Uchukuaji fomu CCM ni Siasa za Urithi, Umaarufu, Uwekezaji ndani ya chama au upendeleo wa uteuzi baadae?

Uchukuaji fomu CCM ni Siasa za Urithi, Umaarufu, Uwekezaji ndani ya chama au upendeleo wa uteuzi baadae?

DodomaTZ

Senior Member
Joined
May 20, 2022
Posts
161
Reaction score
200
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeingia kwenye mchakato wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 kwa kasi ya aina yake. Hadi sasa, zaidi ya wanachama 5,475 wamejitokeza kuchukua fomu za kugombea nafasi za ubunge na uwakilishi. Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa Julai 3,2025 na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla amesema jumla ya shilingi bilioni 2.7 zimekusanywa kupitia ada ya fomu pekee, huku kila mgombea wa ubunge akilipa shilingi 500,000 na wa udiwani shilingi 50,000.

Mchakato huu unaonesha wazi kuwa siasa ndani ya CCM si tena mahali pa wito pekee bali pia sehemu ya uwekezaji, umaarufu, urithi, matarajio ya ulaji na uteuzi wa kuonekana hapo baadae.

Siasa za kurithiana nafasi
Katika orodha ya waliokwisha kuchukua fomu, majina ya watoto wa viongozi wa zamani na waliopo madarakani yameibuka kwa wingi. Hali hii inaashiria kuwa kuna tabia ya kurithishana nafasi za uongozi ndani ya chama, ambapo familia zilizozopo na hata ambazo ziliwahi kuwa kwenye mfumo wa chama hicho zinaendelea kutawala kizazi hadi kizazi.

Mfano wa hayo ni Jesca Magufuli, mtoto wa Hayati Rais John Magufuli, ambaye amejitokeza kuwania ubunge wa viti maalum mkoani Geita. Hili ni kielelezo cha dhahiri cha namna siasa zinavyoendelea kuwa urithi wa kifamilia, ambapo watoto wa viongozi waliowahi kushika madaraka makubwa serikalini sasa wanaendeleza nyayo za wazazi wao kwa kutumia majina yao kama ngazi ya kuingia kwenye mfumo wa uongozi.

Kwa Jesca, jina la Magufuli si tu kumbukumbu ya uongozi uliopita bali pia silaha ya kisiasa inayoweza kumrahisishia safari ya kupenya ndani ya chama katika mchujo. Hali kama hii inaleta changamoto kwa wagombea wengine wasio na majina makubwa au historia ya kifamilia, kwani ushindani hauegemei tena kwenye uwezo au uadilifu bali pia kwenye nasaba na urithi wa kisiasa.

Mwengine ni Rachel Mashishanga, binti wa mwanasiasa mkongwe Stephen Mashishanga, aliyewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), ambaye naye amechukua fomu ya kuwania ubunge wa viti maalum Mkoa wa Morogoro. Vilevile, Dkt. Kellenrose Lwakatale ni mtoto wa marehemu Dkt. Getrude Lwakatakele, ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt Kellenrose sasa anawania ubunge wa Jimbo la Mlimba lililopo Wilaya ya Kilombero, Mkoa wa Morogoro.

Kwa upande wa Salma Kikwete, ambaye ni mke wa Rais wa awamu ya nne, Jakaya Mrisho Kikwete, amechukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Mchinga lililopo Wilaya ya Lindi, Mkoa wa Lindi hii ni mwendelezo wa ushawishi wa familia ya Kikwete ndani ya siasa za Tanzania.

Mchakato huu umeibua mijadala mikubwa mitandaoni na miongoni mwa wachambuzi wa siasa, wakieleza kuwa siasa ndani ya CCM imegeuka kuwa chombo cha kifamilia badala ya majukwaa ya ushindani wa wazi. Wengine wanaona kuwa watoto wa wakubwa wana nafasi kubwa zaidi ya kuaminiwa au kuteuliwa, hata kabla ya kujieleza kwa wananchi au wanachama wa kawaida.

Watu maarufu wasogelea ulaji kwa kasi.
Mchakato wa mwaka huu pia umevutia kundi kubwa la watu mashuhuri kutoka tasnia ya burudani, uandishi wa habari na mitandao ya kijamii. Wapo wanaoamini kuwa umaarufu sasa umetafsiriwa kama mtaji wa kisiasa, hali inayowapa fursa watu wa kawaida kwa majina yao lakini wenye ushawishi mkubwa kwa jamii ya mitandao ya kijamii.

Miongoni mwa waliotangaza nia kupitia kuchukua fomu ni pamoja na msanii na mjasiriamali Zena Mohamed maarufu kama Shilole ambaye anawania ubunge wa viti maalum Mkoa wa Tabora.Kwa Shilole si mara ya kwanza kuonekana kwenye harakati za kisiasa ndani ya Chama cha Mapinduzi alikuwahi kuchukua fomu ya kuwania nafasi ya ubunge wa viti maalum kupitia CCM katika Mkoa wa Tabora. tangu mwaka 2020 na sasa anaendeleaa.

Mwengine Burton Mwemba, anayefahamika zaidi kwa jina la Mwijaku, naye amejitosa kwenye siasa akiwania Jimbo la Mvomero lililopo Wilaya ya Mvomero, Mkoa wa Morogoro. Mwijaku akiwa kama mtangazaji na mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii amekuwa akikipigania na kukutetea Chama Cha Mapinduzi hadharani kwa muda mrefu kupitia majukwaa ya kijamii na vyombo vya habari.

Clayton Chipando, anayefahamika zaidi kwa jina la Baba Levo, amejitokeza pia kuchukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Kigoma Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM). Hata hivyo, kabla ya hatua hii Baba Levo alikuwa na historia ya kisiasa ndani ya chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo, ambako aliwahi kuchaguliwa na kuhudumu kama Diwani wa Kata ya Mwanga Kaskazini katika Manispaa ya Kigoma Ujiji kuanzia mwaka 2015 hadi 2020. Kuhamia wake kutoka ACT Wazalendo kwenda CCM inaweza kuwa ni mkakati wa kisiasa wa kusogea karibu na mfumo wenye nguvu zaidi wa uongozi.

Kwa upande wa viongozi wa vilabu vya michezo, Klabu ya Yanga SC inaonekana Kwenda sambamba na rangi za klabu hio na mapenzi ya Chama cha Mapinguzi kwa mfanano wa rangi huko nako Injinia Hersi Said ambaye ni Rais wa Klabu ya Yanga SC anawania Jimbo la Kigamboni huku Arafat Haji, Makamu wa Rais wa klabu hiyo, akilenga kugombea Ubunge wa Jimbo la Shauri Moyo lililopo Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharib, Arafat ambaye aliwahi kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) pia kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) amejitosa kwenye siasa rasmi.

Kwa upande wa waandishi wa habari nao hawajabaki nyuma. Adam Malima ambaye ni mwandishi wa habari maarufu nchini Tanzania, ambaye kwa sasa anafanya kazi na kituo cha Channel Ten amejipatia umaarufu mkubwa katika tasnia ya uandishi wake wa habari za kijamii, kisiasa, na za maendeleo, na amekuwa akichangia kwa kiasi kikubwa katika vyombo mbalimbali vya habari nchini. Ila nae alijitokeza kuchukua fomu ya kugombea ubunge wa Jimbo la Mpwapwa kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mwengine ni Salim Kikeke, aliyekuwa mtangazaji wa BBC Swahili na kwa sasa akiwa Crown Media amechukua fomu kwa ajili ya ubunge Moshi Vijijini, akisema anataka kutumia uzoefu wake wa miaka mingi kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo hilo.

Kuna mitazamo kuwa baadhi ya wagombea hawa huenda hawana dhamira ya dhati ya kushinda, bali wanataka kujionyesha mbele ya chama, kuchangia fedha, au kufanikisha kujulikana kwa matarajio ya kuteuliwa. Hili linaweka picha kuwa siasa za sasa si tu kazi ya huduma bali pia ni fursa ya kupanua majina, biashara na ulaji mnene wenye maslahi.

Wafanyabiashara na watoto wao
Kundi jingine linalojitokeza ni la watoto wa wafanyabiashara wakubwa na watu wenye mitaji mikubwa ya kifedha. Hawa wanaingia katika siasa wakiwa na nguvu ya fedha zaidi, wakiamini kuwa nafasi ya uongozi ni sehemu ya kuongeza ulinzi wa maslahi yao na kupanua ushawishi wa kifamilia.

Miongoni mwao ni Tinson Nzunda ambaye ni mfanyabiashara na mkulima kutoka Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe, mmiliki wa kiwanda cha kahawa na parachichi, ambaye anagombea ubunge Jimbo la Vwawa lilipo Wilaya ya Mbozi, Mkoa wa Songwe.

Omari Msigwa, anayefahamika pia kama Super Feo, ni mfanyabiashara katika sekta ya usafirishaji, na amejitokeza kuwania ubunge Jimbo la Madaba lipo n Wilaya ya Madaba, Mkoa wa Ruvuma.

Zanzibar nako ni Mohamed Ibrahim Raza Hassanali, maarufu kama Raza Lee, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa mbunge wa Zanzibar na mfanyabiashara mashuhuri Ibrahim Raza, amechukua fomu ya uwakilishi Jimbo la Amani kupitia CCM.

Kwao, siasa inatafsiriwa kama sehemu ya mtandao wa biashara, ambapo kufika bungeni au barazani kunawawezesha kuendelea kushikilia nafasi za kiuchumi na kijamii kwa nguvu ya mamlaka ya kisiasa.

Madaraka, uteuzi na ulaji.
Hali ya watu mashuhuri, matajiri, watoto wa wakongwe na wanahabari kugombea imeibua tafsiri nyingine juu ya mvuto wa nafasi za kisiasa. Kuna mtazamo kuwa siasa ya sasa si tena kazi ya kujitolea kwa jamii bali ajira ya uhakika. Mbunge au mjumbe wa baraza analipwa mshahara mnono, anapata posho za kila kikao, magari ya kifahari, safari za nje na marupurupu mengine mengi ambayo kwa mtu wa kawaida si rahisi kuyapata.

Mbali na hayo, nafasi hizi huwapa viongozi hao ushawishi mkubwa katika jamii, hujihusisha na miradi ya maendeleo, taasisi za kifedha, na hata fursa za uteuzi wa bodi mbalimbali au nyadhifa serikalini. Hivyo basi, si ajabu kuona idadi kubwa ya watu wakijitokeza kwa gharama zao kuchukua fomu, kwa kuwa uwekezaji huu unaweza kurejeshwa kwa njia nyingi ndani ya mfumo wa kisiasa.

Baada ya zoezi la uchukuaji fomu kukamilika mbivu mbichi kujulikana kwenye vikao vya mchujo ngazi ya kata ambavyo vitaanza Ijumaa, Julai 4, 2025 ambapo kamati za siasa ngazi ya kata zinatoa mapendekezo ya waliotia nia ngazi ya udiwani na udiwani wa viti maalum. Vikao hivyo vitafuatia na kamati za siasa za wilaya na baadaye kamati za siasa za mkoa ambazo zitafanya uteuzi wa majina matatu ya madiwani watakaopigiwa kura na wajumbe. Kamati hizo za mkoa zitafanya uteuzi Julai 9, 2025.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom