Ufahamu Ugonjwa wa Kifafa na namna bora ya Kuishi na Wagonjwa wa kifafa

JamiiTalks

JF Advocacy Team
Aug 7, 2018
625
938
JFSpaces 10FEB 2.jpg

Kifafa ni hali ya mshtuko wa ghafla au matokeo yasiyo ya kawaida katika Ubongo wa Binadamu ambayo inaweza kusababisha Mtu kuzimia, kukamaa kwa misuli na mabadiliko ya hisia au fahamu

Hali hii inaweza kuathiri Watu kwa njia tofauti kutegemea na eneo la Ubongo linaloathiriwa.

Kufahamu zaidi kuhusu Kifafa, ungana nasi katika Mjadala utakaoendeshwa na Wataalam kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili Februari 10, 2024 saa 10:00 hadi 12:00 Jioni Kupitia X Space ya JamiiForums.

Link ya Mjadala https://jamii.app/MNHSession

UPDATES:

DKT. KIGOCHA OKENG'O, DAKTARI BINGWA WA MISHIPA YA FAHAMU NA UBONGO - MUHIMBILI

Tunakadiria Watu zaidi ya Milioni moja Nchini Tanzania wana Ugonjwa wa Kifafa

Mtu akipata Degedege zaidi ya mara mbili huyo tunaweza kusema ana Kifafa japokuwa sio kweli kuwa kila mwenye Degedege ana kifafa

Kwenye ubongo kuna ‘Umeme’ na kunapotokea hitilafu ya Umeme ndani ya Ubongo ndipo inasababisha Kifafa

Aidha, Kifafa kinatibika na kupona kabisa japokuwa wamegundua 10% tu ya Watu wenye Ugonjwa huu ndio wanatumia Dawa kwa usahihi, wakati 75% wakipata changamoto ya Kifafa wanaelekea kwa Waganga wa kienyeji

Mgonjwa hatakiwi kuacha kutumia Dawa ghafla, anatakiwa kufuata utaratibu aliopewa na Daktari. Anayeacha Dawa ghafla anaweza kurudiwa na Degedege ikiwa na nguvu zaidi na ikawa ngumu kuidhibiti

Aidha, kwa kuwa Kuna Kifafa kinachotokea sehemu moja na kusambaa Mwili mzima, na #Kifafa cha kutokea sehemu moja tu ya Ubongo, Kila aina ya Kifafa ina Dawa yake. Ukitumia Dawa tofauti inakuwa ngumu kupona

FIDES UISO, MKURUGENZI WA TANZANIA EPILEPSY ORGANISATION
Mtoto wake aligundulika kuwa na Kifafa akiwa na Miezi minne, ambapo alipata taarifa nyingi kuhusu Ugonjwa huu, nyingi zikiwa ni potofu

Kama alivyosema Daktari, Watu wengi wakishapata Wagonjwa wa Kifafa hawatumii Dawa au hawaoni Wataalamu sahihi. Kipindi cha nyuma sikuwa nikienda Hospitali, nilivyoanza kwenda nikagundua napata Huduma sahihi na hata gharama zake zilikuwa ndogo tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo nilikuwa naenda hadi kwa Waganga wa kienyeji

Miaka ya sasa Watu wameanza kuelimika na wanaenda Hospitali wakati zamani Watu wenye kifafa walihusishwa na Wagonjwa wenye changamoto ya Akili

DKT. KIGOCHA OKENG'O, DAKTARI BINGWA WA MISHIPA YA FAHAMU NA UBONGO - MUHIMBILI
Kuna Kifafa cha Ubongo mzima, cha upande mmoja na kingine ni cha kurithi japo ni kwa asilimia chache

Asilimia kubwa ya Kifafa inaweza kusababishwa na Ajali kwenye Ubongo au kwa Mtoto wakati wa kuzaliwa au Mtoto akiwa mdogo kupata Magonjwa kama Degedege

Upande wa Watu wazima inaweza kusababishwa na Maradhi kama Kiharusi (stroke) au maradhi mengine kwenye Ubongo

Kifafa kina visababishi vingi, mojawapo ni ulaji wa Nyama ya Nguruwe, ambapo kuna minyoo inayoweza kwenda kwenye Ubongo na kusababisha kovu ambalo mwisho wake linaweza kusababisha Kifafa

EMMANUEL ASSEY, DAKTARI IDARA YA MISHIPA FAHAMU NA UBONGO - KCMC
Ili kuepuka hali hiyo unashauriwa kula nyama ya Nguruwe ambayo imepikwa sana vizuri ili kuweza kupunguza uwezekano wa kupata Degedege

NORMAN JONAS, DAKTARI HOSPITALI YA RUFAA YA KCMC
Moja ya sababu ya vifo kwa Wajawazito ni Kifafa, hivyo anawashauri Wajawazito wawe wanaenda Kliniki mapema kwa kuwa ujauzito unapoanza kufikisha Wiki ya 20 kunakuwa na dalili mbalimbali ikiwemo Presha

Mjamzito anashauriwa kwenda Hospitali mapema na kama akibainika ana changamoto ya Presha au Degedege atapangiwa muda mfupimfupi wa kwenda Kliniki, inaweza ikawa hata kila baada ya Wiki mbili. Hili suala la Degedege na Kifafa linaweza kusababisha kupotea uhai kwa Mama Mjamzito au Mtoto

Kifafa hakiambukizwi kutoka kwa Mtu mmoja kwenda kwa mwingine, hata kama unamuuguza Mgonjwa kwa muda mrefu haimaanishi nawe utapata Kifafa

Amesema Mtu mwenye Kifafa akidondoka hautakiwi kumng’ang’ania au kumuwekea kitu chochote Mdomoni. Unaweza kumlaza kwa ubavu ili kuzuia kupaliwa sababu ni shida inayowapata sana na kama anapigiza Kichwa chini unaweza kumwekea Mto ili asiumie

Pia, ni vyema kuangalia muda, kwamba ametetemeka kwa muda gani, akishakaa sawa mpeleke Hospitali kwa msaada zaidi

DAVID KOMBO, DAKTARI BINGWA WA WATOTO WENYE SHIDA ZA UBONGO NA MISHIPA YA FAHAMU – MUHIMBILI
Ugonjwa wa Kifafa na Degedege umetawaliwa na imani potofu, hivyo huwa kunakuwa na changamoto kwenye Matibabu kwa kuwa wahusika wanakutana na maneno mengi kama kutakiwa kuombewa, kutoa kafara n.k

Mzazi au msimamizi anayemuuguza Mgonjwa kwenye Mazingira ya Nyumbani anaweza kumrekodi Video mgonjwa kisha anapofika kwa Daktari akamuonesha ikawa msaada kujua ni aina gani ya Degedege

Takwimu za Kisayansi zinaeleza kati ya Watu 100 wenye Kifafa, Watu 70 wanaweza kupona kabisa

Hao 30 waliosalia wanaweza kuendelea kuwa na changamoto huku wakitumia Dawa. Pia, kuna aina za Kifafa ambazo haziwezi kutibika kwa Dawa bali kwa upasuaji
 
Back
Top Bottom