Inaendelea....
Bro alisema tumemuuza maana tumefufua mambo mazito sana hivyo tutashika adabu mule ndani, hakika giza likatanda tena katika akili yangu maana njia niliyodhani itakuwa msaada haikusaidia na badala yake imeleta matatizo zaidi...wakati nikiwaza na kuwazua na huku jamaa akilia pale chini huku kashikilia ubavu mara ghafla akaingia Afande na kutupeleka ubaoni mimi na mdogo wangu.
Tulipofika hapo tukakutana na baba mdogo pamoja na jamaa aliyeibiwa, kumbe aliyeibiwa anatujua vizuri tu tuliishi mtaa mmoja miaka ya nyuma na kupoteana katika harakati za maisha, hivyo akatuomba msamaha kuwa tumsamehe hakujua kama ni sisi, na kwamba anatufahamu tangu ni wadogo hatuna mambo ya ajabu.
Hapo tukapewa nguo zetu na vitu vyetu kama vile mikanda ya suruali na pochi na tuaachiwa kwa maagizo kwamba tukihitajika muda wowote tutaitwa.
Wakati tukivaa vaa vitu vyetu pale nje tulishuhudia karandinga likiingia na kuzungushwa kwa mbwembwe nyingi na kisha likabeba watuhumiwa akiwemo Brother na likaondoka kwa speed kuelekea mahakamani.
Mpaka muda huo tukamshukuru Mungu na kurudi nyumbani japokuwa tulitaniwa kuwa tumekonda kwa usiku mmoja tu, lakini kwetu cha muhimu ni kutoka kule maana ni balaa unapohusishwa katika jambo zito usilolijua mwanzo wala mwisho.
Muda ulipita na jamaa hakupewa dhamana hivyo alikaa mahabusu na hatimae akafungwa ingawa hatukujua alihukumiwa miaka mingapi, ila tu hakutaja wenzake hata mmoja.
Miaka ikakatika kwa amani kabisa ila jioni moja tukashangaa jamaa akaja pale kwa kina mama nyumbani, alikuja akiwa na wenzake kama saba akiwemo mwanamke mmoja ambae pia alionyesha ni hao hao tu, aliniulizia akaambiwa yupo kwake hivyo akachukua genge lake na kuja moja kwa moja kwangu!
Nilipomuona nikajua ohoo yale ya polisi yamekuja kulipiwa kisasi, ila cha ajabu tulisalimiana vizuri kabisa na akasema "mdogo wangu vitu vidogo vile unambwela na kuanza kutiririka mafaili kwa wajinga wajinga, mambo ya kawaida tu ya kwa mwanaume" kisha wenzake wakaunga mkono kuwa kule ni sehemu ya kupangia mipango na ku refresh akili tu hivyo nimeharibu kwa master.
Wakaondoka na kuelekea kule kwenye nyumba ya familia tena, na hapo wakaanza kufungua mabegi waliyokuja nayo na kuanza kugawana mali za wizi bila shaka, na ni wazi kwamba jamaa huenda alitoka muda kidogo na alikuwa akifanya mambo yake na jamaa zake kama kawaida.
Waligawana pesa vibunda, simu na jamaa akampa yule demu cheni nzito ya dhahabu avae, kumbe ni mpenzi wake.
Mama mdogo mwenye mtoto huyo ambae ni mwizi ndiye anaeulea ubovu wote hataki mwanawe asemwe, anasema aachwe kila mtu na majaliwa yake.
Hivyo safari hii jamaa akamuacha demu wake akae pale na mama mkwe na jamaa na genge lake wakasepa maana hakai pale na anapokaa hapajulikani anafanya kuja tu kama mvua.
Bi. Mdogo alikatiwa kibunda hivyo akampokea mkwe na kuona maisha ndiyo haya.
Baada ya siku tatu tu jamaa akaibuka na kumwambia yule demu wake ampe ile cheni akauze kwani hana hata mia, demu akakataa na kusema juzi tu ulikuwa na laki tisa zimekwenda wapi?
Ugomvi ukawa mkubwa jamaa akatoa panga na mke akakimbilia shoka ili zipigwe, ila kwa bahati nzuri wahuni wenzake nao wakaingia na kuongea na shemeji yao vizuri wakapewa cheni na kuondoka.
Katika kipindi ambacho jamaa yupo jela, nilianzisha mfugo wa mbuzi watano na niliwajengea banda pale pale kwa mama na walinawiri na wawili walikuwa na mimba.
Sasa baada ya kupita mkasa wa cheni kama wiki hivi usiku nimelala kwangu nikaota mbuzi wanaibiwa na watu wawili ambao nawajua ni huyo Bro na rafiki ya mwizi mwizi vidole baadhi pia vimekatwa.
Nikashtuka nikataka nitoke niende kule nikaangalie mbuzi ila nikaona ni ndoto tu nikalala, nikakurupuka ni saa kumi na mbili kasoro nikatoka haraka kwenda kuangalia mbuzi, ajabu kufika banda lipo wazi hakuna mbuzi zaidi ya mistari tu ya miburuzo ya kamba, nikaona leo yamenifika.
Nikachukua pikipiki na kwenda sehemu kadhaa za machinjio bila mafanikio ila sehemu ya mwisho nilikuta wamesha chinjwa nimejua hilo kwa sababu ngozi zao zina michoro maana niliwanunua kwa Wamasai na nimezikuta hapo.
Sikutaka kufanya vurugu wala kumshitaki mtu hivyo nilirudi nyumbani maana nilipanga kumshitakia Mungu anipe majibu kwa maadui zangu wa jambo hilo.
Niliomba Mungu nijuavyo mimi (sio uchawi ni kufunga na kumlilia Mungu) na baada ya wiki moja asubuhi, yule rafiki yake bro aliiba simu kwa dada mmoja na kumuwekea kisu shingoni, raia wakamuona na kumpiga mpaka wakamuua.
Siku tatu mbele Bro aliingia kwenye maduka ya wachaga mchana wa saa nane na kuiba fuko moja la ile mifuko myeusi ya nylon iliyopigwa marufuku siku hizi, jamaa kala vitu vyake jicho nyanya akaona haonekani kumbe wenzake wamemuona wanamlia tyming tu, ile kuzama dukani kutoka jamaa wakamzunguka na hapo ukumbuke ni mjini kwenye lami hakuna mawe, hivyo wenye maduka walikuja na mapanga na kumkata kata huku akilia kwa uchungu na kusema hataiba tena, lakini wapi alikuwa amechelewa!
Polisi waliwahi lakini walipoona ni yeye walichoka nae hivyo waliondoka na kuomba wananchi wamalize kazi na ikawa hivyo, akaaga dunia jamaa.
Kizaaa zaa ni siku ya mazishi, ndugu hatukubeba jeneza lake kwani lilibebwa na wahuni kutoka kila pande na walifurika sana, huyu ana sikio moja, huyu jicho moja huku yule ana mguu mmoja basi ilikuwa ni balaa.
Kufika kaburini baada ya kuzika ikabidi Sheikh atoe mawaidha "ndugu zangu maisha ni mafupi hivyo tuishi kwa wema, ona ndugu yetu huyu amekufa katika mazingira magumu ya dhambi..." ghafla Sheikh akapigwa ngumi moja tu ya kichwa na jamaa mmojawapo na akasema "wewe mbwa una msimanga master!!?" Hakuna aliyetarajia jambo hili...