Mwami Theresa Ntare (1922 - 1999)

Mohamed Said

JF-Expert Member
Nov 2, 2008
20,918
30,259

Aisha ''Daisy'' Sykes katika makala ''Abdul Sykes Nimjuaye'' aliyoandika katika kumbukumbu ya miaka 50 ya kifo cha baba yake Abdul Sykes aliyefariki mwaka wa 1968, Daisy alimtaja katika makala hiyo Mwami Theresa Ntare:

"Nyumbani kwetu milango ilikuwa wazi siku zote kwa wageni.

Hivi ndivyo tulivyokuwa na wageni kutoka kila kabila, uwezo na hali tofauti.

Lakini kile ambacho kimeathiri fikra zangu na kubakia na mimi katika kumbukumbu zangu ni kufika pale nyumbani kwa uongozi wa juu wa Waafrika kabla ya uhuru, machifu kutoka makabila mbalimbali ya Tanganyika na viongozi wa vyama vya wazalendo vilivyokuwa ndiyo vinainukia, viongozi wa vyama vya wafanyakazi na wafanyakazi Waafrika katika wa serikali ya kikoloni.

Kutokana na hadhi hii ya baba yangu na umaarufu wake na kule kupenda kukirimu watu, nikawa si mgeni kwa machifu mashuhuri na nikawa nawahudumia walipokuwa mara nyingi wakija nyumbani.

Wageni hawa mashuhuri waliokuwa wakija nyumbani ni pamoja na Mangi Mkuu Thomas Marealle, Machifu Abdiel Shangali, John Maruma kutoka Moshi, Adam Sapi Mkwawa kutoka Iringa, Kidaha Makwaia kutoka Usukuma, Abdallah Fundikira, Harun Lugusha kutoka Tabora, Humbi Ziota kutoka Nzega, Michael Lukumbuzya kutoka Ukerewe na Patrick Kunambi kutoka Morogoro na wengine wengi.

Hawa machifu kwa kawaida walikuwa wakija na wake zao, wanawake warembo ambao hawakuacha kunifanya mimi kuwashangalia.

Nakumbuka katika machifu wale, alikuwapo chifu mmoja na wa pekee mwanamke - Mwami Theresa Ntare kutoka Kasulu Kibondo.

Katika hali kama hii iliyokuwa tabu kufahamika, tukiwa watoto tulipata kujua maisha ya jamii nyingine, lugha zao, utamaduni wa makabila mengi ya Tanganyika kabla ya watu wengi kutoka sehemu nyingine za pwani hawajajua chochote kuhusu watu hawa."

MWAMI THERESA NTARE ANAELEZA ALIVYOIINGIZA TANU KATIKA UTAWALA WAKE BUHA

"Serikali ya kikoloni haikutaka sisi machifu tuwe katika siasa hasa kuisaidia TANU.

Hata hivyo tukiwa wananchi na viongozi wa wanchi wanaotaabika chini ya utawala wa kikoloni, tuliiamua kushiriki siasa kwa siri na kuipa nguvu TANU ili tujitawale.

Kuna wakati taarifa zilinifikia kwamba ujumbe wa Umoja wa Mataifa ulikuwa unakuja kusikiliza maoni ya kudai uhuru.

Utaratibu wa kikoloni ni kuwa chama japo ni cha kitaifa, kilitakiwa kipate pia usajili katika kila jimbo.

Hivyo TANU ikidai kuwa inawakilisha wananchi wote, watawala wa mikoa walikuwa wakijiandaa kukisuta kuwa si kweli na kuonesha sehemu ambako hakikuwa na wanachama.

Moja ya sehemu hizo wakoloni waligundua ni katika himaya ya utawala wangu wa Buha.

Waligundua TANU haipo kwa Waha.

Taarifa za siri zikanifika kwa wakoloni wataiambia tume hiyo ya UNO juu ya hilo.

Nikaamua kuchukua hatua kwa siri na kwa haraka.

Nilitoa pesa zangu binafsi na kuagiza haraka kadi za TANU elfu tatu.

Zikaletwa kwenye vikapu.

Nikaweka mkakati wa siri na watu wangu jinsi ya kuzigawa kadi hizo kwa haraka kwa wananchi wa maeneo ya Buha.

Majira ya saa tatu za usiku lilipigwa baragumu la wito wa dharura watu waje kwa Mwami.

Wito ulifikishwa kwa haraka kila eneo.

Wananchi wakamiminika.

Eneo la makazi yangu lilikuwa na uwanja mkubwa sana.

Niliwapanga watu wangu katika lango la kuingilia wakiwa na vikapo vilivyokuwa na kadi za TANU na karatasi zake za risiti.

Kila mtu alipoingia alipewa kadi na risiti isiyoandikwa.

Kisha akaambiwa aifikiche kadi na hiyo risiti pasipo kuichana.

Na asiongee chochote hadi afike lango la nyuma ambalo ni la kutokea.

Hapo palikuwepo watu wamejipanga katika meza.

