Uhondo na mastori ya Nasri Mgambo

nasrimgambo

JF-Expert Member
Jan 10, 2017
1,898
2,459
wadau karibuni katika uzi wangu huu,

mimi ni mtunzi wa simulizi ninayemiliki blogi ya nasmgambo.blogspot. com

nawakaribisheni katika uzi huu kupata uhondo wa mastori yangu.
ambayo huwa naposti katika hiyo blogi, ila sasa nitawapostia ninyi katika uzi huu, na stori yangu ya kwanza kuwapostia ni hii ifuatayo;
 
JECHA! (Simulizi fupi)


Haikuingia akilini hata kidogo, haikumuingia akilini bi Ramla, hata kidogo.

Alisimama hapo mbele ya kioo cha maliwato ya wanawake akijiangalia.

Akijiangalia uso wake uliojaa machozi, pamoja na nywele zake zilizotimka timka kutokana na timbwili timbwili na kurushiana makonde na Indira, Indira ambaye alikuwa ndiye mchumba mpya wa bwana Hussein Jecha, ambaye ndiye alikuwa mume wa Ramla, wa zaidi ya miaka ishirini.

Yani huyo Hussein Jecha, alikuwa mtu wa ajabu sana.
Ati, miezi miwili mitatu hivi nyuma, alimtamkia mkewe bi Ramla kuwa hana tena mpango nae, hana tena mapenzi nae, na kwamba mapenzi yake juu ya mkewe huyo bi Ramla yalishakufa na hayakuwa yenye kuweza rudi tena kwenye moyo wake.

Bi Ramla wa watu alichanganyikiwa, kwa maana ndoa hiyo na familia yake ndivyo vilikuwa vitu vya thamani zaidi alivyoweza kufanikisha katika maisha yake, kamwe hangeweza kukubali vitu hivyo visambaratike.

Akaamua ya kwamba, kwa kila hali lazima ahakikishe anafanya harakati za kujaribu kudhibiti ndoa yake isivunjike, katika harakati hizo, Ramla akagundua mumewe ana mahusiano na mwanamke mwengine, ambaye ndo huyo aloitwa Indira.

Tena mbaya zaidi iliyomuuma Ramla ni pale Bwana Hussein alipomtamkia mkewe kuwa katu hatoweza achana na huyo Indira.

Maskini mwanamke wa watu!,
Ramla akaanza kujibadilisha mionekano, mara akaanza na kubadili hata manukato alotumia na akabadili kauli na sauti na kujishusha saana, eti apendwe upya na mumewe,
Ila wapi!

Ndo kwanza Bwana Hussein akamtolea kauli ya 'shombo', eti "bibie, nafahamu unatamani sana kufanya ndoa hii iendelee, na naona juhudi zako mama, mana naona tena uko hima, mara upake hina, mara na upake rangi vidoleni na ilhali si kawaida yako, mara kila uchwao ununue kufuli na sidiria mpya za kuvutia ukiamini utanivutia, hakika nashukuru kwa hilo maana unanisisimua na kuninyemshanyemsha kihisia, ila la! baada yaa mechi moyo wangu unaanza kumkumbuka bi Indira."

Kauli hiyo ya bwana Hussein alimtamkia huyo mkewe Bi Ramla wakiwa chumbani kwao kwenye tanda lao la mechi la sita kwa sita. Tena usiku huo Ramla alidhani kamkosha kweli beberu hilo kumbe maawee! jitu lake halina shukrani ndo likamtolea kauli hiyo ya 'shombo'.

Kama hiyo haikutosha ikatukia siku moja bi Ramla kamfuma mumewe akiongea na huyo Indira kwenye simu, maongezi yenyewe bwana Hussein alikuwa akimsifu Indira, "wallahi naapia, najutia kuchelewa kukufahamu mwali Indira, wewe mtoto uloumbika, umbo ka nane namba munu alivyokuumba, na hayo machoyo we mwanamke ka ushanyonya wida, akili ishadata juu yako."

Eti! kusikia Indira akisifiwa hivyo kwenye simu michozi tiii ikaanza kumshuka bi Ramla, maaawe!

