Tusikubali Wanasiasa Wapandikize Chuki Dhidi ya Polisi

Tusikubali Wanasiasa Wapandikize Chuki Dhidi ya Polisi

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Joined
Mar 10, 2006
Posts
34,250
Reaction score
44,579
tanzania-police.jpg
Na. M. M. Mwanakijiji

Mara nyingi napenda kusoma hoja na kuziacha tu hata kama naona zimejengwa vibaya. Hata hivyo kuna wakati inabidi nijirushe ndani kwani hatari ya kuacha hoja hizo zisimame kama zilivyo ni kwamba zinapata uhalali wa kuaminika hasa kwa watu ambao kwa sababu moja au nyingine hawawezi kuona ulaghai wa hoja (fallacy) uliofichika ndani yake.

Yametokea mauaji ya polisi jana usiku ambapo polisi wanne wameuawa, kuporwa silaha na wananchi wengine kujeruhiwa. Mwitikio wa wa baadhi yetu ni kushtushwa na kukasirishwa na kitendo hicho na kukilaani bila kukihusisha na siasa za nchi yetu – iwe upinzani au chama tawala. Tumechukulia tukio hilo kama kitendo cha uhalifu ambao hakina namna yoyote ya kuonekana “kinaeleweka”.

Hata hivyo wapo baadhi ya ndugu zetu – na ninaamini wanaamini wanafanya kwa nia njema kabisa – ambao kwa kutumia ujanja wa maneno wakijificha katika kutoa rambirambi na pole wakijaribu kuhusisha tukio hilo na siasa zinazoendelea nchini. Baadhi yao wanajaribu kuonesha kuwa tukio hilo limetokea kwa sababu ya Polisi kujihusisha na kulinda amani au kuonekana wanatekeleza maagizo ya kisiasa ambayo yanakandamiza au kubana siasa za upinzani.

Julius Mtatiro – akiandika katika ukurasa wake wa Facebook anasema “Baada ya majambazi kuwaua POLISI (RIP), sehemu kubwa ya raia kwenye mitandao ya kijamii wanashangilia. Nimeshtuka sana. Hii ni dalili kuwa jamii yetu imeanza kugawanyika. Kwa nini Raia wanaanza kufurahia unyama wanaotendewa ndugu zao? Hii chuki imeanza lini? Kaileta nani? Serikali ijitathmini upya, kuna tatizo kubwa na litaanza kukua. Mungu awasitiri wafiwa wote”

Kwa ufupi yeye anasema kuwa wapo watu wanafurahia mauaji ya polisi kwa sababu Serikali ndio imewafanya watu wafurahia mauaji ya ndugu zao; kwamba, serikali ikiacha kufanya mambo fulani basi watu hawatofurahia mauaji ya polisi! Hii ni miongoni mwa hoja muflisi kabisa ambazo nimewahi kuzisoma. Hivi ni serikali gani ambayo itaacha kufanya mambo ambayo inaamini kuwa ni ya usalama kwa taifa au ni ya muhimu ati kwa sababu watu wachukia polisi?

Anaposema “Serikali ijitathmini upya” ana maana gani? Serikali ijitathmini katika mambo gani? Na anapozungumzia “chuki” anaitambua vipi? Siyo kweli kwamba mahali pengi duniani watu wanaochukia polisi mara nyingi ama ni wahalifu wao wenyewe au wanufaika wakubwa wa uhalifu? Raia anayetegemea usalama wake na amani kwenye mtaa na nyumba yake nan chi yake anaweza vipi kufurahia polisi wakiuawa? Kwamba, raia mwenye chuki na chama fulani cha kisiasa au kiongozi fulani wa kisiasa – sema Rais kwa mfano – anapata uhalali gani kufurahia mauaji ya polisi ambaye siyo mwanasiasa na siyo kiongozi wa kisiasa bali mtu aliyekubali kupewa jukumu la kulinda nchi na usalama wa raia? Siyo kwamba, mtu anayehamishia chuki za kisiasa kwa polisi anaongozwa siyo na chuki bali ujinga uliopilitiliza; yaani hajui polisi wanatekeleza majukumu yao vipi.

Naye Peter Msigwa – Mbunge wa Iringa Mjini – na yeye anaenda mbali kidogo katika hili lakini akitumia ‘fallacy’ ile ile. Yeye anasema – kwenye mtandao huo huo wa Facebook – “Nichukue nafasi hii kutoa pole sana kwa familia za Askari wetu waliouwa kikatili na Majambazi , hii haikubaliki kabisa . Nashauri jeshi la polisi liimarishe kitengo cha intelejensia kukabiliana na uhalifu wa aina hii badala ya kitengo hicho kuwa cha KISIASA kuKABILIANA NA UPINZANI na kuilinda CCM”

Na yeye pia anafanya (commit) kosa lile lile la Mtatiro. Yeye anaona kuwa mauaji haya ya polisi yasingefanyika kama Polisi wasingekabiliana na upinzani au “kuilinda CCM”. Hata tukichukulia kwa ajili ya hoja hii kuwa kweli Polisi wanatumika kukabiliana na upinzani au wanailinda CCM ni kwa vipi hili linaelezea au kuhalalisha kwa namna yoyote mauaji ya vijana wetu ambao walikuwa wanaenda kupokea lindo kulinda Benki ya CRDB?

Vinginevyo tunaweza vipi kuhusisha kwake tukio la mauaji ya polisi na suala la siasa za upinzani?

Hivi ni kuwa kama kungekuwa hakuna huu mgongano hewa kati ya upinzani na serikali hawa polisi wasingeuawa? Hivi wahalifu (wawe majambazi au vinginevyo) wanaamua kushambulia polisi na kuwaua kwa sababu polisi wanatekeleza maagizo yao ambayo yana athari kwa vyama vya siasa maagizo ambayo wao hawana namna ya kuyakataa? Hivi ni kweli kama polisi wakiamua kukaa pembeni na kuacha wapinzani wafanye mambo yao, wanaandamane popote na kwa namna yoyote bila ulinzi wa polisi hivi kweli likiharibika jambo hawa viongozi wa upinzani watasema “polisi” ndio wakulaumiwa?

Bila ya shaka wengi mnakumbuka lile tukio lililotokea wiki si nyingi zilizopita huko Dallas, Texas ambapo waandamanaji wenye kutetea haki za weusi katika mwamko wa Black Lives Matter walikuwa wanaandamana kupinga vitendo vya kikatili ambavyo wameona vikifanyika kwa weusi na baadhi ya polisi weupe. Katika kuandamana kwao kule kupinga polisi bado walihitaji ulinzi wa polisi! Na Polisi wale wakiwa wanawalinda waandamanaji wakajikuta wanashambuliwa na polisi watano wakauawa siku ile!
05FUNERALWEB10-master675.jpg

(Pichani msafara ya mazishi Afisa Liu huko Marekani, aliuawa kwa kushtukizwa akiwa ndani ya gari na askari mwenzie. Chini msafara mwingine wa polisi wa New Jersey aliyeuawa Melvin Santiago).

funeral-police-officer-melvin-santiago.jpg


Na baadaye kulikuwa na tetesi za baadhi ya makundi ya vijana walikuwa wakishangilia mauaji ya polisi wale; lakini wakati huo huo baadhi ya waandamanaji wale wale wakati milio ya bundi inashambuliwa wakaenda kujificha nyuma ya polisi wale wale ambao walikuwa wanawaona wabaya! Baadhi ya watu wakagundua kuwa maneno makali dhidi ya Polisi na kuwapaka rangi ile ile polisi wote ni kutowatendea haki na kuhatarisha usalama wa jamii yenyewe.

Sasa, kama itatokea – na nadhani inaweza ikawa hivi – CHADEMA na vyama vya upinzani vikaruhusiwa kuandamana au wakalazimisha kuandamana na polisi wakaamua kuwaacha waandamane bila ulinzi wowote hivi ikitokea watu miongoni mwao wakaanzisha vurugu siyo kwamba viongozi hao hao wa CHADEMA watakuwa wa kwanza kulalamika kwanini “Polisi” wale wale wabaya hawakutoa ulinzi? Na kama polisi wataamua kutoa ulinzi halafu watu wakawashambilia Polisi kwa sababu wameaminishwa kuwa ni wabaya wao kwa vile wamekuwa ni “kitengo cha CCM” hawa viongozi wa upinzani watakubali kuwajibika au wataendelea kuona kuwa wao hawahusiki katika kupandikiza hii chuki dhidi ya polisi nchini?

Maneno makali – ambayo wengine labda wanayaona ni rahisi kuyatoa – dhidi ya Polisi wetu hayajengi upinzani wala kuimarisha uhusiano bali yanazidisha chuki na kwa namna fulani yanajibu swali lao la “nani ameleta chuki hii”. Ingawa wanaweza kudhani kuwa kile kinachoonekana chuki dhidi ya polisi kinatokana na Serikali au CCM wakati umefika kwa viongozi wa upinzani wenyewe nao kujiangalia kama kauli zao na maneno yao dhidi ya Polisi hayachangii katika kuongeza chuki dhidi ya polisi.

Leo hii, kama viongozi hawa wa upinzani nchini mwetu nao wakipatwa na majanga na wakatafuta msaada wa polisi hivi wataelewa polisi wakiamua kuwaziria na kugoma kwenda kutoa msaada kwa vile wanachangia kupandikiza chuki dhidi ya polisi kuna mtu ataelewa?

Ukweli ni kuwa wapo watu ambao wanachukia polisi na wataendelea kuchukia polisi kwa sababu zao. Lakini kwa jamii inayojidai kutaka kujenga utawala wa kidemokrasia haiwezi hata kidogo kuvumilia au kuchekea matukio dhidi ya polisi ati kwa vile polisi wakati mwingine wanapotekeleza majukumu yao wanaweza kujikuta – kihalali au kwa makosa – wamesababisha madhara ya watu au vitu.

Mtu anayeshambulia polisi na hata kuwaua anakuwa katika uhalali gani wa kutekeleza jambo gani ambalo linaweza kumuweka sawa na askari polisi ambaye akitekeleza majukumu yake akiamini anailinda jamii akajikuta amemuua mtu au kumdhuru? Polisi anayefanya hivyo hata kwa makosa kuna taratibu za kisheria na kijeshi za kuchunguza jambo hilo (kama tulivyoona katika baadhi ya kesi); lakini Raia anapomuua Polisi ni kwa vipi tunaweza kudhani naye anatekeleza jambo fulani kiasi kwamba kuna moral equivalency kati yake na polisi?

Binafsi, nakataa na nalaani vikali kauli za kisiasa ambazo zinaonekana kuchochea baadhi ya wananchi kuchukia polisi n ahata kujaribu kufafanua ni kwanini mauaji ya polisi yanaweza kuwa yanahusiana na hali ya kisiasa nchini. Kufanya hivyo ni kutokuwa wawajibikaji na watu ambao wanajaribu kufafanua vitendo viovu ili kuhalalisha au kupata magoli fulani ya kisiasa.

Kama demokrasia hatuwezi kusimama bila kuwa na vyombo vya usalama ambavyo wananchi wake siyo tu wanavitegemea lakini wanasimama navyo.

Ni matumaini yangu askari hawa waliouawa watachukulia kama mashujaa ambao majina yao yatakumbukwa na Serikali iwazike siyo tu kwa heshima za kijeshi bali pia kwa heshima za mashujaa ambao waliuawa wakiwa kazini kuitumikia Taifa lao hata kwa damu yao. Ni matumaini yangu, misafara ya mazishi yao itaongozwa na makundi ya polisi na raia wema waliojipanga barabarani kuenzi utumishi wao na kuona fahari kwa vijana wao hawa na kuwapa moyo polisi wengine kuwa mamilioni ya Watanzania bado wako nyuma ya polisi wao na wanawategemea pamoja na changamoto zote zilizopo.



Wakati umefika tuanze kuwakatalia viongozi wa kisiasa kupandikiza chuki au kutetea chuki dhidi ya polisi kwa kisingizio au sababu yoyote ile.

Niandikie: Mwanakijiji@klhnews.com
 
mtahangaika sana kutafutia maneno ya magufuli ya zuio la mikutano uhalali lakini ukweli upo pale pale yupo against na sheria,taratibu za nchi.chuki dhidi ya polisi wanasababisha polisi wenyewe kwa kutotumia utashi katika kulinda haki za raia.Tukutane September 1
 
MM siku hizi post zako hazichangiwi na wengi na hao wachache wanaochangia wengi wanakupinga, jiulize kwanini?

....Jitahidi kutochukua upande, nyeupe ita nyeupe huenda hadhi yako ikarudi kama zamani, ni ushauri tu, take it or leave it
 
Tuwakatalie wanasiasa kupandikiza chuki hii, tena tuanze na mwenyekiti wa chama tawala tumkatalie kuwatumia polisi kwa maslahi ya chama chake!!!

Na alisema hakuna mambo ya polisi jamii, polisi anapaswa kuogopwa!!!!

Hii ni mbegu mbaya sana
 
Nikisikia polisi kauwawa kwa vyovyote vile roho yangu husuuzikaa, nafurai sanaa.

Tofauti na wenzetu huko ulaya ambao wengi hupata huzuni, kwasababu kwao police ni chombo cha ulinzi wa mali za usalamaa, lakini huku kwetu ni chombo cha kukandamiza demokrasia na mauaji ya raia wasio na hatia (rejea mauaji ya zombe, mwangosi, morogoro) na kuhakikisha ccm inabakia madarakani kwa namna yoyote ilee.

Yaweza kuwa police waliouwawa hawana hatia lakini acha wafe tu maana wengi huwakilisha wachachee
 
Nikisikia polisi kauwawa kwa vyovyote vile roho yangu husuuzikaa, nafurai sanaa.

Tofauti na wenzetu huko ulaya ambao wengi hupata huzuni, kwasababu kwao police ni chombo cha ulinzi wa mali za usalamaa, lakini huku kwetu ni chombo cha kukandamiza demokrasia na mauaji ya raia wasio na hatia (rejea mauaji ya zombe, mwangosi, morogoro) na kuhakikisha ccm inabakia madarakani kwa namna yoyote ilee.

Yaweza kuwa police waliouwawa hawana hatia lakini acha wafe tu maana wengi huwakilisha wachachee
RIP ALLY ZONA
RIP MAWAZO
RIP MWANGOSI
RIP MASHUJAA WA ARUSHA
RIP MASHUJAA WA SOWETO ARUSHA

Mungu awalaze mahala Pema peponi
 
Mbona huwahoji wanaohusisha mauji haya na upande wa pili?Umejiuliza wana dhamira gani?Huoni hao ndio watu hatari zaidi?Acha kuwa mnafiki!
 
Sio leo tena! Hivi kale kagazeti kako ka cheche siku hizi kalifia wapi?
 
Mzee mwanakijiji nashukuru sana kwa andishi lako refu ambalo kwa kadiri ulivyoweza umekwepa aidha kwa makusudi ama kwa bahati mbaya kuogopa kuongea ukweli. Hapa umejitahidi kama kawaida ambayo umejijengea siku hizi ya kuhakikisha unaupaka upinzani rangi mbaya. Hilo hatuna tatizo nalo kwani kidemokrasia unaruhusiwa kuutetea upande unaoutaka, ila ni vyema kweney maandishi marefu hivyo ujitahidi kuchimba chanzo cha tatizo na hisia hizi unazoziona. Kwa taarifa yako hiyo chuki unayajaribu kuipinga hapa jukwaani kwa kuukwepa ukweli ndio inazidi kumea kwa ajili ya watu kama nyie. Wewe ni mmojawapo ya wapo wanaopandikiza chuki dhidi ya upinzani hapa jukwaani, una hoja kidogo lakini kwa kiasi kikubwa wewe ni mmoja kati ya watu wanaopandikiza chuki dhidi ya upinzani hapa jukwaani. Leo hii unatoa wapi nguvu ya kupinga chuki dhidi ya polisi wakati wewe unapandikiza chuki dhidi ya kundi jingine?

Naomba nikupe mifano michache hapa chini uone jinsi gani jeshi la polisi limekengeuka aidha kwa kujipendekeza ama kutekeleza maagizo yenye double standard. Mwezi uliopita ccm imefanya mkutano wa kumpata mwenyekiti wao, kila mtu alijionea jinsi jeshi la polisi lilivyohakikisha uchaguzi wa ccm unafanyika bila hata mende kupoteza maisha. Hivi majuzi kumefanyika mkutano mkuu wa cuf kupata mwenyekiti wake, polisi walikuwepo kulinda usalama, je uliona ile fujo iliyotekea huku polisi wakiacha kutekeleza wajibu wao tena kwa makusudi kamili. Tulimuona kamanda Siro akipiga picha tena kuonyesha ushujaa jinsi gani atapambana na ukuta, lakini hatukumuona akiwa na hata muhalifu mmoja aliyeharibu mkutano wa cuf!! Mzee mwanakijiji katika mazingira kama hayo unashangaa nini unapoona chuki za namna hii wakati sababu ziko wazi kabisa. Hivi kweli unaweza ukaandika maandishi marefu ya kiwango kile bila kuonyesha udhaifu huu wakati chanzo cha hizo chuki kiko wazi na hujaonyesha popote zaidi ya kuandika kishabiki na hisia zako.

Umeshindwa nini kuwaleza watawala hicho wanachokipanda kupitia jeshi la polisi sasa ndio maua yaanaanza kujitokeza tayari kuelekea mazao kubeba? Kwa taarifa yako hii chuki iliyojionyesha hapa hata hao watawala wenyewe wameona kile wanachokipanda kinaanza kumea, na wao walidhani kutumia nguvu ni suluhisho wakati sio kweli. Kwenye mioyo ya watu kumeshajengeka hiyo hali ambayo haiwezi kuondoka kwa vitisho bali kusameheana na kila mtu kutekeleza wajibu wake.

Napenda kurudia, wewe ni sehemu ya kueneza chuki hapa jukwaani ni vyema ukajirekebisha na sio kuja kujifanya unarekebisha wenzio wakati wewe ni sehemu ya tatizo.
 
Back
Top Bottom