Walipofika hapo walimpa huyo aliyekuwepo katika meza hiyo kadi na risiti kisha kumtajia majina yake, anakoishi nk.

Yule karani aliiiandika ile kadi na risiti kwa tarehe za miezi ya nyuma, meza nyingine ilipiga muhuri.

Mwisho mwenye kadi aliambiwa kuwamba ameisha kuwa mwanachama wa TANU wa muda mrefu.

Akiulizwa atoe kadi na aitetee TANU pasipo kumtaja Mwami wala kilichotokea usiku ule; kwake hicho ni kiapo cha utiifu kwa Mwami.

Aliruhusiwa na kusisitizwa kuitunza hiyo kadi na risiti yake.

Mwami Theresa alitufahamisha kuwa zoezi lile lilikamilika mnamo saa tisa za usiku.

Meza zikaondolewa na wafanyakazi wakatawanyika na kwenda kulala.

Mzee Ngua akasema, “Sisi machifu tulikuwa na utiifu mkubwa toka kwa wananchi.

Hata hili tatizo la Ukimwi, kama ingelikuwa enzi zile, tungetoa tamko la muongozo wa kuacha zinaa, Ukimwi ungeishatokomezwa.”

Mwami akaendelea kutuhadithia:

Ilipofika alfajiri karibu ya saa kumi na mbili za asubuhi, nikaambiwa kuna msafara wa magari ya polisi unaelekea kwenye makazi yangu.

Niliyategemea hayo, maana vibaraka wapelelezi walikuwepo enzi hizo.

Hata hivyo, kwa tukio lile walikuwa wameshachelewa.

Mimi siku ile sikuwa nimelala wala kupata usingizi.

Nilikuwa katika nguo zangu za kawaida.

Nilipoletewa taarifa ile, nikaingia chumbani na kuwaambia walinzi wangu kuwa wakifika, kwanza kuweni imara kuhusu siri ya kilichotokea usiku.

Pili waambieni kuwa Mwami hajamka.

Ngoja tukamwamshe.

Kisha mje kunigongea. Na kwamba nitakapotoka na kufokeana nao, nyiye onesheni utiifu kwangu na kuwakasirikia wao; wala msioneshe kuwahofu.

Mkakati huo ukaeleweka.

Mwami Theresa akatueleza kuwa wakaingia maofisa wa polisi akiwemo mmoja Mzungu na DC (District Commissioner) Mzungu pia.

Wakauliza kama Mwami yupo.

Wakaambiwa amelala, na kwamba wanaenda kumuamsha.

Walinzi wa Mwami wakaenda kugonga mlango wake.

Baada ya muda akaitikia na kuuliza kwa sauti ya juu, “Kuna nini mnanigongea usiku huu?” wakamjibu, “Kuna Bwana DC na mkubwa wa polisi.”

Mwami akajibu kwa sauti kali, “Wanataka nini wakati hakujakucha ngoja nije.”

Akatuambia kuwa alijiandaa kwa kuvaa “night dress” akatimua nywele zake kisha akajiviringisha shuka na blanketi akatoka akiwa ameshikilia na alipofika sebuleni na kuwaona hakuwa salimia wala kusubiri salam zao.

Alianza kwa kuwafokea kwa lugha ya Kiingereza:

“How dare you wake me up at this time of the hour?

Can you do this to the Queen of the UK?

Don’t you know I am the the Queen of Buha?

Is it because I’m an African that’s why you are doing this to me?

I will file my complaints and report you to the Governor for this.”

Mwami akatuhadithia kuwa wale maofisa wa kikoloni walichanganyikiwa na kuanza kujitetea kuwa walipata taarifa kwamba alikuwa akigawa kadi za TANU usiku.

Akawajibu, “Je, mmkuja na ‘’Search Warrant?”

Kisha akaongeza kwa kuwaambia, “Nyiye askari wanaume watupu pamoja na DC mmekuja kunipekua mimi mwanamke?

Nitamlalamikia Gavana.''

Hawakuwa na ‘’Search Warrant.’’

Mwami akawageukia walinzi wake na kuwataka wawaambie wale DC na mapolisi wake watoke mara moja au wapige baragumu kuashiria Mwami amevamiwa ili waje wamhami.

Yule DC na watu wake waliomba radhi haraka na kuondoka.

Baada ya kutuhadithia kisa hicho Mwami Theresa Ntare alituambia bora turudi pale siku ya Jumamosi iliyofuata kwa mazungumzo na mahojiano zaidi.

“Jumamosi mtapata mengi.

Maana kuna waandishi Wamarekani watakuja kunihoji kuhusu harakati za wanawake kuhusu kupigania uhuru wa Tanganyika.”

Bahati mbaya hatukuweza kupata fursa ya kwenda siku hiyo.

Mwami akasafiri.
Na hatukuonana nae tena.

1708422392899.jpeg

Mwami Theresa Ntare
(1922 -1999)​
 
Back
Top Bottom