Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,783
- 14,975
Akizungumza wakati wa ziara ya kamati hiyo eneo la Holili, wilayani Rombo Mkoa wa Kilimanjaro, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii Mhe. Timotheo Mzava amesema kazi ya kuweka alama kwenye mipaka sio kazi ndogo na kuipongeza wizara ya ardhi kwa kazi kubwa iliyofanya.
Aidha, Kamati imeitaka Serikali kukamilisha kazi ya uimarishaji mpaka huo wa kimataifa kati ya Tanzania na Kenya huku ikitarajia kuona mipango ya kifedha na bajeti inayoonesha mwelekeo na nia ya dhati ya kukamilisha kazi hiyo kwenye bajeti ya sasa na inayokuja katika mwaka wa fedha 2026/2027.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Kaspar Kaspar Mmuya amewataka wataalamu wa Wizara ya ardhi kuendelea kutoa elimu kwa wananachi wa maeneo ya mipakani kwa lugha ile ile ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili waelewe na kuwa sehemu ya ulinzi wa mipaka ya nchi.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Rombo Mhe. Raymond Mwangwala ameiambia kamati hiyo ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii kuwa mpaka wa nchi hizo mbili uko salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi na wana uhusiano mzuri na kuweka wazi kuwa wote walishiriki vizuri kwenye zoezi la kuweka alama kwenye mipaka.
Mpaka wa Tanzania na Kenya umekuwa ni eneo la mfano wa kuigwa kwenye ukanda wa Afrika kwa mujibu wa Taasisi ya Uimarishaji wa Mipaka Afrika inayojulikana kama African Union Border Program.