Tamko la wasomi kuhusu ufisadi

Judy

Senior Member
Aug 13, 2007
191
4
TANZANIA HIGHER LEARNING INSTITUTIONS STUDENTS ORGANIZATION.
(TAHLISO)
P.O BOX 35080 DSM Email; tahliso2006@yahoo.com
Mobile +255 754 629 322 juliusmtatiro@yahoo.com
+255 755 855 144
+255 717 233 551
Date; February 23, 2008

TAMKO LA UMOJA WA WANAFUNZI WA VYUO VYA ELIMU YA JUU TANZANIA (TAHLISO) JUU YA UFISADI PAMOJA NA BEI GHALI ZA UMEME ZINAZOWAKABILI WATANZANIA WENGI.

TAMKO HILI LIMETOLEWA KATIKA MIKOA TOFAUTI BAADA YA MAANDAMANO YALIYOHUSISHA WANAFUNZI NA WANANCHI KATIKA MIKOA YA IRINGA,MOROGORO,MOSHI,ARUSHA,ZANZIBAR, MWANZA na DAR ES SALAAM,MAANDAMANO HAYA YA AMANI YAMEONGOZWA NA VIONGOZI WA TAHLISO TAIFA NA KUHUTUBIWA NA WAO PAMOJA NA MARAIS WA VYUO MBALIMBALI VYA ELIMU YA JUU KATIKA KILA MIKOA TAJWA.

MAAMUZI YA KUFANYA MAANDAMANO HAYA NI UTEKELEZAJI WA MAAMUZI YA KIKAO CHA SENETI YA TAHLISO (KIKAO CHA MARAIS WA VYUO VYOTE) KILICHFANYIKA SIKU YA JUMAMOSI 16/02/2008 KATIKA CHUO CHA SALVATORIAN MOROGORO.

23/02/2008


TAMKO LA TAHLISO JUU YA UFISADI NA BEI KUBWA ZA UMEME .


Ndugu watanzania wenzetu,kwanza kabisa tuwapongeze nyote kwa kutembea umbali mrefu kabisa hadi katika eneo hili ili tu kutumia uhuru wenu wa Kikatiba wa kusema yale mliyonayo,kupaza sauti zenu ili mabwana wakubwa popote pale walipo wazisikie,kwa hakika kwa mara nyingine tena TAHLISO ndiye kipaza sauti chenu.

Kwa wale wasioifahamu TAHLISO Ni kifupi cha maneno TANZANIA HIGHER LEARNING INSTITUTIONS STUDENTS ORGANIZATION yaani kwa Kiswahili Umoja wa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini Tanzania, umoja huu uliundwa ili kutetea na kulinda maslahi ya wanafunzi pamoja na watanzania kwa ujumla.

Kwa hakika TAHLISO itaendelea kupaza sauti hadi wafu wafufuke,hadi baba wa taifa hili Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aamke kutoka usingizini ili ajiunge nasi kulia kilio hiki,kilio chenye simanzi kubwa,ni simanzi kwa sababu ni mwisho wa watanzania,ni msiba wa wale ambao Mwalimu uliwasemea,ukawapigania,ukawafukuzia wakoloni ili waishi kwa uhuru mkubwa,ukamfukuza mkoloni na kuwafundisha maisha ya kiungwana,ya uwazi na ukweli,ukawaachia dhamana kubwa waliongoze taifa hili hadi mwisho wa safari.

Watu hawa uliowaachia tunu kubwa namna hiyo hawaitaki tena,wamegeuka kuwa wakoloni,miungu watu,mabwanyenye,majasusi wa nchi yao wenyewe,wamegeuka kuwa majangili wauwao wanyama wa pori lao,wamegeuka kuwa vibaka katika mitaa ya kwao,wamegeuka kuwa majambazi waibao ndani ya nyumba zao,wamegeuka kuwa wabakaji wa mama zao,hawana haya tena,hawana hata chembe ya aibu,wamekosa hata dalili za soni-wamewageuza watanzania kuwa watumwa wao na dola inawalinda(viongozi hawa ni sawasawa na kijana ambakaye mama yake,wamelaaniwa kwa madhambi haya na madhila waliyo/wanayowasababishia watanzania.

Tangu kung'atuka kwa Marehemu Mzee wetu Mwalimu Julius Nyerere viongozi wengi waliobakia wamekuwa na sifa hizo hapo juu(wamekuwa wakiwabaka wananchi bila aibu ,soni wala huruma,wamekuwa na roho mbaya zaidi ya wakoloni,wamekuwa madikteta na wasio na fadhila tena pindi wamalizapo kuchaguliwa.
Leo hii TAHLISO itaongelea ubakaji wa namna mbili unaofanywa na viongozi wengi kwa maslahi ya matumbo yao familia zao na koo zao.

UBAKAJI WA KWANZA NI UFISADI
Taasisi za elimu ya juu zinautambua ufisadi kwa maana ya rushwa,wizi wa mali za umma,uuaji wa demokrasia na uhuru wa kuongea na mengineyo mengi. Ufisadi katika nchi yetu umegeuka kuwa wimbo wa kawaida kabisa kiasi kwamba hata mtoto mdogo kabisa hukua akiuona na kisha huuzoea kabisa(akiwa kafisadi katoto) na wakati akikua huanza kubadilika na kuwa kafisadi kakubwa kidogo na kisha huingizwa kwenye jando ya wanaotaka kuwa mafisadi milele,hapa ndipo huanza kuchukua sura halisi ya fisadi na hupelekwa kuwafisadi watu ,akifuzu hupewa cheo cha fisadi mwandamizi kabla ya kuwa fisadi mkuu kabla ya kutunukiwa cheti cha ufisadi bora na hapo sasa huwa siyo tena mkuu wa mafisadi bali KUU LA MAFISADI la KIJIJI,KATA,WILAYA,MKOA,KANDA,TAIFA na hata MATAIFA.

Ndugu zangu sasa hivi Tanzania mafisadi hulindwa na dola,hulindwa na mitandao yao,hulindwa na vyama vyao,hulindwa na washikaji wao,hulindwa na majeshi,hulindwa na dini zetu wenyewe na zaidi ya yote na kwa uchungu kabisa hulindwa na sisi wasomi wenyewe kwa kuwakenulia meno yote na kuwashabikia tukitegemea siku moja kupewa vyeo au madaraka nao – Hatumhitaji rais BUSH au washirika wake kuja kupambana na mafisadi,hatuhitaji bunduki wala mizinga kupambana na mafisadi na wala hatuhitaji mabomu ya kujitoa mhanga.Tunahitaji umoja tu-tunahitaji kuusimamia ukweli tu,tunahitaji kupata taarifa na tunahitaji kuwa na nia ya dhati ya kupambana nao bila kurudi nyuma.Kama watanzania hatutaamka,kusimama imara na kupigana kishujaa tutalaumiwa sana na vizazi vijavyo,tutalaumiwa sana na mungu na hata shetani atatulaumu na kutucheka sana,Ukimya wetu hautatusaidia lolote lile utatutafuna kama ambavyo hasara za ufisadi zinatukondesha,zinatupuputisha na kuimeza nchi hii kama vile haina wenye nayo.Kwa Mfano;

1. KASHFA YA BENKI KUU YA TANZANIA KATIKA AKAUNTI YAKE YA MADENI YA NJE (EPA).
Pesa zilizoibiwa kupitia EPA ni nyingi ajabu kuliko ambavyo watu wengi wamekuwa wakifikiria bilioni 133 ni sehemu ya pesa tu TAHLISO inaamini kunapesa zaidi ya hizo ambazo zimeibiwa na bado haijajulikana-hizi sio pesa za mchezo.Kwa mfano pesa hizi (bilioni 133) zingeweza kufanya yafuatayo;

(a)Zingeweza kujenga zahanati 13,300 na kwa hiyo kila kijiji cha Tanzania kingeweza kuwa na Zahanati 4.

(b)Zingeweza kununua neti 44,333,333,neti ambazo zingewatosha watanzania wote na tena zingebakia neti milioni 10,majuzi watu wengi sana waliacha midomo wazi wakishangaa mpango wa rais Bush kuisaidia Tanzania vyandarua milioni 56,watu walichekelea kwa furaha kumbe vicheko vyao ni mchezo wa kitoto tu,kumbe pesa zilizozama mifukoni mwa mafisadi kutoka benki kuu zingeweza kuleta neti zilezile kama atakazoleta rais Bush,ama Tanzania nayo ingekuwa na uwezo huohuo wa kutumia pesa hizo hizo kutoa vyandarua kwa raia wake wote bila kumuomba msaada mtu au bepari yeyote.

(c)Pesa hizohizo zilizochukuliwa kinyemela na mafisadi huku serikali ikijidai haikuwa ina fahamu lolote zingeweza kulipa karo ya Vyuo vya elimu ya juu ya Tsh 800,000/= bure kwa wanafunzi 166,250/= ambao ni zaidi ya wanafunzi wote wanaosoma elimu ya juu Tanzania au zingeweza pia kuwalipia ada/karo wanafunzi 55,416 kwa miaka mitatu mfululizo hadi wanafunzi hao wangehitimu kozi zao-kwa maana nyingine zingeweza kuiletea Tanzania walimu 10,000/=,wahandisi 10,000,madaktari 10,000,wachumi 10,000,viongozi 10,000 na pamoja na wanajiolojia 5416. Ni utajiri ulioje kupata wataalamu wote hawa! iweje wataalamu wote hawa wamezwe matumboni na watu wachache tu?Kwa nini watanzania tuendelee kubung'aa tu?

(d)Pesa hizo pia zingeweza kujenga barabara ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilomita1,330 ikiwa na maana ya shs 100,000,000 kwa kila kilometa moja.Hapa nina maana kwamba pesa hizi zingeweza kujenga barabara ya lami kuzunguka kila kona na mtaa kwenye visiwa vya unguja na Pemba au barabara ya moja kwa moja kutoka Dar es salaam hadi Musoma-tungeweza kuendelea na uchambuzi wa ubadhirifu huu hadi jua lizame ili kila mtanzania adondoshe machozi yake na kuelewa hasa ni nini leo wasomi wa taasisi za elimu ya juu tunamwambia-Ukimchekea Nyani-Utavuna mabua na pia ukimshikilia ndege vibaya hukimbia na kukuachia manyoya – HIVI NDIVYO WATANZANIA TUNATENDWA SASA HIVI.

TAHLISO inatumia fursa hii kumpongeza rais Jakaya Mrisho Kikwete kwa ujasiri alioufanya kumfukuza kazi aliyekuwa Gavana wa benki kuu Daudi Balali baada ya Wizi huu kutokea chini ya gavana huyo,lakini tuseme ukweli wenyewe-

• Vyuo vya elimu ya juu havikuridhishwa kabisa na hatua alizozipendekeza rais baada ya kumfuta kazi balali kwa mfano kuipa muda wa kutosha tume ya kuchunguza suala hili mi!Hivi rais ametoa muda huo ili uchunguzi kweli ufanyike?au ndio ametoa muda wa kutosha ili hao mafisadi wakafiche mabilioni haya nje ya nchi?Ina maana rais Kikwete hajui supu ya mbwa hunywewa ikiwa ya moto au ameshasahau methali hii?
• Vyuo vya elimu ya juu vinaamini kabisa kwamba ndugu Balali ni mhusika kivuli tu katika kashfa hii kwani yeye kama kiongozi wa benki kuu alikuwa akifanya kazi chini ya wizara ya fedha na ikulu,TAHLISO inakuuliza rais wetu kikwete na inawataka watanzania watafakari,Mbona afukuzwe mdogo wakubwa wakiachwa,mbona rais Kikwete husemi rais wa wakati huo Ndugu Mkapa naye achunguzwe,mbona husemi achukuliwe hatua?Na kama unamkingia kifua unadhani unafanya hivyo kwa maslahi ya umma?Mbona husemi waziri wa fedha wa wakati huo achukuliwe hatua?Hivi huyu Balali angewezaje kuamuru mabilioni yaibwe kila siku bila kumulikiwa na mabosi wake(rais Mkapa na waziri wa fedha wa wakati huo).Ni nini kinachofichwa hapa?Kwa nini hajakamatwa hadi sasa huku akiwa amesababaisha upotevu wa mabilioni wakati hapahapa Tanzania kuna raia wengi wanaozea magerezani eti kwa sababu wameiba kuku au baiskeli?lazima watanzania tuwe macho,tusimame imara kabisa.

