Ufisadi umeifanya Dar isiwe kitovu cha mabadiliko | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ufisadi umeifanya Dar isiwe kitovu cha mabadiliko

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by TrueVoter, Oct 22, 2009.

 1. T

  TrueVoter JF-Expert Member

  #1
  Oct 22, 2009
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 868
  Likes Received: 282
  Trophy Points: 80
  Mwandishi Wetu
  Oktoba 21, 2009


  RAFIKI yangu mmoja aliwahi kusema kuwa ufisadi ukikoma nchini "tutaandamana". Alikuwa anawazungumzia watu wote waliolifanya jiji la Dar es Salaam kuwa maskani yao na makazi yao ya kudumu au ya muda mrefu.
  Wakazi hao ni kuanzia Rais Kikwete, mawaziri wake, makatibu wake, watendaji wa ofisi mbalimbali, wafanyabiashara binafsi, hadi watoto wa shule ya msingi na kuendelea!

  Rafiki yangu huyo alisema kuwa kama ufisadi ukikomeshwa nchini, watu wa Dar ndio watakuwa waathirika wa kwanza na maisha yao yatakuwa magumu. Hivyo, akaniasa nisipigie kelele sana ufisadi; kwani endapo utakoma maisha yatakuwa magumu na akaapa kuwa “wallahi tutaandamana”!

  Sikumuelewa

  Sikuelewa ana maana gani kuwa ufisadi ukikoma watu wa Dar watapata maisha magumu na watalazimika kuandamana ili urudishwe? Hii ilikuwa ni muda mrefu uliopita na nilichukulia kauli hiyo kama utani wa aina fulani. Sikuipa umakini unaostahili hadi hili suala la Dowans lilipoibuka!

  Mwitikio wa wakazi wa Dar, wa baadhi ya vyombo vya habari na baadhi ya wale wanajiona ni viongozi wetu, umenifanya nifikirie tena kauli ya rafiki yangu huyo na kuielewa.

  Ufisadi umefanikisha zaidi maisha ya wakazi wengi wa Jiji la Dar kuliko sehemu nyingine yoyote nchini, na hivyo kutokomezwa kwake kutakuwa ni pigo kubwa kwa maelfu kama siyo mamilioni ya wakazi wa Jiji hilo. Tuangalie.

  Ufisadi umefanya rushwa ionekane ni “rafiki wa haki”.

  Kwa miaka mingi sasa tumekuwa tukisema kuwa “rushwa ni adui wa haki”. Kauli hii kifalsafa imejaa ukweli lakini kihalisia na katika maisha ya mtu wa kawaida haiangalii ukweli unaotokea.

  Kama mtu akifuata njia ya uhalali na sheria na taratibu zilizopo naye akawa anahangaika kila kukicha kupata haki yake, je njia hiyo halali na ufuataji huo wa sheria unampa motisha gani kuvifuata kama kwa kufanya hivyo haki yake inachelewa?

  Itakuwaje mtu huyo anapoona haki yake imechelewa na kumetokea “udhia” naye akaamua kupenyeza “rupia” (huu msemo ungepigwa marufuku kichwani kwa kila Mtanzania) na ndani ya dakika au mapema zaidi akapata haki yake itawezekana vipi kumshawishi kuwa kupenyeza rupia ni “adui” wa haki?

  Taifa letu limekubali rushwa kama sehemu ya maisha yake na watu wetu wamefikia mahali wanapopanga bajeti zao za mambo mbalimbali inabidi waweke humo gharama ya rushwa ili “kulainisha” watu mbalimbali katika mchakato wao wa kupata haki.

  Mtu ameambiwa ana kesi mahakamani na anaitwa huko ambako faini yake ni kati ya Shilingi 5,000 na 10,000 yeye anajipanga na Shilingi 20,000 mfukoni kwani anajua kuwa ili kesi yake isirushwe siku nyingi au adhabu isiwe kali au hata asipatwe na hatia inabidi “apenyeze rupia”.

  Sasa huyo ndugu yetu akiweza kupenyeza rupia; halafu kesi ambayo alikuwa aende jela miezi mitatu ikaweza kufutika kwa ghafla utamuambia vipi kuwa “rushwa ni adui ya haki”? Inawezekana kuwa ni adui kwa yule mshitaki lakini kwa mshitakiwa, rushwa imekuwa ni rafiki.

  Sasa katika jiji letu la Dar, pamoja na kelele zote za ufisadi, wataishi vipi bila kupenyeza rupia na mambo yao yakawanyokea? Mtu akitaka leseni haraka haraka anajua namna ya kuipata; mtu akitaka kutoa mizigo bandarini kwa haraka na gharama “nafuu” anajua nini cha kufanya; mtu akitua uwanja wa ndege ili mizigo yake isipotee au kupoteza vitu anajua nini cha kufanya!

