Uchambuzi wa Kina: Nike Fuelband

Uchambuzi wa Kina: Nike Fuelband

ManiTek TV

JF-Expert Member
Joined
Jun 3, 2011
Posts
410
Reaction score
159
25/03/2013

​

Mwaka 2013 kwenye ulimwengu wa teknolojia ni mwaka wa gajeti za kuvaa (wearable tech). Kampuni kubwa zote zimeshaingia kwenye uwanja huu; Tetesi za iWatch ya Apple, Google wameshatangaza rasmi Google Glass na pia kuna taarifa kwamba Google wako mitamboni kutengeneza saa, Samsung wameshatangaza S Band kwa ajili ya Galaxy S4, Pebble Watch zinauzwa kwa kasi kubwa, lakini zote hizi zilitanguliwa na Nike Fuelband, gajeti iliyojipatia umaarufu mkubwa kwa wanamichezo na hata wasio wanamichezo. Tumeijaribu gajeti hii katika shughuli mbali mbali za kimichezo na za kawaida ikiwa ni pamoja na kukimbia, kuendesha baiskeli na mazoezi ya aina ya taebo, tumepata matokeo mchanganyiko, yaani mazuri na kasoro kadhaa.

Kabla ya kuingia kwenye faida na kasoro za gajeti hii, kwanza tuanze na kujibu swali ni nini hasa Nike Fuelband? Kwa mujibu wa Nike wenyewe, hichi ni kifaa halisi cha kuonyesha uanamichezo. Kifaa hichi ambacho huvaliwa mkononi mithili ya saa huonyesha mambo manne makubwa ambacho huvaliwa mkononi: Kwanza inaonyesha wakati, kwa hiyo ni saa ya mkononi. Pili inaonyesha kalori ambazo mvaaji ameunguza na anaendelea kupunguza mwilini mwake, tatu inaonyesha idadi ya hatua ambazo mvaaji ametembea na kukisia masafa katika maili na mwisho inaonyesha kitu kilichotungwa na kampuni ya Nike walichokiita Fuel.
​
Fuel ni kipimo mithili ya kalori lakini hakitofautishi mwanamke wala mwanamme, umri wala ukubwa wa mwili kwa wafanya mazoezi na hata kwa shughuli za kawaida katika siku. Kwa kitumia kipimo cha fuel Nike huweza kukushauri unahitaji fuel kiasi gani ili kuishi maisha ya afya njema, au unahitaji fuel kaisi gani ili kuweza kujiweka vyema kiafya kwa ajili ya mashindano katika mchezo fulani. Mbali ya kushauri unaweza kupanga malengo yako mwenyewe.

Pia Nike ina mtandao wa kijamii ambapo watumiaji wa Fuelband huweza kulinganisha mwenenod wao dhidi ya watumiaji wengine wa rika lao au hata kujilinganisha na wanamichezo maarufu Duniani kama vile mcheza tenisi Serena Williams. Mtandao huu hufanya watumiaji wa gejeti hii kuwa na aina fulani ya starehe au furaha.
​
Sasa tuingie kwenye kasoro za Nike Fuelband gajeti hii haifai kwa waendesha baskeli, kwa sababu unaweza kutambua shughuli uzifanyazo kwa mtikisiko wa mkono ambao FuelBand imevaliwa, kwa vile mkono katika kuendesha baiskeli huwa umewekwa tu kwenye usukani, basi Fuelband huwa haiwezi kufanya kazi sawa sawa. Hata hivyo katika majaribio yetu tukaona kwa vile mguu huzungusha pedeli basi tuivae kwa kuifunga kwenye nyuzi za viatu, kwa ujanja huu Fuelband imetoa matokeo mazuri zaidi katika fuel, hata hivyo imeshindwa kutoa takwimu sahihi kwa masafa tuliotembea, yaani umbali halisi uliorekodiwa na app ya Cyclist tukitumia kompyuta ya Wahoo Blue SC ulikuwa mkubwa kuliko ule tulioupata kwenye Fuelband, kwa hiyo kwa waendesha baiskeli au wenye kushiriki michezo ya baiskeli basi hichi si kifaa kinachowafaa.

Uzuri wa Fuelband kwanza unaweza kuweka kumbukumbu zako zote za mazoezi na shughuli za kila siku kwenye ama kompyuta yoyote kati ya Mac na Windows (kuanzia XP service pack 2) au simu za iPhone (kuanzia iOS 5), hivyo kasoro kubwa ya pili ya gajeti hii ni kwamba haina App ya Android, hata hivyo unaweza ku-sync na kupata matokeo kwa kutumia browser yoyote katika simu au tablet za Android. Mtandao au app ya gajeti hii ina dashbodi ambayo inaonyesha kalori, fuel, umbali (kwa maili), na jumla ya wakati uliofanya mazoezi au ulioushughulisha mwili wako. Pia huonyesha ni kaisi gani umefanya mazoezi ukilinganisha na malengo uliyoyaweka.

​
Sehemu ya Activity: Huonyesha rekodi ulizoweka na malengo uliyoyafikia au kushindwa kuyafikia kwa muda wa siku, au wiki, mwezi au hata mwaka kwa kutumia Bar Chart na takwimu nyingine. Pia huonyesha wastani wa mazoezi au shughuli zako kwa wiki, mwezi au mwaka. Vipimo vya taarifa hizi vinapatikana kwa vipimo vya umbali, fuel, kalori na muda.

Katika muda wa siku sita tuliotumia Fuelband kwa majaribio, tumeweza kufikia malengo katika siku tatu (2,500 Fuel), na pia tumeweza kuwa na wastani bora kuliko wastani wa jamii nzima ya watumiaji wa Nike Fuelband,. Takwimu rasmi za Nike Plus zinaonyesha kwa wastani jamii ya wana-Nike Plus hupata Fuel 876, nasi tumeweza kufikisha wastani wa Fuel 1,900 kwa siku. Hivyo basi uzuri wa gajeti hii hukufanya ujihimize kuishi maisha ya kiafya hata ukiwa si mwanamichezo, na malengo yake si magumu sana kuyafikia iwapo utajituma kwa muda wa kiasi cha dakika 45 tu kwa siku.

​
Tukiingia kwenye Nike Fuelband yenyewe, hupatika katika rangi tatu nyeusi, nyeusi inayoonyesha (translucent) na nyeupe inayoonyesha (translucent) Ina mita inayoonyesha ni kiasi gani umefikia ukilinganisha na lengo la siku, ina skrini inayoonyesha saa, fuel, hatua ulizotembea na kalori ulizounguza. Pia Skrini hiyo inaonyesha kama Fuelband inapeleka taarifa kwenye mtandao na simu (sync). Skrini pia huonyesha kiasi cha chaji ya betri. Pia inapoingia kwenye stting za simu au mtandao utaweza kuona kiwango cha chaji kilichosalia kwenye betri. Pia gajeti hii inazuia maji yaiingie na kuiathiri hivyo huna hawa ya kuwa na wasi wasi wa majasho au kuoga nayo.
​
Fuelband huunganishwa na simu kwa teknolojia ya bluetooth na pia ina uwezo wa kutambua hatua na mitikisiko kwa teknolojia ya akselerometa. Fuelband haina GPS, hivyo hupanga umbali kwa kutegemea akselerometa tu. Kwa upande wa ramani inabidi mtumiaji aingize mwenyewe njia anazopita kwenye mazoezi, na hii ndio hasara ya ukosefu na GPS. Watumiaji wa Fuelband huwa na akaunti katika mtandao wa Nike Plus.
​
Gajeti hii pia huweza kutumika bila ya kuwa na simu yako karibu nawe kwani huhifadhi yenyewe takwimu zote, na baadae unaweza kuzihamisha takwimu hizo kwenye mtandao na simu kwa kubonyeza kifungo cha sync.

Kifungo kimoja kilicho kwenye gejeti hiyo hutumika kuonyesha taarifa zote nne muhimu, pia huonyesha salio la chaji kwenye betri na hutumika ku-sync na iPhone, na kabla ya ku-sync kifungo hicho hutumika kuunganisha na simu (pair) kwa mara ya kwanza. Pia kifungo hicho kinatumika iwapo unataka kufuta takwimu zote na kuanza upya (reset) kwenye gajeti hiyo, haya yote hutofautiana kulingana muda wa mbonyezo.
​
Gajeti hii huchajiwa na chaja ya USB yoyote ambapo katika boksi unapata tu waya, gajeti yenyewe, kifaa cha kuongeza au kupunguza ukubwa (sizing tool), na vipande 2 vya kuongezea ukubwa (flinks for a fine-tuned fit). Kwa mujibu wa Nike chaji ya gajeti hii hudumu kwa siku nne na katika majaribio yetu Fuelband ilipitiliza siku tatu na kubakiwa na chaji karibu na robo. Bei yake kwa UK ni £129 (TSh. 316, 332).

Kwa kifupi mpaka sasa Nike Fuelband ni bora kuliko gajeti nyingi za aina hii kwa muenekano na kwa hata kwa utendaji kazi, hasa baada ya mashaka ya hivi karibuni yaliyoikumba Pebble Watch. Kwa wale ambao wangeweza kukushangaa umevaa kitu gani unaweza kutoa jibu rahisi bila ya maelezo nalo ni; saa, tofauti na nyingine ambazo hazina skrini na wala hazina saa kama vile S band ya Samsung na Jawbone. Mpaka hapo Google na Apple watakapotoa zao, iwapo watatoa kweli, kwa sasa Nike Fuelband ni mfalme wa gajeti za mkononi.
Chanzo: Gajetek Habari: Uchambuzi wa Kina: Nike Fuelband

​
 
Back
Top Bottom