2. MKATABA FEKI WA RICHMOND DEVELOPMENT COMPANY
Ndugu watanzania,malaria nyingine inayohitaji vyandarua vya kutosha tena vya chuma ni huu mkataba wa kinyonyaji wa Richmond,Mkataba ulisainiwa na TANESCO baada ya kushinikizwa na viongozi kadhaa wababe wa serikali tena bila kufuata ushauri wa wataalam na watu mbalimbali waliokuwa na nafasi ya kufanya hivyo.Baada ya TANESCO kuingia mkataba huo,ulianza kulalamikiwa kuambatana na vitendo vya upendeleo na huku ikisemekana kampuni hiyo haina uwezo hata wa kufunga Bulb achilia mbali kutokuwa na spana kama bisibisi n.k.Ilipogundulika kama mkataba na Richmond haukuwa sahihi hata kidogo tume ya rais iliundwa ili kufanya uchunguzi wa kina,tume yenyewe ni TAKUKURU chini ya ndugu Hosea-ilipomaliza uchunguzi wake ilioubainisha kama wa uhakika na makini TAKUKURU ilikuja na majibu yafuatayo;

(i)Mchakato wa kumpata mzabuni ulikuwa wa wazi na shindanishi Hakuna ushahidi uliopatikana kuthibitisha vitendo vya rushwa, uzembe na hata kupokea kamisheni.
(ii)Pia hakuna ushahidi uliopatikana wa Afisa yeyote Serikalini kumiliki hisa au kuwa na madaraka katika Richmond Development Company LLC;
TAKUKURU wakawadanganya watanzania,wakamdanganya rais wa Tanzania,TAKUKURU iko chini ya ofisi ya rais-wakathubutu kunyea kambi,wakamtukana bosi wao-rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania-Bosi akakaa kimya,hakusema chochote.

(a) Kila wabunge walipojaribu kuhoji hili bungeni walifungwa midomo-wasiseme lolote tena,Waziri mkuu aliyekuwepo ndugu Lowassa alisisitiza mara zote kwamba serikali inalifuatilia suala hili na eti bunge lisilijadili huyu naye akalihadaa bunge na akamhadaa rais pia,shinikizo zilipozidi zaidi na kwa uwazi sana hasa kutoka kwa baadhi ya magazeti,wabunge wa vyama vya upinzani na wachache sana wa kutoka Chama kinachotawala ndipo bunge likaunda tume teule kwa mujibu wa Kanuni ya 119 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la 2007,Kamati hiyo Teule ya Bunge iliundwa tarehe 13 Novemba, 2007 ili kuchunguza mchakato wa zabuni ya uzalishaji umeme wa dharura uliofanyika mapema mwaka 2006 na kuipa ushindi Richmond Development Company LLC ya Houston, Texas, Marekani.

Tume ilipomaliza uchunguzi wake ikabaini yafuatayo;
1. Richmond Company haipo na wala haijasajiliwa Marekani, haina hata ofisi ukiachilia mbali kijiwe,ni kampuni hewa ambayo haijulikani ni ya nani.

2. Mkataba huo wa Richmond umejaa upendeleo, rushwa, ubabaishaji na kila aina ya uchafu.

3.Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndugu Lowassa,Mawaziri Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha,wanasheria wakuu wa serikali aliyepo na aliyepita,Mbunge Rostam Azizi na Mkurugenzi wa TAKUKURU ni baadhi tu ya watu muhimu katika serikali wanaohusika moja kwa moja au kimbadala na mkataba huo feki.Tume hiyo ilipendekeza mambo mengi ikiwamo kuwachukulia hatua wahusika;ikumbukwe kwamba,kila kukicha TANESCO wanawalipa Richmond kupitia kampuni ya DOWANS shilingi 152,000/= na mkataba huu ni wa miaka miwili,hadi leo hii kila kukicha saa mbili kamili asubuhi TANESCO wamekuwa wakiwahi benki kabisa na kuwa wa kwanza kwenye foleni na kuwalipa RICHMOND(Kampuni isiyokuwepo) tshs 152,000,000/= hii ina maana kwamba siku mkataba huu ukiisha TANESCO itakuwa imetumia tshs 113,088,000,000/= kodi za watanzania kulipa mifuko ya mafisadi wachache na kuzineemesha famili zao na za marafiki zao wachache.

TAHLISO inamsisitiza rais Kikwete aache masihara kabisa,tabasmu lake ligeuke kuwa dhoruba kali kwa madhalimu na mafisadi,rais Kikwete historia yako inaonesha hupendi Pesa na huu ndio ukweli,kwa nini usitumie mwanya huo wa usafi wako kuwawajibisha watu wote wachafu chini yako?

Hao akina Chenge umewakumbatia wa nini?wao si ndio walikuwa wanasheria wakuu enzi hizo serikali ikiingia mikataba mibovu kila kukicha?chukua hatua za dhati,uwatetee watanzania na siyo mafisadi kama ambavyo umeanza kufanya-huu si wakati wa kuwachekea tena hata kama ni marafiki zako wa kudumu,hata kama wamekusaidia sana katika kampeni zako wewe u msafi kwanini huwasafishi walio chini yako,hujui kama ukiendelea kukaa kimya tutakuweka kwenye kundi lao,una muda kidogo sana ndugu Kikwete kuwadhihirishia watanzania utaendelea kuwa msafi!U rais wa nchi hii,u mkuu wa kila kitu hapa kwa nini watanzania waendelee kukamuliwa na mafisadi?Nguvu mpya ari mpya na kasi mpya watendaji wako wanaifahamu vizuri kweli?Kwa nini wanatumia nguvu mpya kuingia mikataba feki kasi mpya kuwaibia wananchi na ari mpya kutudanganya baada ya kutuibia?

Ndugu watanzania,TAHLISO inaona kuna kila dalili ya kufanyiwa danganya toto kwenye utekelezaji wa maoni ya kamati teule ya bunge na maoni ya wananchi na hatua zote za kibinadamu watakazoona zinafaa kwani sasa hivi badala ya serikali na bunge kuyatekeleza bado imewakumbatia mafisadi na watuhumiwa wote wa wizi huu wa mabilioni tena bila aibu.Kwa mfano hadi leo hii wakati tunaongea hapa watu wote wanaohusika moja kwa moja katika tuhuma za ufisadi wanadunda kwa madaha kila sehemu,wakiwa bungeni na hata maofisini kwao.TAHLISO na watanzania hadi sasa hawaelewi kwa nini hadi sasa Lowassa,Karamagi,Msabaha, Rostam na washirika wao wote bado hawajafukuzwa bungeni-Bunge letu halijafanya kazi yake.

Sote tutakumbuka kwamba kuna wabunge wawili wa CUF kutoka Zanzibar walifukuzwa bungeni kwa aibu na kwa nguvu zote kwa sababu na kujihusisha na vitendo vidogo vya kughushi n.k bunge likawafukuza kwanguvu kwamba wananukarushwa na uchafu,khawastahili kuwemo bungeni kabisa eti wanaliaibisha bunge.

Watanzania wote mtakumbuka namna ambavyo maajabu ya dunia yalizuka katika bunge letu pale ambapo bunge hilihili lilitumia maguvu yake yote na kumfukuza kwa kishindo Mbunge wa Kigoma Kaskazini ndugu Zito kabwe eti kwa kosa la KUHOJI mkataba wa BUZWAGI – eti kosa lake lilikuwa kuutilia shaka mkataba wa BUZWAGI na tena eti alifanya makosa zaidi kutumia haki yake kama mbuge kuliomba bunge liunde tume huru kuchunguza-akaonekana eti kalikosea heshima bunge,akaonekana mchochezi,masikini!akafukuzwa bungeni kama mbwa,eti SPIKA na KANUNI,KANUNI na SPIKA!

Leo hii tunaona maajabu mengine,watu wachache wanakula mabilioni waziwazi tena kwa vithibitisho vyote lakini wao hawaguswi,hawatishiwi na hawafukuzwi na kanuni zilezile zilizowafukuza wengine bila huruma,na Spika yuleyule yeye na kanuni zake-Na wabunge walewale waliotenda yaleyale.Hivi Zito alikula pesa ya mtu?wale wabunge wa CUF walikula hela ya nani?Kwa nini waliadhibiwa kikatili namna ile?Why?

TAHLISO tunajua kinachotokea na leo tunawaambia watanzania-Akina Zito na wale wa CUF walifukuzwa na kudhalilishwa kwa sababu wao ni wapinzani na LOWASA,Karamagi,MsabahaRostam na Chenge wao hawafukuzwi na hawataguswa kwa sababu wao ni Chama tawala-Chama tawala nacho kiko katika sehemu kuu mbili(Chama tawala kinachoongozwa na wenye mikataba na chama tawala kinachotafuta maisha bora kwa kila mtanzania)Kwa hakika CHAMA Tawala hiki cha mikataba kina nguvu kubwa na tayari zimemzidi rais hiki chama tawala cha maisha bora kwa kila mtanzania,watanzania lazima tusimame mpaka mafisadi wote waondoke bungeni-mahali pao ni magerezani tu,tena magereza yenye giza nene.

TAHLISO haifungamani na upande wowote ule na bila kuficha leo hii tunawaambia watanzania,rais Kikwete pamoja na usafi wake wote haoneshi nia ya kupambana na mafisadi hawa,labda kwa sababu ni marafiki zake wa siku nyingi na sasa wanaimarisha ushikaji badala ya kuwatumikia watanzania.tuna kila sababu ya kusema hana nia ya kuwafuta mafisadi na kama hatutakuwa waangalifu yeye(rais) ndio ataanza kutumika kuwa kinga yao,ni kazi yetu watanzania kuhakikisha rais wetu anaendelea kuwa msafi na hanuki harufu za mafisadi,tunapaswa kutumia njia moja tu kumuokoa-NI KUMWAMBIA UKWELI BILA KUMFICHA ,TUKIMFICHA MAFISADI WATAMMEZA KWANI WAMEMZUNGUKA KILA KONA,kila sehemu anayoenda na ni haohao wanaojidai kuwa marafiki zake wa karibu kabisa wanaojidai wamekula yamini naye.

Tunasema hana nia kwa sababu zifuatazo;
Kwanza kabisa tangu ripoti ya Mwakyembe isomwe bungeni hadi leo hii rais wetu hajawahi kutamka mahali popote kwamba amesikitishwa na ufisadi mkubwa wa mabilioni iliofaywa chini ya swahiba wake wa karibu Lowassa,hadi leo hii rais Kikwete hajasema namna alivyoguswa na kuumizwa na utapeli,wizi na ubadhirifu uliofanywa na watu wa chini yake(alipaswa hata kutoa machozi mbele ya watu kama ntetezi wa watanzania).

Pili,tayari ameshaonesha kwamba ufisadi uliofanywa na watendaji wake hawa si kitu na haumgusi kabisa, Kwa mfano wakati anatoa hotuba muhimu baada ya matukio haya alisikika akisema '‘YALIYOMKUTA Lowassa ni ajali ya Kisiasa tu na tena anaendelea kumsifia Lowassa''.Hii ni ajabu sana rais wa nchi hakupaswa hata kujisahau hadi kutamka maneno hayo,Je mara hii tu baada ya Lowassa na wenzake kula mabilioni ya watanzania rais Kikwete ameshasahau na hana uchungu na mabilioni haya tena na tayari amem-miss sana swahiba wake?Yaani rais anawamiss mafisadi!Ni nani sasa atathubutu kuwachukulia hatua?

Tatu,rais Kikwete hana nia na kuwashughulikia watu hawa waliolitia taifa hasara kubwa kwa sababu hadi leo hii ameendelea kuwakumbatia mafisadi wakuu na tena waliomdanganya yeye kama bosi wao na mkuu wa nchi,hadi leo Mkurugenzi wa TAKUKURU aliyetoa ripoti feki kuipamba Richmond yuko kazini na tena amepewa cheo kingine kikubwa cha kuongoza Ma-TAKUKURU mengine ya Afrika mashariki,hatuelewi rais wetu anakotupeleka,huku ni shimoni-siko kwenye maisha bora-Je kuwakumbatia akina Chenge na mwanasheria mkuu wa serikali wa sasa ambao inasemekana wameingia mikataba mingi ya nyuma mibovu ndiyo kutuletea maisha bora?

