Elections 2010 Tumuombee Dr Slaa, Apone Haraka!

Mdau

JF-Expert Member
Mar 29, 2008
1,789
470
Slaa avunjika mkono
• Alianguka bafuni, apanda jukwaani na POP


na Kulwa Karedia




SAFARI ya mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Wilbrod Slaa imeingia doa, baada ya juzi usiku kuvunjika mkono wake wa kushoto baada ya kuanguka bafuni.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema tukio hilo lilitokea majira ya saa 1:45 usiku, mara baada ya Dk. Slaa na timu yake kuwasili katika hoteli waliyopangiwa na wenyeji wao.

“Jana (juzi) baada ya mkutano wetu hapa tulirudi kwenye hoteli tuliyopangiwa ya Nyumbani kwa ajili ya kujiandaa na vikao vingine, Dk. Slaa alipata ajali kidogo, aliteleza akiwa bafuni na kuvunjika mkono wake wa kushoto,” alisema Mbowe.

Alisema baada ya tukio hilo, uongozi wa CHADEMA ulichukua hatua mara moja kwa kumwita daktari bingwa wa mifupa, ambaye alimpatia huduma ya kwanza kabla ya kukimbizwa Hospitali ya Bugando kupatiwa matibabu.

“Tulimwita Dk. Vincent Mhada, alimchunguza na kuthibitisha kuwa amevunjika, alipewa huduma zote muhimu, lakini jambo la kushukuru, pale Bugango alisimamiwa na madakatari bingwa wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Bugando, Dk. Majinge,
“Walimhudumia kwa utaalamu wa juu sana, tunaomba kuwaambia Watanzania waelewe kuwa hali ya Dk. Slaa inaendelea vizuri na tunaye kwenye msafara wetu,” alisema Mbowe.

Alisema baada ya matibabu hayo, madaktari kwa kauli moja wamemruhusu Dk. Slaa kuendelea na safari zake huku akiwa amefungwa POP kwa ajili ya usalama zaidi.

Akizungumzia hali yake, Dk. Slaa alisema kuwa anaendelea vizuri huku akijinasibu kuendelea kuchanja mbunga kutembeza fomu yake kwa lengo la kusaka wadhamini, huku akiwataka Watanzania wasiwe na wasiwasi juu ya afya yake.

“Ni kweli nimepata ajali juzi kati ya saa 1:45 na saa 2 usiku, pale bafuni kulikuwa na maji kwenye sakafu yaliyosababisha niteleze, nilipata maumivu makali sana, lakini nawashukuru madaktari wa mifupa walinisimamia vizuri na kunifunga POP.

“Nimelala salama hapa hotelini kwangu, nimeamka salama kabisa kama mnavyoniona hapa, nawahakikishia Watanzania kwamba mapambano haya yataendelea kama kawaida,” alisema Dk. Slaa.

Alisema Watanzania wasiwe na wasiwasi kabisa kwani katika mapambano jambo lolote linaweza kutokea, na kwamba malengo yake ya kuendelea na vita hiyo yako palepale.

“Nawaambia jambo jema haliwezi kupatikana bila matatizo, hivyo basi ni kama haya, namuachia Mungu nikiamini kuwa nitapona,” alisema Dk. Slaa.

Naye Dk. Mhada, alisema baada ya Dk. Slaa kupigwa picha ya X-ray ilionyesha amevunjika, hali iliyosababisha afungwe mhogo mgumu (POP).

“Kama mnavyomuona hali yake ni nzuri, ameruhusiwa kuendelea na majukumu yake, tunaamini eneo lililopata ajali litaimarika tu,” alisema Dk. Mhada.

Wakati huo huo, Dk. Slaa aliendelea na ziara zake za kusaka wadhamini ambapo alipokewa na mamia ya wananchi wa mji wa Bukoba, mkoani Kagera, shamrashamra zilizosababisha shughuli mbalimbali kusimama.

Mara baada ya msafara wa Dk. Slaa kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Bukoba, ambapo mamia ya wananchi walifurika nje ya uwanja huo, walimsindikiza kwa kukimbia mchakamchaka kwa mwendo wa umbali wa kilomita mbili hadi kwenye Uwanja wa Uhuru Platform, ambako mkutano huo ulifanyika.