Loh!, kama haikutosha Ramla akaanza kumsikia mumewe akimsengenya
"yani Indira mtoto mzuri nakuapia, huyu mke wangu mwezi huu hauishi nampa talaka tatu, aende zake"
"yani nimemkinai hasaa, kwa mapenzi unayonipa unanifanya nijiulize sana, juu ya hivi nimewezaje ishi na hili janamke zaidi ya miaka ishirini"

hapo michozi kudadeki ndo ikazidi kummiminika bi Ramla wa watu, macho yakaanza na kuwa mekundu ka mfiwa maaaawe!

"yani huku bara kuna wanaake wengine wa ajabu ajabu, sasa kama huyu bi Ramla kwa jinsi alivyo mwanamke aliyekosa sifa wallahi naapia kanifanyia uchawi wa kabila lao, wallahi limbwata waziwaazi kanifanyia huyu mwanamke, hata sielewi nilimpendea nini"
"wallahi mi naona ni mihemko ya mwili ndo ilinipeleka nikamuoa, ila hana sifa za kike"

hapo Ramla akakosa uvumilivu akalia kwa nguvu na kumfuata mume wake humo sebuleni hadi kochini alipojilaza eti amnase vibao.

Hussein Jecha alipoona mkewe anamvamia kwa kilio na makofi, akajiinua haraka toka kochini na kumdaka mikono. Na wakaanza kugombana kwa sauti kubwa.

Mwisho wa ugomvi wao, Hussein akamtamkia mkewe kuwa anamwandikia talaka amuache, kitu ambacho Ramla aliogopa zaidi. Kisha Huseein akatoka zake nje ya nyumba hiyo, na vile ilikuwa usiku hakurejea tena usiku huo.
Ramla wa watu alibakia kochini akitizama saa ya ukutani ikisoma namba, saa nne, saa tano, sita saba, nane hizo zote za usiku, akaona huyo mtu hangerejea usiku huo, akajiinua na kutia kufuli mlango wa nyumba na kuendea dirisha kuchungulia nje.
aliuona usiku huo ulikuwa ule usio na mbalamwezi usiku wa giza totoro.
huku machozi yakimtiririka bi Ramla alikumbuka jinsi miaka ishirini ilopita alivyokuwa akisimama dirisha hilohilo na akichungulia vivyo hivyo, ila kwa tabasamu na hamu na ghamu ya kumuona bwana hussein akirejea, enzi hizo alizokuwa akimkaribisha mumewe kwa bashasha na mbwembwe na mapenzi, ila sasa alisimama hapo na uso wa huzuni, machozi, macho mekundu na juku akielewa fika hatorudi tena usiku huo mana Indira, alishateka akili ya mwenye nyumba.

Siku zilizofuatia Jecha hakurejea kwake kabisa na hakupokea simu za mkewe.

Siku moja ikatokea jirani mmoja mdaku kamuona Jecha na Indira waakielekea pamoja kwenye sherehe ya harusi ya watu fulani ambao yeye Ramla hakuwafahamu, tena katika kuuliza vizuri jirani huyo alimwambia Ramla kuwa mumewe alikuwa anaelekea ukumbi wa uloitwa "Primrose Hall" ulokuwako pande za Mbezi Beach, huko kulikuwa na harusi ya binti ambaye alikuwa ni mpwa ake Indira na kuwa kilicho mpa jeuri hiyo Indira kumpeleka Hussein Jecha kwenye hadhara ya nduguze bila aibu ilikuwa ni kwamba Hussein kesha mchumbia Indira, na kuwa siku si nyingi wangefunga ndoa, na Jecha alijitangaza mitaani kote alikofahamika kuwa anaachana na mkewe kwa talaka tatu.

Ramla, ilimuuma sana, ila safari hii akajikaza kaza na akaelekea hadi huko Mbezi Beach na gari ake.

Wakati anaweka gari lake katika maegesho ya magari ya ukumbi huo aliliona gari la Hussein.
Akatamani ashuke humo garini na kulipasua pasua gari hilo.
Ila akaona walinzi wangemkamata.

Akafikiria aelekee ndani ya ukumbi huo kwenye hiyo harusi ya mpwake Indira, akakumbuka hana kadi ya kuingilia. Akabaki kakaa kwenye gari hadi akawaona walinzi wa maegesho kupitia vioo vya kuonea nyuma wakiongea jambo huku wakitazama gari lake

Akahisi huenda walinzi hao walishangaa kwanini hakutoka garini muda wa zaidi ya robo saa baada ya kuegesha gari.

Akaona hataki kuvutia hao walinzi.

Sasa akaamua kutoka garini na kuelekea humo ndani ya ukumbi.
Huku akiwaza atachoenda fanya, aliwaza gomvi ataloenda fanya kwa Indira mbele ya familia yake na jinsi atavyomuanika
Hussein na kumtia aibu.

Moja kwa moja Ramla akapanda ngazi na kuelekea ghorofa ya pili ya jengo hilo la 'Primrose' ambako ndiko kulikuwa na sherehe ya mpwae Indira.

Kufika langoni akabaini watu wa kamati waliopo mlangoni hawakuwa makini sana, hivyo akaingia tu humo ndani ya holi moja kwa moja.

Ukumbi ulikuwa umependeza na huyo mpwae Indira alikuwa yuko mbele pamoja bwana harusi tena skrini kubwa ya ukumbi huo ili muonesha binti huyo hivi kwamba woote waliokuwamo humo ukumbini, hata walokaa nyuma walimuona vizuri binti huyo maharusi.

Ramla akapitisha macho yake na kumuona Jecha kakaa na Indira wake.
Midomo wamekenua huku wakichekelea yaliyojiri harusini humo.

Kwa hasira Ramla akamuelekea mumewe na alipomfikia akamrushia kofi kwenye shavu la kushoto kisha akatupia mikono yake kichwani mwa Indira na kuanza kumvuta wigi ya 'brazilian hair' alilovaa mwanamke huyo huku akimrushia makofi, magumi na makwenzi ya kichwa kudadeki zake!

ukumbi mzima uka geukia meza hiyo.

Jecha akamkamata mkewe na kumsukumia pembeni kisha akamkumbatia Indira ambaye sasa alikuwa minywele tim tim na macho yaloshtuka kwa hofu na woga kama jizi la nguo lilokamatwa kariakoo mtaa wa kongo, kumbe jizi la mwenza wa mtu.

walinzi na watu wengine wakafika hapo kwenye meza hiyo na kumkamata Ramla.

Ramla akaanza kupayuka kuwa Hussein na Indira ni wagoni, kuwa yeye ndiye mke halali wa Jecha.

Jecha na Indira nao kwa upande wao walimjia juu na mitusi, tena ya nguoni.
Aibu ikatamalaki ukumbini humo, mwali harusi machozi yakimlenga kwa jinsi shangazi ake kamletea vurugu kwenye harusi yake.

Basi Ramla akatolewa ukumbini humo ila ajabu alipotoka tu humo ukumbini kwa nguvu za ajabu alijitoa mikononi mwa hao walomshikilia na kuwachoropoka na akazamia maliwato ya wanawanake ilokuwapo jirani na lango la ukumbi alimotolewa.

Na alipoingia tu akajifungia hata wakashindwa kuingia kumtoa.

Basi alipoingia humo akaelekea kwenye sinki na kioo na kusimama hapo na kujia galia manywele yake yalotimka na macho yake ambayo sasa yalianza kujawa na machozi.

na akawaza alichotoka kukifanya na akawaza kuwa sasa kweli Jecha aliamua kuwa ndoa yao ivunjike.

Haikumuingia akilini kabisa, iwaje Jecha aachane nae, yeye Ramla waloishi pamoja kwa zaidi ya miaka ishirini, ambaye tena kwa muda huo wote walikuwa washajijenga na hata walikuwa na mtoto mkubwa kabisa mwenye umri wa miaka ishirini na tatu, kijana aliyeitwa Waimani. eti kisa kiwe ni Indira, hata yeye Ramla aachwe.

