Uibukaji wa biashara ya utumwa mamboleo nchini Libya, nani alaumiwe?

mtanganyika wa kweli

JF-Expert Member
Apr 12, 2015
2,420
1,718
UIBUKAJI WA BIASHARA YA UTUMWA MAMBOLEO NCHINI LIBYA: NANI ALAUMIWE?

Na Sabatho Nyamsenda

Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kukasirishwa na taarifa kuhusu uibukaji na ueneaji wa biashara ya utumwa nchini Libya, ambapo watu weusi – wengi wao wakiwa ni wahamiaji toka nchi nyingine za Kiafrika – hukamatwa, huteswa na kufungwa, kisha kuuzwa katika masoko ya wazi kama watumwa. Taarifa kutoka vyanzo mbali mbali zinasema kuwa Waafrika hao huuzwa kati ya dola za kimarekani 400 hadi 500. Wanawake wanaonunuliwa hupelekwa katika masoko ya ngono ilhali wanaume hupelekwa katika ufanyaji kazi mashambani au katika viwanda. Picha za mnato na video zilizoenezwa na vyombo vya habari zinaonyesha watu weusi wakiwa wamefungwa na kuning’inizwa kichwa chini miguu juu, ama wakiwa katika soko la wazi. Haya yanatendeka nchini Libya, nchi iliyokuwa mstari wa mbele kupigania Muungano wa Afrika, ili tuwe na dola moja.

Nchi za kibeberu, kwa unafiki mkubwa, zimetoa matamko ya ‘kulaani’ biashara hii ya utumwa. Matamko hayo, yanayotolewa na wazungu, yana lengo la kuonyesha kuwa “Waarabu” wa Libya ndio wanawatesa Waafrika weusi na kuwageuza watumwa. Mathalani, Novemba 28, 2017, akiwa ziarani nchini Burkina Faso, Rais wa Ufaransa Emmanuel Macro alitoa kauli zenye ili kufuta uhusika wa Ulaya katika biashara ya utumwa mamboleo.

“Nionyesheni Mfaransa, Mbeligiji au Mjerumani aliyehusika na usafirishaji haramu wa watu kati ya Naijeria na Libya. Hayupo mtu huyo,” alisema Macron, akiongezea kuwa “Siku hizi, kuna Waafrika ambao wanawageuza wenzao kuwa watumwa, huo ndio ukweli.”

Mbali na kuifutia Ulaya hatia ya kuwa chanzo cha biashara ya utumwa wa kale na huu wa leo, kauli ya Macron pia ililenga kuhalalisha uwepo wa majeshi ya Ufaransa katika Afrika, hususan katika makoloni ya zamani ya Ufaransa. Alipowasili Burkina Faso, Macro alikaribishwa kwa maandamano yaliyolaani na kupinga ubeberu wa Ufaransa, huku vijana wakichoma matairi na kuitaka Ufaransa kuondoa majeshi yake nchini humo. Akiwa katika chuo Kikuu cha Ouagadougou ndipo wanafunzi walipomtwanga maswali, mojawapo likiwa ni hilo la kuhusu biashara ya utumwa mamboleo. Jingine lilihusu idadi ya wanajeshi wa Ufaransa katika Afrika, ambayo ni kubwa kuliko wanafunzi wa Kiafrika wanaosoma nchini Ufaransa. Hapo Macron akang’aka, akishadadia ‘haki’ ya nchi yake kuendelea kuikalia kijeshi Afrika huku akisema kuwa wanajeshi hao wa Kifaransa walipaswa “kupongezwa” na sio kulaaniwa kwa kuivamia Afrika.

Ikichukuliwa kama ilivyo, kauli za Macron na viongozi wengine wa mataifa ya kibeberu zitachochea mgawanyiko zaidi katika bara la Afrika kati ya nchi za Kaskazini mwa Afrika, na zile za kusini mwa jangwa la Sahara. Na hata ndani ya nchi za Kusini mwa Sahara, makaburu weusi nao watazidisha chuki dhidi ya Waafrika wenye asili ya Kiarabu na Kihindi na hivyo kupelekea mgawanyiko zaidi.

