Uchunguzi ufisadi bungeni usiwe wa kulindana

sir.JAPHET

JF-Expert Member
May 18, 2012
699
133
NI jambo jema kwamba Spika wa Bunge, Anne Makinda ameunda kamati kuchunguza tuhuma za ufisadi bungeni, baada ya baadhi ya wabunge katika Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini kutuhumiwa kuhongwa au kudai rushwa ili kushawishi uamuzi wa mamlaka mbalimbali kuhusu sekta hiyo. Tunasema ni jambo jema kwa kuwa Spika ametambua kwamba hasira za wabunge na wananchi zingesababisha mtafaruku, iwapo tuhuma hizo zingefichwa chini ya zulia kwa kuwakingia kifua watuhumiwa.

Uamuzi huo ambao Spika Makinda aliutangaza bungeni siku nne zilizopita, uliweka kando uamuzi wake wa awali, ambao ulikuwa ni kulipeleka suala hilo katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Hatua yake hiyo ilitokana na baadhi ya wabunge kutokuunga mkono kamati hiyo kuchunguza suala hilo, kwa maelezo kwamba baadhi ya wajumbe wake walikuwa na mgongano wa kimasilahi na suala linalopaswa kuchunguzwa.

Ni jambo la ajabu kwamba baadhi ya wabunge katika kamati hiyo na ile ya Nishati na Madini walikuwa na masilahi binafsi katika sekta za gesi, mafuta na madini na hali hiyo ni moja ya mambo yaliyomsukuma Spika kuunda kamati ndogo ya watu watano inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi. Kamati hiyo imetakiwa kuchunguza ukweli wa tuhuma hizo na kuwasilisha ripoti yake kwa Spika ndani ya siku 14 kuanzia siku hiyo. Spika Makinda hakusema bayana kama ataruhusu ripoti ya kamati hiyo isomwe bungeni, lakini kama atakuwa amesoma alama za nyakati, zinazotoa picha kwamba Bunge lote linanuka rushwa, itambidi afanye hivyo kutokana na wabunge wengi kutaka wenzao wasio wasafi watajwe bungeni ili walio wasafi wasafishike mbele ya wapigakura wao.

Haijulikani hadi sasa kama kamati hiyo itaweza kufanya uchunguzi wa kina na kutoa ripoti isiyoacha maswali wala kutia shaka siyo tu kutokana na muda mfupi iliyopewa kuwasilisha ripoti hiyo, bali pia kutokana na kutokuwapo kwa uzoefu wa kutosha kwa wabunge kuwachunguza wabunge wenzao. Pengine ndiyo maana wananchi wengi wamemtaka Spika kuhakikisha kamati hiyo haifanyi kazi hiyo katika misingi na utamaduni wa kulindana.

Vinginevyo, hatuna sababu ya kutilia shaka hatua ya Spika ya kuteua kamati hiyo, hasa baada ya kusema wazi kwamba anataka kamati hiyo ifanye uchunguzi kwa haki na weledi, ikiwa ni pamoja na kupitia kumbukumbu rasmi za Bunge (Hansard) ili kujua michango ya wabunge wakati wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini kwa nia ya kuwahoji. Hiyo pia ni fursa nzuri kwa wabunge waliotaka kuwataja bungeni wenzao wakiwatuhumu kupokea rushwa kupeleka ushahidi mbele ya kamati hiyo sasa.

Sisi tunaitakia kamati hiyo mafanikio na kuwataka wajumbe wake kufanya kazi kwa uadilifu ili kurudisha hadhi na heshima ya Bunge ambalo hakika sasa liko njia panda,,:israel:
A%20S%20465.gif
A%20S%20465.gif
 
Back
Top Bottom