Nne,rais Kikwete hana nia yakuwatisha mafisadi hadi washindwe kwa sababu hivi karibuni gazeti moja la kuaminika liliripoti Ndugu Lowassa anatuzwa na serikali na sasa anapewa mamilioni ya pesa kama posho ya kustaafu kila mwezi, hivi Lowassa kageuka kuwa mstaafu lini?Jamani mbona watanzania tunachezewa?Hii ni aibu kubwa kama watu waliotia hasara kubwa serikali badala wachukuliwe hatua eti tena wanaitwa,wanapigiwa magoti na kupewa viinua migongo!Watanzania tunacheka tu!

Lazima hapa tueleweke vema, tunapaza sauti zetu kusema tunamuamini sana rais na tunatambua juhudi zake na tunathamini sana mchango wake lakini kama wasomi lazima tuusimamie ukweli, ukweli ambao rais anatambua ni jukumu letu kumwambia bila woga wowote atakayechukia na achukie lakini najua rais anapenda kusemwa na hata kukosolewa!

UBAKAJI WA PILI NI BEI ZISIZOLIPIKA ZA UMEME.
Ndugu watanzania mliokusanyika hapa leo, nchi yetu haiendi tunakotaka, nchi yetu sasa imewasahau kabisa walalahoi,nchi yetu haitambui tena kilio cha watanzania,Tangu enzi za uhuru wa nchi yetu baba yetu Mwalimu Nyerere alitumia rasilimali nyingi kuhakikisha umeme unasambazwa kila kona nchi na aliacha misingi hiyo,mwalimu aliamini kwamba nishati ya umeme ndiyo mkombozi wa kweli wa maisha ya kila mtanzania,nishati hii ndiyo ingesaidia kuleta viwanda vidogovidogo na ndiyo ingebadilisha sura ya maisha ya watanzania.

Sasa hivi mambo ni tofauti kabisa,gharama za kuunga umeme kwa ni zaidi ya Shilingi milioni moja au pungufu kidogo ya milioni moja,Tanzania ina wakazi milioni 35 na kati yao asilimia 90 yaani watu milioni 30 ni masikini hohehahe,kipato chao ni chini ya dola moja kwa siku yaani shilingi 350,000/= kwa mwaka.Kwa hiyo asilimia tisini hii ya watanzania inahitaji kutokula wala kuvaa kwa miaka mitatu ili waweze kupata gharama ya kuunganishiwa umeme na kuachana na giza.Je haya maisha bora yatatoka wapi,atayashusha nani,maisha bora gizani?Rais Kikwete si unayajua haya?Mbona umendelea kukaa kimya ndugu yetu?hii si ni dhuluma kwa watanzania?Msimamo wako ni upi,tutaelewa nini hapa sisi,unawatetea masikini au mafisadi wamekukaba kooni?amka mheshimiwa rais,nchi hii haina rais mwingine kwa sasa,ni wewe tu na ndio maana tunalia na wewe,hatuna namna.

Ukiacha hilo la bei kubwa za kuunganisha umeme, kinachowaumiza, kuwakandamiza na kuwadidimiza watanzania ni gharama kubwa za kodi ya umeme kwa wale wote waliokwisha unganishwa - bei hizi za sasa zinawatisha hata wale walio na nia ya kuunganishiwa kwa sasa na kwa ujumla ni kiini kikubwa cha kupanda gharama za uzalishaji nah ii ndi sababu hasa ya mfumuko wa bei ambao unamuathiri mwananchi wa chini kabisa.

Haingii akilini kuona kila mwezi TANESCO wanaoiomba serikali yako kupandisha bei za umeme na bila aibu serikali yako tukufu inawakubalia, Ni majuzi tu serikali yako iliwaruhusu wakapandisha kwa asilimia 20 wiki iliyopita tena wameleta ombi la kupandisha na waziri wa Nishati na Madini kijana mwenzetu anadai analifanyia ombi hilo la TANESCO kazi,mbona hiki ni kiama cha watanzania,yaani mtanzania ndiye amegeuka kuwa mlipaji wa madeni ya Richmond,SONGAS,IPTL n.k. mbona mzigo huu wasihamishiwe hao mafedhuli wenye kampuni hizo hewa,wanaowatafuna watanzania kila siku?Hii ni dhambi kubwa sana na kwa hakika kama serikali yako itasahau jukumu lake la kuwasaidia raia,hatutafika popote .

Hata kama ni amani tunayojivunia ipo siku itatoweka kwani taifa letu linaenda kwenye mkondo wa mataifa ambayo amani zilitoweka baada ya watu wa chini kuona wanaishi kwa shida huku wachache wakiwaibia mabilioni halafu dola inawakumbatia na kuwapa pongezi na kuwaongezea viinua mgongo,ipo siku maskini watachoka kuonewa,ipo siku watasimama wote wasiende mashambani na makazini tena,wasifanye lolote wakae na kupambana na mafisadi – Raia watafanya hivi iwapo tu wewe mheshimiwa rais utaacha kuwafutilia mbali wezi na mafisadi kwa sababu mahali popote pale,dola ikishindwa kuwalinda wananchi wengi,maisha yao na uchumi wao ni jukumu la dhati la raia hao kujilinda wao wenyewe na hili litatokea.

Tanzania kama viongozi hawatabadilika na leo hii wasomi wa vyuo vya elimu ya juu tunaahidi kama Serikali yetu haitabadilika tutachukua jukumu zito la kupambana na mafisadi popote pale walipo bila kujali watatumwagia tindikali au la,bila kujali watatunyima kazi au la,nchi hii ni yetu sote na ni lazima tusimame.

PONGEZI ZA DHATI
1. Kwa vyombo vyote vya habari vinavyowatumikia watanzania, (vinavyowatumikia watanzania tu) mchango wa vyombo vya habari ndio umetufikisha hapa tulipo,bila vyombo vya habari ni muhimu sana katika sayari yoyote ile,tunawapa pole waandishi wote ambao hupata misukosuko kila kukicha kwa sababu ya kuwatumikia raia,endeleeni na uzalendo wenu hadi mwisho,kweli Tanzania sasa hivi ina waandishi

2. Kwa wabunge wa vyama vya upinzani,japokuwa mko wachache bungeni kazi yenu imekuwa kubwa kupita ya mwingine yeyote,mmekuwa mhimili wa bunge la jamhuri kweli,vyuo vya elimu ya juu na wananchi wote tuko nyuma yenu kwa sala na nguvu zote ilimradi mnachopigania ni kwa manufaa ya watanzania,tunaomba muendelee na kazi hiyo kwani ndiyo kila mbunge alitumwa kuifanya hapo bungeni.