Ramla alijiangalia hapo kwenye kioo cha maliwato kisha akanyanyua mikono yake na kuitupia kichwani kisha akafunga nywele zake vizuri, na kisha akajifuta machozi.
kwa mda akatupia viganja vyake usoni mwake na kujipapasapapasa kwa muda, kisha akageukia mlango wa maliwato hiyo na akatoka nje.

.....................................
.....................................

Majira ya saa nne za usiku, ndio Ramla aliwasili nyumbani kwake, mitaa ya Msasani.
Akiwa anaingia na gari lake alishangazwa na taa zilizokuwa zikiwaka kwenye vyumba vya nyumba hiyo, pamoja na mziki uliokuwa ukipiga toka sebule ya nyumba hiyo.

ikabidi amuulize mlinzi ndani kuna nani, ilhali hakuacha mtu katika nyumba hiyo siku hiyo.

Mlinzi ndo akamuambia kuwa mwanae Waimani alikuwa karejea toka huko chuoni Dodoma.

Ramla akashuka toka kwenye gari lake na kuingia ndani ya nyumba. Moja kwa moja akaelekea, hadi sebuleni na kuzima mziki uliokuwa, ukipiga, toka spika za sebuleni humo.

Mara Waimani, alokuwa yumo humo ndani akaingia sebuleni kwa furaha, "supriiiiiise" alimshtua mama ake

yani Waimani alisafiri toka huko chuoni kwao UDOM hadi hapo kwao Msasani kwaajili ya likizo na lengo la kufanya hivyo lilikuwa ni kumsuprise tu mamake.

Kwanza mamake hakuwa katika mudi ya kusapeaiziwa, na hakupenda hiyo sapraizi

"sasa wewe ungepata tatizo njiani, unadhani nani angefuatilia kujua umepatwa na nini humo njiani", aliongea Ramla, hakuwa kafurahia hiyo sapraizi yenyewe.

Sasa, Waimani akamuuliza mama ake babake yuko wapi hata usiku huo hakuwapo, ndipo Ramla akamkumbatia mwanae na kuangua kilio na kisha kuelekea kwenye kochi na kuanza kumsimulia kuwa Jecha siku hizo alishahamisha makao toka kwenye nyumba hiyo hadi kwenye maskani yake mpya kwa mwanamke aliyeitwa Indira.

Waimani aliyekuwa hana maelewano mazuri na babake toka zamani alijikuta kupatwa na hasira sana kwa mambo ambayo baba yake alikuwa anayafanya.

basi akachukua simu na kumpigia babake, na mazungumzo yao yalikuwa ya kuzozana na zogo kubwa.

"yani we mzee unatukatisha tamaa, na unazeeka vibaya mimi nakwambia, we rika hilo la kuacha mkeo na familia na kufakamia mashangingi"
"unasikitisha babangu, yani wewe mzee badala ya rika hilo kuacha mambo ya hovyo ama kumrudia mungu ndo kwaanza unafanya mambo ya kufanya mimi mtoto mdogo ili wewe mtu mzima unionye, ila eti mimi leo ndo wa kukutoa wewe akili"

"ama kweli mimi baba sina, yani wazee ka nyie hata pepo za mungu hamtakaa mzione na ndo mnaotuletea mikosi ya kimaisha, kwa mambo ya hovyo mtendayo, yani matendo yako we mzee hata mungu, manabii zake na malaika zake wote wanayachukia, mana si matendo ya akili za binadamu mtu mzima alokamilika kichwani, una matatizo we mzee",

mineno mizitomizito ilimtoka Waimani akimwambia babake, kijana alijikuta kafyatuka kichwani.
Ila Hussein Jecha nae akili zake alizijua mwenyewe, wala hazikuwa ndefu bali fupi ka za Waimani, mana nae akatamka maneno mazitomazito pia.