  Baadhi ya wakazi wa jiji la Dar (kutokana na mwitikio wao naweza kusema “wengi wao”) wamefikia mahali ambapo wanatambua rushwa kama sehemu ya maisha yao na wapo wanaoichukia kimaadili na sababu za kidini lakini inapokuja wakati wa kuamua, wanajikuta “wanalazimika” kutoa rushwa.

  Ufisadi umetoa “ajira mbadala”!

  Kuna kundi la watu ambao wananufaika na ufisadi kwa sababu umewatengenezea ‘ajira’. ‘Ajira’ hizi ni zile ambazo zinatokana na uvunjaji wa sheria na kwa vile wanajua kuwa kuna udhaifu katika usimamizi wa sheria (law enforcement) watu hawa wametengeneza maisha yao na kuhudumia familia zao.

  Watu hawa ni wale ambao wanaweza kukupatia kitu chochote katika Jiji la Dar ilimradi tu una pesa za kuwapa na unawapa muda. Hawa ni watu wa ma-dili na mitkasi. Ni vijana wa mjini na “wachangamkiaji tenda”. Hawa wanaweza kukupatia kuanzia rekodi ya muziki, simu ya mkononi iliyoibwa hadi kiwanja cha nyumba!

  Kutokana na kukomaa kwa mfumo wa kifisadi, watu hawa wamekuwa wategemezi wa mbinu za kijanja katika kuishi maisha yao. Hawa siyo tu wale walioko mitaani; bali pia walioko kwenye maofisi mbalimbali ya umma na binafsi na ambao wana uwezo wa kufanya kitu chochote kifanikiwe nje ya taratibu; alimradi na wao wanapata “mshiko” wao.

  Ufisadi na utajiri wa haraka haraka


  Kati ya mambo ambayo tumejifunza miaka hii michache ni kuwa ufisadi umewawezesha vijana na wazee kutajirika haraka haraka na kujitofautisha katika jamii kwa utajiri huo. Fedha zinazoibwa katika asasi mbalimbali za umma zimetumika kuanzishia miradi mbalimbali ambayo imepewa usajili wa “uhalali”.

  Tamaa ya vijana wetu na hata watu wazima waliogundua kuwa ufisadi mkubwa ni mlango wa utajiri usio kifani umefanya baadhi ya watu kutaka na wao kujaribu bahati yao. Kuanzia wakati wa kesi ya Simbaulanga na nyingine zilizofuata baadaye, tumeona watumishi mbalimbali wa umma wakithubutu pasipo kufikiria sana kujaribu bahati yao kuchota pesa za walipa kodi wa Tanzania.

  Hivyo, Dar imekuwa ndio uwanja mpana wa majaribio ya bahati nasibu hii ya jitajirishe na ufisadi. Na kwa kadri Serikali ya CCM inavyoendelea kutawala kwa mtindo huu, ndivyo pia wengi zaidi watazidi kuthubutu kujitajirisha; hata kama kuna wachache wanaotolewa kafara kwa kupelekwa mahakamani.

  Ufisadi umefanya watumishi “wamudu” maisha


  Mojawapo ya vitu ambavyo vinaonekana kama athari kubwa ya ufisadi ni hisia kuwa katika maisha ya mfumo huu, watu wameweza “kumudu” maisha. Sijui ni watu wangapi katika Jiji letu la Dar wanaweza kumudu maisha yao kwa kipato chao peke yake. Kujenga nyumba, kulipia pango, kusomesha watoto, chakula, mavazi, dharura, n.k

  Hayo ni mambo machache tu ambayo yanagusa maisha ya watu wa Dar kama vile watu wa miji mingine. Lakini kwa namna ya pekee jiji la Dar, kwa sababu kama inavyosemwa kuwa “mwelekeo wa California ndiyo mwelekeo wa Marekani”, vivyo hivyo “mwelekeo wa Dar ndiyo mwelekeo wa Tanzania.”

  Mambo yanayofanyika Dar na mwitikio wa wakazi wa jiji hilo unatoa mwanga wa kuelewa kile kinachoendelea sehemu nyingine nchini. Lakini kipo kikubwa ambacho kinaonyesha ni jinsi gani wakazi wa Dar wameshindwa kutoa mwelekeo kwa taifa, na hivyo kuonyesha kuridhishwa na maisha yao, na hawajawa kichocheo cha mabadiliko ya kitaifa.