3. Kwa wabunge wa chama tawala (CCM) kwa kujua makosa yenu,kwa kujua mlikuwa mbali na wananchi,kwa kujua kumbe mlikuwa mnatetea watu binafsi kwa kudanganywa eti mnatetea chama.Kwa kuamua sasa kuungana na watanzania na kurudi kundini.Tunawapongeza kwa ujasiri wenu wa kukiri na kusema waziwazi namna mlivyokuwa RUBBERSTAMP ya kuitetea serikali bila sababu za msingi.Siyo Siri,tunawapongeza sana ila ni lazima muwafukuze mafisadi na wote wenye kashfa chamani-mkisafishe chama chenu vinginevyo mtaendelea kuwa rubberstamps hadi ndani ya chama na mkumbuke.

4. Kwa tume teule ya bunge iliyochunguza mkataba wa Richmond, endeleeni kuwa wapiganaji na hata mkifia vitani ni tunu tosha kwa vizazi vyote vinavyokuja.

5. Kwa rais Kikwete,kwa kuamua sasa viongozi wachague kuwatumikia watu ama biashara zao,tunakuunga mkono katika suala hili na kamwe hatutakuficha tuonapo madhaifu katika serikali yako,tunaomba uendelee kuwa msikivu na mwadilifu na utumie uadilifu wako kuwawajibisha bila uoga walio chini yako hata kama ni marafiki zako.

MSIMAMO WA VYUO VYA ELIMU YA JUU KUHUSU UFISADI NA BEI KALI ZA UMEME.

1. Kuanzia leo tunataka kuisikia serikali ikitangaza mchakato wa namna ya kushusha bei za umeme, iwapo serikali haitaki kutangaza namna ya kushusha gharama hizi iwaeleze watanzania kwamba seruikali hii ni mzigo kwao na siyo msaada,sisi wasomi wa vyuo vya elimu ya juu hatuwezi kukubali hali hii uiendelee,serikali lazima ichague inamtumikia nani,mafisadi na Richmond yao au inamtumikia mwananchi.

2. Kwa sababu serikali katika kipindi kifupi imepoteza mabilioni ambayo ni ya watanzania ina maana kwamba serikali hii isiendelee kuwalilia wananchi kwamba haina uwezo, uwezo inao na ndio maana inawalipa Richmond n.k kumbe mabilioni yanaliwa kila kukicha,ianze sasa kusomesha wanafunzi wa elimu ya juu wote bure bila kuwadai hata senti moja,tumechoka kukopeshwa huku madhalimu tunawapa pesa nyingi bure.

3. Hatutaki kuona watu wote wanaotajwa kwenye ufisadi na tuhuma mbalimbali wakiwemo serikalini(Hosea,Mwanasheria mkuu wa sasa,Chenge,Fulgence Kazaura na wenzao wote) wala bungeni(Lowassa,Msabaha,Karamagi na Rostam),tunataka wahamishiwe magerezani haraka iwezekanavyo,kujiuzulu tu haitoshi,siyo adhabu hata kidogo,tukiendekeza tabia hii ya kuwaacha watu watuibie kisha wanajiuzulu tutakuwa wajinga sana, hatutaki kuvumilia ufisadi kabisa,ni lazima serikali ianzishe mchakato wa kuwafilisi wote,mabilioni waliyoiba wanyang'anywe,hawa ni wahaini na kama serikali haitakuwa makini nao ipo siku wataipindua,mtu anatengeneza kampuni hewa anachota bilioni 100 hizi anazipeleka wapi?Kama tukimuachia halafu akanunue silaha akituletea vita tutaiepuka vipi,yaani pesa zetu tunawaachia watu wazitumie hata kutuua,wafilisiwe haraka sana hawa kabla hawajatugeuka.TAHLISO insema lazima serikali isimame na kuwanyang,anya mali zao zote walizoiba,Nyerere angekuwepo angefanya hivyo bila kusita,hata Kikwete anaweza kufanya hivyo na ndiyo jukumu tunalompa leo.

4. Tunaiomba serikali kwa manufaa ya umma isitishe haraka mkataba kati yake na Richmond uliopasishwa kwa Dowans,Mkataba huo uondolewe kwani hata vigezo vya kisheria haukidhi,ni mkataba wa kihuni,tukiukumbatia watanzania wote na serikali yetu tutaonekana wahuni na tusiojali maisha na maendeleo yetu na ya vizazi vijavyo.Na wakati huohuo serikali iimarishe tume yake ya kuchunguza mikataba ya madini ichunguzwe yote katika ngazi zote kwani hata ngazi za chini vijijini na kwenye kata mafisadi wanakula kila kitu na kuwaacha wananchi wakiteseka.

5. Muda uliowekwa na bunge(miezi mitatu) kuwashughulikia wahusika ni mrefu sana,bunge kwa hiyo limeidhinisha watuhumiwa wapate muda wa kuhamisha mabilioni waliyoiba na kuyaweka katika akaunti zingine na limewapa mwanya wa kutoroka na kwenda wanakotaka,(mbona bunge hilihili halikutoa miezi mitatu ili kumchunguza zaidi Zito) uchunguzi unaofanyika ni upi,kama tuna uchunguzi mpya zaidi ya ule wa tume teule ya bunge huu umetokea wapi?Hatutaki uchunguzi mwingine,tunataka watu wachukuliwe hatua haraka.

6. Rais Kikwete atuambie ni nini kiko kati yake yeye na Lowassa na aongee hili waziwazi,tunataka kumsikia rais Kikwete akisema amesikitishwa na yaliyotokea na akiri kwamba pesa zile ni nyingi sana.Na zaidi ya yote tunamtaka rais wetu awaombe radhi watanzania wote kwa yale yaliyotokea,awaambie na akiri kwamba yalitokea chini yake na kwa sababu yeye ndiye rais aliyechaguliwa na watu alipaswa kuwawajibisha watendaji wake kabla bunge na hata wananchi hawajawa na hasira,Ni ukweli usiopingika kwamba ingekuwa katika nchi zilizoendelea,hata yeye mwenyewe rais Kikwete angekuwa amejiuzulu na kuitisha uchaguzi mpya na kama ili agombee upya na kupima imani ya wananchi kwake,huu ndio utawala bora,hii ndiyo demokrasia.Tunasema hivi kwa sababu haiwezekani serikali na wananchi waibiwe mabilioni kila kukicha bila mkuu wa nchi kujua,lazima alikuwa anajua lakini alikosa namna ya kufanya(mafisadi walimzidia).