"wewe mtoto kama mamako kakutuma unitusi katika simu mwambie anakupoteza. tena anakupoteza hasa. mana sasa mtoto kama wewe ndo hukosa radhi za mzazi na wewe nishaona nitakuachia radhi wewe uwe kichaa mbwa wewe"

"unarumbana na mimi ka unabishana na njuka wezio wa huko vyuoni, tena ukiwa upo chini ya paa ya nyumba nilojenga mimi kwa pesa zangu, kuku wewe"
"shika adabu wewe Wainani, unakaa tu huko chuo unakula unak*nya, bure kabisa, ni mimi ndo nakugharamia mpuzi wewe"

"huna adabu hata kidogo, sasa mwambie mamako kwa aloyafanya mbele za watu yamempa talaka, na wewe na mamako mjipange pa kuhamia mnaondoka chini ya paa la hiyo nyumba siku si nyingi, shenzi sana"

mineno hiyo ilimtoka Jecha na kisha akakata simu.

ilikuwa ni mshikemshike kwenye familia hiyo, ya mzee Jecha.

...................

kesho yake asubuhi, Ramla alikuwa keshavalia kwenda ofisini na alikuwa akiagana na Waimani ndipo mara wakasikia geti likifunguliwa na gari likiingia nyumbani hapo,

Ramla akakimbilia kwenye dirisha la sebuleni nyuma yake Waimani alimfuatia kuchungulia hapo dirishani na wakaona kuwa ni Hussein Jecha ndo anawasili hapo nyumbani.

Kwa haraka wakatoka hapo dirishani na kutoka sebuleni humo kuelekea nje barazani, mama mbele mtoto nyuma na wakakutana ana kwa ana na Hussein Jecha, aliyekuwa akitaka kuingia ndani ya nyumba hiyo.

Jecha akijivimbisha uso, huku mkewe nae kajivimbisha uso na mkono mmoja kautupia kiunoni mwake, huku Waimani akiwa nyuma ya mamake akiwa kajivimbisha uso kwelikweli huku kamtolea macho babake.

mineno ikaanza kumtoka bi Ramla,
"mimi na mwanangu, hatubabaishwi na wewe dume la shupaza, baba mtu mzima uliye hovyo" "unaeacha familia yako na kufakamia mashangingi ya mjini, na utakufa darisalama hii kwa ushamba ako ka si kwa ukimwi basi huyohuyo mwanamke wako atakumaliza, na atakufilisi ufe kapuku"

Jecha akajikuta akinyanyua mkono wake amrushie mkewe kofi la nguvu, mara Waimani akaingia kati akajiweka mwili wake yeye na kumuweka mamake pembeni,
"piga mimi, wewe ka una nguvu piga mimi" aliongea Waimani.

huku mamake akijikuta kujua akamsogeza Waimani pembeni na kujiweka tena yeye, "muache anipige, muache athubutu tuone, anajikuta ujanja wa jogoo kujitutumua kwa mabavu, kudadeki zake tutampasua na kumnyonganyonga mxiiiiiiew"

Jecha nae, aliyekuwa pande la mtu alikuwa si mtu wa kupepeswa pepeswa, hivyo akawapa maneno yao nao,
"wewe na mwanao hamfahamu kimbunga mnachochezea, nitawatafutieni siku yenu manyang'au ninyi kazi kubishana na mababa wenye nyumba, mnabishana na vichwa vya familia, punguani kweli ninyi, hakika mnahitaji vipimo kubaini kama mu wazima kwenye hivyo vichwa kuku ninyi pambaf", Jecha alitoa kauli hizo chafu kwa mkewe na mtoto.

Kisha akaingiza mkono wake mfukoni kutoa bahasha na kuwaning'inizia, "hii muonayo nyie ndama mmoja na mamake ni talaka tatu talaka tatu, pambaf zenu, nawakata ka nilivyowaahidi, mashudu nyinyi" alitamka Jecha na kumtupia mkewe hizo akizodai ni talaka tatu usoni.

Ramla sasa akashindwa kuvumilia michozi ikaanza kumshuka tena na akaanza kupayuka.

"wewe mwanaume si mzima, una matatizo hakya mungu, tena matatizo makubwa", alilia Ramla huku Jecha akiondoka zake akielekea gari yake.

Waimani hakukubali akaona lazima ampe mzee huyo japo ngumi moja ya uso.

hivyo basi Waimani akamfuatia kwa nyuma mzee huyo na kwa haraka kabla mzee wa watu hajapanda gari yake Waimani akamtupia kabali moja ya shingo na kumkaba kwa nguvu.

Ila Jecha alikuwa pande la mtu alijibidua kidogo tu na kujitoa mikononi mwa Waimani na akamgeuzia kibao mtoto huyo kwa kumtupia ngumi zito kwenye shavu lake la kulia na kumfanya amtoe damu na kisha akamtupia ngumi shavu la kushoto na kumuangusha kabisa.

Ramla huku akipiga mikelele akamkimbilia mwanae huku akimlani Jecha.

Waimani akajiinua hapo chini huku machozi yakimlengalenga na kumtoka machoni na mkono mmoja kashikilia mdomo wake wenye damu, akatema damu toka mdomoni, mamake alipomfikia akamsogeza nyuma kuwatenganisha kisha kwa kufoka akamuomba Jecha aende zake na mzee huyo akapanda gari yake na kusepa.

Nyuma akamuacha Ramla akilia na kumuuliza mwanae kaumia kiasi gani huku Waimani machozi yakimtoka kwa kutoamini kuwa mikonde alokula alipigwa na babake, hakuwahi kufikiri babake angeweza kufikia kumpiga, hakufikiria hivyo, sasa aliona kuwa mzee wake ni mwenye roho ngumu sana.

siku ilianza vibaya.

Ramla akaelekea kazini kwake, lakini siku aliwahi kurudi mapema.

..........

Jioni ya siku hiyo baada ya kukaa kwenye kochi muda mrefu wakimlani Jecha, Ramla akaamua atoke aende kununua vitu vya kutumia hapo nyumbani na Waimani akang'ang'ana waende wote.

Basi wakainuka na kwenda huko kwenye manunuzi sokoni ila wakiwa huko wakaamua waelekee kwenye 'shopping mall' kabisa, tena wakaelekea kwenye moli maarufu iloitwa jina la 'Dar free market'.

Wakiwa huko mara kwa mbali Ramla akahisi kamuona Indira, kavalia nguo nyekundu, akamtazamaa kisha taratibu bila kumuaga Waimani akamfuata huyo Indira huku kahamaki na hasira zikimjaa kadiri alivyozidi kumfikia, na akamfikia na kumvuta mkono kwa hasira, ndipo huyo mwanmke alovutwa mkono akageuka,
kumbe hata hakuwa Indira, bali Ramla alifananisha. Huyo mwanamke alishtuka sana kwa jinsi alivyovutwa mkono na Ramla, na Ramla akabaki akiomba msamaha na kujieleza kuwa alimfananisha na mwanadada mwengine.

Kisha Ramla akarejea alipomuacha Waimani.

Muda mfupi baadae, Ramla na mwanae wakiwa wanatoka kwenye moli hiyo, huku wakielekea garini na mizigo yao, kwa mbali kwenye maegesho ya magari ya moli hiyo waliona gari ya Jecha.

Na mara wakamuona Jecha mwenyewe akiongea kwa furaha na Indira nao wakitoka humo kwenye moli wakielekea kwenye maegesho ya magari, huku wakionekana kuwa ni wenye furaha kwelikweli, huku wamebeba mizigo yao.
Walipofikia gari la Jecha wakaweka mizigo yao humo na wakawa wamesimama kwa pembeni wakiongea, na huku Indira akiwa anajipiga selfie.

Wakiwa wamekaa kwenye gari, mtu na mamake, Waimani na bi Ramla waliwakodolea macho hao Jecha na Indira, huku mioyoni mwao wakiwa wameudhika na hasira zikawapanda hasa, Ramla akajikuta akiwasha gari
huku macho kamtolea Indira alokuwa kasimama pamoja na Jecha.

Wao Indira na Jecha hawakuiona gari ya Ramla.

Kichwani mwake Ramla alitaka kwenda kumgonga na kumkanyaga kanyaga Indira kwa gari na kumuulia hapo.