  Ukiangalia majiji ya Paris (Ufaransa), Washington DC (Marekani), Kiev (Ukraine), Tiblis (Georgia), Tehran (Iran), Nairobi (Kenya), Harare (Zimbabwe), Lusaka (Zambia) na majiji mengine makubwa ambapo moto wa mabadiliko ya kisiasa uliwaka kwa watu kukataa watawala madarakani, utaona kuwa ni watu wa majiji hayo waliochoshwa na ufisadi ndio waliowasha moto wa mabadiliko na kukataa kabisa kurushiwa mifupa wakati watawala wanakula nyama!

  Wakazi wa Dar wameshindwa kuandamana kwa sauti moja kutaka Rais Mkapa ashtakiwe. Wakiuliza kidogo wanaambiwa “si kawajengea uwanja wa mpira wa kisasa?” Kisha wanabakia kutikisa vichwa na kuona haya! Wakisema wapinge ununuzi wa mitambo ya kampuni ya kilaghai ya Dowans, wao wanasema “lakini mbona giza jamani”!

  Wakazi wa Dar wanakesha na usumbufu mkubwa wa usafiri kutoka mahali A kwenda mahali B. Hili ni tatizo la miaka nenda rudi, lakini katika akili zao ‘zilizojanjaruka’ wameendelea kuchagua chama kilekile chenye sera zile zile na uongozi ule ule! Ukiwauliza kwa fahari kubwa wanasema; “zimwi likujualo”!

  Mitaa yao ikinyesha mvua inafurika kupita mto Rufiji; badala ya kuwang’oa kwa kura madiwani na wabunge wao, wao wanatafuta magurudumu na magunia ya michanga na kuyapanga ili waweze kupita. Na kama vile ufisadi unavyotoa ajira, basi, watu wanatoa migongo yao kubeba watu kutoka kwenye magari hadi ofisini; wenyewe wanasema wamechangia kutoa ajira!

  Wakazi wa Dar wameambiwa kuwa sasa kuna mpango wa kujenga “barabara za juu kwa juu” wao wanashangilia na kusubiri kwa hamu wakati watawala hao hao wameshindwa hata kutengeneza mitaro ya maji machafu na ni asilimia 5 tu ya wakazi wa Dar wana vyoo vya kisasa! Ukiwauliza wanasema “CCM nambari wani!”

  Wakazi wa jiji la Dar wanatia aibu! Wanatia aibu kwa sababu ndio jiji lenye fedha nyingi, lenye vyuo vikuu vingi, lenye wasomi wengi, na ndicho hasa kiini cha uchumi wa taifa letu. Lakini, vile vile maeneo yake mengine yanaweza kushangaza hata mbinguni!

  Unaweza kupita katika vijiji huko Manyoni (Singida), au Ileje (Mbeya) au Misungwi (Mwanza) au hata maeneo ya Lushoto (Tanga) na utaona shule za msingi zinazopendeza kwa maua na maeneo yaliyopakwa chokaa vizuri. Lakini nenda katika jiji la Dar! Kama siyo shule ya “International” basi ni matatizo tu.

  Katika jiji hilo hilo ambalo kuna mabalozi, rais, wabunge kibao, wafanyabiashara wa mabilioni, wananchi wanapanga foleni kutafuta maji!
  Leo hii ukiangalia wakazi wa jiji la Dar kwa kweli wanapendeza! Wanavaa nguo nzuri, wanaendesha magari ya kisasa na wengine wanatamba na digrii zao walizozipata kutoka vyuo mbalimbali hadi vya huko Marekani na Uingereza. Wanazungumza ung’eng’e hadi unafikiri ni wacheza filamu fulani hivi. Lakini angalia mazingira yao. Wafuate wakirudi kwenye majumba yao na mitaa yao! Utashangaa!

  Lakini kinachonitibua mimi na ukweli wake ni wa asilimia 100, ni kuwa wakazi hawa hawa wiki hii watachagua CCM tena katika mitaa yao na mwakani watachagua CCM katika ubunge na CCM katika urais!

  Wakazi wa Mbagala kulikotokea mlipuko wa mabomu nina uhakika watarudisha viongozi wa mitaa wale wale wa CCM wakiamini kwamba huko mbele ya safari mambo yatakuwa tofauti.

  Ndugu zangu, wananchi wa Dar hawawezi kubadilisha kura zao au kukataa uongozi mbovu na uzembe uliokubuhu pasipo kubadilisha fikra zao.Wakazi wa Dar wasipokataa ubovu kwenye mitaa yao na kukataa mambo yale yale mabovu, basi, wataendela kufuata njia ile ile.

  Na tukiangalia vizuri tutaona kuwa Dar ni kioo tu cha Watanzania wengine. Bado hatuamini kuwa na sisi tunastahili vitu vizuri na vilivyo bora. Hatuamini hivyo kwa sababu bado tunachagua watu wale wale ambao tunajua hawawezi kufanya tofauti. Lakini kwa vile tunafikiri ni wenzetu na tumewazoea, basi, tunaendelea na maisha yale yale ya kifisadi.

  Ni kwa sababu hiyo ninaamini kabisa Dowans italipwa ilimradi waondoe “kero ya mgao”. Hakuna wakazi wa Dar wenye moyo wa mabadiliko na kukataa kuuza utu wao. Matokeo yake wao na taifa zima litaendelea kuburuzwa na viongozi wazembe na makuwadi wa ufisadi.

  Nchi yetu itaendelea kuogolea kwenye tope la kashfa (na zipo nyingi zinakuja) hadi watu wa Dar watakapoamua kuamka na kukataa ufisadi kwa sababu japo wanaweza kuona kuwa unafaida kwa mtu mmoja mmoja, kiukweli kitaifa ni maangamizi makubwa.

  Mafisadi wameshakubalika Dar, na uzao wao utaendelea kutawala Dar na taifa zima. Ufisadi utaendelea kuota kama uyoga katika jiji la Dar hadi pale wakazi wa Dar watakaposema wamechoka na mambo yale yale.

  Tanzania italipuka kwa mwamko wa mabadiliko mwakani endapo wakazi wa Dar wataamka na kukataa ufisadi kwa sababu unawahukumu wao, watoto wao, na watoto wa watoto wao katika uombaomba wa milele na utegemezi wa kiakili wa wageni.

  Wakazi wa Dar ambao wamebahatika kuona mengi, kuwa na vyanzo vingi vya habari na ujuzi mkubwa wa mambo na nafasi nyingi za kuona makubwa ya dunia hii tangu kale wanaitwa na historia kuonyesha mwanga kwa taifa letu.

  Lakini vyovyote vile ilivyo, wakazi wa Dar wakichagua tena viongozi wa CCM kwenye mitaa yao wajue wanapoteza haki yote ya kulalamika huko mbeleni; kwani kwa miaka karibu 40 na ushee sasa wameendelea kufanya uchaguzi ule ule.

  Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kuwa “demokrasia ni pamoja na haki ya kuchagua serikali mbovu; lakini uchaguzi ndiyo njia ya kusahihisha kosa hilo” na aliongeza wakati fulani kuwa “demokrasia inaamini kuwa hatimaye watu watafanya uchaguzi sahihi”.

  Katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa wakazi wa Dar lazima wajipime maisha yao na yale wanayoyataka kwa watoto wao. Kama wameridhika na nafasi na maisha ya heri yanayotokana na mazao ya ufisadi uliokubuhu na mfumo uliojengwa nao, basi, waendelee kuchagua CCM na wagombe wake; kama wanataka kilicho bora kwa taifa letu na kwa watoto wao, basi, waoneshe njia.

  Vinginevyo, wakazi wa Dar (wote) ndiyo walioujenga ufisadi katika taifa letu na wao pekee walipe gharama yake. Ni wao ndiyo wanufaika wakubwa wa ufisadi na ni wao waamue kuukataa. Wafuate mifano ya wakazi wa majiji mengine makubwa duniani ambao walikataa ufisadi na kusababisha mapinduzi makubwa ya kifikra katika watu wao hadi kuporomosha tawala zao zilizodumu kwa muda mrefu.

  Wakifanya hivyo, Tanzania mpya inawezekana. Wasipofanya hivyo, wasubiri kuongozwa na watu wa vijijini ambao wameuona mwanga. Unafikiri kwa nini hakuja jimbo hata moja la upinzani katika jiji la Dar?


  Chanzo: Raia Mwema
   
 2. T

  TrueVoter JF-Expert Member

  #2
  Oct 22, 2009
  Joined: Feb 13, 2008
  Messages: 868
  Likes Received: 282
  Trophy Points: 80
  Sasa hivi ndio ninafahamu sababu kubwa iliyomfanya mwl. aamue kuhamisha makao makuu kupeleka dodoma.
  Dar imeharibiwa na USWAHILI wengi wa wakazi wa dar ni wenye asili ya uislamu, ambao kwao elimu si kitu muhimu!! ndio maana ni rahis kuandamana kwa sababu ya kutetea wapalestina na wakakesha wakipiga ngoma lakini hawako tyr kuandamana kiongozi mbovu awajibishwe!!

