Inakubalika katika mitazamo ya watu kadhaa,kwamba vyombo vya habari ni mhimili wa nne wa dola. Ni dhahiri mhimili huu ukiendelea kuliwa na mchwa(ufisadi,rushwa au takrima na ukengeufu kimaadili)dola itaporomoka na mahali pake litasimama chukizo la uharibifu litakalowatesa raia wasio na hatia hadi siku watu wema watakapoamua kuingila kati kwa nguvu zao zote.
Mlio na dhamana ya kuuendesha mhimili wa nne hatutegemei muisaliti jamii kwa manufaa ya mafisadi wachache. Eti nini,mwapewa vihela ili msafishe majina yao! Kabla hamjavipokea,mwogopeni Mwenyezi Mungu aliyewaumba watanzania,fikirieni madhara ya tendo hilo kwa watu milioni 40 walio hai na wengine watakaozaliwa baadaye, angalieni msishiriki dhambi ambayo si yenu ili hukumu halisi itakapoanza mpate pa kuponea.
Watanzania hawajashindwa kuamua kutonunua magazeti yatakayojaribu kuwaambia eti fulani msafi ilihali uchafu wake unaonekana kwa macho pasina miwani. Anayetaka usafi atokeze hadharani atubu dhambi zake alizoutendea umma wa watanzania.
Watanzania hawajashindwa kususia kupeleka matangazo ya biashara na mengine katika vyombo vya habari vitakavyoendeleza usaliti.
Tufike mahali vyombo vya habari vyote, nasema vyote viwe mstari wa mbele katika vita dhidi ya wanaoliangamiza taifa.
Aidha haitatosha tu kuwa na habari na mijadala juu ya ufisadi huu ama ule bila hatua kuchukuliwa. hapa naukumbuka usemi usemao, Njia pekee inayouwezesha uovu kutamalaki ni watu wema kutofanya chochote. Asomaye na aelewe.