Wakati wa Uchaguzi Mdogo wa Kata nne kule mkoani Arusha,nilisema kikaoni na hapa JF kwamba nisingekwenda Arusha. Na ni kweli.Sijaenda. Nilisema kuwa CCM yetu haikuwa na nafasi hata ya kushinda kata moja. Nilibezwa,nilidhihakiwa,nikadharauliwa na kukosolewa. Matokeo yalionekana.Tukapigwa 4-0.
Uchaguzi mdogo mwingine umeshatangazwa na Tume ya Uchaguzi iliyo chini ya Jaji Damian Lubuva. Imesema kuwa Februari kutakuwa na Uchaguzi wa Madiwani wa Kata 29. Kati ya hizo,1 ni ya Arusha:Sombetini. Kule alikotokea Mawazo.Kule alikoacha uongozi Mawazo na kuhamia CHADEMA.Kule ambapo Mawazo na CHADEMA wana nguvu. Kule ambapo,tayari CHADEMA imemsimamisha mtu maarufu pia: Ally Bananga; M-CCM wetu wa zamani.
Kuna Kata 29.Ni heri CCM yetu ijielekeze kata 28. Ijielekeze kule ambapo tunaweza kupita bila kupingwa.Kule ambapo wananchi bado wanakitambua na kukipenda 'chama cha Nyerere' pasipo kufuatilia hasa kinachofanya na jinsi kinavyowahudumia. Kule ambapo CCM huchaguliwa kwa rangi yake;takrima yake;'mbinu zake' na 'mizengwe yake'. Lakini si Sombetini.
Twende kule ambapo idadi ya wapigakura yaweza kubadilishwa bila ya vikwazo vyovyote. Kule ambapo majina ya waliojiandikisha yaweza kuwa yoyote yale na hatuhojiwi.Twende kule ambapo mgombea wetu aweza kutangazwa mshindi 'kwa dharura na chini ya ulinzi mkali'.Kwakuwa watu wanakipenda chama chetu.Kwakuwa watu wanapenda CCM na viongozi wake.Kwakuwa daftari la kupigia kura laweza kutupa ushindi.Kwakuwa wananchi wanaweza 'kuzuiwa' kwenda kupiga kura zao. Lakini si Sombetini.
Sombetini tusiende. Hakuna haja. Twendeni kwingineko katika Kata 28. Hima chama changu,tusonge mbele!
Mzee Tupatupa wa Lumumba,Dar es Salaam