Uhuru wa Kuabudu na Haki ya Askofu Gwajima Kufundisha Amri za Mungu: Usiue mtu asiye na hatia, Usiue jina zuri la mtu baki, na Usiibe mtu kwa Kumteka

Doctor Mama Amon

Platinum Member
Joined
Mar 30, 2018
Posts
2,311
Reaction score
3,490

I. Usuli

Uamuzi wa serikali wa kukurupuka kufunga kanisa la ufufuo na uzima na matawi yake 2,000 nchini Tanzania, tena bila kutoa nafasi ya kujitetea kwa viongozi wake, ni ushahidi kwamba huenda viongozi wetu hawaelewi kwamba uhuru wa kuutafuta ukweli wa kiimani, ikiwemo imani ya kidini, ni tunu ya msingi inayopaswa kuheshimiwa na kufukuziwa na kila mtu, kila mahali na kila wakati, mpaka hapo dhamiri yake itakaporidhika kwamba "ukweli halisi ni huu" hata kama haukubaliki kwa watu wengine wengi.

Hivyo, hapa chini, nimeandika dokezo la kisera kuchunguza uamuzi huo, kukosoa itakapobidi, na kutoa mapendekezo stahiki kuhusu sera ya Taifa kuhusu uhudu wa kidini. Nakusudia kutetea hoja ifuatayo:

  1. Katika nchi ambayo, kwa mujibu wa katiba yake, ni Jamhuri ya Kikiberali na Kidemokrasia, serikali hupata mamlaka halali kutoka kwa wananchi, na baada ya kusimikwa kazi ya serikali huwa ni kukuza na kuhami haki za binadamu zilizotajwa kwenye katiba ya nchi, zikiwemo haki ya kuhesabiwa mtakaifu mpaka mamlaka inapotamka hatia baada ya kumsikiliza mtuhumiwa, na haki za kidini zenye kujumuisha uhuru wa kuabudu, kufundisha na kueneza dini.
  2. Kwa mujibu wa Katiba yake, Tanzania ni nchi ambayo ni Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia, yenye kutambua uwepo wa mseto wa jumuiya za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, kila jumuiya ikiwa na uhuru wa kubuni tunu, malengo na mikakati yake.
  3. Kwa hiyo, tofauti na maamuzi ya serikali, askofu Gwajima, na raia yeyote baki, anazo haki za kidini ikiwa ni pamoja na kutoa mahubiri juu ya ubaya wa utekaji, utesaji na uuaji, kulingana na mtazamo wa kidini, tena akiwa amesimama kwenye altare ya Kanisa.
  4. Hata hivyo, majuzi serikali imefuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kwa sababu ya madai kwamba Askofu Mkuu Gwajima ameonekana katika "mimbari ya Kanisa" hilo akitoa "mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha serikali na wananchi."
  5. Kwa hiyo, serikali imekengeuka kwa kiwango cha kuvunja Katiba ya nchi.
  6. Mkuu wa serikali, Rais Samia, amekula kiapo cha kulinda, kuhifadhi na kutetea katiba ya nchi, kwa maana kwamba Rais Samia alikiri ukuu wa katiba juu ya serikali anayoiongoza.
  7. Kwa hiyo, uamuzi wa serikali dhidi ya kanisa la Gwajima unapaswa kubatilishwa ili kuheshimu ukuu wa katiba ya nchi juu ya serikali.
Kwa ajili ya kufanya utetezi huu dokezo hili limegawanyika kwenye sehemu zifuatazo:
  1. Usuli
  2. Utangulizi
  3. Utambulisho wa tatizo: Kwani kuna shida gani?
  4. Methodolojia
  5. Mafundisho ya Biblia Kuhusu Heshima ya KIutu na Haki za Kidini
  6. Mafundisho ya Katiba ya Nchi Kuhusu Heshima ya Kiutu na Haki za Kidini
  7. Ufanano kati ya mafundisho ya Katiba ya nchi na Mafundisho ya Biblia
  8. Utofauti kati ya mafundisho ya Katiba ya nchi na Mafundisho ya Biblia
  9. Msingi wa Kifalsafa wa Sera ya Taifa Kuhusu Uhuru wa Kidini
  10. Hitimisho na mapendekezo
  11. Marejeo
II. Utangulizi

Tarehe 02 Juni 2025, b
arua iliyoambatanishwa hapa chini ilisambazwa mitandaoni, ikieleza uamuzi wa serikali kufuta usajili wa "Kanisa la Ufufuo na Uzima," linaloongozwa na Askofu Mkuu Josephat Gwajima.

Sababu iliyotolewa na serikali ni kwamba, Askofu Gwajima ameonekana katika "mimbari ya Kanisa" hilo akitoa "mahubiri yenye mwelekeo wa kisiasa na nia ya kuichonganisha serikali na wananchi."

Kwa mujibu wa barua hiyo, “vitendo hivi ni kinyume cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 chini ya kifungu cha 17 kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya Mwaka 2019 kwa kuwa vinaathari ya kuhatarisha amani na utulivu nchini.”

Mahubiri yanayoongelewa yanahusu kitendo cha Askofu Gwajima kutumia altare kuikosoa serikali kwa kushindwa kuzuia matukio endelevu ya utekaji, utesaji na uuaji wa raia wasio na hatia iliyothibitishwa kimahakama.

Kwa sababu hii, Msajili wa Vyama vya Kijamii anadai kwamba alitumia mamlaka yke, chini ya Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kama kikisomwa pamoja na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019, kufuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, kuanzia tarehe 02 Juni 2025.

Kwa mujibu wa barua ya kufuta Kanisa la Ufufuo na Uzima, ni kwa sababu hizi za kisheria, Askofu Gwajima alitakiwa “kusitisha shughuli za Kanisa [lake] mara moja,” hata bila kupewa nafasi ya kujitetea dhidi ya tuhuma, japo Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kinampa Gwajima haki hiyo.

Haki ya kusikilizwa kabla ya kuadhibiwa ni haki ya kikatiba. Kila mtu na kila taasisi iliyo na utu wa kisheria, wanayo haki kuhesabiwa watakatifu hadi hapo mamlaka halali inapomtia hatiani baada ya kumsikiliza (Katiba, ibara ya 16(3)(a)).

Kwa hiyo, hapa chini napendekeza na kutetea rai kwamba, kwa uamuzi huu, serikali imeingilia uhuru wa kidini unaotambuliwa Kikatiba. Yaani serikali imekengeuka. Ufafanuzi unafuata baada ya methodolojia.

