MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dodoma, jana ilifutilia mbali kesi iliyokuwa ikimkabili Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu (Chadema) na kusema kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kimakosa hivyo haiwezi kuendelea kusikilizwa.
Jaji Sivangilwa Mwangesi,alisema kuwa kesi hiyo ilikuwa na kasoro nyingi kutokana na vifungu vya kisheria na akasema haiwezi kuendelea kusikilizwa mahakamani hapo.Kesi hiyo ilifunguliwa na wanachama wawili wa CCM, Shaban Itambu na Pascal Hallu ambao wamewafungulia kesi ya kupinga matokeo Mbunge wa Singida Mashariki, Tindu Lissu, msimamizi wa uchaguzi na mwanasheria wa serikali.
Hata hivyo wakati kesi hiyo ikifutwa jana, Lissu mwenyewe hakuwepo mahakamani baada ya kuelezwa kuwa aliharibikiwa na gari akiwa njiani kuja Dodoma ambapo aliwakilishwa na ndugu yake Samson Mkotya ambaye alisema kuwa mbunge huyo alikuwa Morogoro baada ya juzi kuharibikiwa na gari lake.
Kufutwa kwa kesi hiyo ni ushindi kwa Tundu Lissu ambaye tangu mwanzo wa kesi hiyo alionekana kujiamini zaidi na kusema kuwa kesi hiyo ingeishia katika hatua za mwanzo bila ya kufika mbali.
"Mimi nasema kuwa,kesi hii naisimamia mwenyewe na ninatambua kuwa haiwezi kufika mahali popote kwa kuwa imejaa makosa mengi ya kisheria ambayo kimsingi kama Jaji ataamua kufuata haki hakuna kesi hapa," alisema Lissu siku alipowasilisha ombi la kufutwa kwa kesi hiyo.
Mbunge huyo ambaye kitaaluma ni mwanasheria aliwasilisha kumbukumbu za hukumu za kesi nyingi ambazo zilifunguliwa kwa mtindo huo ambazo alisema kuwa yeye (Lissu) alizisimamia lakini alishindwa.
Baadhi ya kesi alizonukuu Lissu ni pamoja na kesi ya John Mnyika na Charles Keenja, Joyce Chitende na Zainabu Gama, John Jomba na Christopher Ole-Sendeka ambazo alisema kuwa zote zilifunguliwa kwa mtindo huo lakini zilishindwa kuendelea.
Jana Jaji Silivangira alisema licha ya Kifungu cha 111 (b) ambacho Lissu alisema kuwa kimekosewa kutokuwa na mapungufu ya moja kwa moja, lakini kwa kutumia sheria hiyo katika kifungu 112 (a),(b) bado ufunguaji wa kesi hiyo ulionekana kuwa na makosa.
Moja ya vitu ambayo Lissu alitaka viwekwe ni pamoja na wadai hao kulipa gharama za kesi ya uchaguzi ambazo walishindwa kuzilipa,kingine ni pamoja na kufutilia mbali ombi la wadai walilotaka kusamehewa kulipa gharama hizo akidai kuwa kama hawana fedha wasingeweza kuweka mawakili.
Kwa upande wao Mawakili waliokuwa wakisimamia kesi hiyo kwa upande wa wadai kampuni ya Uwakili la Wasonga walishindwa kuzungumza chochote kwani mara baada ya kumalizika kwa kesi hiyo waliondoka mahakamani hapo.
Source: Mwananchi