  Dawa ni kupeleka makao makuu na shughuli zote za serikali dodoma, hapo labda tutaweza kujenga jiji linalowajibika, lakin si dar.
   
 3. K

  Koba JF-Expert Member

  #3
  Oct 22, 2009
  Joined: Jul 3, 2007
  Messages: 6,144
  Likes Received: 495
  Trophy Points: 180
  ...acha kulaumu uswahili au uislam,wezi/mafisadi wengi ni hao wanaosali makanisani na hawana asili ya uswahili,tukubali tuu rushwa na uvivu na kupenda mikato vinamaliza nchi yetu!
   
 4. Bluray

  Bluray JF-Expert Member

  #4
  Oct 22, 2009
  Joined: Mar 25, 2008
  Messages: 3,446
  Likes Received: 31
  Trophy Points: 135
  Huu ni udini / ukabila usio mfano.

  Kwa ujumla Wakristo na waislam wanaweza kuwa na tofauti kama utawaangalia kutoka level ya chini, lakini ukienda level ya juu sana hawana tofauti kubwa kihivyo.

  Kwa ujumla, ingawa kunaweza kuwa na imbalances katika elimu, lakini watu wetu wote -wakristo na waislam- bado hawaja elimika vya kutosha.

  Kwa ujumla kuna sentiments miongoni mwa -sio wote, miongoni, kama wewe TrueVoter- watu wa bara kuwaona watu wa pwani wavivu, na watu wa pwani kuwaona watu wa bara washamba.Hizi tendencies ni destructive, ziko based katika cultural differences na historia zilizokuwa kubwa kuliko uwezo wa watu hawa collectively kuzielewa, zimekuwa overblown na itakuwa vizuri kama tukiweza kuzishinda.

  Kwa ujumla Tanzania sasa hivi inaondoka katika provincial regionalism/ tribalism na kuingia katika urbanization na umoja wa kitaifan unaoanza na watu wenyewe ambao wenzetu wanaouonea gele. Jamii nzima zinahama kutafuta maisha bora, Wazaramo wanaoana na Wasukuma, Wanyakyusa wanaona na Wachagga, Wabondei wanaoana na Wahaya, watoto wanalelewa kuanzia Dar, Moshi, Mwanza, Nairobi, Kampala, mpaka London na New York, hizi definition narrow zinashindwa ku apply.

  Comments zako hapo juu hazisaidii lolote katika kujenga umoja wa watu ila zinaonyesha utovu wa kufikiri unaoendana na kutafuta majibu rahisi kwa matatizo magumu.
   
 5. F

  Fundi Mchundo JF-Expert Member

  #5
  Oct 24, 2009
  Joined: Nov 9, 2007
  Messages: 4,706
  Likes Received: 61
  Trophy Points: 145
  Mkuu na wewe umeingia kwenye mtego! Kwani hakuna waswahili wamisheni? Mbona nina rafiki wakizaramo wengi tu ambao ni wamisheni? Huyu jamaa ungemtolea nje bila kujishusha kufikia level yake.

  Amandla.........
   
 6. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #6
  Oct 24, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,384
  Trophy Points: 280
  Sitoshangaa kuwa Dar-es-Salaam itachagua CCM kwa wingi zaidi kuliko sehemu nyingine yooyote nchini hapo kesho.
   
 7. Tumain

  Tumain JF-Expert Member

  #7
  Oct 24, 2009
  Joined: Jun 28, 2009
  Messages: 3,158
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Mpuuzi tu wewe usiposema uislamu hufurahi..Lol..waislamu na uislamu watakuwepo huko Dodoma vilevile "Jinyonge kama huwapendi **** wewe"
   
 8. Tumain

  Tumain JF-Expert Member

  #8
  Oct 24, 2009
  Joined: Jun 28, 2009
  Messages: 3,158
  Likes Received: 9
  Trophy Points: 0
  Tatizo siyo kuchagua au kutochagua..tatizo kuhesabu na kutangaza kura..inawezekana wananchi wakachagua CUF lakini Tume ikaamua kutanganza wanachokifahamu??? na wanachokitaka
   
 9. Mzee Mwanakijiji

  Mzee Mwanakijiji Platinum Member

  #9
  Oct 25, 2009
  Joined: Mar 10, 2006
  Messages: 31,362
  Likes Received: 6,384
  Trophy Points: 280
  tatizo haliko kwenye kuhesabu kuwa tatizo liko kwenye kupiga kura. Wakazi wengi wa jiji la Dar hawahusishi matatizo yao na utawala wa kisiasa ulioko madarakani. Kwao haya yote yawezekana ni mapenzi ya Mungu au kayaleta shetani!
   
Loading...