III. Utambulisho wa tatizo: Kwani kuna shida gani?

Katika nchi ambayo, kwa mujibu wa katiba yake, ni Jamhuri ya Kikiberali na Kidemokrasia, serikali hupata mamlaka halali kutoka kwa wananchi, na baada ya kusimikwa kazi ya serikali huwa ni kukuza na kuhami haki za binadamu zilizotajwa kwenye katiba ya nchi, zikiwemo haki ya kuhesabiwa mtakaifu mpaka mamlaka inapotamka hatia baada ya kumsikiliza mtuhumiwa, na haki za kidini zenye kujumuisha uhuru wa kuabudu, kufundisha na kueneza dini.

Kwa mujibu wa Katiba yake, Tanzania ni nchi ambayo ni Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia, yenye kutambua uwepo wa mseto wa jumuiya za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kidini, kila jumuiya ikiwa na uhuru wa kubuni tunu, malengo na mikakati yake.

Kifungu cha 17(b) cha Sheria ya Jumuiya Sura ya 337 kinasema kwamba:

“Msajili anaweza, kwa uamuzi wake, kufuta wakati wowote usajili wa jumuiya yoyote ya ndani, kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya kifungu cha 12, ikiwa ameridhika kwamba ni muhimu kufanya hivyo kwa misingi kwamba jumuiya inayohusika inatumiwa, au kuna uwezekano wa jumuiya hiyo kutumika kwa madhumuni yasiyo halali, au kutumika kwa madhumuni yoyote yanayoweza kuathiri au kutoendana na udumishaji wa amani, utulivu na utawala bora... uamuzi ambao utakuwa halali ikiwa tu kabla ya kufutwa kwa usajili, jumuiya inayohusika itakuwa imepewa fursa ya kuwasilisha sababu za kueleza kwa nini usajili huo haupaswi kufutwa.”

Na kifungu cha 39 cha Sheria Namba 3 ya mwaka 2019 kinasema kwamba:

“Neno ‘jumuiya’ maana yake ni chama cha watu kumi au zaidi kisichoegemea upande wowote wa kisiasa, kilichoanzishwa kwa manufaa ya kitaaluma, kijamii, kitamaduni, kidini, kiuchumi au ustawi wa wanachama wake, kilichoundwa na kusajiliwa hivyo chini ya Sheria hii, lakini hakijumuishi:

  • (a) kampuni iliyoundwa na kusajiliwa chini ya Sheria ya Makampuni;
  • (b) dhamana iliyoundwa na kusajiliwa chini ya Muungano wa Wadhamini;
  • (c) Chama cha Wafanyakazi kilichoundwa chini ya Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini;
  • (d) chama cha ushirika kilichoundwa na kusajiliwa chini ya Sheria ya Vyama vya Ushirika;
  • (e) chama cha kilimo kilichoundwa na kusajiliwa chini ya sheria yoyote iliyoandikwa isipokuwa Sheria hii;
  • (f) chama cha kisiasa kilichoundwa na kusajiliwa chini ya Sheria ya Vyama vya Siasa;
  • (g) shirika lisilo la kiserikali lililoundwa na kusajiliwa chini ya Sheria ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali;
  • (h) kikundi cha huduma ndogo za fedha za jamii (VICOBA) kilichosajiliwa chini ya Sheria ya Mikopo Midogo;
  • (i) chama cha michezo kilichoundwa na kusajiliwa chini ya Sheria ya Baraza la Michezo la Taifa la Tanzania; na
  • (j) jumuiya yoyote ambayo Waziri anaweza, kwa amri iliyochapishwa kwenye Gazeti la Serikali, kutangaza kuwa si jumuiya kwa madhumuni ya Sheria hii."

Kwa hiyo, kila raia, akiwemo Askofu Gwajima, anayo haki ya kutumia Kanisa lake kutoa mahubiri juu ya ubaya wa utekaji, utesaji na uuaji, kulingana na mtazamo wake wa kidini, ilimradi, kupitia mahubiri hayo, pasiwepo na uwezekano wa kutaka kufanikisha "madhumuni yasiyo halali," au kutaka kufanikisha "madhumuni yoyote yanayoweza kuathiri au kutoendana na udumishaji wa amani, utulivu na utawala bora."

Lakini, kutoa mahubiri juu ya ubaya wa utekaji, utesaji na uuaji, bila kujali kama mahubiri hayo yametolewa kwa kuzingatia mtazamo wake wa kidini au mtazamo wa kisekulari, ni mbinu inayoendana na "udumishaji wa amani, utulivu na utawala bora," kama inavyosema sheria ya Jumuiya za Kijamii.

Kwa hiyo, Askofu Gwajima ametembea ndani ya sheria za nchi. Lakini, serikali inasema amekosea. Ama Gwajima yuko sahihi na serikali imekosea, au serikali iko sahihi na Gwajima amekosea, lakini pande zote mbili haziwezi kuwa sahihi kwa wakati ule ule, kuhusu suala lile lile na katika nchi ile ile moja.

IV. Methodolojia

Utafiti huu umefanyika kwa kusoma maandiko na kusikikiza video kadhaa ili kujibu swali lifuatalo: Nani yuko sahihi kati ya serikali na Gwajima? Swali hili linajibiwa katika dokezo hili. Kwa ajili kulijibu swali hili, maswali madogo yafuatayo yatajibiwa:

  1. Je, tunaweza kukir8 na kutetea uwepo wa haki za binadamu, ikiwemo haki ya uhuru wa kidini, bila kukiri wala kukanusha uwepo wa Mungu?
  2. Kuna Ufanano gani kati ya Mafundisho ya Katiba ya nchi na Mafundisho ya Biblia Kuhusu Heshima ya Kiutu na Haki za Kidini?
  3. Kuna Utofauti gani kati ya Mafundisho ya Katiba ya nchi na Mafundisho ya Biblia Kuhusu Heshima ya Kiutu na Haki za Kidini?
  4. Sera ya Taifa inayoongoza mahusiano kati ya vyombo vya dola na taasisi za dini ni ipi na msingi wake wa kifalsafa ni upi?
  5. KItendo cha kiongozi wa dini kusimama katika altare na kukemea uovu kama vile wizi, uwongo, ubakaji, rushwa, utekaji, utesaji na uuaji wa raia wasio na hatia kinakiuka katiba ya nchi yetu?
  6. Ni kwa kiasi gani uamuzi wa serikali umezingatia kanuni za kifikra zinazoongoza michujo ya kimantiki?
  7. Kufuatia kitendo cha serikali kufuta usajili wa Kanisa la ufufuo na uzima kwa sababu ya kutumia altare ya kanisa lake kinatokana na matakwa kwa kisheria na Kikatiba?
  8. Hatua gani za kikatiba, kisera, kisheria na kiutawala zinapaswa kuchukuliwe baada ya sasa?
V. Mafundisho ya Biblia Kuhusu Heshima ya KIutu na Haki za Kidini

