Tundu Lissu na Mchungaji Msigwa, acheni chuki za kitoto kwa Zitto

assadsyria3

JF-Expert Member
Apr 9, 2013
6,904
4,050
Imeripotiwa na vyombo viñgi vya habari juu ya wabunge hawa kukataa kumpa mkono wa kwaheri ndani ya bunge.Hata ingekuwa wewe MTU umpe mkono halafu yeye asikupe utajisikiaje?

Huu si utamaduni wetu hata kama MTU mnatofautiana.Siasa sio chuki tena twajiita wachungaji sijui ni wa kinigeria?
======================

KITENDO cha aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kutangaza bungeni kuwa anang'atuka ubunge, kilisababisha Bunge kuzizima huku akipewa pole na wabunge wengi.

Hata hivyo mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu na alikacha kumpa mkono.

Zitto ambaye alisoma barua aliyomwandikia Spika Anne Makinda, kuwa analazimika kuachia wadhifa wa ubunge baada ya chama chake kutangazia umma kuwa sio mwanachama wao, kulisababisha simanzi kwa wabunge wengi ambao baada ya kikao cha Bunge kusitishwa wengi walienda kumpa pole.

Hata hivyo, Zitto ambaye alikuwa amekaa pamoja na wabunge wengine wa Chadema ambao wengi wao walimkumbatia kama ishara ya kumpa pole na kumtakia kila la heri aendako, Lissu na Msigwa waligoma kumpa mkono mbunge huyo.

Kitendo cha Lissu na Msigwa kukacha kumpa mkono Zitto, kiliwafanya baadhi ya wabunge kupigwa na butwaa, lakini hata hivyo Lissu alipoulizwa kwa nini hakumpa mkono mbunge mwenzake huyo, ambaye wametumika pamoja kwenye chama cha Chadema kama viongozi, alisema yeye sio mnafiki.

Msimamo wa Zitto

Zitto aliliambia Bunge kuwa licha ya kutopokea barua rasmi ya kumjulisha juu ya uamuzi wa kumtimua uanachama, ameona ni vyema akachukua uamuzi huo mapema kwa sababu jamii inaamini kwamba yeye sio mwanachama wa Chadema.

"Nashukuru, ushirikiano nilioupata kwa Bunge la Tisa na la 10, limenijenga na kunifanya niwatumikie Watanzania kwa kiwango nilichostahili. "Naondoka katika Bunge hili lakini naamini nitarudi tena kwa mapenzi ya Mungu na tunaweza kuonana mwezi Novemba," alisema.

Kuhusu mafao mbalimbali anayostahili kupata kutokana na utumishi wake kwa Bunge, alisema hilo kwake si muhimu na akaendelea kukumbusha kuwa kama Watanzania wanakumbuka ni siku nyingi yeye aliomba kuondolewa posho mbalimbali, ili ziende kusaidia Watanzania wenye shida.

"Suala la mafao kwa sasa kwangu si kipaumbele, cha msingi niende msituni kufanya kazi ya siasa," alisema Zitto ambaye alipoulizwa na waandishi wa habari anaenda wapi, alisema kuwa siku sio nyingi kuanzia sasa atatangaza mustakabali wake wa kisiasa.

Hata hivyo wachambuzi wa mambo ya siasa wanaamini kuwa mbunge huyo atajiunda na Chama cha ACT ambacho maswahiba wake wengi ambao walitimuliwa Chadema, walienda kukianzisha.

Wanasiasa hao pamoja na Profesa Kitilya Mkumbo, Samson Mwigamba na wengineo wengi. Chama hicho licha ya uchanga wake wa kisiasa, lakini kinaelezwa kuwa kina wafuasi wengi mkoani Kigoma hasa katika Jimbo la Kigoma Mjini ambako wachambuzi wa mambo wanasema mwanasiasa huyo ana mpango wa kwenda kugombea katika jimbo hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na Peter Serukamba (CCM).

Filikunjombe

Mmoja wa wabunge marafiki wa Zitto, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM), ambaye amefanya kazi na Zitto kwenye kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma (POAC) na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC), akiwa kama Makamu wake wa Mwenyekiti alisema kazi iliyofanywa na mbunge huyo, haitasahaulika.