Ukweli utabaki pale pale. Mabeberu ndio chanzo kikuu cha biashara haramu ya utumwa inayoendelea nchini Libya. Kwanza, hata kabla ya uibukaji wa soko mamboleo la utumwa ndani ya Libya, Waafrika wengi waliohamia Ulaya bila kufuata sheria, waligeuzwa watumwa. Taarifa mbali mbali za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji zilionyesha kuwa zaidi ya wanawake 5,000 kutoka nchini Naijeria hutorokea Ulaya, na zaidi ya asilimia 80 ya wanawake hao huishia kuwa watumwa wa ngono katika nchi za Ulaya. Wanaume huishia kuwa watumwa wa kazi za mikono, hasa viwandani, kwa kuwa ndio njia pekee ya kuwafanya waishi.

Pili, ni mabeberu ndio walioivamia Libya mwaka 2011 na kuiharibu nchi hiyo iliyokuwa ikipigiwa mfano Afrika kwa kutumia rasilimali zake kuboresha maisha ya wananchi wake. Majeshi ya NATO yaliwaua wananchi wa Libya na kumchinja kiongozi wao, Muammar Gaddafi. Kisha wakapora utajiri wa nchi hiyo, zikiwemo akiba ya dhahabu yenye uzito wa tani 150, na kiasi kama hicho cha fedha (silver).

Libya, nchi iliyopigiwa mfano kwa miundo mbinu na teknolojia ya kisasa, ikaharibiwa na kugeuzwa magofu. Ule utulivu na uimara uliokuweko Libya ukatoweka. Badala yake, makundi mbali mbali ya wanamgambo yanapigania mamlaka, hali inayopelekea kuwepo kwa ombwe la utawala. Kwa mabeberu, hali hiyo ya mapigano yasiyo na ukomo ndani ya Libya inawapatia mazingira mazuri ya kupora utajiri wa nchi hiyo, hasa mafuta.

Kabla ya kupinduliwa Ghaddafi, waafrika weusi walipokelewa Libya na kupewa ajira, na hata uraia. Hivi sasa, waafrika weusi na hata waafrika wenye asili ya kiarabu (wakiwemo Walibya wenyewe), wamekuwa wakizikimbia nchi zao na kutorokea Ulaya kukimbia vita na ufukara uliopo katika nchi zao, na uliosababishwa na uvamizi na uporaji wa mabeberu. Nchi za Ulaya zimejibu kwa sera za kifashisti, zikiwarudisha wahamiaji hao katika nchi walizotokea. Mathalani, Italia huwalipa pesa zaidi watoroshaji wanaovusha watu baharini ili kuwarudisha wahamiaji nchini Libya, licha ya kujua hatari zinazowakumba katika nchi hizo. Hali hii imechochea biashara ya utumwa nchini Libya.

Natoa mapendekezo yafuatayo ili kutatua hali iliyojitokeza Libya:

(1) Serikali ya Tanzania itoe mara moja tamko la kulaani biashara hiyo haramu.

(2) Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na serikali nyingine za Kiafrika ichukue hatua madhubuti na za haraka kuwaokoa Waafrika wenzetu waliogeuzwa watumwa nchini Libya na kuwarudisha katika nchi zao.

(3) Serikali za Kiafrika zichukue hatua madhubuti kuhakikisha kuwa nchi ya Libya inarejea katika hali ya usalama na utulivu, chini ya serikali ya umoja wa kitaifa.

(4) Tusikome kulaani kitendo cha mabeberu kuivamia nchi ya Libya na kuwauwa wananchi wake, pamoja na kumchinja kiongozi wa nchi hiyo Muamar Gadaffi ili kuhalalisha uporaji wa utajiri wa nchi hiyo. Kwa kuwa kati ya viongozi waliohusika katika uvamizi huo ni aliyekuwa rais wa Marekani, Barack Obama, ninaisihi serikali ya Tanzania kuibadili jina barabara ya Ikulu, ambayo ilipewa jina la Barack Obama mwaka 2013. Ni fedheha kwa anuani ya Ikulu ya nchi yetu kubeba jina la Barack Obama, aliyewakilisha maslahi ya mabeberu katika kuivamia na kuipora Afrika. Tunashauri barabara hiyo ipewe jina la Muammar Ghaddafi ili kumwenzi kiongozi wa Libya aliepinga ubeberu na alietumia rasilimali za Libya kuiendeleza Afrika.

(5) Serikali za Kiafrika ziyaondoe majeshi yote ya nchi za kibeberu yaliyomo barani humu.

(6) Serikali za Kiafrika na wananchi wake zipinge sera za kifashisti za nchi za Magharibi zinazolenga kuzuia wahamiaji katika nchi hizo, na vitendo vya kitumwa vinavyofanywa dhidi ya wahamiaji katika nchi hizo.

(7) Ni wakati sasa wa viongozi wa Kiafrika kutumia rasilimali zilizomo katika bara hili ili kuleta maendeleo kwa watu wake, pamoja na kushirikiana kiuchumi ili kuondoa utegemezi kwa mabeberu na kujenga uchumi wa Kiafrika ulioshikamana na unaojitegemea.

Wakati umewadia kwa Afrika kuachana kabisa na sera za utengano, kwani zinawafaidisha mabeberu na kuwafukarisha Waafrika. Tuanze kupiga hatua madhubuti kwa kujenga shirikisho la kijamaa la Afrika. Hili sio jambo la kesho. Linapaswa kufanyika sasa!
 
Hawatakuelewa kabisa, tena upinzani wagumu zaidi wa jambo hilo wako humu ndani ya Africa. Sijawahi kusikia vyama vya kisiasa ama NGOs na mashirika mengine yalio humu yenye mafungamano na ya nje, wakilaani ama kupinga uwepo wa majeshi ya kigeni ktk nchi zetu.

Tumejawa na unafiki na uvibaraka wa mataifa ya kibepari kwa mgongo wa Haki za binadamu na demokrasia, hawana mana kabisa.

Ni ushauri mzuri, na ulishatolewa miaka nenda rudi, ikashindikana. Sioni picha nzuri kwa Afrika ya kesho, lazima taifa litanyanyuka na kulivamia lingine na kulitawala kikoloni, ubinafsi ndo asili ya kila OVU duniani. Mungu ilinde Afrika, wenyewe tumeshashindwa kabisa.
 
Wakuu, hii mambo inakwendaje?
Ninaona picha za mateso, watu wakivuja damu...yote nasikia ni biashara haramu ya binadamu huko Libya...

Mwenye mzigo kamili, kuhusu hii mambo atujulishe tafadhali ilianza lini?
 
Naiona Afrika yangu iliyojikatia tamaa. Huwa nahuzunika sana naposoma articles kama hizi. Afrika yetu ilikwisha kufa zamani.
 
9ee6f95f8b5a09be1751cead1c7f1493.jpg
 
edb9769189d301031e418b30254b524a.jpg


Bags containing the bodies of migrants who died when a boat sank off Libya's western coast, seen in Tripoli, Libya, on Nov. 25. (Ismail Zitouny/Reuters)
 
9bcc98d9d4cbc85cd6dad17b05410de7.jpg

Migrants quartered in a detention center in Zawiyah, a city west of Tripoli, on June 17. (Taha Jawashi/Agence France-Presse/Getty Images)
 
Very sad!
They say if we don't learn from history then we are doomed to repeat it.
A slave auction put a global spotlight on Libya.It did indeed.
So now people seem touched after all these days of acting blind to human trafficking and sex slavery happening everywhere in the world!
An auction in Africa is a trigger indeed.These people just did the real thing.
And that's just a hint of what we've become.
 
Waarabu wana roho mbaya sana. Wao kwa wao wanachinjana kila siku.
 
Back
Top Bottom