#COVID19 Twitter kuanzisha mfumo wa kupambana na taarifa potofu kuhusu chanjo ya corona

Sam Gidori

Senior Member
Sep 7, 2020
165
414
Twitter imesema kuwa inaanzisha mfumo mpya wa kubaini na kuondoa machapisho yanayopotosha kuhusu chanjo ya COVID-19 na kuwafungia watumiaji wa mtandao huo watakaoonekana kusisitiza kuenea kwa habari za uongo.

Kampuni hiyo yenye makao yake San Fransisco nchini Marekani imesema katika chapisho la blogu kuwa inaamini hatua hiyo itasaidia kupunguza madhara yatakayotokana na kuenezwa kwa taarifa potofu kupitia jukwaa lake.

Mfumo huo utahusisha kuwajulisha watumiaji wa mtandao huo ikiwa chapisho litakuwa na taarifa potofu kuhusu maambukizi ya virusi vya corona, hasa chanjo ya virusi hivyo, ikiweka alama kuwa taarifa iliyopo katika chapisho hilo si sahihi.

Ikiwa mtumiaji ataendelea kuchapisha taarifa zisizo sahihi kwa mara ya pili na ya tatu, akaunti yake itafungiwa kwa saa 12, na akiendelea kupotosha kwa mara ya nne, akaunti ya mtumiaji huyo itafungwa kwa muda wa siku 7. Mtumiaji atakapoendelea kupotosha kwa mara ya tano, Twitter imesema kuwa italazimika kuifungia akaunti hiyo moja kwa moja.

Mtandao huo ulitoa wito kwa watumiaji wake kuondoa machapisho yanayotoa taarifa zisizo sahihi kuhusu maambukizi ya virusi vya corona mwishoni mwa mwaka jana, taarifa hizo zikihusisha zile zinazosema kuwa chanjo ya virusi vya corona inatumika kuwadhuru watu au kuhoji uhalisia wa kuwepo kwa virusi vya corona.

Tangu hapo, Twitter imeondoa machapisho 8,400 na kuwajulisha watumiaji zaidi ya milioni 11.5 kote duniani kuhusu kukiuka taratibu za taarifa kuhusu virusi vya corona.

Mfumo huu mpya wa Twitter unafanana na ule uliotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Marekani ambapo akaunti ya Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump ilifungiwa moja kwa moja kwa kurudiarudia kupotosha umma na kutumia lugha ambayo mtandao huo umesema inaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuhoji uhalali wa matokeo ya uchaguzi huo.

Kampeni za chanjo ya virusi vya corona inafanyika katika nchi mbalimbali duniani katika juhudi za kuwaweka watu salama na kurudia hali ya maisha iliyokuwepo kabla ya kuzuka kwa maambukizi ya virusi hivyo.

Mitandao ya Facebook na YouTube pia imechukua hatua kupambana na taarifa potofu kuhusu virusi vya corona na chanjo.

Chanzo: AFP
 
Ukiona hivyo ujue tayari kuna mtu kaiweka Twitter mfukoni.

Ukweli siku zote hupingwa.
 
Back
Top Bottom