Ubalozi wa Marekani Dar wanusurika kulipuliwa

BabuK

JF-Expert Member
Jul 30, 2008
1,845
329
UBALOZI wa Marekani Dar es Salaam umenusurika kulipuliwa.

Mwanafunzi wa shule ya msingi anayedaiwa kuhamasishwa na mafunzo aliyopewa na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda amekiri kutaka kuulipua.

Taarifa kutoka ndani ya ubalozi huo, zimeeleza kuwa kijana huyo ambaye hakufahamika jina lake, amekamatwa, yupo katika kituo cha polisi, Oysterbay, Dar es Salaam.

Habari zinadai kuwa,mwanafunzi huyo mwenye umri wa kati ya miaka 15 na 17 aliingia ndani ya ubalozi huo Jumapili iliyopita saa tatu usiku, akiwa na vifaa alivyotaka kutumia kufanyia ugaidi huo.

Inadaiwa alikuwa na dumu la lita tano la mafuta ya taa, utambi na kiberiti cha gesi.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari, baada ya kuingia ndani ya ubalozi huo, alikwenda moja kwa moja kwenye tangi linalohifadhi zaidi ya lita 1,000 za dizeli kwa nia ya kulilipua.

Habari zilidai kuwa, kijana huyo alipoingia ndani ya ubalozi huo akipitia geti namba tatu ubalozini hapo, walinzi walikuwa wamelala.

Alipolifikia tangi hilo, kijana huyo anayedaiwa kuwa mwanafunzi wa shule ya msingi Mtambani wilayani Kinondoni, alijaribu kufungua koki za tangi hilo kwa nguvu na kuwaamsha walinzi hao usingizini.

Walinzi walimkamata na baada ya kumhoji, alikiri kuingia katika ubalozi huo kihalifu akitaka kuulipua, hatua ambayo ingesababisha mshituko mkubwa kama wa asubuhi ya Agosti 7, 1998, ubalozi huo ulipolipuliwa na kuua watu kadhaa wakiwamo Watanzania na Wamarekani.

Kijana huyo alidai kuwa yeye na wenzake wapatao 15 walipatiwa mafunzo kwa njia ya video na mtandao huo, kwa ajili ya maandalizi ya kuulipua ubalozi huo Juni mwaka huu.

Alidai baada ya kuhamasika na mafunzo hayo, yeye na mwenzake aliyekuwa amemwacha katika eneo linalotumika kuuzia maua karibu na ubalozi huo, walikwenda kujaribu kutekeleza mafunzo hayo kwa vitendo.

Taarifa zilisema walinzi hao walimpeleka kijana huyo katika kituo cha Polisi cha Oysterbay, ambako anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Ofisa Habari wa habari katika Ubalozi wa Marekani nchini, Halima Mbaruku, alithibitisha kuwapo kwa jaribio alilosema ni la kuuchoma moto ubalozi, lakini akasema kwa sasa hauko katika nafasi ya kulizungumzia, kwa kuwa polisi wanalifanyia uchunguzi.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova alipoulizwa kuhusu tukio hilo, hakutaka kulizungumzia zaidi ya kusema yeye hayuko Kinondoni.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mtambani, Daudi Mwinyijuma, alipoulizwa kuhusu habari hiyo, alitaka atajiwe kwanza jina la mwanafunzi huyo, ili afuatilie, lakini hakuna mtu aliyekuwa tayari kumtaja mshukiwa huyo.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Elias Kalinga, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, kwani simu yake ilikuwa haipatikani.

Agosti saba mwaka 1998, balozi mbili za Marekani katika Afrika Mashariki; wa Tanzania na Kenya, zililipuliwa kwa kipindi cha muda mfupi ambapo jumla ya watu 258 waliuawa na wengine 5,000 walijeruhiwa.

Kwa ubalozi wa Dar es Salaam, gari lenye milipuko lilifika asubuhi ulipokuwa ubalozi huo barabara ya Laibon na kutaka kuingia katika moja ya malango na kuzuiwa na lori la maji lililokuwa linamilikiwa na ubalozi huo.

Ilipofika saa 4.39 gari hilo lilifyatua mlipuko kutoka umbali wa meta zipatazo 35 nje ya ukuta wa ubalozi na kusababisha vifo na majeruhi.

Watanzania waliopoteza maisha yao katika shambulizi hilo la kigaidi ni Abdulahaman Abdulah, Elisha Paulo, Elia Hassan, Siyad Harane, Ramadhani Mahundi, Mtendeje Rajabu na Mbegu Abdallah.

Wengine ni Mohamed Abas, William Mwila, Almosaria Yussuf, Mzee Shamte, Yusuph Ndale Bakari, Yusuph Nyumbo na Dotto Seleman.

Katika kujibu mashambulizi hayo, Serikali ya Rais Bill Clinton wakati huo, ilishambulia kituo cha mafunzo cha Afghanistani na kiwanda cha dawa cha Khartoum Sudan, ambacho kinadaiwa kutengeneza gesi inayotumika kulipulia mabomu.

Mashambulizi hayo yalidaiwa kufadhiliwa na Osama bin Laden, ambaye anaaminika kuendesha mtandao wa ugaidi dhidi ya Marekani.

Chanzo: Habarileo
 
Back
Top Bottom