7. Tunaitaka serikali kuanzia sasa ijifunze, kesho tena wasituambie pesa zimeibiwa, wajifunze kusikiliza ushauri wa wataalam ambao ndiyo nguzo ya utendaji mahali popote pale, serikali isifanye maamuzi yoyote bila kuwasikiliza wadau wake, iwashirikishe wananchi katika mambo muhimu yanayoligusa taifa letu.Na watalaam wetu wawe makini kabisa,wasiogope kusema wazi na kuijulisha jamii iwapo viongozi fulani wanawalazimisha kutenda mambo fulani kinyume na misingi ya kazi zao.Ni aibu kubwa kuona msomi mzima anaburuzwa na kiongozi Fulani na yeye anakubali tu,huu siyo usomi hata siku moja.

8. Kuanzia sasa tunataka TAKUKURU iwe chini ya Bunge,ifanye kazi kwa maamuzi ya wabunge na tena iwasilishe ripoti zote kwa bunge,rais tunaomba aridhie pendekezo hili,yeye kazi yake iwe kuhakiki utendaji wa kazi alizowapatia watendaji wake,Tayari TAKUKURU imeshindwa kufanya kazi ikiwa chini yake asisubiri ishindwe mara nyingine,aibu alizozipata kwa TAKUKURU kuwa chini yake nainamdanganya zinatosha,aamue moja kuiacha TAKUKURU iwe huru kabisa.

9. Tunawataka wabunge wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania warudi kwa wananchi kama walivyofanya katika Kashfa ya Richmond, washirikiane katika kuupigania ukweli bila kujali itikadi, itikadi ni wakirudi majukwaani kupiga kampeni, huu si wakati wa kampeni, ni wakati wa kazi tu, lazima watanzania warudishe imani iliyopotea kwa wabunge (hasa wa Chama cha Mapinduzi), wasidanganywe eti wanalinda chama huku wanaliwa wao na mabilioni yanapotea- huu ni wakati wa ukombozi tu!

10. Mwisho tunawataka wananchi wote kwa ujumla wao wazitumie kura zao vizuri,wawachague viongozi waaminifu siyo wanaowadanganya kwa vipesa kisha wakipewa madaraka wanaanza kuwa wezi(wanatokomeza mabilioni).Waige mfano wa Uchaguzi wa Kenya ambapo mabilionea wakubwa Afrika kama Patni walinyimwa ubunge na pesa zao,na ili kupata viongozi thabiti lazima wananchi wachague watu(watu wenye sifa mahsusi) siyo vyama,mkumbo wa kuchagu a chama fulani na siyo mgombea fulani ndio umetufikisha hapa.Watanzania tuamke,tujipiganie sisi wenyewe na wala tusimsubiri Bush aje kukemea ufisadi hapa kwetu(tumuache na vita zake huko).

HITIMISHO
Taasisi za elimu ya juu zinaitaka serikali yetu iwaondoe mafisadi haraka sana madarakani bungeni na kwingineko, iwafilisi na kuwashitaki kwa uhaini (wizi wa mabilioni) na kasha iwashitaki na kuwafunga haraka iwezekanavyo.Tayari Taasisi za elimu ya juu kupitia umoja wao (TAHLISO) zimeanza mchakato wa kuandaa mashitaka dhidi ya mafisadi wote Benki Kuu,BoT na Buzwagi kupitia kwa wanasheria wa umoja huu.Iwapo serikali itaamua kutowachukulia hatua yoyote ikiwamo kuwashitaki na kuwafilisi TAHLISO itachukua jukumu hilo haraka sana Kwani hata kama mafisadi watatuua ama kutudhuru Kesi tayari itakuwa mahakamani na itapandikiza mbegu kwa vizazi vinavyokuja kwani ni bora kufa ukiwa huru na ukipigania haki na ukweli kuliko kufa ukiwa mtumwa na mshirika wa wezi na mafisadi.

Mungu mpe nguvu, afya na moyo wa ujasiri rais wetu wakati anapigana na vita hii ya ufisadi(kama amenuia)
Ibariki Tanzania na Afrika,

Wape wakenya haki yao na amani pia.

Tunawashukuru sana kwa kutusikiliza, TAHLISO idumu milele, watanzania waupiganie ukweli.

IMETOLEWA NA UMOJA WA VYUO VYA ELIMU YA JUU TANZANIA
Leo Jumamosi,tarehe 23/02/2008
 
Kweli sasa Wasomi tunao . . . .

Ningependa tu kutoa changamoto moja zaidi . . . . What if Serikali itaziba masikio au haitayafanyia kazimadai yenu?

What will be the next course of action? We need you to be like the Mwakyembe and the like waliotutoa kimasomaso wasomi wote.

It is a good start but you need to define the next course of action.
 
kwa waheshimiwa wabunge wa ccm, mnalo moja la kuchagua au kuwatumikia wananchi au mafisadi, mjue kuwa hao wanaowafadhili kwa mamilioni wakati wa uchaguzi, wakijidai kuwa zinatoka mfukoni mwao ni waongo, wanachota mabilioni toka hazina ya wanyonge, wanawaletea visenti, kataeni hivyo visenti na muwatumikie wananchi,huo ndo utakuwa mwisho wa mafisadi kwani watakufa njaa
 
HAPA KWELI VIJANA TUNAO KAZI NZURI TUKO MBELE NA NYUMA YENU LIWALO NA LIWE

TUTABANANANA NAO NYIE LIANZISHENI SISI HATUWAACHI VIJANA WETU
 
Heshima ya wanafunzi wa vyuo vikuu inarudia enzi za Nyerere na Mwinyi!! Taarifa nzuri sana, tunataka the PLAN OF ACTION sisi tupo tayari kuchangia kwa HALI NA MALI Tuondoe hili wingu zito la mafisadi tz!!
 