Filikunjombe alisema kamati yake na Bunge zima linatambua uwezo na mbegu iliyopandwa na mbunge huyo kijana katika kusimamia maslahi ya umma na kwamba katu haitasahaulika.

"Ni mwanasiasa kijana, lakini kichwa chake ni kizuri, tumesikitishwa na hatua hii; lakini hatuwezi kuingilia mambo ya ndani ya chama chake. Tunaamini ni kiongozi mzuri hivyo anaweza kuongoza kwa namna yoyote akiwa sehemu yoyote na kuleta mchango wake kwa Taifa," alisema Filikunjombe.

*Lissu, Msigwa

Lissu ambaye alitangaza kuvuliwa uanachama wa Zitto baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa pingamizi la mbunge huyo kijana, jana alisema licha ya upungufu alionao mwanasiasa huyo kijana, lakini kuna mengi mazuri amekifanyia chama.

Alisema Zitto licha ya ujana wake lakini alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuongoza Chadema miaka ijayo, kurithi viongozi wa sasa ambao ni Mwenyekiti Freeman Mbowe au Katibu Mkuu, Dk Willibrod Slaa.

"Hakuna mtu shetani wala malaika sote ni binadamu wa kawaida, licha ya upungufu aliouonesha bado atakumbukwa kwa mchango wake ndani ya chama chetu," alisema Lissu.

Akizungumzia hatua yake ya kukacha kumpa mkono Zitto, Lissu alisema alichelewa kufanya hivyo kwani kungemfanya aonekane kuwa ni mnafiki, kwani yeye binafsi anasimamia kile alichosema na kuwa anakiamini kuwa kuna kasoro nyingi zilizosababisha Zitto avuliwe uanachama.

"Ameamua kuondoka kwa kuwa alijua ndicho kinachofuata kwa kuwa haya makatazo ya kikatiba ya kukataza mambo ya chama kupelekwa mahakamani alishiriki kuyatengeneza," alisema.

Naye Msigwa alisema Zitto alitumia muda mwingi wa maisha yake ya kisiasa kuijenga Chadema na kufanikiwa kuingiza vijana wengi ndani ya chama hicho.

Alisema binafsi anamkubali Zitto ingawa hamuungi mkono katika mambo yake ya hovyo yaliyokuwa yakielekea kupasua chama chao. "Sisi kama chama tuna taratibu zetu na mtu anapozikiuka ni lazima ataadhibiwa tu, na hili ni kwa vyama vyote sio Chadema tu," alisema Msigwa.

Profesa Mosha Akizungumza na gazeti hili jana kuhusu mustakabali wa Zitto kisiasa, Profesa Raymond Mosha wa Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Nelson Mandela Arusha, alisema hawezi kutabiri kitakachotokea.

Alisema amekuwa akifuatilia siasa za Zitto siku nyingi na alipenda mawazo yake na hata maandishi yake, yaliyokuwa yakitokana na usomaji wake wa vitabu na hata alipokwenda nje ya nchi, alikuja na mawazo yanayoweza kusaidia nchi.

Pamoja na kuvutiwa na siasa hizo, alisema hana uhakika na uhusiano wa Zitto na viongozi wenzake Chadema, kwa kuwa alikuwa akituhumiwa kusaliti chama hicho na kulikuwa na madai kuwa alitaka kupata uongozi bila kufuata utaratibu.

Profesa Mosha alisema anapenda siasa ziwe za busara, lakini historia ya vyama vya siasa nchini, inaonesha kumekuwa na kawaida ya kufukuza wanachama, huku akisisitiza kuwa kama watu wanataka demokrasia, inapaswa kuanzia ndani ya chama.

Kuhusu kitakachotokea kwa Chadema, alisema haoni kama chama hicho kitapata msukosuko mkubwa, kwa kuwa kinapendwa na watu vijijini hasa Arusha.

Alifafanua kuwa Chadema imekuwa ikionekana ina nia ya dhati ya kusaidia wananchi na hasa kupigana na ufisadi, ambao Zitto alijitokeza kupambana na uovu huo na anatarajia ataendelea kupambana huko anakokwenda.

