UDHAMINI WA ELIMU UGHAIBUNI - MAKULILO, Jr.

MAKULILO

Member
May 30, 2010
84
94
101_0097.JPG
ERNEST BONIFACE MAKULILO (MAKULILO, Jr.)

(Nimekuwa naandika makala kwenye gazeti la Jamhuri ambalo linatoka kila siku ya Jumanne. Hii ni makala yangu ya kwanza kutoka kwenye gazeti hilo. Hadi sasa zaidi ya makala saba zimeshatoka gazetini. Nimeona ni vyema msome hii)

Elimu ya juu ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo ya taifa lolote lile duniani. Ukiangalia nchi zote zilizoendelea zimewekeza kwa kiasi kikubwa kwenye elimu hususani elimu ya juu kuhakikisha inakuwa na wataalamu wengi waliobobea. Katika nchi ya Tanzania, kumekuwepo na kauli mbiu nyingi ambazo zinasisitiza umuhimu wa elimu na maendeleo. Moja ya kauli ambayo ni maarufu sana ni ile ya “Elimu ni Ufunguo wa Maisha”. Kwa haraka haraka, maisha na maendeleo ya nchi yoyote ile yanategemea sana elimu. Ndio maana hata Rais mstaafu wa Afrika Kusini Ndugu Nelson Mandela anasema “Elimu ni nyenzo ya nguvu ambayo unaweza kuitumia kuleta mabadiliko duniani” [Education is the most powerful weapon which you can use to change the world].


Elimu ya juu nchini Tanzania imekumbwa na tatizo la ufadhili. Tatizo la ufadhili linatokana na umasikini wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla wake. Pia tatizo la vipaumbele na mipango ya kiserikali kupelekea watanzania wengi kushindwa kupata ufadhili (mikopo) ili kuweza kupata elimu ya juu katika vyuo vikuu hata kama wamefanya vizuri kwenye masomo yao ya sekondari.
Serikali katika kutafuta utatuzi wa tatizo la ufadhili wa elimu ya juu iliamua kuanzia Bodi ya Mikopo ifahamikayo kama Higher Education Students’ Loan Board (HESLB). Bodi hii imekutana na matatizo mengi pamoja na upinzani mkubwa. Jambo kuu ni kushindwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wengi wenye sifa za kupata mikopo, na wasio na sifa wanapewa mikopo. Mbaya zaidi ni kwamba Bodi ya Mikopo na serikali kwa ujumla wake mikopo ya elimu ya juu itolewayo ni kwa shahada ya kwanza (Bachelor) na kutotoa ufadhili kwa Shahada ya Uzamili (Master) na Shahada ya Uzamivu (PhD). Je, wataalamu wetu nchini wakitaka kujiendeleza zaidi kielimu hadi Uzamivu watapata wapi ufadhili?


Utakuwa ni ukichaa kama mtu ukiamua kugoma kujiendeleza kielimu eti sababu serikali kupitia bodi ya mikopo haitoi udhamini kwenye shahada za uzamili na uzamivu. Ni wakati sasa wa mtu kujua ni mbinu gani wewe binafsi utumie kuhakikisha unapata udhamini na kutimiza ndoto yako kimasomo na kimaisha kwa faida yako binafsi na jamii yako kwa ujumla wake. Kwakuwa serikali imekiri kushindwa kutoa ufadhili huu, basi yatupasa kutafuta njia mbadala wa kupata ufadhili huu.


Ufadhili wa elimu ya juu ughaibuni ni moja ya suluhisho la tatizo hili. Serikali, vyuo vikuu na taasisi mbalimbali za nchi zilizoendelea zina utaratibu wa kutoa udhamini wa masomo ya juu katika vyuo vikuu vya nchi zao kwa watu wanaotoka nchi zinazoendelea kama vile Tanzania. Hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunazitumia fursa hizi vizuri ili wengi wapate udhamini wa elimu ya masomo yao. Mfano wa udhamini kutoka nchi au taasisi hizo ni Fulbright Scholarship (Marekani), Quota Scheme (Norway), NOMA (Norway), Erasmus Mundus (Ulaya kwa Ujumla), NUFFIC (Uholanzi) nk.


Kwa utafiti wangu niliofanya nimegundua kwamba watanzania wengi hawazichangamkii fursa hizi. Moja ya kikwazo kikubwa ni kutokuwa na taarifa za kutosha kwa uwepo wa fursa hizi, na kwa wengine ni kutokujua ni mbinu zipi za ushindi katika uombaji udhamini toka kwenye taasisi husika. Nini kifanyike sasa kuhakikisha kuwa watanzania wengi wanapata kujua uwepo wa fursa hizi na kutambua mbinu za ushindi katika uombaji wa ufadhili huu?


Gazeti hili la Jamhuri litakuwa kila toleo linakuletea makala maalumu inayohusu masuala ya ufadhili wa elimu ya juu ughaibuni. Na mwandishi wa makala hizi si mwingine bali ni Ndugu Ernest Makulilo, anayefahamika zaidi kama MAKULILO, Jr. Ndugu Makulilo ni mmoja wa watanzania ambaye alipata udhamini wa elimu yake nchini Marekani. Mnamo mwaka 2008 alipokea udhamini wa Fulbright (Fulbright Scholarship) wa dola 30,000 ambayo ni sawa na shilingi 48,000,000/= ili kufundisha Kiswahili na utamaduni wa kiafrika katika chuo kikuu cha Marshall kilichopo jimbo la West Virginia. Na mwaka 2009 alipokea udhamini wa dola 24,000 (sawa na shilingi 38,400,000/=) kutoka Rotary International iliyopo Marekani na dola 36,000 (sawa na shilingi 57,600,000/=) kutoka Joan B Kroc Scholarship kwa ajili ya kusoma Shahada ya Uzamili katika Chuo Kikuu Cha San Diego (University of San Diego).
Ukiachilia kupata udhamini huo, Ndugu Makulilo kwa zaidi ya miaka mine amekuwa ni mdau mmoja mkubwa katika kuwasaidia watu watokao nchi zinazoendelea kupata udhamini wa elimu ya juu ughaibuni. Kupitia tovuti zake Makulilo Blog www.makulilo.blogspot.com na Makulilo Forum www.scholarshipnetwork.ning.com anawaelimisha watu wengi ni jinsi gani mtu unaweza kupata udhamini wa elimu ughaibuni. Pia ni mwasisi na mkuu wa Taasisi ya Makulilo (Makulilo Foundation).


Makala hizi za uelimishaji kuhusu udhamini wa elimu ya juu ughaibuni zitakuwa na sehemu kubwa tatu. Ya kwanza ni kutoa mtiririko wa kitaalamu wa jinsi gani unaweza kuomba udhamini na kuweza kupata. Ya pili ni kujibu maswali muhimu ya wasomaji kuhusu udhamini nay a mwisho itakuwa inatoa tovuti mbalimbali zenye hizo taarifa za udhamini ambapo unatakiwa kufanya maombi yako.


Swali la changamoto kwako ni kujiuliza: Kwanini mimi Makulilo nimeweza kuomba na kupata udhamini wa elimu Marekani na kupewa zaidi ya dola 90,000 ambazo ni sawa na shilingi 144,000,000/= ndani miezi 24? Mimi nina nini ambacho wewe huna? Kama mimi nimeweza kwanini wewe ushindwe? Karibu sana katika mfululizo huu wa makala za Udhamini wa Elimu Ughaibuni katika kila toleo

Mawasiliano na Maswali ninandikie hapa makulilo@makulilofoundation.org


MAKULILO
CALIFORNIA, USA
 
Nashukuru sana ndugu kwa kutufungua macho lakin ingekuwa vizuri sana kma ungetuambia njia zipi zinazotumika kupa hizo nafasi za kwenda kusoma huko ughaibuni.
 
Back
Top Bottom