Tumkumbuke Bi. Titi Mohamed pamoja na Mwami Theresa Ntare Chifu Mwanamke Aliyeunga TANU Mkono

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,925
30,273
PAMOJA NA BI. TITI MOHAMED TUMKUMBUKE MWAMI THERESA NTARE CHIFU MWANAMKE ALIYEJITOKEZA KUUNGA MKONO TANU

Aliyotuhadithia Mwami Theresa Ntare Jinsi Alivyoipa Nguvu TANU Buha

Mzee Dantes alitushauri tumsikilize Mama Theresa kisha tumpe nafasi akapumzike.

“Mama yenu msimuone hivyo, ana mengi sana,” alisema Chief Ngua, na kuongeza, “Tena yeye uhuru ulipopatikana alipewa uwaziri.”

Kwa maneno hayo ya sentensi ya mwisho ya Mzee Dantes Ngua, Mwami Theresa akaitikia; “Ah, nikikumbuka yale niliyokumbana nayo katika mapambano ya kudai uhuru wetu na kitendo nilichofanyiwa na kuondolewa uwaziri, ah, basi tu.”

Mwami Theresa hakutaka kuzungumzia kilichomtoa katika uwaziri.

Aliamua kutuhadithia kisa cha mpambano wake na maafisa Wazungu wa serikali ya kikoloni kwa ajili ya kuipa nguvu TANU ili nchi hii iwe huru:

Serikali ya kikoloni haikutaka sisi machifu tuwe katika siasa hasa kuisaidia TANU.

Hata hivyo tukiwa wananchi na viongozi wa wanchi wanaotaabika chini ya utawala wa kikoloni, tuliiamua kushiriki siasa kwa siri na kuipa nguvu TANU ili tujitawale.

Kuna wakati taarifa zilinifikia kwamba ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulikuwa unakuja kusikiliza maoni ya kudai uhuru. Utaratibu wa kikoloni ni kuwa chama japo ni cha kitaifa, kilitakiwa kipate pia usajili katika kila jimbo.

Hivyo TANU ikidai kuwa inawakilisha wananchi wote, watawala wa mikoa walikuwa wakijiandaa kukisuta kuwa si kweli na kuonesha sehemu ambako hakikuwa na wanachama.

Moja ya sehemu hizo wakoloni waligundua ni katika himaya ya utawala wangu wa Buha.

Waligundua TANU haipo kwa Waha.

Taarifa za siri zikanifika kwa wakoloni wataiambia tume hiyo ya UNO juu ya hilo.

Nikaamua kuchukua hatua kwa siri na kwa haraka.

Nilitoa pesa zangu binafsi na kuagiza haraka kadi za TANU elfu tatu. Zikaletwa kwenye vikapu.

Nikaweka mkakati wa siri na watu wangu jinsi ya kuzigawa kadi hizo kwa haraka kwa wananchi wa maeneo ya Buha.

Majira ya saa tatu za usiku lilipigwa baragumu la wito wa dharura watu waje kwa Mwami.

Wito ulifikishwa kwa haraka kila eneo. Wananchi wakamiminika. Eneo la makazi yangu lilikuwa na uwanja mkubwa sana.

Niliwapanga watu wangu katika lango la kuingilia wakiwa na vikapo vilivyokuwa na kadi za TANU na karatasi zake za risiti.

Kila mtu alipoingia alipewa kadi na risiti isiyoandikwa.
Kisha akaambiwa aifikiche kadi na hiyo risiti pasipo kuichana.

Na asiongee chochote hadi afike lango la nyuma ambalo ni la kutokea. Hapo palikuwepo watu wamejipanga katika meza.

Walipofika hapo walimpa huyo aliyekuwepo katika meza hiyo kadi na risiti kisha kumtajia majina yake, anakoishi nk. Yule karani aliiiandika ile kadi na risiti kwa tarehe za miezi ya nyuma, meza nyingine ilipiga muhuri.

Mwisho mwenye kadi aliambiwa kuwamba ameisha kuwa mwanachama wa TANU wa muda mrefu.

Akiulizwa atoe kadi na aitetee TANU pasipo kumtaja Mwami wala kilichotokea usiku ule; kwake hicho ni kiapo cha utiifu kwa Mwami.