Msafara huo ulizidi kuwa na watu wengi pale ulipofika katikati ya mji wa Bukoba, ambako watu wakiwa na matawi ya miti huku wakiimba mageuzi yanawezekana walijiunga na msafara huo kuelekea uwanjani.

Mapokezi ya jana mjini hapa yanaweza kulingana na yale yaliyotokea mkoani Arusha, hasa Wilaya ya Karatu, ambako zaidi ya watu 48,000 walijitokeza kumdhamini.

Akihutubia mamia ya wananchi kwenye mkutano huo, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema uongozi wa taifa hili si jambo la masihara, kwa vile unagusa maisha ya Watanzania.

“Wana Bukoba napenda kuwaambia suala la uongozi si jambo la masihara hata kidogo, suala hili linagusa maisha ya watu, lazima tutafakari tunakwenda wapi mwaka 2010, si mwaka wa kupeana vyeo bali kushughulikia matatizo ya watu,” alisema Mbowe.

Alisema kwa kipindi kirefu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimewageuza Watanzania kuwa mtaji wao wa kupigiwa kura kila uchaguzi unapofika.

Aliwataka wananchi wa Bukoba kuungana na Watanzania kumuombea Dk. Slaa ambaye amevunjika mkono wake wa kushoto baada ya kuanguka bafuni katika Hoteli ya Nyumbani mjini Mwanza.

Naye Dk. Slaa akizungumza kwenye mkutano huo, aliwatupia lawama wafanyabiashara wa kada mbalimbali kwa kuweka bendera za CCM kwenye maduka yao, kwa kile alichosema wanaogopa wasifungiwe.

Alisema CCM imekuwa ikiwatumia kila uchaguzi unapofika kwa ajili ya kuwaomba michango ambayo alidai ni jambo linalopaswa kupingwa.

Katika hatua nyingine, zaidi ya watu 60,000 wamejitokeza mkoani Manyara kwa ajili ya kumdhamini Dk. Slaa kuwania kiti cha urais.

Akizungumza na Tanzania Daima mjini hapa, msaidizi maalum wa mgombea urais wa chama hicho, Wilfred Lakwatare, alisema idadi hiyo ni kubwa, ingawa bado wanaendelea kusaka wadhamini wengine.

“Napenda kukwambia kwamba mgombea urais wetu amefanikiwa kudhaminiwa na watu 60,000 katika Mkoa wa Manyara pekee, hili ni jambo la kujivunia kwetu kwani kunaonyesha namna ambavyo anakubalika kwa Watanzania,” alisema Lwakatare.

Mapema akihutubia mamia ya wananchi wa mkoani Shinyanga kwenye Uwanja wa Shycom, Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, alisema chama chake kimedhamiria kuwaunganisha Watanzania ili kuondoa matabaka ambayo yamekuwa yakizalishwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Nawaambia ndugu zangu wa Shinyanga, tumemteua Dk. Slaa kugombea urais kwa sababu moja kubwa, ni mtu makini ambaye ana uchungu wa taifa hili, ni kiongozi makini anayetambua shida za Watanzania, lakini kubwa zaidi ni kuondoa matabaka ambayo yanazalishwa na CCM,” alisema Mbowe.

Naye Dk. Slaa, akihutubia umati wa wananchi hao, alilaani kitendo cha Rais Jakaya Kikwete kutamka hadharani kuwa hataki kura 350,000 za wafanyakazi kwa vile wamekuwa wakidai nyongeza ya mishahara.

“Rais Kikwete ametamka kwa kinywa chake mwenyewe jamani, amesema hahitaji kura 350,000 za wafanyakazi wa taifa hili, mimi nawaambia nazihitaji kwa ajili ya kuwakomboa Watanzania maskini, waliopigika,” alisema Dk. Slaa.

Katika mkutano huo CHADEMA imekisambaratisha Chama cha Tanzania Labour (TLP), baada ya madiwani wake watatu wanaomaliza muda wao kujiunga CHADEMA.

Madiwani hao na kata zao kwenye mabano ni Israel Mraki (Kibeta), Zeulia Kagirwa (Viti Maalumu) na diwani Dismas Rutagwelera.
 
Mungu akulinde na mabaya yote na upone haraka. Wananchi welewa watakupa kura zao.
 
Let us all come together and pray for Dr. W. Slaa for a quick recovery. "Doctors treat but God heals" I wish you a quick recovery
 
Back
Top Bottom