Ni upotoshaji au uzuzu mkubwa kufikiria kuwa wizi wa kiwango cha import support, EPA, rada, ndege ya serikali, Richmond, n.k. Unaweza kuhusishwa na mtu mmoja mmoja kipekee (individuals). Wizi wa aina hizo huhusisha michakato yenye hatua kibao kupitia taasisi kuu za maamuzi nchini. Sioni ni vipi rais, waziri mkuu, waziri wa sekta husika, mwanasheria mkuu, wanaweza kupona katika kashfa za aina hiyo. Labda tu kama wahusika halisi wamekamatwa na kuchukuliwa hatua stahiki katika wakati muafaka.
Na kama hao niliowataja hawahusiki basi si rahisi ufisadi aina hiyo ukafanikiwa; lazima utakwama katika hatua fulani za mchakato. Ndio maana katika nchi za waelewa (wasio wapumbavu na malofa), kashfa ya aina hiyo ikitokea, rais au serikali inaachia ngazi. Hawawezi kukubali porojo za watu wenye dhamana kubwa za uongozi wa nchi kunyoosheana vidole mitaani na kuitana mafisadi kwa kuviziana kwenye majukwaa ya kisiasa bila hatua stahiki kuchukuliwa. Ndio maana nakubali kabisa kuwa sisi Watanzania ni wapumbavu na malofa. Watu wanatuibia kimfumo halafu wanakuja kutuchezea komedi ya kuitana mafisadi na sisi tunadandia ngoma tusiyoijua kwa ushabiki mandazi!
Nimemsikia mgombea wa CCM anadai atatoa elimu bure hadi sekondari na dawa hospitalini zitapatikana kwa sababu PESA ZIPO SERIKALINI ILA TATIZO NI MAFISADI WANAZILA; YEYE ATAWAFAGILIA MBALI! Halafu akashangiliwa sana na wananchi! Kwa nini tusimpe kudos Mh. Mkapa kwa kutupa sifa inayotustahili! Nasubiri kampeni ya UKAWA nione kama nayo itaendeleza dhe komedi.