Wakristo wapatao bilioni 2.5 duniani kote, sawa na 37% ya watu wote duniani, wanaunganishwa na mafundisho ya kidini ("religious doctrine") yanayoweza kufupishwa katika matamko matatu bila kubaki. Kuna:

  1. Maarifa kuhusu ukweli juu ya Mungu, Mazingira na Watu na uhusiano kati ya pande hizi tatu, kama yalivyofupishwa kwenye Kanuni za Imani kama vile Kanuni ya Imani ya Mitume, Kanuni ya Imani ya Athanazi, Kanuni ya Imani ya Nikea, na kadhalika (Credenda);
  2. Malengo yanayopaswa kuombewa kwa Mungu, katika matumaini, ili mahusiano kati ya Mungu, Mazingira na Watu yaimarike, kama yalivyofupishwa kwenye Sala ya Baba Yetu (Speranda); na
  3. Majukumu yanayopaswa kutekelezwa ili kuonyesha upendo kwa vitendo, kwa ajili ya kudumisha mahusiano mema kati ya Mungu, Mazingira na Watu, kama yalivyofupishwa kwenye Amri Kumi za Mungu (Agenda).
Hivyo, Katekisimu zote za Ukristo zinaongelea na kufafanua mambo haya matatu, kwa kutumia lugha tofauti na mpangilio tofauti.

Uandishi wake unafuata mwongozo wa Mtume Paulo, asemaye: “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo.”—1 WAKORINTHO 13:13.

Kwa ajili ya kuweka msingi wa uelewa mpana kuhusu kosa la serikali, nitaeleza kwa kifupi ninachokifahamu kuhusu maneno yaliyotamkwa na Askofu Gwajima katika muktadha wa "Ajenda" ya Taasisi za dini ya Ukristo.

Kulingana na uchambuzi wangu wa Biblia (tazama marejeo), "Ajenda" ya Taasisi za dini ya Ukristo, likiwemo Kanisa la Ufufuo na Uzima, yaani Amri Kumi za Mungu wa Biblia, inavyo vipengele vifuatavyo:

  1. Mwabudu Mungu mmoja aliyeumba Ulimwengu na anayepigania heshima ya utu wa kila binadamu (Kutoka 20:2-8)
  2. Fanya kazi kwa siku sita za wiki kwa kutumia mbinu za sayansi na tekinolojia mamboleo (Kutoka 20:9)
  3. Pumzika kazi zote siku ya saba (Kutoka 20:10-11)
  4. Waheshimu wazazi wako walioasisi familia yako (Kutoka 20:12)
  5. Usiue mtu yeyote asiye na hatia wala kuua jina lake zuri kwa kumpaka matope (Kutoka 20:13)
  6. Usizini mke wa jirani yako yeyote, mahali popote na wakati wowote (Kutoka 20:14)
  7. Usiibe mali wala kuiba mtu kwa kumteka na kumpoteza (Kutoka 20:15)
  8. Usimdanganye mtu yeyote, mahali popote, wakati wowote, na kwa njia yoyote (Kutoka 20:16)
  9. Usitamani mke wala kitu chochore cha jirani yako yeyote, mahali popote na wakati wowote (Kutoka 20:17)
  10. Usitende uovu kama mbinu ya kufanikisha lengo jema (Kutoka 20:2-18)
Amri zizi zinataja majukumu ya Mkristo ambayo Yesu aliyaongelea na kuyafupisha katika kitabu cha Mathayo, 22:36-40, anapoongelea majukumu matatu, yaani
  1. Jukumu la Kumpenda Mungu,
  2. Jukumu la Kumpenda jirani, na
  3. Jukumu la kuyapenda mazingira yaliyo rafiki kwa ustawi wa jirani.
Kumpenda mtu ni kufanya kitendo chochote kinachomsogeza karibu na mema ya kiutu au kumsogeza mbali na mabaya dhidi ya utu, na hivyo, kukuza na kuhami tunu za kiutu.

Hivyo, amri kumi za Mungu zinachora mstitari kati ya tunu hasi na tunu chanya kama ifuatavyo:

  1. Umungu dhidi ya ushetani
  2. Utu dhidi ya unyani
  3. Uchapa kazi dhidi ya Uzembe
  4. Ajira dhidi ya ukosefu wa ajira
  5. Kuheshimu familia dhidi ya kuidharau familia
  6. Ukweli dhidi ya uwongo na fitina
  7. Uhai dhidi ya mauaji
  8. Uzinzi dhidi ya uaminifu katika ndoa
  9. Rushwa dhidhi ya nidhamu ya kimamlaka
  10. Kuridhika dhidi ya kutamani mali ya wengine.
  11. Utulivu wa nafsi dhidi ya wasiwasi wa nafsi.
Na kwa pamoja, hizi tunu, haki na majukumu vinaunda mfumo kamili wa maadili uliowekwa na Mungu wa Biblia kwa ajili kuratibu mahusiano kati ya Mtu-na-Mungu, mtu-na-mtu, na mtu-na-mazingira yake asilia. Nimebuni mchoro ufuatao ili kufafanua zaidi uchambuzi wangu huu.


VI. Mafundisho ya Katiba ya Nchi Kuhusu Heshima ya Kiutu na Haki za Kidini

Katika nchi ambayo ni Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia serikali inapata mamlaka kutokana na ridhaa ya raia na baada ya kukabidhiwa mamlaka kazi ya serikali ni kukuza na kuhami haki za raia, ikiwemo haki ya kuheshimiwa utu binafsi, haki ya usawa mbele ya sheria, na haki ya kuabudu na kueneza mafundisho ya kidini yanayokubaliana na tunu za kiutu. Na katiba ya Tanzania inasema kuwa Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia. Inatambua haki na majukumu mengi yaliyotajwa kwenye Biblia. Mfano:

  1. Serikali inawajibika kuhakikisha kuwa, utu na haki nyinginezo zote za binadamu zinaheshimiwa na kuthaminiwa--Ibara ya 9(a).
  2. Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba heshima ya binadamu inahifadhiwa nakudumishwa kwa kufuata Kanuni za Tangazo laDunia kuhusu Haki za Binadamu--Ibara ya 9(f).
  3. Kila mtu anastahili heshima ya kutambuliwa na kuthaminiwa utu wake--Ibara ya 12(2).
  4. Wanadamu wote ni sawa, bila kujali asili, hali ya kijamii, kabila, ukoo, chama cha siasa, utaifa, dini, au rangi ya ngozi--Ibara ya 13(1).
  5. Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria--Ibara ya 14.
  6. Kila mtu anastahili kuheshimiwa na kupata hifadhi kwa nafsi yake, maisha yake binafsi na familia yake na unyumba wake--Ibara ya 16(1).
  7. Kila raia wa Jamhuri ya Muungano anayo haki ya kwenda kokote katika Jamhuri ya Muungano na kuishi katika sehemu yoyote--Ibara ya 17(1).
  8. Kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote--Ibara ya 18(1)
  9. Kila mtu anastahili kuwa na Uhuru wa dhamiri, imani na uchaguzi katika mambo ya dini, pamoja na Uhuru wa mtu kubadilisha dini au imani yake--Ibara ya 19.
  10. KIla mtu anayo haki ya kumiliki mali anayoimiliki kihalali--Ibara ya 24(1).
Kwa hiyo, serikali ambayo ni Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia, kama ilivyo Serikali ya Tanzania, haina mamlaka ya kuingilia uhuru wa kidini kwa kufanya maamuzi ya kupunguza au kuongeza lolote katika "Agenda, Speranda na Credenda" ya Wakristo, isipokuwa mafundishi yanayokiuka katiba ya nchi.

Hakuna mafundisho yaliyotolewa na Gwajima yanayokiuka misingi ya katiba ya nchi iliyonukuliwa hapo juu.

Hivyo, katika uamuzi wa kufuta usajili wa Kanisa la Ufufuo na Uzima kuna kashfa kuu dhidi ya serikali, maana katika kipengele cha weledi wa kikatiba wakubwa wameangukia pua.

VII. Ufanano kati ya mafundisho ya Katiba ya nchi na Mafundisho ya Biblia

Mfumo wa haki na majukumu unaotajwa katika Biblia unalenga kulinda, kukuza na kuhami tunu muhimu za kiutu. Tunu hizo ni utu wa binadamu, uhai, mali, ukweli, ndoa, familia, na urafiki.

Vivyo hivyo, Mfumo wa haki na majukumu unaotajwa katika Katiba ya nchi ambayo ni Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia, kama ilivyo Tanzania, hulenga katika kulinda, kukuza na kuhami hizi tunu za kiutu kwa kusimamia utekelezaji wa haki.

Kwa hiyo, serikali ya nchi ambayo ni Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia inayozingatia matakwa ya kikatiba haina sababu ya kugombana na viongozi wa dini ya Kikristo wanaohubiri Amri Kumi za Mungu altareni.


VIII. Utofauti kati ya mafundisho ya Katiba ya nchi na Mafundisho ya Biblia

Kuna tofauto kuu mbili kati ya mafundisho Kuhusu Heshima ya Kiutu na Haki za Binadamu katika Biblia, kwa upande mmoja, na mafundisho hayo katika Katiba ya nchi.

Mosi, wakati Biblia inatumia maneno kama vile "Mungu" na "haki," katiba ya nchi inatumia maneno kama vile "utu" na "upendo," kwa maana kwamba, maneno ya "Mungu" na "haki" sio misamiati ya kikatiba.

Na pili, tumeyafahamu mafundisho Kuhusu Heshima ya Kiutu na Haki za Binadamu katika Biblia kwa njia ya "ufunuo" wa Amri za Mungu, kulingana na yeye alivyoona inafaa (J. Caleb Clanton na Kraig Martin 2022:49-85)..

Lakini, tumeyafahamu mafundisho Kuhusu Heshima ya Kiutu na Haki za Binadamu katika Katiba ya nchi kwa njia ya "mchujo wa kimantiki" kuhusiana na hulka ya ubinadamu.

Yaani, Mchujo wa kiakili uliofanyika wakati wa kutunga katiba ya nchi yetu haukutumia taarifa za kiufunuo, bali uliongozwa na kanuni za kimantiki, katika mipaka ya sheria ya maadili asilia (J. Caleb Clanton na Kraig Martin 2022:3-48).

Nitafafanua jambo hili katika hatua inayofuata.

IX. Msingi wa Kifalsafa wa Sera ya Taifa Kuhusu Uhuru wa Kidini


Kuna kanuni kuu tatu za mantiki zinazoongoza mchujo wa kiakili bila kutegemea msaada wa ufunuo katika misahafu (Tuomas E. Tahko 2009). Sheria hizo ni:

  1. Mosi, “kanuni ya wasifu unaokitambulisha kitu na kukitofautisha na vitu vingine,"
  2. Pili, “kanuni ya kuepuka mkanganyiko,” na
  3. Tatu, "kanuni ya pembetatu ya ukweli, uwongo na mashaka."
Nitaeleza kila kanuni kwa ufupi kwa njia ya mifano rahisi.

Kanuni za kimantiki zinazoongoza mchujo wa kiakili

Mosi, kanuni ya wasifu unaokitambulisha kitu na kukitofautisha na vitu baki," yaani “the law of identity and difference” au "the principle of individuation," inasema mambo mawili kwa mpigo, yaani upekee wa kitu kwanza, na kisha utofauti wa kitu

Kuhusu upekee wa kitu, inasema kwamba, ikiwa kuna kauli inayotaja kitu kimoja kwa jina mojawapo (X), na kuna kauli ya pili inayotaja kitu kingine kwa jina la pili (Y), halafu ikathibitika kwamba idadi ya sifa zilizotajwa kwenye wasifu wa kitu cha kwanza (X) ni sawa na idadi sifa zilizotajwa kwenye wasifu wa kitu cha pili (Y), basi jina la kitu cha kwanza (X) linamaanisha kitu kile kile kilichotajwa kwa jina la pili (Y).

Hii maana yake ni kwamba, vitu viwli vilivyo sawa vina wasifu mmoja, kwa maana kwamba, kunakuwa na kitu kimoja badala ya vitu viwili.

Mfano, Ikiwa "Julius ni Kambarage" na “Kambarage ni Nyerere,” basi ni sahihi kwamba, "Julius ni Nyerere." Kimantiki, tunao uhakika huo kwa 100%.

Kuhusu utofauti wa vitu, kanuni hii inasema kwamba, ikiwa kuna kauli inayotaja kitu kwa jina moja (X), na kuna kauli ya pili inayotaja kitu kingine kwa jina la pili (Y), halafu ikathibitika kwamba idadi ya sifa zilizotajwa kwenye wasifu wa kitu cha kwanza (X) ni tofauti na idadi ya sifa zilizotajwa kwenye wasifu wa kitu cha pili (Y), basi jina la kitu cha kwanza (X) linataja kitu kilicho tofauti na kitu kilichotajwa kwa jina la pili (Y).

Mfano, Ikiwa "Julius ni Kambarage" na “Kambarage sio Nyerere,” basi ni sahihi kwamba, "Julius sio Nyerere." Kimantiki, tunao uhakika huo kwa 100%.

Pili, “kanuni ya kuepuka mkanganyiko,” yaani “the law of non-contradiction,” inasema kwamba, kila tamko husindikizwa na kauli ambayo ni kanusho la tamko, ambapo, tamko na kanusho lake haviwezi kuwa kweli kwa wakati mmoja na katika mtazamo mmoja.

Mfano, Kama tamko kwamba "Mvua inanyesha sasa hivi hivi Dodoma." basi, kanusho lake, yaani tamko kwamba, "Mvua hainyeshi sasa hivi Ddoma," ni tamko la uwongo. Tunao uhakika huo kwa 100%.

Hivyo, mtu akiunga sentensi mbili na kusema kwamba "Mvua inanyesha sasa hivi hivi Dodoma na Mvua hainyeshi sasa hivi Ddoma," anakuwa ametamka kauli unganifu yenye mkanganyiko.

Anakuwa ameongea kauli mbili zinazotaja kitu kisichowezekana, maana kauli ya pili inafuta kilichotamkwa na kauli ya kwanza. Yaani, mvua haiwezi kunyesha na isinyeshe katika eneo lile lile na katika wakati ule ule.

Kwa ujumla, mkanganyiko wa kimantiki unakuwepo pale tunapokuwa na seti ya matamko, ambayo hayawezi kuwa kweli kwa mpigo. Mkanganyiko huu hutokea kwa njia tatu, na hivyo kupata aina tatu za mikanganyiko.

Mosi, kuna mkanganyiko wa wazi (explicit contradiction) unaotokana na seti ya matamko kuwa na angalau matamko mawili yanapingana. Mifano:

  • “Afrika inazo nchi 54 ikiwemo Tanzanoa’; ‘kwa hiyo, Tanzania iko Afrika’; na ‘Tanzania haiko Afrika’.” Kauli ya pili na ya tatu zinapingana.
  • “‘Pembetatu inazo kona tatu’; ‘kwa hiyo, pembetatu sio mraba’; na ‘Pembetatu ni mraba.’” Kauli ya tatu na nne zinapingana.
  • “‘Watanzania wote huongea Kiswahili’; ‘Juma ni Mtanzania’; kwa hiyo, ‘Juma anaongea Kiswahili’; ‘Juma haongei Kiswahili.’” Kauli ya tatu na nne zinapingana.
  • "Dunia inalizunguka jua; na jua linaizunguka dunia."
  • "Mimi nakupenda; na Mimi sikupendi."
Pili, kuna mkanganyiko uliojificha na unaoweza kufichuliwa kwa kutumia kanuni za mchujo wa kimantiki kuzalisha hitimisho (formal contradictions), ambapo katika matamko yaliyomo kwenye seti huongezeka tamko moja jipya ambalo ni hitimisho, likiwa linapingana na madokezo. Mifano:
  • “‘Watanzania wote huongea Kiswahili’, ‘Juma ni Mtanzania’, ‘Juma haongei Kiswahili.’” Wakati kauli ya tatu inasema kuwa, “Juma haongei Kiswahili,” kauli mbili za kwanza, zinazalisha hitimisho kinzani kwamba, “Juma anaongea Kiswahili.”
  • “‘Pembetatu inazo kona tatu’; ‘mraba unazo kona nne’; na ‘Pembetatu ni mraba.’” Wakati kauli ya tatu inasema kuwa, “pembetatu ni mraba,” kauli mbili za kwanza, zinazalisha hitimisho kinzani kwamba, “pembetatu sio mraba.”
Na tatu, kuna mkanganyiko uliojificha na unaoweza kufichuliwa, sio kwa kutumia kanuni za mchujo wa kimantiki kuzalisha hitimisho, bali kwa kuongeza sentensi mpya ambayo unafahamika kuwa ni ya kweli (implicit contradictions), ambapo katika matamko yaliyomo kwenye seti huongezeka tamko moja jipya ambalo, sio hitimisho kutokana na matamko yaliyopo, lakini linapingana na matamko hayo. Mfano:

  • "Nina shauku juu ya ulinzi wa mazingira na mimi huendesha gari langu kila wakati badala ya kuchukua usafiri wa umma." Mkanganyiko utafichuka ikiwa sentensi ifuatayo itaongezwa: "Kuendesha gari binafsi kunasababisha uharibifu wa mazingira."
  • "Mimi ni rafiki mwaminifu na huwa sitoi msaada wakati rafiki yangu ana uhitaji." Mkanganyiko utafichuka ikiwa sentensi ifuatayo itaongezwa: "Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki."
  • "Mimi ni mtu anayewajibika na huwa nasubiri hadi dakika ya mwisho kukamilisha kazi." Mkanganyiko utafichuka ikiwa sentensi ifuatayo itaongezwa: "Mtu anayewajibika huchukua hatua mara bila bila kusubiri dakika za mwisho."
Na tatu, “kanuni ya pembetatu ya ukweli, uwongo na mashaka,” yaani “the law of the excluded middle,” inasema kwamba, kwa kila tamko la kweli husindikizwa na matamko mengine mawili, moja likiwa na kanusho lisilo kweli, na jingine likiwa kauli yenye mashaka.

Mfano, tamko kwamba, "Mvua inanyesha sasa hivi Dodoma," linasindikizwa na matamko mengine mawili, yaani, "Mvua hainyeshi sasa hivi Dodoma" na "Ama mvua inanyesha sasa hivi Dodoma au mvua hainyeshi sasa hivi Dodoma.” Katika mfano huu kuna mambo matatu yanawezekana:

  1. Tamko kwamba "Mvua inanyesha sasa hivi Morogoro" litakuwa ni kweli ikiwa limebeba ushahidi ulio juu ya 50%,
  2. Tamko kwamba "Mvua hainyeshi sasa hivi Morogoro" litakuwa ni uwongo ikiwa limebeba ushahidi ulio chini ya 50%, na
  3. Tamko kwamba "Ama mvua inanyesha sasa hivi Morogoro au mvua hainyeshi sasa hivi Morogoro” litakuwa ni tamko la mashaka ikiwa matamko mawili ya kwanza yana uwiano sawa wa ushahidi! Yaani kuna ushahidi wa nusu kwa nusu, ushahidi wa 50% kwa 50%, kiasi kwamba tunajikuta katika njiapanda ya ukweli na uwongo.
Kanuni hizi tatu zinaitwa kanuni za kimantiki. Lakini kuna jambo la ziada katika kanuni hizi.

Kwa kuwa tunatumia maneno kuwakilisha mawazo yetu kuhusu udhati wa vitu halisi vilivyoko katika ulimwengu ulioko nje ya vicha vyetu, hizi kanuni tatu za mantiki hutusaidia kujua ukweli kuhusu uhalisia wa vitu vilivyo katika ulimwengu huo.

Yaani, kanuni hizi hutusaidia kufahamu ni wakati gani kitu kipo na wakati gani kitu hicho hakipo hapa ulimwenguni. Katika ngazi hii zinabadilika na kuwa kanuni za kimetafizikia. Ni hivi:

Mosi, “kanuni ya usawa na utofauti wa vitu viwili," inamaanisha kwamba, “kila kitu kilichopo duniani kinao wasifu wake ambao ni seti ya sifa zinazotaja utambulisho wa kipekee wa kitu hicho.”

Yaani, hakuna vitu viwili tofauti vyenye idadi ile ile ya sifa zilizotajwa kwenye wasifu wa kila kitu husika.

Pili, “kanuni ya mkanganyiko wa kimantiki” inamaanisha kwamba, “hakuna kitu kinaweza kuwepo na kisiwepo pale pale na wakati ule ule.”

Hii, maana yake ni kwamba, “hakuna kitu kinaweza kuwa na wasifu wenye kutaja sifa fulani na kikawa na wasifu usiotaja sifa hiyo wakati huo huo, mfano, kuwa na namba shufwa na kutokuwa na namba shufwa.”

Pia, kanuni hii inamaanisha kwamba, “hakuna kitu kinaweza kuwa na wasifu wenye kutaja sifa mbili zinazobatilisha, mfano, kuwa na sifa ya utu na kuwa na sifa ya unyani pale pale na wakati ule ule.
Tahko (2009:32-33) anasema kuwa, kanuni ya kuzuia mkanganyiko ni kanuni ya kimetafizikia inayohusu muundo msingi wa uhalisia duniani.

Inataja mipaka inayohusu udhati wa mambo badala ya kuchukuliwa kama kauli ya kisemantiki pekee.

Kwa hivyo tafsiri ya kimetafizikia ya kanuni ya kuzuia mkanganyiko ni sawa na hii: vitu vilivyo katika ulimwengu halisi nje ya fikra za watu hutawaliwa na aina fulani za kanuni, ambapo kanuni mojawapo inasema kwamba, "sifa ile ile haiwezi kumilikiwa na kitu na isimilikiwe na kitu hicho wakati huo huo."

Kwa mfano, anasema, atomu haiwezi kuwa na protoni na isiwe na protoni kwa wakati mmoja; au kitu hakiwezi kuwa kijani kwa silimia mia moja na kikawa na rangi nyekundu kwa asilimia mia moja katika wakati mmoja.

Mifano hii inaonyesha kwamba udhati wa vitu (the essense of things) unaongozwa na kanuni ya kuzuia mkanganyiko.

Na tatu, “kanuni ya pembetatu ya ukweli, uwongo na mashaka” inamaanisha kwamba, kila kitu ama kipo, au hakipo, au hatuna uhakika kama kipo au hakipo.

Pia, kanuni hii maana yake ni kwamba, kila kitu ama kina sifa fulani au sifa iliyo kinyume na sifa hiyo, mfano, kila namba ama ni namba shufwa au sio namba shufwa.

Kwa kutumia kanuni zilizotajwa hapo juu, mchujo wa kiakili kwa ajili ya kuibua haki za binadamu kutokana na hulka ya binadamu ulifanyika kama kama inavyoelezwa hapa chini.


Haki za binadamu, sheria asilia ya maadili na sheria ya ufunuo

Mfano bora zaidi wa mchujo wa kiakili, ambapo haki za binadamu ziliundwa, unajioyesha katika mchakato wa kihistoria ulioleta Tangazo la Dunia Kuhusu Haki za Watu.

Kulingana na Luca Di Donato na Elisa Grim (2018:53-72), waandishi wa Tangazo la Dunia Kuhusu Haki za Bnadamu walifanya uchambuzi wa hatua kwa hatua wa kiakili, kama ifuatavyo:

Moja, walibaini kuwa, haki ya binadamu ni madai ya mtu mmoja, anayeitwa mleta madai, kuhusu kitendo fulani chenye kuhusiana na tunu fulani, madai hayo yakiwa dhidi ya mtu mwingine, anayeitwa mtekeleza wajibu, madai husika yakiwa yanatambuliwa na kanuni fulani, ama ya kisheria au ya kimaadili.

Mbili, walibaini kuwa, mleta madai na mtekelezaji wajibu ni binadamu, ambapo, binadamu anafafanuliwa kuwa ni kitu chenye mwili hai ulio kitovu cha akili, utashi na matendo huru ya kimwili.

Tatu, walibaini kuwa, kila binadamu anatenda kwa hiari na kwa kujua, chini ya udhibiti wa urazini, ambao unamruhusu kuamua mwisho wake mwenyewe kwa kuchagua mbinu na malengo baada ya kukagua malengo anuwai yanayowezekana.

Nne, walibaini kuwa, kwa mujibu wa asili ya mwanadamu, kuna tamaa asilia inayomwelekeza kila mtu katika aina fulani za tunu za kimsingi, tunu ambazo ni sababu zinazojulikana za matendo ya watu ya kila siku.

Akili ya binadamu huzigundua tunu hizi na nia ya mwanadamu lazima itende ipasavyo ili kujipatanisha na tunu hizi muhimu kwa ajili ya ustawi na ukamilifu wa kibinadamu.

Tano, walibaini kuwa, kila tunu ya msingi ni “hali ya mambo” ambayo kwa kawaida karibu wanadamu wote huvutiwa nayo.

Tunu hizi ni pamoja na maarifa, urafiki, muungano wa kijinsia, utunzaji wa watoto wa mtu, uzuri, mwelekeo wa kibinafsi katika kuchagua njia ya maisha, uadilifu wa mwili, uzalendo, mazoezi ya kimwili, na uhai ambao ni msingi wa tunu zingine zote. Bila tunu hizi za msingi binadamu hawezi kustawi.

Sita, walibaini kuwa, ni jambo la busara kwa wanadamu kufukuzia tunu za msingi na sio busara kuzishambulia tunu za msingi, kwa kuwa kwa kawaida, wanadamu tunafuatilia mambo yaliyo mema na yenye kuvutia, na tunaepuka mambo yaliyo mabaya na yenye kuchukiza.

Saba, walibaini kuwa, tunu hizi hazilinganishwi kwa kuwa hakuna kipimo chochote cha kawaida kwa ajili ya kuopima thamani ya kila mmoja kiasi kwamba tunu hizo mbili ziweza kupambanishwa kwa kusema tunu hii ni bora kuliko tunu ile.

Kwa maoni haya, ni makosa kusema kwamba ujuzi ni tunu ya thamani zaidi kuliko tunu ya urafiki au kinyume chake. Kila tunu ya msingi ina upekee wake.

Nane, walibaini kuwa, katika kuchunguza sifa za tunu za msingi, tunapata mfumo wa tunu asili ambao huweka msingi wa haki na majukumu yote.

Hii ina maana kwamba, tunapaswa kuangalia tunu za msingi kama malengo ya matendo ya kimaadili ambayo yanapelekea kustawi kwa utu wa mwanadamu.

Tisa, walibaini kuwa, kudai kwamba tabia ya kuvutiwa kufanya "jambo fulani" (X) ni jambo asilia, na hivyo kuhitimisha kwamba, tabia hiyo ni halali kimaadili, na kushuku uadilifu wa tabia zingine zote kwa sababu tu tabia hizi hazina uasilia, ni mtazamo wenye utata, kwa kuwa dhana ya “uasilia” inaweza kumaanisha mambo yafuatayo:

Kwamba "jambo fulani" (X) ama ni (a) tabia ya wastani kitakwimu, au (b) tabia ambayo watu wengi wanatarajia, au (c) tabia inayotokea kutokana na silika tu bila kufikiria, (d) tabia isiyo bandia, au (e) tabia inayosaidia kustawisha tunu za kiutu; ambapo, kwa kila mfano uliotajwa hapa ni rahisi kukumbana na pimgamizi, isipokuwa kwa mfano wa mwisho.

Kumi, walibaini kuwa, mfano mzuri wa mapingamizi yanayowezekana, ni kudai kwamba tabia ya kuvutiwa kufanya "jambo fulani" (X) ni jambo ambalo halina uasilia, na hivyo kuhitimisha kwamba, tabia hiyo ni haramu kimaadili, husababisha hitimisho lifuatalo lisilokubalika:

Kutumia vifaa vya kuboresha usikivu ni kinyume cha uasilia wetu na hivyo kitendo haramu kimaadili. Lakini hitimisho hili halikubaliki, kwa kuwa, kutumia vifaa vya kuboresha usikivu ili kuelewa wengine wanasema nini huendeleza urafiki na ni haki muhimu, wakati mwingine hata wajibu.

Kumi na moja, walibaini kuwa, kinyume na mfano uliotajwa hapo juu, tabia asili ya binadamu kuvutiwa na tunu fulani fulani unapaswa kutumika kama msingi wa kimaadili kwa kuzingatia mantiki ifuatayo:

Kigezo kinachofaa cha kuthibitisha kwamba tabia ya kuvutiwa kufanya "jambo fulani" (X) ni jambo asilia na hivyo kuthibitishwa kimaadili ni ukweli kwamba tabia hiyo inasaidia kustawisha tunu za ili kumsogeza binadamu karibu na ukamilifu wake. Hivyo, kwa sababu hii, “tunu hasi” kama vile “hasira” haziwezi kukubalika, japo ni tunu asilia.

Kumi na mbili, walibaini kuwa, kuelewa uhusiano kati ya tunu za msingi na ustawi wa watu namna hii ni katia muhimu ya kufafanua maana ya sheria asilia ya maadili.

Ni wazi kwamba, kustawi kwa tunu za kimsingi hutegemea uwepo wa nyenzo na mazingira rafiki kijamii, ambazo ni “manufaa ya wote.”

Kwa mfano, kustawi kwa tunu ya ujuzi hutegemea, kati ya mambo mengine, uwepo wa zana za mawasiliano.

Pia hutegemea uelewa wa lugha ambayo ni nyemzo ya kueneza maarifa ya kitamaduni. Maelezo kama haya yanazihusu tunu za msingi baki.

Hii maana yake ni kwamba, “manufaa ya wote” ni maneno yanayorejea hali mbalimbali za upatikanaji wa nyenzo za kijamii zinazotuwezesha kufukuzia tunu za kimsingi, pamoja na tunu za msingi zenyewe.

Kumi na tatu, walibaini kuwa, “manufaa ya wote” ni jumla ya nyenzo zinazohitajika kwa ajili ya kuendeleza maisha ya pamoja katika jumuiya ya kisiasa, ambayo ni pamoja na upatikanaji wa bidhaa na huduma za kijamii, kama vile barabara, bandari, na shule; huduma za kifedha, nguvu imara za majeshi; mfumo wa utoaji haki; urithi wa kumbukumbu za kihistoria na alama za utukufu Taifa.

Kumi na nne, walibaini kuwa, kanuni ya msingi katika sheria ya maadili asilia, kama ilivyoainishwa katika mambo yaliyojadiliwa hapo juu, ni kama ifuatayo:

“Tendo la kibinadamu litakuwa ni halali kimaadili ikiwa tu linachangia katika ustawi wa tunu ya msingi yoyote, na katika kufanyi hivyo, halihujumu kwa makusudi tunu za msingi baki.”

Na kumi na tano, walibaini kuwa, kanuni hii ya kwanza ya sheria asilia ya maadili inaweka msingi wa haki za binadamu zote. Hebu tuchunguze baadhi ya mifano.

Kuna haki ya kutouliwa na yeyote kwa kukusidia tena bila hatia, kwa sababu maisha ni tunu ya msingi. Kuna haki ya kutoshambuliwa kingono kwa sababu ukamilifu wa kijinsia ni tunu ya msingi. Kuna haki ya kutofanyiwa udanganyifu na serikali kwa kutekeleza sera za kilaghai kwa kwa sababu urafiki wa kisiasa kati ya raia na serikali yao ni tunu ya msingi. Zote hizi ni haki zinazotumia misamiati hasi, yaani “kutofanyiwa” moja, mbili, tatu.

Hebu sasa tuchunguze baadhi ya mifano ya haki za binadamu zenye misamiati chanya, yaani “kufanyiwa” moja, mbili, tatu.

Kuna haki ya kupata matibabu lakini haki hii ina masharti. Ni mara chache inawezekana kutoa huduma bora ya matibabu kwa kila mtu anayehitaji. Kuna haki ya kulindwa dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia lakini haki hii ina masharti.

Huenda kusiwe na taarifa na nyenzo za kutosha za polisi kulinda kila mtu aliye hatarini. Kuna haki ya uwazi wa serikali na mapitio ya umma, lakini tena haki hiyo ina masharti. Kuna vigumu kwa serikali kufanya sera zote kuwa wazi na kuwaruhusu watu wote kuzikagua kila wanapotaka.

Kwa njia hii, tunaweza kuendelea kutathmini haki zilizoorodheshwa katika katiba ya nchi na Tangazo la Gunia Kuhusu Haki za Watu, tukiwa tunabainisha aina ya tunu inayoongelewa katika kila haki iliyotajwa.