Basi Ramla akawasha gari na kuiondoa kwa kasi kuelekea waliposimama Indira na Jecha, hata Waimani humo garini alishtuka, hadi hapo alikuwa bado hajatanabahi dhamira ya mamake kuwa ilikuwa ni kummaliza Indira.

Kwa tukio la haraka sana Jecha alishaangaa kuona gari lililo kasi likimuelekea Indira, na kwa haraka sana aka msukumia Indira pembeni na akajiweka yeye mwili wake na gari hilo la Ramla likamgonga yeye Jecha na kumsukumia kwa mbali kwa kumrusha kabisa na akaanguka huko puuu!.
Ramla baada ya tukio hilo akapiga breki kali sana na akasimamisha gari huku haamini kuwa kamgonga Jecha na si Indira.

Waimani alishtuka sana kwa kile ambacho mama yake alitoka kukifanya.
Japo babake alikuwa na mambo ya 'kiduwanzi', Waimani hakufikiria mamake angeweza kumgonga babake na gari, kwanza alimpenda sana babake japo kukorofishana ilikuwa ndio ada yao.

Kwa kuchanganyikiwa kabisa Waimani aliteremka kwenye gari na kumfuata baba ake alipoangukia, huku Indira nae ambae alisukumiwa pembeni ili asigongwe na gari, akawa keshainuka kasimama kando ya Waimani, pahala hapo Jecha alipoanguakia.

"Jecha, Jecha", alipayuka Indira na kumfikia Jecha na kumsukuma Waimani huko pembeni na kumshikilia Jecha kwa uchungu wa hali ya juu na kuangua kilio, mara, Ramla akawa keshashuka kwenye gari kakaribia hapo Indira alipomshikilia Jecha, nao walinzi wa mahala hapo na mashuhuda wenginewe wakawakimbilia pahala hapo kutoa msaada.

Jioni ya siku hiyo Jecha alilala hospitali, kutokana na kuvunjika kiuno, huku mkewe bi Ramla na mtoto wao Waimani Jecha walilala rumande, kituo cha 'central' barabara ya Samora.

..............
..............

Siku moja miezi michache badae, watu walifurika, mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, kwa lengo la kusikiliza hukumu atakayopewa bi Ramla na mwanae Waimani.

Wengi ya watu walisikitika sana kilichoipata famila hiyo.
Mana ilikuwa kama riwaya ya Eric Shigongo.

Wakati watu wako mahakamani, Jecha mwenyewe alikuwa kashindwa kufika hapo mahakamani kutokana na ulemavu wa kupooza viungo aloupata.
Mana sasa alikuwa kabaki kichwa tu, mwili wote umepooza, na bado alihitaji uangalizi wa daktari.

Zamu ya kutoa ushahidi ya bi Indira ilipowadia, Ramla na mwanae waliudhika sana mwanamke huyo alijiliza na kuongezea chumvi na kudai ni njama za Ramla na mtoto wake kutaka kumuua tu Jecha ndicho kilichopelekea kwa maksudi Ramla na mwanae kumgonga kikatili bwana Hussein Jecha na kumtia ulemavu.

"mhesshimiwa hakimu, hakika sijawahi ona mwananke mwenye roho ya ajabu kama huyu bi Ramla, mwanamke awezaye kumgonga na gari baba wa mtoto wake tena, na hakika sijawahi ona kijana mwenye roho mbaya kama huyu Waimani Jecha, ambaye ana uwezo wa kuthubutu kula njama na mamake kwa lengo la kukatisha uhai wa babake, ila mungu wetu aliye mkuu mwingi wa rehma na mwenye kuneemesha na kurehemu
ameepusha mauti kwa bwana Jecha, japo wamemtia ulemavu"

"mheshimiwa hakimu matendo maovu ya hawa bi Ramla na mwanaye yamepelekea kukatisha ndoto zangu na mchumba angu, mzee Hussein Jecha za kufunga ndoa" aliendelea kuongea Indira, huku akiwa kasimama kwenye membar' akishuhudu mbele ya hakimu.

Basi baada ya kusikiliza pande zote za washtakiwa na upande wa Indira na mashuhuda wa kosa hilo la jinai, hatimaye hakimu akatoa hukumu yake.

Bi Ramla, mtaliki wa Jecha akahukumiwa kwenda jela miaka kadhaa na Waimani Jecha akaachiwa huru, kwa maana mahakama iliona kuwa kitendo cha Waimani kuwapo garini muda wa tukio hakukuthibitisha kuwa alipania ana alipanga pamoja na mamake kumgonga Jecha na gari, hata kama kijana huyo alionekana kuwa aliyekosa maelewano mazuri na babake siku chache kabla ya tukio la babake kugongwa kwa gari bado haikuwa sababu tosha ya kuthibitisha juu yake hatia ya kudhamiria babake agongwe na gari kwa makusudi na mamake.

Baada ya hukumu hiyo Waimani alirudi chuo kumalizia semista yake ya nwisho, huku jitihada zote za kufanya mawasiliano yeyote na babake zilizuiliwa na bi Indira.

Uovu wa Indira haukukomea hapo,
Sasa akamjaza fitna Jecha, hivi kwamba mzee huyo akataka kuuza nyumba ambayo Waimani aliishi, ambayo Jecha aliijenga enzi yupo na bi Ramla.

Safari hiyo kesi ikawa kubwa hata zaidi, Indira akiwa kidete upande wa Jecha kuwa nyumba ni ya Jecha hivyo iuzwe na ikiwezekana mali zote za familia hiyo zigawanywe.

Nao upande wa Waimani na mamake wakajitetea kwa vielelezo na hoja kuwa mali nyingi ikiwamo nyumba ambayo Waimani anaishi zilichumwa Jecha alipokuwa na Ramla hivyo mali hizo haziwezi uzwa wala gawanyishwa bila kuhusishwa kwa bi Ramla.

Hatima yake mahakama ikaamuru nyumba hiyo ibaki kuwa mali ya Bi Ramla na mwanae, Waimani huku Indira na Jecha wakabaki na mali nyenginezo.

Miezi kadhaa mbele Jecha alifariki, katika kile kilichosemekana kuwa aliugua ghafla na maelezo mengineyo ambayo Ramla na Waimani hawakuyaelewa na wakaona kafa kwa mkono wa mtu tena si mkono mwengine bali wa bi Indira.

Na hisia zao hazikwenda patupu, maana baada ya mazishi ya bwana Jecha, wosia ukasomwa na kuonesha mali zote alizoacha Jecha mrithi ni bi Indira.

Ramla alikuwako jela wakati huo alihuzunika sana kupata taarifa hizo za mgawo wa mirathi.
Na Waimani hakuwa na la kufanya zaidi tu ya kumuombea dua babake huko aliko na kumuombea asamehewe dhambi zake.

Watu wengi walomfahamu bwana Jecha enzi za uhai wake walisikitika sana, almarhum Hussein Jecha alikuwa bosi mwenye cheo kikubwa katika shirika moja la hifadhi za jamii.

Watu walisikitika jinsi bwana Jecha alivyoisambaratisha familia yake yeye mwenyewe.

Kwa upande wa Indira ambaye hadi Jecha anakufa alikuwa mchumba wala alivyoisambaratishaj mke, alijiingiza kwenye starehe kabla hata mwaka hauja katika na akamsahau kabisa bwana Jecha.

Miaka miiingi ikapita, ila mara ya mwisho Indira kusikika masikioni mwa Waimani na Bi Ramla ilikuwa alikuwa kaolewa na tajiri mmoja jijini aliyesemekana akijihusisha na kuuza mihadarati ya heroine na cocaine na pia aliyehisiwa sana kuwa alipata kuwa jambazi jijini huko miaka ya nyuma. Na walisikia kuwa Indira hasaa alikuwa kahamisha makazi toka nchini na kuwa anaishi huko jijni Lagos nchini Nigeria na mme wake muuza unga.

MWISHO....
 
Back
Top Bottom