Balozi Sanga

Mmoja wa wasomi wa Chuo cha Diplomasia, Mhadhiri Mwandamizi wa chuo hicho, Balozi Charles Sanga alinukuliwa hivi karibuni akisema kuwa pamoja na umuhimu wa kuheshimu katiba ya chama, chama hicho kingefanya uvumilivu na sio kuchukua hasira.

Alisema ni vyema uvumilivu ukatumika katika kukijenga chama hicho na sio kufanya uamuzi wa hasira ambao unaweza kupunguza nguvu ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

"Kujenga chama cha siasa sio jambo jepesi na la siku chache, ni kitu kinachochukua muda mrefu na huko ndani kuna watu tofauti, sasa ni vyema jambo kama hili, Chadema ingefanya uvumilivu, ujenzi wa chama sio lele mama," alisema na kuongeza: "Nchi za Kiafrika bado zinajaribu kujenga vyama vyao, kwani ni changa, tunahitaji kuvilea, tuvumiliane, ila pia sheria mama za vyama zisivunjwe, ila pia sheria za kawaida ziangaliwe tuvumiliane kidemokrasia na sio kuchukua hasira," alisema.

Dk Bana, Mkosamali

Msomi mwingine, Dk Benson Bana ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi wa Idara ya Sayansi ya Siasa katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mchambuzi wa masuala ya siasa za Tanzania, pamoja na Robert Mkosamali, msomi na mchambuzi pia wa siasa hizo walisema, kwa nyakati tofauti pia kuwa, kwa kumvua uanachama Zitto, Chadema itajibomoa kwa kupunguza wanachama.

Akizungumzia kipengele cha Katiba ya Chadema, kinachokinzana na Katiba ya nchi ya mwaka 1977, pamoja na haki za binadamu, Bana alisema; "Msajili wa vyama vya siasa ana kila sababu ya kufanya mapitio ya katiba zote za vyama vya siasa kuhakikisha hazina vipengele vinavyomzuia mwanachama au kiongozi wa chama kwenda mahakamani kutafuta haki anayoamini kuwa hawezi kuipata ndani ya chama chake".

Kwa upande wake, Mkosamali alisema, Mahakama ndicho chombo pekee kinachotajwa na Katiba ya nchi kuwa ndipo mtu yeyote anapoweza kukimbilia kupata haki yake ya msingi.

"Ni kweli Ibara ya 71 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 katika ibara ndogo ya 1 (e) inasema; "Mbunge atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake katika Bunge itokeapo mambo yafuatayo; (f) Iwapo Mbunge ataacha kuwa mwanachama wa chama chake na iwapo chama chake kitakuwa kimemvua uanachama.

Kwa maelezo ya Mkosamali, kulingana na maelezo hayo ya Katiba, Zitto amevuliwa uanachama, lakini bado chama chake kupitia mikutano ya ndani, kingeweza kumpa nafasi nyingine kwa kuyajadili mambo hayo kwa uvumilivu ndani ya mikutano yake.
Chanzo:Habarileo
 
Mchungaji Msigwa akumbuke yeye ni Mtumishi hivyo awe mfano wa kusamehe kwa vitendo.
 
Msigwa atapata anacho stahili

Kipi we gamba msigwa atapata? Unajua swala la ubunge iringa mjini tulishalifunga? Tunampa madiwani na majimbo yetu mawili kalenga na mufindi kwa mgimba pale kuna kamanda willy ndo ufahamu gamba au msaliti wa Act kwanza iringa kuna Act?
 
Nimewapenda bure Msigwa na Lema, hakuna unafiki na MSALITI!!!
Huyu kidudumtu kumbe hata mwigamba 2009 alishaung'amua usaliti wake!!!
 
Kipi we gamba msigwa atapata? Unajua swala la ubunge iringa mjini tulishalifunga? Tunampa madiwani na majimbo yetu mawili kalenga na mufindi kwa mgimba pale kuna kamanda willy ndo ufahamu gamba au msaliti wa Act kwanza iringa kuna Act?
Chadema mnapata wapi nguvu ya kujiteua peke yenu wakati ndio mnajitanabahisha kama AUKAWA
 
Back
Top Bottom