Kama ambavyo kuna tunu za msingi na tunu za ziasa, vivyo hivyo, kuna haki za msingi na haki ambazo sio msingi. Lakini aina zote mbili za haki zinatokana na mchujo wa kiakili bila kurejea popote katika misahafu ya kiufunuo.

Uhuru wa kidini ni mojawapo ya tunu za msingi

Hapo juu tumeona kuwa, kanuni ya msingi katika sheria ya maadili asilia inasema kwamba:

“Tendo la kibinadamu litakuwa ni halali kimaadili ikiwa tu linachangia katika ustawi wa tunu ya msingi yoyote, na katika kufanyi hivyo, halihujumu kwa makusudi tunu za msingi baki.”

Neno mahsusi katika kanuni hii ni "tunu ya msingi". Tumeona kuwa kuna tunu za msingi nyingi kama vile uhai, ukweli, na urazini.

Hapa, kwa kutumia mchujo wa kiakili unaoongozwa na sheria ya maadili asilia, nataka kujenga hoja kwamba "uhuru wa kidini" ni tunu ya msingi kama zilivyo tunu hizi baki.

Yafuatayo ni maelezo mafupi kuhusu dini ni nini, jinsi ilivyo tofauti, jinsi ilivyo kwa wote, kwa nini ni tunu chanya, na kwa nini kila mtu ana haki ya kuabudu kwa uhuru.

Ili kuelewa dini, tunapaswa kuchukua msimamo wa watu wanaofuata mafundisho ya kidini.

Wanahesabika katika mabilioni, wanaweza kupatikana katika kila bara, na kwa kipindi zaidi ya milenia moja.

Hivyo, tunapaswa kujiuliza, Watu hawa wanatafuta nini? Jibu ni kwamba wanatafuta majibu ya mafumbo ya maisha kutoka kwa nguvu ipitayo nguvu za kibinadamu.”

Yaani, "religion is man’s search for ultimate meaning of the mysteries of life and death, pain and happiness, goodness and badness” kama anavyoripoti Juan Manuel Burgos(2022:276).
Kisha, Juan Manuel Burgos (2022:277) anatwambia kwamba:

"God and religion constitute the response to the crucial questions of my life, questions that clamor for a solution. So, in a certain sense, one can affirm that every human being is necessarily religious, since inevitably, he or she has to stand before the ultimate questions and give an answer."

Hivyo, haki ya uhuru wa kidini imejikita katika hadhi ya dini kama tunu ya msingi ya kibinadamu, ambao hata hivyo inahusiana na tunu nyingine zilizo sehemu ya mfumo wa manufaa ya wote.

Ulinzi wa uhuru wa kidini, kwa hiyo, pia ni sehemu ya jukumu letu la kukuza na kuhami manufaa ya pamoja ya jamii ya kisiasa.


X. Hitimisho na mapendekezo

Hivyo, basi, Askofu Gwajima, awapo kwenye mimbari ya Kanisa lake, anayo haki ya Kikatiba Kufanya siasa ya kuhubiri Amri Kumi za Mungu, zikiwemo amri namba 6 na namba 8, zinazomaanisha kwamba:

  1. Usiue mtu yeyote asiye na hatia,
  2. Usiue jina zuri la mtu yeyote,
  3. Usiibe mali ya mtu yeyote, na
  4. Usiibe mtu yeyote kwa Kumteka na kumpoteza
Kwa hiyo kosa la Gwajima ni lipi? Hakuna.

Hivyo, barua ya kufuta usajili wa Kanisa la Gwajima ni batili, chini ya ibara ya 19 ya Katiba ya Tanzania Kama ikisomwa pamoja na ibara ya 13(6)(a) ya Katiba hiyo.

Na hii maana yake ni kwamba, serikali inabidi ichague kati ya mawili, ama kuendesha nchi kwa kutumia katiba inayoitambulisha Tanzania kama Jamhuri ya Kiliberali na Kidemokrasia au kuendesha nchi kwa kutumia Katiba ya kiimla kutoka nchi za ng'ambo zinazoendeshwa kisultani, kichifu, kimwami, kifalme, au kijeshi.

Vyovyote iwavyo, Wakristo na Watanzania wenye mapenzi mema na nchi, endeleeni kupigania:

  1. Upendo Tele,
  2. 𝗜mani Kubwa, na
  3. Matumaini Mapana
Sisi wanazuoni tunaendelea na tafiti makini ili kuwapatia chakuka cha kiroho wasomaji.

XI. Marejeo:

  1. "Amri Kumi za Mungu," Biblia, Kutoka (Exodus), 20:2–14.
  2. "Amri Kumi za Mungu," Biblia, Kumbukumbu la Torati (Deuteronomy), 5:6–18.
  3. "Sala ya Baba Yetu," Biblia, Mathayo, 6:9-13.
  4. "Sala ya Baba Yetu," Biblia, Luka, 11:2-4.
  5. "Amri Kuu Tatu za Yesu," Mathayo, 22:36-40
  6. "Uhuru wa Kuabudu," Katiba ya Tanzania (1977), Ibara ya 19.
  7. J. Caleb Clanton and Kraig Martin (2022), Nature and Command: On the Metaphysical Foundations of Morality (Knoxville, TN: The University of Tennessee Press)
  8. Holter, K. (2011), "The second Commandment and the Question of Human Dignity in Africa: A creation-theological perspective," Scriptura, 106:51-60.
  9. Juan Manuel Burgos(2022), Personalist Anthropology: A Philosophical Guide to Life (Delaware, USA: Vernon Press).
  10. Luca Di Donato and Elisa Grim (2018), ( Eds), Metaphysics of Human Rights, 1948–2018: On the Occasion of the 70th Anniversary of the UDHR (Delaware, USA: Vernom Press).
  11. Tuomas E. Tahko (2009), "The Law of Non-Contradiction as a Metaphysical Principle," The Australasian Journal of Logic, 7:32-47.
  12. Tore Lindholm (2004)(ed.), Facilitating Freedom of Religion or Belief: A Deskbook (Leiden: Martinus Nijhoff)





 

Attachments


Asante @dr mama amon for this literacy good job you did!, its very unfortunately jf ya sasa,hatuna members wa kusoma hizi literacy works kama hii and grasp,na wale vijana wa kule waliotamalaki humu,wako busy na trivia issues za nani kamtukana mama,na vi issuesvya mediocrity na sio serious issues kama hii.

ingekuwa ni jf ya enzi zile, kwanza bandiko hili linapigwa sticky, kisha linabebwa zima zima na kutua mezani kwake!.

Keep on。doing the good works that you do, Mungu akubariki sana!。
P
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…