Aliruhusiwa na kusisitizwa kuitunza hiyo kadi na risiti yake.

Mwami Theresa alitufahamisha kuwa zoezi lile lilikamilika mnamo saa tisa za usiku.

Meza zikaondolewa na wafanyakazi wakatawanyika na kwenda kulala.

Mzee Ngua akasema, “Sisi machifu tulikuwa na utiifu mkubwa toka kwa wananchi.

Hata hili tatizo la Ukimwi, kama ingelikuwa enzi zile, tungetoa tamko la muongozo wa kuacha zinaa, Ukimwi ungeishatokomezwa.”

Mwami akaendelea kutuhadithia:

Ilipofika alfajiri karibu ya saa kumi na mbili za asubuhi, nikaambiwa kuna msafara wa magari ya polisi unaelekea kwenye makazi yangu.

Niliyategemea hayo, maana vibaraka wapelelezi walikuwepo enzi hizo. Hata hivyo, kwa tukio lile walikuwa wameshachelewa.

Mimi siku ile sikuwa nimelala wala kupata usingizi.

Nilikuwa katika nguo zangu za kawaida.

Nilipoletewa taarifa ile, nikaingia chumbani na kuwaambia walinzi wangu kuwa wakifika, kwanza kuweni imara kuhusu siri ya kilichotokea usiku.

Pili waambieni kuwa Mwami hajamka.

Ngoja tukamwamshe.

Kisha mje kunigongea.

Na kwamba nitakapotoka na kufokeana nao, nyiye onesheni utiifu kwangu na kuwakasirikia wao; wala msioneshe kuwahofu.

Mkakati huo ukaeleweka.

Mwami Theresa akatueleza kuwa wakaingia maofisa wa polisi akiwemo mmoja Mzungu na DC (District Commissioner) Mzungu pia. Wakauliza kama Mwami yupo.

Wakaambiwa amelala, na kwamba wanaenda kumuamsha.

Walinzi wa Mwami wakaenda kugonga mlango wake. Baada ya muda akaitikia na kuuliza kwa sauti ya juu, “Kuna nini mnanigongea usiku huu?” wakamjibu, “Kuna Bwana DC na mkubwa wa polisi.”

Mwami akajibu kwa sauti kali, “Wanataka nini wakati hakujakucha ngoja nije.”

Akatuambia kuwa alijiandaa kwa kuvaa “night dress” akatimua nywele zake kisha akajiviringisha shuka na blanketi akatoka akiwa ameshikilia na alipofika sebuleni na kuwaona hakuwasalimia wala kusubiri salam zao.

Alianza kwa kuwafokea kwa lugha ya Kiingereza:

“How dare you wake me up at this time of the hour? Can you do this to the Queen of the UK?

Don’t you know I am the the Queen of Buha? Is it because I’m an African that’s why you are doing this to me?

I will file my complaints and report you to the Governor for this.”

Mwami akatuhadithia kuwa wale maofisa wa kikoloni walichanganyikiwa na kuanza kujitetea kuwa walipata taarifa kwamba alikuwa akigawa kadi za TANU usiku.

Akawajibu, “Je, mmkuja na ‘’Search Warrant?” Kisha akaongeza kwa kuwaambia, “Nyiye askari wanaume watupu pamoja na DC mmekuja kunipekua mimi mwanamke?

Nitamlalamikia Gavana.''

Hawakuwa na ‘’Search Warrant.’’

Mwami akawageukia walinzi wake na kuwataka wawaambie wale DC na mapolisi wake watoke mara moja au wapige baragumu kuashiria Mwami amevamiwa ili waje wamhami.

Yule DC na watu wake waliomba radhi haraka na kuondoka.

Baada ya kutuhadithia kisa hicho Mwami Theresa Ntare alituambia bora turudi pale siku ya Jumamosi iliyofuata kwa mazungumzo na mahojiano zaidi, “Jumamosi mtapata mengi.

Maana kuna waandishi Wamarekani watakuja kunihoji kuhusu harakati za wanawake kuhusu kupigania uhuru wa Tanganyika.”

Bahati mbaya hatukuweza kupata fursa ya kwenda siku hiyo. Mwami akasafiri.

Na hatukuonana nae tena.

NTARE%252C%2BMwami%2BTheresa%2B%2528Mhina%2529.jpg
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom