Tunduru: Walionunua Korosho kwa fedha taslimu katika vituo vya kukusanyia korosho wakamatwa

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,848
12,082
KOROSHO ZA MTATIRO" ZAKAMATA 11.

IMG-20191124-WA0009.jpeg


Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Tunduru vinawashililia makarani na waandishi 11 wa vyama vya msingi kwa tuhuma za kununua korosho za wakulima kwa fedha taslimu katika vituo vya kukusanyia korosho.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru Ndg. Julius Mtatiro kuendesha oparesheni maalum ya kupambana na biashara haramu ya korosho maarufu jina la "kangomba".

Makarani na waandishi hao wanatuhumiwa kujihusisha na ununuzi wa korosho kwa fedha taslimu katika vituo vya kukusanyia korosho na kisha kuziingiza kwenye mfumo rasmi wa stakabadhi ghalani.

"Mmekuwa mkiwashinikiza wakulima wawaaachie korosho zao kisha mnawalipa fedha taslimu shilingi 1,500 kwa kilo moja, na kisha korosho hizo mmekuwa mkiziingiza kwenye mfumo rasmi kwa kutumia majina ya matajiri waliowakabidhi fedha ili kufanya uhuni huo", ameeleza DC Mtatiro katika kikao na viongozi na waandishi na makarani wa vyama vya msingi.

"Siyo tu kwamba mmeripotiwa na wakulima, bali hata korosho za mtego za DC zilipowafikia mlizinunua na ndipo tukabaini kuwa nyinyi ni vinara wa kuvunja viapo vyenu vya kazi kwenye vyama vya msingi", amesisitiza Mtatiro.

Pamoja na kukamatwa kwa watumishi hao 11 wa vyama vya Msingi wilayani Tunduru, Mtatiro amewasimamisha majukumu hayo na kuwapiga marufuku kukihusisha na masuala ya korosho kwenye vyama vya msingi katika msimu huu. Mtatiro amewataka viongozi wa vyama vya msingi ambavyo watuhumiwa hao wanafanya kazi, viwaondoe kazini mara moja ifikapo kesho Jumatatu.

DC Mtatiro amechukua hatua hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi, waandishi na makarani wa vyama vya msingi wapatao 500 katika ukumbi wa Cluster wilayani Tunduru na kusisitiza kuwa oparesheni kangomba ni endelevu.

"Nawahakikishia kuwa, ikiwa mtaendelea kujihusisha na mchezo huu wa hovyo, sitasita kuchukua hatua zilezile; kuwakamata, kuwaondoa kwenye shughuli za Amcos na kuwashtaki, korosho za DC zitawamaliza".

Katika hatua nyingine Ndugu Mtatiro amemtaka Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU) kuhakikisha TAMCU inakuwa na orodha ya vijana wengi waliohitimu kidato cha nne ili waweze kuchukua nafasi za makarani na waandishi wasio waaminifu mara moja kwani zoezi la kuwabaini na kuwaondoa makarani na waandishi wasio waaminifu litaendelea msimu mzima wa korosho.

Imeandaliwa na Idd Mohamed M,
Tunduru,
21 Nov 2019.
 
Back
Top Bottom