labda mlikuwa hamjui kuwa JK amekuwa Senior Intelligency Crue wa TZ kwa miaka kibao... mngelijua hilo mngekuwa mnajudge utendaji wake kwa staili nyingine kabisa... kwa taarifa yenu kukaa kwake kimya kuna kishindo. subirini vikao vya bunge vya Mei na July mtaelewa hili.

kashfa ya Richmond imethibitika kuwa ni yeye aliiuza kwa wapinzani ili kuondokana kwanza na fisadi namba moja "PM" ili atakaposhughulikia hawa wengine, kusiwe na kikwazo toka ngazi ya juu.

kwa taarifa yenu pia Mizengo Pinda ni one of the Senior Intelligency Crues... suburini muone watu wazima wakilambwa bakora hadharani bungeni...

ukiacha kashfa ya EPA na Richmond, kikao cha bunge cha mwezi Mei itaibuliwa scandal nzito kuliko zote.

hii inahusisha ulaji wa Tsh 300,000,000/= kila siku kupitia mradi mwingine "..."

kwa wasioelewa mambo wanaweza kuona kama vile JK anatapatapa. Men you are deadly wrong!

The Guy is in full control and he is playing his cards so nicely.
nilitegemea educated people like you guys mtakuwa at least mna fununu ya hizi hot unbroken news...
 
mjamaa kama una news toa, sio kuanza kujaribu watu.
kama unazo ziweke....
what if huyo JK asipoziongelea huo mwezi May? haonekani kujua anafanya nini, lakini tusiandikie mate wakati wino upo
 
Katika kundi ambalo liko nyuma ya harakati za kutetea maslahi ya Taifa hili lnaongoza labda sasa limetoka usingizini. Jitihada zao zitachangia katika mapambano haya.
 
nashangaa gharama ya kuunga umeme ni karibu a million na bei ya umeme ni kubwa kuliko hata bei ya chakula na 90% ya watanzania hawana umeme,lakini cha ajabu majority ya wana jamboforums na wabunge wao bado wanatetea sheria ya kuipa monopoly TANESCO na hawataki private companies zifanye hiyo biashara...mmekwisha kwa mawazo kama hayo na uchumi utaendelea kuwa mbaya kila siku maana hakuna mtu ataweka pesa zake kwenye nchi isiyo na umeme,ningekuwa JK ingawaje bunge wamegoma kupitisha hiyo bill ningelazimisha kwa kutumia executive privilledge kuruhusu makampuni binafsi kuzalisha na kuuza umeme,nilifikiri tulijifunza kwenye makampuni ya simu lakini kumbe bado saaaana!!
 
Kwa hapa mimi niko sambamba na wasomi wetu kwa yote waliyoyasema sio kama kipindi cha nyuma eti wasomi mnakaa kupinga ujio wa Bushi,kwa haya mlioyasema nimewakubali.

Hoja kwamba nini kitafuata endapo JK hatasema lolote juu ya mafisadi,tusubiri hapo atakapokaa kimya.What we can do ni kuja na staili mya ya maandamano ya kulala barabarani hadi kieleweke
 
nashangaa gharama ya kuunga umeme ni karibu a million na bei ya umeme ni kubwa kuliko hata bei ya chakula na 90% ya watanzania hawana umeme,lakini cha ajabu majority ya wana jamboforums na wabunge wao bado wanatetea sheria ya kuipa monopoly TANESCO na hawataki private companies zifanye hiyo biashara...mmekwisha kwa mawazo kama hayo na uchumi utaendelea kuwa mbaya kila siku maana hakuna mtu ataweka pesa zake kwenye nchi isiyo na umeme,ningekuwa JK ingawaje bunge wamegoma kupitisha hiyo bill ningelazimisha kwa kutumia executive privilledge kuruhusu makampuni binafsi kuzalisha na kuuza umeme,nilifikiri tulijifunza kwenye makampuni ya simu lakini kumbe bado saaaana!!

Koba

Siyo kwamba hawaoni haya unayoyasema. Tatizo lililoko Tanzania ni sawa na kuwa na kakondoo kako halafu akaja FISI eti anaomba kukaazima. Unategemea nini?

Unapoona Mtu ni waziri Mkuu lakini bado anajifikiria yeye na watoto wake(Mfano Mkuu Lowasa na Richimonduli, Karamagi style, Rostamu(Mbunge) style nk)ujue unakuwa umefika pabaya.

(Hawa wananikumbusha kitabu kimoja- Manenge akisema Tumbo niache nimwachie madawa uji wakati huo anaendelea kunywa).

Wananchi/wabunge/JF wamekosa Imani na watendaji wa serikali ndio maana utaona miswada kama hiyo inasusiwa si kingine. kama ulisikia wabunge wengine walitamka hadharani kuwa Isije ikawa EPA inaenda kununua Tanesco.

Ukiwa kiongozi mzuri wa Nchi unaondoa hisi hisia kabla ya muswaada. katika hali kama hizi usishangae yakatukuta makubwa.
 
Du, Aibu... yaani taasisi ya the so called wasomi wanatumia domain ya yahoo.com.

Kweli nchi ina matatizo makubwa!!! Du heri ningezaliwa wakati wa ukoloni ningeweza kujitetea na sasa je?
 
Du, Aibu... yaani taasisi ya the so called wasomi wanatumia domain ya yahoo.com.

Kweli nchi ina matatizo makubwa!!! Du heri ningezaliwa wakati wa ukoloni ningeweza kujitetea na sasa je?

Mzee aibu ya nini? Utasikia PESA za EPA na MAFISADI(Richmond, IPTL nk)?

Hivi unajua kuna vyuo vyetu ambavyo kuangalia Net ni shida?

Hivi unajua kuwa tanzania bado kuna shule ina mwalimu mmoja? akienda kufuatilia Mshahara shule inafungwa?

Hivi unajua kuna shule ambazo zimejengwa kwa msonge na Mvua zikinyesha wanafunzi hawaji shule?

Hivi unajua kuna shule wanasomea chini ya miti?

Hivi unajua kuwa hata shule zetu zinazosifika walimu hazina?

Tuwaonee huruma wasomi wetu?

Mzee ni kweli hafadhali wakati wa mkoloni, wakoloni weusi ni wabaya hata kuliko hao weupe.
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom