikiri bila kuwa sahihi hatuwezi kuwa na heshima. Tunatumia ‘ujuaji’ kama silaha ya kulinda heshima zetu. Lakini je, huwezi kuwa sahihi na mwenzako pia akawa sahihi? Hatuwezi kuwavumilia wenzetu kwa kuona kile tusichokiona?

Nikirudi kwenye picha niliyoitumia kwenye makala haya. Hakuna mtu anayeweza kudai kuwa kile anachokiona yeye ndicho sahihi zaidi kuliko wanachokiona wengine. Mazingira tuliyokulia, mambo tuliyozea kuyasikia yanaweza kufanya ikawa rahisi zaidi kuona kichwa cha kijana wa ki-Hindi anayetazama kulia. Lakini hiyo haifanyi wanaomwona kijana mfupi wa ki-Eskimo wasiwe sahihi.

Lugha sahihi tunayoweza kuitumia ni kwamba wanaomwona kijana wa ki-Hindi wako sahihi, lakini pia wanaomwona kijana mfupi wa ki-Eskimo nao wako sahihi. Hakuna walio sahihi kuliko wengine hata kama hawaoni kile wanachokiona wengine.

Siku nyingine unapojadiliana na wenzako masuala yoyote yale iwe ni imani/dini, siasa, utamaduni, taaluma zingatia kuwa unachokiona wewe sicho wanachokiona wenzako. Taarifa ulizonazo wewe, sizo alizonazo mwenzako. Upande unaoona kuwa ndio sahihi, kwa wengine ni upande usiosahihi. Ukizingatia hilo, hutalazimisha kuwa sahihi wakati wote na hivyo utakuwa mwepesi kuvumilia mawazo tofauti na yale uliyonayo.

Kusoma zaidi makala kama hizi, fuatilia blogu ya Jielewe kwa bonyeza kiungo hiki. Pia unaweza kusoma makala za mwandishi Christian Bwaya kila Jumanne na Ijumaa (Mwananchi) na Alhamisi (Mtanzania).
 
Mkuu nimekuelewa sana,hongera kwa kua mtu unaependa kujifunza kile wakionacho wenzako
 
Back
Top Bottom